20 Oct 2014

Wakati Mbunge wa jimbo la Kawe, Dar es Salaam (Chadema), Halima Mdee akiahidi kuvalia njuga utata unaogubika mradi wa uwekezaji wa treni za kisasa jijini Dar, utata zaidi umeibuka kufuatia uchunguzi uliofanywa na mtaalam mmoja kutoka hapa Uingereza anayeishi nchini Tanzania (siwezi kutaja jina lake kwa vile sijapata idhini yake). 

Hapa chini ni tafsiri ya sehemu ya maelezo/ushauri alionipatia kwa barua-pepe:

Ni vigumu kujua wapi pa kuanzia kuhusu Shumake kwani anaonyesha kuwa ni mtu mwenye utata. Nyenzo zake za kibiashara zipo tupu na majibu yake kwa maswali uliyomtumia hayaridhishi.Pia ameonyesha dalili za jeuri pale aliposema  'do your research (fanya utafiti).

Unaweza kumkamata katika udanganyifu wake. Anadai kuwa kitabu chake cha 'Climbing Your Inner Mountain' ni 'number one seller' (kinaongoza kwa mauzo). Katika Amazon Kindle edition kinashika nafasi ya 472,476 kwa mauzo. Kwenye orodha ya vitabu vyenye 'jalada' (paperback), kitabu hicho kinashika nafasi ya 3,374, 824.

Hivi kweli (kiwa takwimu hizo) kitabu hicho kinaweza kweli kuitwa 'Number One Bestseller'? Huyu mtu si wa kuaminika, kinyume kabisa na anavyodai.

Kuhusu Shumoja na Shumake Global Partners: Kati ya maelezo yake aliyokutumia kwa email na tovuti yake, ni utata mtupu. Anasema Shumake Global Partners ni 'kampuni ya kibenki ya uwekezaji' (investment banking firm). Nneo 'banking' lipo bayana. Je kuna mahala popote Shumake Global Partners imeandikishwa kama benki? Nina hofu kuhusu hilo, lakini ni yeye pekee anayeweza kujibu. Je anaweza kutaja miradi yoyote ambayo imegharamiwa na Shumake Global Partners?

Kuhusu Shumoja Rails, lini ilianzishwa? Je yupo tayari kuwataja wawekezaji katika kampuni hiyo japo kama ni kampuni binafsi anaweza kupata sababu ya kutfanya hivyo)? Lini Shumoja Industries LLC ilianzishwa? Kuna uhusiano gani kati ya Shumoja Rails na Shumoja Industries LLC?

Je mtaji wa uwekezaji unatoka wapi (tukiamini kuwa kweli anao)? Je katika hilo, kuna fedha zozote zinazotoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo amehusishwa nayo huko nyuma kama ilivyo kwenye taarifa hii ya Bloomberg?




15 Oct 2014

Oktoba 20 mwaka huu itakuwa siku muhimu kwa Nigeria kwani siku hiyo taifa hilo litaadhimisha siku 42 tangu mtu wa mwisho kuthibitishwa kuwa na maambukizi ya Ebola. Idadi hiyo ya siku ni mara maradufu ya muda ambao Ebola yaweza kujitokeza hadharani (incubation period). Kwa maana hiyo, siku hiyo, Nigeria itakuwa na haki ya kujitangaza kuwa ipo huru dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Hata hivyo, jana, Nigeria iliadhimisha tukio jingine ambalo pengine isingependa kulikumbuka: miezi sita kamili tangu kikundi cha kigaidi cha Kiislamu cha Boko kilipowateka wanafunzi wa kike 276 na kupelekea kelele takriban kila kona ya dunia kwa kampeni ya #BringBackOurGirls (Warejesheni Mabinti zetu).

Hata hivyo, licha ya kampeni hiyo, mabinti 219 bado wanaendelea kuwa mateka wa magaidi hao tangu walipotekwa katika eneo la Chibok. Licha ya tukio hilo la kinyama kuvuta hisia na sapoti ya watu wengi duniani, magaidi hao wanaendelea kufanya unyama wao uliopelekea maelfu ya mauaji, hususan katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Maadhimisho hayo mawili yanazua swali linalokanganya: imewezekanaje kwa Nigeria kumudu kuidhibiti Ebola lakini imeshindwa kuidhibiti Boko Haram? Kwanini taifa hilo limeweza kulishughulikia tatizo moja kwa ufanisi mkubwa ilhali ikilishughulikia jingine kwa udhaifu mkubwa?

"Ebola inamgusa kila mtu."

Moja ya sababu ni jiographia ya kisiasa (political geography) ya Nigeria.ambayo tangu nchi hiyo kupata uhuru wake imekabiliwa na machafuko. Taifa hilo lenye watu milioni 170 ambao wamegawanyika katika makabila lukuki, limeshindwa kwa kiasi kikubwa kujenga umoja,mshikamano na maelewano kati ya wengi wa Wakristo wanaojiweza kwa upande wa kusini mwa nchi hiyo na wengi wa Waislamu wanaokabiliwa na ufukara upande wa kaskazini mwa nchi hiyo.

Boko Haram ambayo maana yake ni ni 'elimu ya kimagharibi ni dhambi,' inautumia mwanya huo.Kundi hilo linafanya zaidi shughuli zake katika majimbo matatu ya kaskazini mashariki, yote yakiwa chini ya uongozi wa chama cha upinzani cha All People's Party (APP), na ambako imani kwa Rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan, ni haba.

"Watu wengi kaskazini mwa Nigeria wanaichukia Boko Haram," anaeleza Rudy Atallah wa taasisi ya The Atlantic Council na mtaalam wa masuala ya nchi hiyo. "Lakini kwa vile idadi kubwa ya watu wa kaskazini mwa nchi hiyo wanaona kama wametelekezwa na wenzao wa kusini kwa muda mrefu, wengi wanaiona Boko Haram kama chombo kinachoweza kuambana na serikali," anatanabaisha mtaalam huyo.

Katika hali tofauti, Patrick Swayer, Mwamerika mwenye asili ya Liberia alipogundulika kuwa na Ebola alipowasili Lagos, alijikuta katika jiji lililosheheni miundominu ya kisasa ya huduma za afya na makao makuu ya taasisi nyingi za kimataifa, Na tofauti na mapambano dhidi ya Boko Haram, mapambano dhidi ya Ebola yanavuka mipaka ya ukabila, siasa na dini.

"Ebola inamgusa kila mtu," anasema Atallah. "Haina madhehebu wala kundi maalum."

'Kasheshe' nyingine nchini humo yatarajiwa Februari mwakani wakati taifa hilo litakapofanya uchaguzi wa Rais. Baada ya mhula mmoja madarakani, Rais Jonathan anaruhusiwa kugombea tena. Ushindi kwa chama chake cha People's Democratic Party, ambacho kimeitawala Nigeria kwa miaka 14, na ambacho kina sapoti kubwa kusini mwa nchi hiyo, waweza kuchochea mgawanyiko zaidi nchini humo, sambamba na ugumu wa kuwaokoa mateka waliosalia mikononi mwa Boko Haram.

CHANZO: Makala hii imetafsiriwa kutoka hifadhi yangu ya habari muhimu, ninazokutana nazo mtandaoni na kuzihifadhi katika app ya Instapaper. App nyingine ninayoitumia kwa hifadhi ya habari ninazozitumia kama reference ni Pocket. Kadhalika, app nyingine muhimu ninayoitumia kuhifadhi vitu mbalimbali ninavyokutana navyo mtandaoni au hata mtaani ni Evernote





Chris Brown is sharing his thoughts about Ebola. (Getty Images)
Dunia yetu imesheheni watu wanaoitwa 'conspiracy theorists,' Sina uhakika wa tasiri ya kiswahili ya neno hilo, lakini nadhani neno la karibu ni 'wazushi.' Hata hivyo, tofauti ya wazushi tuliowazowea ambao mara nyingi huzusha jambo kwa minajili ya kuzusha tu, kwa conspiracy theorist uzushi wao huambatana na 'ushahidi wa kimazingira,' japo si ajabu ushahidi huo nao kuelemea zaidi kwenye uzushi kuliko facts.

Sasa msanii maarufu wa Marekani, Chris Brown, nae ameingia katika kundi la conspiracy theorists baada ya kudai kuwa ugonjwa hatari wa Ebla ni moja ya mbinu za kudhibiti idadi ya watu duniani.

Msanii huyo ali-post mtizamo wake huo kwenye ukurasa wake wa Twitter, ambapo ana 'wafuasi' (followers) milioni 13.7. Hata hivyo, baadhi yao walipingana nae waziwazi

"Wajua mjadala kuhusu ugonjwa wa Ebola ulichokuwa unahitaji? Upuuzi zaidi. Hapa anaingia Chris Brown..." aliandika mmoja wa wafuasi wake.

"Chris Brwon anadai Ebola ni moja ya mbinu za kudhibiti idadi ya watu. Ajaribu ugonjwa." alitwiti mwingine  huo  akimaanisha msanii huyo ni miongoni mwa watu wanaohitaji kudhibitiwa.

"Chris Brown anadai kuwa Ebola ni njia ya kudhibiti widadi ya watu. Kwa hakika hiyo si kweli, na laiti ingekuwa kweli basi tungempa ugonjwa huo yeye kwanza," aliandika mwingine.

Brown ambaye hivi karibuni alitumikia kifungo cha siku 108 jela kwa kukiuka taratibu za uangalizi wa kimahakama (probation) kufuatia kosa la kumpiga mpenzi wake wa zamani, msanii Rihanna, baadaye alionekana kutafakari upya kauli yake, na kutanabaisha kuwa 'anafunga mdomo wake,' japo si kwa maneno ya kistaarabu.

Lakini muda mfupi baadae 'alipandisha mzuka' na kuwashambulia waliopingana na mtizamo wake huo, na kutwiti maneno makali: "naandika ninachotaka. Kama hutaki nyonya %$*£$ yangu (tusi)

Hata hivyo, licha ya baadhi ya watu kupingana na conspiracy theory hiyo ya msanii huyo, watu kadhaa katika mtandao huo wa Twitter walionekana kuafikiana nae kwa tweet hiyo kupata takriban  'Retweets' 30,000 na 'Favourites' 22,000.

Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola umeshasababisha vifo zaidi ya 4000 huku Afrika ya Magharibi ikiwa ni eneo lililoathirika vibaya zaidi japo tayari kuna wagonjwa wachache waliokumbwa na maradhi hayo huko Hispania na Marekani.

CHANZO: Imetafsiriwa kutoka mtandaoni



14 Oct 2014

These were the questions I put forward to Mr Robert Shumake (haya ndiyo maswali niliyomuuliza Robert Shumake)
And below are series of Shumake's responses, click photo to enlarge (na chini ni mlolongo wa majibu ya Shumake, bonyeza picha kuikuza)






My final request to Shumake was advising he publishes the provisionary Memorandum of Understanding between his company M/S Shumoja a.k.a Shumake Rails (he has so far failed to concisely clarify on this) and the Government of Tanzania. While he is yet to respond, I will continue with my investigation, and will definitely keep you posted. As for now, I leave to you wananchi to pass a verdict whether this guy a genuine investor or not? (Ombi langu la mwisho kwa Shumake ni kumshauri aweke wazi kataba wa awali kati ya kampuni yake ya M/S Shumoja au Shumake Rails (kwa ujumla ameshindwa kufafanua kuhusu hili) na serikali ya Tanzania. Wakati bado hajanijibu kuhusu ombi hilo, mie ninaendelea na uchunguzi wangu na nitawajuza maendeleo yake.Kwa sasa nawaachia ninyi wananchi kutoa hukumu iwapo mtu huyu ni mwekezaji kweli au la)





12 Oct 2014

Kama mtu mwenye uelewa kiasi kuhusu utendaji kazi wa Idara yetu ya Usalama wa Taifa, nimekuwa 'nikipiga kelele' mara kwa mara kuhusu haja ya mageuzi ndani ya taasisi hiyo nyeti. Kwa bahati mbaya sio tu kelele hizo ni vigumu kueleweka kwa Watanzania wengi, uwezekano wa kusikilizwa ni mdogo hasa ikizingatiwa kuwa asili ya taasisi hiyo ni kutekeleza majukumu yake kwa siri, na kama hiyo haitoshi, mara nyingi wahusika wa taaluma hiyo inayopaswa kuhusisha matumizi ya hali ya juu ya akili, hawapendi kusikia ushauri wa 'walio nje' kama akina sie.

Mageuzi ninayoyapigia kelele ni ya kimfumo. Kubwa zaidi ni haja ya uwepo wa mazingira ya uwajibikaji pale watu wanapoboronga. Moja ya dhana zinazotawala fani ya ushushushu ni ile isemayo 'kushamiri kwa matishio ya usalama katika nchi husika ni dalili kuwa taasisi ya ushushushu katika nchi husika ina mapungufu.' Sasa huhitaji uelewa wa fani hiyo kutambua kushamiri kwa matishio kadhaa ya usalama katika Tanzania yetu, kubwa zaidi likiwa ufisadi. 

Labda waweza kujiuliza, iweje ufisadi uwe tishio la usalama? Jibu jepesi ni kwamba ufisadi unatoa fursa kwa maadui wa ndani na nje wa taifa kutimiza azma zao kwa urahisi. Kwa mfano, laiti kukiwa na ufisadi kwenye mipaka ambapo wahusika wanaruhusu kirahisi tu wageni kuingia nchini pasi kuzingatia taratibu zilizopo, ni rahisi kwa magaidi kutumia mwanya huo. 

Ufisadi unaweza kutuletea tapeli la kimataifa kuwekeza kwenye maeneo yanayofahamika kiusalama kama 'vituo muhimu' (vital installations) kama vile viwanja vya ndege na bandarini.

Sasa tukichukulia mfano wa ufisadi, sio tu umeshamiri vya kutosha lakini ndo wazidi kuongezeka. Kuna wanaojiuliza je TISS (Idara yetu ya Usalama wa Taifa) ipo likizo ndefu, wahusika wapo katika usingizi fofofo au kazi imewashinda? Mie sina jibu la moja kwa moja lakini nadhani tatizo la TISS ni la kimfumo zaidi kuliko kiutendaji, japo utendaji wao nao una walakini.

Lakini kabla ya kuingia kwa undani katika mada hii, nirejee kwenye kichwa cha habari. Majuzi, mkuu wa taasisi yenye jukumu la ulinzi wa viongozi wakuu wa Marekani, Secret Service, Bi Julia Pierson alilazimika kujiuzulu wadhifa huo baada ya mtu mmoja kuingia uzio wa Ikulu ya nchi hiyo na kutishia usalama wa Rais Barack Obama. Kwa wenzetu tukio hilo lilikuwa na uzito mkubwa sana, na lilitawala sana katika vyombo vya habari.


Hata hivyo, kwa vile wenzetu wanaendesha mambo kwa uwazi, mwanamama huyo aliitwa mbele ya kamati moja ya bunge la juu la nchi hiyo na kupewa fursa ya kuieleza, ambapo watunga sheria waliafikiana kwamba anapaswa kujiuzulu.
Tukirejea huko nyumbani, ukweli usiopingika ni kwamba licha ya vikwazo vya kimfumo vinavyoikabili TISS, ksingizio  cha 'taasisi hii yafanya kazi kwa siri na hakuna anayepaswa kuhoji' kinatoa fursa kwa wazembe kupata kinga katika utendaji wao mbovu. Ndio, kazi za TISS ni za siri lakini so far usiri huo haujafanikiwa kuwawezesha kukabiliana ipasavyo na matishio ya kiusalama, la wazi likiwa ni ufisadi.

Miongoni mwa mapendekezo yangu (yapo mengi) kuhusu haja ya mageuzi ni kama ifuatavyo.

Kwanza, uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu unapaswa kufanywa kwa uwazi zaidi, ikiwezekana kuidhinishwa na Bunge. Hiyo itazuia uwezekano wa Rais kumpatia wadhifa huo mtu yeyote yule bila kuzingatia uadilifu na uwezo wake kikazi. Kwa kumpa Rais 'blank cheque' ni rahisi kwake kumchagua mtu wake, au mshkaji wake kwa minajili ya kumlinda au kuwa kibaraka wake badala ya kulitumikia taifa kiufanisi.
Pili, ni muhimu TISS kama taasisi iwajibike kwa umma, na si kwa Rais pekee (maana huyo Waziri Katika Ofisi ya Rais mwenye jukumu la kuisimamia TISS anakwazwa na mazingira yalivyo, sambamba na 'uoga' wa kawaida). Ifike mahali, watendaji wakuu wa TISS waweze kuitwa Bungeni, kwa mfano, kuhojiwa kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu taasisi hiyo.

Kiutendaji, ni muhimu kwa taasisi hiyo kupewa uhuru wa kioperesheni utakaoiwezesha kuondokana na hali iliyopo sasa ambapo kwa kiasi kikubwa imekuwa kama tawi la usalama la chama tawala. Sambamba na hilo ni haja ya kuitengenezea mazingira yatayoiwezesha kuhakikisha mapendekezo yake kwa Rais yanafanyiwa kazi hata pale Rais anapoyapuuza. Ikumbukwe kuwa licha ya Rais kuwa 'mkuu halisi wa TISS,' yeye bado ni mwananchi kama wananchi wengine ambao TISS inawajibika kuhakikisha sio tu usalama wao bali hawawi tishio kwa usalama huo. Rais anapopuuza ushauri unaotishia usalama wa taifa basi TISS ijengewe mazingira ya kuhakikisha kuwa ushauri wake unafanyiwa kazi.

Nimalizie kwa kutumaini kuwa 'kelele' hizi zitasikika kwa wahusika. Tujifunze kwa wenzetu waliotatutangulia na wahusika wasione aibu kusikia ushauri wa wenye uelewa hata kama wapo nje ya 'uwanja wa mapambano.'

Endelea kutembelea blogu hii kwa habari mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hizi za ushushushu (bonyeza hapo kwenye menu ya INTELIJENSIA upelekwe moja kwa moja)





bbb 



The Gatekeeper ni filamu (documentary) inayoeleza kuhusu shirika la ushushusu wa ndani wa Israel, Shin Bet (au Shabak kwa Kiyahudi) kutoka kwa mtizamo wa wakuu sita wa zamani wa shirika hilo (pichani juu) kwa njia ya mahojiano.


 

Endelea kutembelea blogu hii kwa habari mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hizo zinazohusu ushushushu (bonyeza kwenye menu INTELIJENSIA kwenda moja kwa moja). Kuhusu makala ya 'Shushushu ni nani? Anafanya kazi gani?' ninaahidi kuiendeleza katika siku chache zijazo. Ninaomba samahani kwa kuichelewesha.

10 Oct 2014

Kwanza soma taarifa ifuatayo kutoka Ikulu kisha tuijadili pamoja
Kweli Tanzania yetu haina uhaba wa mazingaombwe. Lakini hilo dogo, kubwa ni 'akili' za baadhi ya wasaidizi wa Rais. Binafsi nimekuwa mpinzani sana wa hoja kuwa 'tatizo si JKI bali wasaidizi/ watendaji wake,' kigezo changu kikubwa kikiwa 'kwani walimshikia mtutu wa bunduki awateue na kisha kumtahadharisha kuwa akiwatimua pindi watapoboronga watamdhuru'?

Lakini ukiangalia mlolongo wa 'makanusho' yanayotolewa na wasaidizi wa Rais, unaweza kukubaliana na wanaosema kuwa 'wasaidizi/ watendaji wa JK wanamwangusha' (japo siafiki wanaotaka kutumia sababu hiyo kama excuse ya kumsafisha JK mwenyewe.)


Hebu tuichambue kauli hiyo ya Ikulu hatua kwa hatua. Kwanza, Ikulu haikuwahi kukanusha lundo la picha (kama hiyo inayoambatana na kichwa cha habari hii) zilizowekwa mtandaoni zikimwonyesha Rais Kikwete akipokea zawadi ya saa, huku maelezo yakibainisha waziwazi kuwa 'Rais Jakaya Kikwete akipokea zawadi ya saa..." Najua kwanini hawakuhangaika na taarifa hizo za awali: hazikuhusiana na 'utata' unaomkabili mwekezaji aliyetoa zawadi hiyo.
Lakini baada ya gazeti la Raia Mwema kueleza bayana kuwa mwekezaji wa mradi wa treni ya kisasa Dar ndiye huyo alompa zawadi ya saa Rais Kikwete, na kutanabaisha maswali kadhaa yanayouzunguka mradi husika na wasifu wa mwekezaji huyo, Ikulu ikakurupuka na kanusho hili. WALIKUWA WAPI MUDA WOTE HUO?

Mwandishi wa taarifa hiyo ameonyesha ni mtovu wa nidhamu wa kutokana na matumizi ya maneno yasiyopaswa kutoka ofisi iliyopo sehemu 'tukufu' kama Ikulu. Matumizi ya maneno kama "ni habari ya uzushi na UPUUZI..." na  "...kumhusisha Rais na zawadi ya KIPUUZI kama saa..."Huwezi kuita upuuzi habari inayohoji suala la msingi, ambapo logically, mfanyabiashara anaonekana akitoa zawadi kwa Rais (iwe saa au suti), kisha siku chache baadaye mfanyabiashara huyo anatangaza 'mradi wa utata'...Kwanini wananchi (waandishi wa gazeti hilo ni sehemu ya wananchi hao) wasihoji suala hilo ambalo mwandishi wa Ikulu anaona ni la kipuuzi?

Na kwa kinachoweza kuelezwa kama uhuni na si ubabaishaji, taarifa hiyo ya Ikulu imekwepa kabisa kuzungumzia maswali lukuki yanayoiandama kampuni inayomilikiwa na mfanyabiashara huyo, wasifu wa mfanyabiashara mwenyewe, sambamba na 'sintofahamu' lukuki kuhusu uwekezaji huo.

Kimsingi, habari Ikulu 'imejishtukia' tu inapodai "Ni habari ya uzushi na upuuzi. Ni habari inayolenga kumdhalilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwamba amepokea zawadi kutoka kwa mtu ambaye anajaribu kupewa kandarasi ya kujenga ya usafiri wa treni jijini DSM na ambaye pia anahusishwa kwenye shughuli nyingine za kibiashara zenye utata huko kwao Marekani."

Kwa wapambe hao wa Rais ni upuuzi na kumdhalilisha Rais kupokea zawadi kutoka kwa mtu ambaye WANAKIRI BAYANA kuwa anahusishwa na shughuli nyingine za kibiashara ZENYE UTATA huko Marekani. 

Kwanini taarifa hiyo isingewekeza nguvu katika 'kumsafisha' Rais kwa 'kujihusisha' na mtu huyo wanayekiri kuwa na shughuli zenye utata, badala ya kung'ang'ania hoja moja tu 'ya kipuuzi' kuhusu 'zawadi ya kipuuzi' ya saa?

Kilicho bayana ni kasumba iliyoota mizizi kwenye utawala wa Kikwete wa kudhani Watanzania wanaishi karne ya 18, hawana access na internet kufuatilia masuala mbalimbali yanayoihusu nchi yao, na hata wakifuatilia na kupatwa na hofu basi wakae kimya!

Suala la msingi si Rais kupewa zawadi, iwe ni Rolex au 'souvenir watch' nyingine, bali ni utata unaozunguka kampuni inayotaka kuwekeza katika mradi wa treni za kisasa, na inayomilikiwa na mtu ambaye anazungukwa na habari zenye utata, na ambaye alimzawadia Rais saa (iwe halisi au souvenir' tu) siku chache kabla ya kutangazwa taarifa za uwekezaji huo. Surely huu sio upuuzi bali ni kuihoji serikali yetu ambayo ina historia 'nzuri tu' ya kuingia mikataba ya 'ajabu ajabu' kama ule wa kitapeli wa Richmond.

Nihitimishe makala hii kwa kuwakumbusha wasaidizi wa Rais Kikwete kwamba Watanzania wana haki ya msingi kuuliza maswali kuhusu masuala yanayohusu taifa lao. Kadhalika, wanahabari wana haki ya kuhoji utata unapojitokeza katika mahusiano ya serikali au viongozi wake (hususan Rais) na watu au taasisi mbalimbali.

By the way, ajira ya mwandishi wa taarifa hiyo inategemea kumtetea bosi wake, na hakuna cha ajabu katika kujitokeza kwake kwa ukali kukanusha taarifa hiyo. Lakini kama wana ujasiri, basi wajibu maswali haya tuliyomuuliza mwekezaji huyo badala ya kung'ang'ania 'hoja ya kipuuzi ya "SIO ROLEX" au kutuhadaa kuwa "saa aliyopewa Rais Kikwete ni mali ya Watanzania" (mbona hawakutangaza kuwa Rais amekabidhiwa saa ambayo ni mali ya Watanzania hadi walipoona habari hiyo kwenye gazeti la Raia Mwema?)

Rais Kikwete amekuwa ajitianabaisha kama muumini wa dhana ya 'open goverment' inayopigia mstari haja ya wananchi kufahamu utendaji kazi wa serikali yao. Lakini wakati huohuo, wasaidizi wake huwa wakali kweli pindi wananchi wanapotaka kufuata dhana hiyo na kuhoji 'maswali magumu' kama hayo yanayouzunguka mradi wa treni za kisasa Dar.

Ni muhimu kwa watendaji wa serikali yetu kutambua kwamba Rais wanayemtumikia ni mwajiriwa wa Watanzania, na kila mwajiriwa anatambua haki ya mwajiri wake kuhoji masuala mbalimbali yanayomtatiza. Tanzania ni yetu sote na si ya kikundi kidogo cha miungu-watu wasiotaka kuuliza 'kulikoni?' hata katika masuala yanayohitaji 'akili ndogo' tu ya ku-Google kuhusu mtu au taasisi flani (kama ilivyo kwa ishu ya 'M/S Shumoja a.k.a Shumake Rails.'


m
 

8 Oct 2014

Jana usiku, mwekezaji wa mradi wa treni za kisasa Dar, Bwana Robert Shumake, aliomba kutumiwa maswali kuhusiana na mradi huo. Kufuatia baadhi ya mapendekezo ya wanaharakati wanaofuatilia suala hilo, niliamua kumtumia Bwana Shumake maswali yafuatayo kama inavyoonekana kwenye nyaraka hapo chini.

Iwapo utakuwa na maswali zaidi basi tuwasiliane ili niyaongeze kama nyongeza ya hayo niliyokwishamtumia.

Tusubiri matokeo



Kuna msemo kuwa historia huandikwa na wenye uthubutu. Kadhalika, kuna msemo mwingine kwamba ile kushiriki tu katika shindano ni sehemu ya ushindi. 

Kwa siku kadhaa sasa, kundi la wanaharakati mtandaoni wakitumia mtandao wa kijamii wa Twitter wamekuwa wakiuliza maswali mbalimbali kuhusu mradi wa treni za kisasa jijini Dar ambao Wizara husika imeshasaini mkataba wa awali na kampuni moja ya Kimarekani.

Naomba kukiri kuwa najiskia fahari kuwa miongoni mwa wanaharakati hao ambao wameendelea kuuliza maswali kadhaa yanayotokana na utata unaozunguka mradi huo na mwekezaji husika. Ukifuatilia makala zangu zilizopita utaelewa vizuri nini kilichopelekea harakati hizi.

Pengine ni watu wachache walioshuhudia historia mpya ikiandikwa katika suala la uwekezaji nchi Tanzania, ambapo kwa mara ya kwanza kabisa, mwekezaji mtarajiwa amelazimika 'kuibuka' na kujaribu kujibu maswali kadhaa yanayoelekezwa kwake kuhusu mpango wake wa uwekezaji huko nyumbani. 
Hili si jambo dogo hata chembe kwani laiti moto huo uliaonzishwa na wanaharakati hao ukiweza kusambaa kwa wananchi wengi zaidi, basi kwa hakika tutakuwa tumeingia katika zama mpya ya 'uongozi wa wananchi wenyewe' au wananchi kama viongozi' kwa maana ya nguvu za umma/umoja wao kutumika kufuatilia masuala mbalimbali yanayowahusu, badala ya kusubiri taasisi za serikali au wanasiasa washughulikie.








Historia imeonyesha jinsi gani kero mbalimbali za wananchi zikiyeyuka huko Dodoma licha ya vichwa vya habari magazetini kudai 'Bunge kuwaka muhutu kuhusu ufisadi wa X au Y.' Kimsingi moto pekee huko Bungeni huishia kuwa vijembe na matusi kama sio kuteketea kwa fedha za walipakodi.
Nimeandika hapo juu kuhusu msemo 'ile kushiriki tu ni sehemu ya ushindi.' Japo ni mapema mno kubashiri matokeo ya jithada za wanaharakati hao, ukweli kwamba wameweza kumwibua mwekezaji kutoa ufafanuzi, ni kama ushindi flani wa kihistoria. Lakini ni muhimu kutambua kuwa ninaposema 'ushindi' simaanishi kuwa haya ni mashindano. Hapana. Hizi ni jithada za kutumia uwezo, akili na vipaji kuihudumia jamii ipasavyo. Ukiangalia wasifu wa wanaharakati hao ni watu wanaotoka katika kada mbalimbali kimaisha. Na tofauti na harakati za wanasiasa ambazo mara nyingi husukumwa na matarajio ya kupata kura au kujijenga kisiasa, jitihada za wanaharakati hawa ni kusaka haki kwa niaba ya wananchi wenzao. Ni kile Waingereza wanakiita 'sauti ya wasio na sauti (voice of the voiceless).
Japo hadi wakati ninaandika makala hii hakujapatikana 'majibu ya maana' kutoka kwa mwekezaji huyo, nina matarajio makubwa kwamba harakati hizi zitazaa matunda ya aina flani. Na hata kama matokeo yatakuwa tofauti, basi kwa hakika kinachofanyika sasa kinaweza kuuhamasisha umma kutambua kwamba kwa vile wao ndio wahanga wakubwa wa amsuala mbalimbali yanayofanywa na viongozi kwa niaba yao (na wakati mwingine pasi ridhaa yao), kamwe wasitarajie watu haohao 'wanaochanganya madawa' wajitokeza kutatua matatizo yanapojitokeza. 

Endelea kutembelea blogu hii kufuatilia maendeleo ya harakati hizo kuhusu utata unaokabili mradi huo wa treni za kisasa jijini Dar.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.