1 Apr 2015


Pengine kabla ya kueleza kwanini naunga mkono muswada wa kudhibiti uhalifu wa mtandaoni (The Cyber Crime Bill),ni vema nikaeleza background yangu kidogo ili kutanabaisha sio tu ninavyothamini uhuru wa habari bali pia nilivyonufaika nao.

Nilianza uandishi kwenye vyombo vya habari mwaka 1996,mwaka mmojabaada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.Aliyenishawishi kuingia kwenye fani hiyo ni mwanahabari mkongwe, Albert Memba.Nikiwa mwaka wa pili, na yeye mwaka wa kwanza chuoni hapo, Memba aligundua kuwa 'utani wa busara' niliokuwa nikifanya eneo la 'kijiweni' (nyuma ya ukumbi wa mihadhara ya Sanaa -ATB,mkabala ya Maktaba Kuu ya chuo hicho) ungeweza kunipatia fursa katika gazeti 'lisilo serious.'

Nikafuata ushauri wake na kuanza kuandika 'unajimu wa utani' katika gazeti la 'udaku' la SANIFU lililokuwa linamilikiwa na kampuni ya Business Times, wachapishaji wa gazeti la Majira.Sanifu ni gazeti la kwanza kabisa la udaku Tanzania. Gazeti hilo lilinipa safu (column) niliyoipa jina 'nyota za Ustaadh Bonge.' Nyota hizo licha ya kutumia alama za unajimu kama 'Mshale' (Sagittarius), Ng'e (Scorpio),nk hazikuwa na ukweli wowote zaidi ya burudani. Kwa mfano, ungeweza kukutana na utabiri 'wa kisanii' kama huu: "Wiki hii utakumbwa na nuksi itakayokuletea ulaji mbeleni.Mwanao atagongwa na gari la ubalozi wa Marekani,lakini hatoumia.Ubalozi huo utakufidia kwa kukupatia viza ya kuishi Marekani.Usimzuwie mwanao kucheza barabarani."

Sio siri, watu wengi tu walivutiwa na 'Nyota za Ustaadh Bonge' na hii ilipelekea mie kupewa jina la utani la Ustaadh Bonge kwa muda wote niliokuwa hapo Mlimani (UDSM), na hadi leo, baadhi ya marafiki zangu wananiita Bonge.

Baada ya gazeti la Sanifu 'kufa' nilijiunga na gazeti jingine la udaku la Komesha, na baadaye Kasheshe, magazeti yaliyokuwa yanamilikiwa na kampuni ya IPP. Huko nako niliendeleza safu ya 'Nyota za Ustaadh Bonge.'

Hatimaye niliamua kuachana na magazeti ya udaku na kuhamia kwenye magazeti yenye 'serious news.' Nikafanikiwa kupata safu kwenye gazeti la KULIKONI,na safu hiyo ndio iliyopelekea jina la blogu hii yaani KULIKONI UGHAIBUNI ambalo lilikuwa jina la safu yangu katika gazeti hilo.Lengo la awali la blogu hii niliyoianzisha mwaka 2006 lilikuwa kuwapatia fursa wasomaji wa gazeti la Kulikoni walio nje ya Tanzania kusoma makala zangu kwa vile gazeti hilo halikuwepo mtandaoni.

Ni katika uandishi wa makala katika gazeti la Kulikoni ndipo nilipojitengenezea matatizo makubwa baada ya kuandika makala moja mwishoni mwa mwezi Oktoba 2006 ambapo nilikemea jitihada za aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa, kukwamisha mjadala wa sakata ya Richmond. Makala hiyo ilipelekea Press Secretary wa Lowassa, Said Nguba, kunikaripia vikali hadharani. Mwendelezo wa sakata hilo hatimaye ulipelekea mwisho wa ajira yangu serikalini mwaka 2008.

Baadaye nikapewa safu katika gazeti la MTANZANIA,ambapo safu yangu ilijulikana kama MTANZANIA UGHAIBUNI. Lilipoanzishwa jarida la RAIA MWEMA, nikafanikiwa kupata safu, ambayo niliita RAIA MWEMA UGHAIBUNI, ambayo imedumu kwa miaka kadhaa hadi hivi leo.

Kwahiyo kwa kuangalia background hii utabaini kuwa sio tu nimeutumia vema uhuru wa habari bali pia nimenufaika nao vya kutosha.Nitakuwa mtu wa mwisho kuwa kikwazo cha uhuru huo kwani nami ni mnufaika mkubwa.

Nirejee kwenye mada halisi ya makala hii.Sababu kuu zinazonifanya niunge mkono muswada wa kudhibiti uhalifu wa mtandaoni ni TATU:

Kwanza, KITAALUMA/KITAALAM: Kwa zaidi ya miaka 10 huko nyuma, nilisomea na hatimaye kufanya kazi katika sekta ya usalama. Japo kimsingi kwa sasa si mwajiriwa katika taasisi ya usalama, nina interest kubwa kuhusu stadi na taaluma hiyo, ndani na nje ya Tanzania. Licha ya kujihusisha na usalama kwa maana ya intelijensia, pia nina interest kubwa kuhusu usalama wa mtandaoni hususan uhalifu wa mtandaoni (cybercrime). 

Sambamba na hilo, nimekuwa nikiutumia sana mtandao kwa minajili ya kupashana habari.Licha ya blogu hii, nimekuwa nikiweka mabandiko katika mitandao mingine ya kijamii kama vile Tumblr, Google+, Facebook, Instagram, Pinterest na hata Jamii Forums. Kutokana na uwepo wangu mkubwa mtandaoni, nimelazimika kufuatilia kwa karibu umuhimu wa usalama mtandaoni ikiwa ni pamoja na njia na nyenzo za kujikinga na wahalifu wa mtandaoni, sambamba na kuhabarisha masuala mbalimbali yanayohusiana na suala hilo.

Vilevile, kwa miaka ya hivi karibuni nimepata interest mpya ya software hususan za simu, kwa maana ya maendeleo na matumizi ya apps mbalimbali, pamoja na masuala ya teknolojia kwa ujumla.Katika hilo, nimelazimika pia kufuatilia usalama wa software mbalimbali, za kompyuta na simu.

Kwahiyo, uzoefu wangu mdogo kitaaluma/kitaalam unanituma kuunga mkono umuhimuwa muswada huo hasa kwa vile suala la kompyuta kwa ujumla bado ni geni kwa Watanzania wengi, na hiyo inaota fursa kwa wahalifu wa mtandaoni kufanya hujuma zao kirahisi.Lakini pia hali hiyo inapelekea matumizi yasiyofaa ya teknolojia hiyo ngeni.

Kiintelijensia, kama ilivyosikika hivi karibuni, kuna jitihada za makundi ya kigaidi ya ISIS na Al-Shabaab kufanya hujuma eneo la Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania. Kwa bahati mbaya, mtandao umekuwa nyenzo muhimu ya vikundi vya kigaidi, hususan ISIS, katika harakati zao za kidhalimu. Na hivi karibuni tumesikia matukio mbalimbali yanayoelezwa kuwa ya kigaidi huko nyumbani. Hatuwezi kupuuzia taarifa hizi kwa sababu ugaidi, kama ilivyo kifo au tukio la wizi/ujambazi, hausubiri kualikwa.Unatokea tu. Kwahiyo ni muhimu kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kudhibiti matumizi ya kompyuta kwa minajili ya kufanya uhalifu. Naomba kusisitiza kuwa huu ni mtizamo wa kitaalam (kiinteliujensia) zaidi, na pengine si rahisi sana kueleweka.

Pili, KIJAMII: Ni ukweli usiopingika kuwa Tanzania yetu inaweza kuwa inashika nafasi ya juu kabisa katiika matumizi yasiyofaa ya mtandao.Ninaamini kuwa wengi wetu tumeshuhudia utitiri wa blogu za ngono mtandaoni. Ashakum si matusi, uki-Google 'picha za uchi' utakumbana na mlolongo wa mambo yasiyoendana na mila na desturi zetu.

Kama kuna sehemu inayotoa ushahidi mkubwa wa matumizi mabaya ya mtandao kwa Tanzania yetu basi ni INSTAGRAM.Huko imekuwa 'dunia uwanja wa fujo.' Kama si mzoefu wa matusi basi dakika chache tu katika mtandao huo utakutana na kila aina ya matusi. Wenyewe wameanzisha 'timu' za kusapoti au kupinga watu flani maarufu, na kwa hakika lugha inayotumika huko inachefua. Busara pekee hazitoshi kuwadhibiti watu hawa.Dawa pekee ni kuwa na sheria, sio tu ya kuwakumbusha umuhimu wa kuzingatia maadili bali pia kuwazuwia kuendeleza maovu yao.Ifike mahala, kabla mtu hajabandika picha za uchi ajiulize mara mbili iwapo hatochukuliwa sheria.

Matumizi ya simu za kisasa zenye kamera yamechangia 'kumfanya kila mwenye simu kuwa paparazi,' na katika hili, tumekuwa tukishuhudia picha zisizofaa kabisa mitandaoni.Hivi ni mara ngapi tumekwazwa na picha za maiti kwenye mitandao ya kijamii? Ni mara ngapi tumeitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya uhuni wa kubandika picha zisizofaa mtandaoni? Naam, serikali imesikia kilio chetu kwa kuleta muswada wa kuzwia uhalifu wa mtandaoni ili kupata sheria itakayosaidia angalau kupunguza kadhia hiyo inayokera wengi.

Pia kuna blog zisizo za picha za ngono lakini zinazosababisha utengano mkubwa katika jamii. Ukimtkana mtu kwa mdomo unaweza kusahau na hata huyo aliyetukanwa anaweza kusahau, lakini mtandao wa kompyuta (internet) hausahau kitu. Uki-Google jina langu, moja ya mambo utakayokutana nayo ni 'ugomvi' wangu wa zamani sana na gazeti moja huko Tanzania uliotokana na mimi kulilaumu kwa kutumia picha za uongo kuhalalisha habari waliyochapiusha.Japo ugomvi huo uliisha miaka mingi iliyopita na wahusika ni marafiki zangu kwa sasa, na tumeshasdahau yaliyopita, lakini internet bado inakumbuka.

Sasa blogu zinazoendekeza matusi, kuchafuana, uzushi na vitu kama hivyo sio tu zinawathiri wahanga kwa muda huo wa tukio lakini zinaweka kumbukumbu ya milele mtandaoni...kwa sababu mtandao hausahau kitu. Tuendelee kuvumilia uhuru huu usio na ukomo wa kumchafua mtu yeyote kwa vile tu mlikorofishana? 

Baba wa Taifa aliwahi kutuusia kuwa "Uhuru bila utii ni ujinga" na "uhuru usio na mipaka ni uwendawazimu." Sasa pasipo sheria ya kudhibiti ujinga na uwendawazimu huu unaotokana na dhana fyongo kuwa 'hakuna anayeniona ninapobandika mabaya mtandaoni' tutaendelea kuumizana.

Tatu, sababu BINAFSI: Japo sitaki kuwa mbinafsi kwa maana ya 'kuunga mokono muswada huu kwa sababu mie pia ni mhanga' lakini pia sitaki kuwa mnafiki kwa kukwepa ukweli kwamba nimeshawahi kuwa mhanga wa matumizi mabaya ya uhuru mtandaoni. Mfano mmoja halisi ni kilipotokea kifo cha binti mmoja aliyekuwa miongoni mwa watumiaji mahiri wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Marehemu Betty Ndejembi (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi). Kwa vile kabla ya tukio hilo la kusikitisha nilikuwa nikihamasisha upinziani dhidi ya unyanyasaji mtandaoni, kifo cha marehemu Betty kilinipa changamoto mpya, hasa ikizingatiwa kuwa siku chache kabla ya kukutana na mauti, binti huyo alinyanyaswa vya kutosha huko Twitter. Kwahiyo haikuwa jambo la kushangaza nilipoungana na baadhi ya wanaharakati kutumia hashtag #StopCyberbullying.

Lakini kwa sababu ambazo hadi leo sizielewi, lilijitokeza kundi katika mtandao huo sio tu kupambana na jitihada hizo za kukemea unyanyasaji mtandaoni bali pia kunichafua kwa maana ya jitihada kuonyesha kuwa eti nami ni mnyanyasaji pia huko mtandaoni. Kama kuna kitu kiliniuma na kinaendelea kuniuma hadi leo ni pale mmoja wa watu hao aliponiita MUUAJI. Yaani kuhamasisha mapambano dhidi ya unyanyasaji mtandaoni ni sawa na UUAJI? Ningeweza kumburuza mtu huyo mahakamani kwa kosa la kunidhalilisha (defamation) lakini ukosefu wa sheria halisi inayohusu unyanyasaji mtandaoni (cyberbullying) ungeweza kuniathiri.

Ni rahisi kuzungumzia 'uhuru usio na ukomo' kwa jamii iwapo hujawahi kuwa mhanga wa matumizi ya uhuru huo. Naomba nisieleweke vibaya.Siungi mkono muswada huo kwa vile tu mie ni mhanga huko nyuma, au utakomoa watu flani, lakini pia kuna sababu nyingine muhimu kama nilivyobainisha hapo juu.

MWISHO, japo ninatambua umuhimu wa wananchi kushirikishwa katika utungaji wa sheria zinazowahusu, na pia ninaafikiana na hoja ya kutoharakisha miswada inayohitaji ushirikishwaji wa umma, ninaunga mkono muswada huo kwa sababu UNAHITAJIKA SASA. Na kwa hakika umechelewa sana. Hatuwezi kuendelea kuvumilia matumizi mabaya ya mtandao wa kompyuta kwa kisingizio cha uhuru wa habari. Hatuwezi kuendelea kuvumilia picha za ngono na maiti zikiwekwa hadharani kama mapambo.Jamii yeyote yenye kuzingatia maadili inapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo kama hivyo. Hatuwezi kuwatengenezea mazingira mazuri magaidi kwa kisingizio cha 'umbeya si dhambi.' Madhara ya kutochukua hatua ni makubwa kuliko kuchukua hatua.

Mie ninaweza kuwa mhanga wa sheria hiyo (ikipitishwa) hasa kwa vile ni mtumiaji mkubwa wa mtandao, na pia mkosoaji wa serikali ninapoona inastahili kukosolewa. Ni kweli kwamba sheria hiyo ikipitishwa inaweza kudhuru hata watu wasio na hatia.Lakini katika hili, tatizo si sheria bali CORRUPTION. Tunapozungumzia corruption hatumaanishi tu kuhonga au kuhongwa fedha, bali hata kupindisha sheria kwa maslahi binafsi au kukomoana.Sasa katika hilo, tuna tatizo katika nyingi ya sheria zetu.Ni wangapi wanaporwa viwanja kutokana na corruption katika sheria na sekta ya ardhi? Ni wangapi wapo gerezani muda huu kwa sababu tu walishindwa kuhonga polis au hakimu? Ni vigumu kwa sheria yoyote kuwa na ufanisi katika mfumo corrupt.Ni jukumu letu sote kupambana na corruption ili sheria zenye maslahi kwa jamii zisiishie kuathiri wasio na hatia.

Muswada huu ni kwa maslahi ya kila Mtanzania. Kama wewe si mhalifu wa mtandaoni, sheria hii haitokudhuru. As to itatumika vibaya na serikali, tatizo hapo sio sheria husika bali corruption.Kuna sheria nyingi tu na pengine kali zaidi ya hii tarajiwa, kwa mfano Sheria ya Usalama wa Taifa 1970, Sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa 1996 na Sheria ya Kuzuwia vitendo vya Ugaidi ya mwaka 2002, zinazoweza kutumika vibaya kutokana na corruption. Sina hakika wangapi miongoni mwa wanaopinga muswada wa Cybercrime wameshakuwa wahanga wa 'matumizi mabaya' ya sheria hizo kali kuliko hii tarajiwa.

Hofu yetu dhidi ya matumizi mabaya ya sheria isiwe sababu ya kutokuwa na sheria kabisa. Tusielemee kwenye hofu yetu tu bali tutambue kuwa takriban kila siku kuna victims kadhaa kutokana na ukosefu wa sheria ya kudhibiti uhalifu wa mtandaoni.

ANGALIZO: Huu ni mtizamo wangu binafsi na unaweza kuonekana fyongo kwa mwingine.Twaweza kujadiliana pasipo haja ya 'kupigana.'

MUNGU IBARIKI TANZANIA




Kuanzia leo April Mosi, Watanzania wanaokuja hapa Uingereza hawatahitaji viza kufuatia uamuzi uliotolewa jana na kutangazwa na 'Wizara ya Mambo ya Ndani' ya hapa (Home Office) Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Uingereza kushirikianana nchi kadhaa za jumuiya ya madola, ikiwemo Tanzania, katika maeneo kadhaa ya kiuchumi.

Kwa habari zaidi BONYEZA HAPA

29 Mar 2015



Kwa muda mrefu, baadhi ya watumiaji wa mtandao wa kompyuta (Internet) wamekuwa na wakati mgumu kufuatia kushamiri kwa unyanyasaji mtandaoni, kwa kimombo CYBERBULLYING.

Kwa kiasi kikubwa, tatizo hili linaakisi tabia zetu nje ya mtandao. Mtu aliyezowea kunyanyasa wenzie mtaani, akiingia mtandaoni anaweza kuendeleza tabia hiyo kirahisi. Kadri mtandao unavyozidi kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku ,ndivyo unavyoakisi maisha yetu 'ya kawaida' nje ya mtandao. 

Kwa upande mwingine, mtandao unatoa fursa ya watu wenye tabia tofauti kukutana. Ndio maana si ajabu kukuta mtu mmoja akiweka bandiko kuhusu dini, mwingine akaweka bandiko kuhusu matusi.

Licha ya tabia, mtandao pia huwakutanisha watu wenye sifa tofauti: wapole na wakorofi, wapenda amani na wagomvi, wenye elimu na mbumbumbu, wenye aibu na wasio na mishipa ya aibu, nk. 

Kadhalika, mtandao unatoa fursa mbalimbali, nzuri na mbaya. Kwa mfano, mtandao unatuwezesha kuwa karibu na viongozi wa nyanja mbalimbali, kutoka mawaziri hadi viongozi wa taasisi binafsi.Uzuri wa fursa hiyo ni pamoja na kurahisisha mawasiliano baina ya watu wanaotoka 'madaraja' tofauti ya kijamii. Kadhalika, fursa hiyo inatuwezesha kujifunza kutoka kwao, sambamba na kufuatilia masuala mbalimbali ambayo kutokana na nafasi zao yanagusa maisha yetu binafsi au ya jamii kwa ujumla.

Fursa hiyo pia inatuwezesha kuwa karibu na watu mbalimbali, muhimu na wa kawaida. Katika mazingira ya kawaida, ni vigumu kufahamiana na Waziri, kwa mfano, labda kuwe na undugu, kufahamiana au mahusiano kikazi.

Hata hivyo, mtandao pia unatoa fursa 'mbaya.' Binadamu tupo tofauti, kuna wenzetu ambao wakiiona fursa wanaitumia kwa manufaa, lakini kuna wengine sio tu hawataki kujifunza 'mazuri' ya wenzao (ambayo wao hawana) pia hujenga chuki na jitihada za kuwachafua au kuwadhalilisha wenzao wenye 'mazuri.' Kwa mfano, unaweza kukutana na mtu ambaye hakubahatika kupata elimu ya kutosha, au hakusoma kabisa. Anapokutana na mwenye elimu kiasi au ya juu, badala ya kutumia fursa hiyo kama 'darasa nje ya shule' anaanzisha chuki na uhasama usio na manufaa.

Kama dunia ilivyo uwanja wa fujo, ndivyo ilivyo kwa mtandaoni. Kuna mazuri na mabaya. Kuna baadhi yetu ambao tumenufaika sana kwa uwepo wetu mtandaoni, kwa maana ya kutengeneza urafiki na watu muhimu, lakini pia kuna nyakati tumejikuta tukikutana na 'maadui.'

Ofkoz, mtandano sio sehemu ya kubadilisha mawazo, kujifunza au kuuliza maswali tu bali pia ni sehemu ya burudani. Utani ni ruksa lakini utani wenyewe usizidi kiwango. Na kanuni ya mtaani kuwa usimtanie mtu asiyekutania, ina-apply mtandaoni pia.

Kwa bahati mbaya kuna wenzetu ambao hulazimisha utani.Wengine huenda mbali zaidi kwa kulazimisha kumjua mtu zaidi ya anavyojijua yeye mwenyewe.

Kwa bahati nzuri, hatimaye serikali imesikia kilio dhidi ya unyanyasaji wa mtandaoni na Jumanne ijayo inatarajia kuwasilisha muswada kuhusu uhalifu wa mtandaoni ambao pamoja na mambo mengine unaharamisha unyanyasaji wa mtandaoni (cyberbullying) 

Katika muswada huo unajulikana kwa kimombo kama The Cyebrcrimes Act, 2015, ibara ya 23 inaharamisha unyanyasaji mtandaoni (cyberbullying) na kutaja adhabu husika. 

Muswada unafafanua maana ya cyberbullying, kwamba "mtu hataruhusiwa kuanzisha au kutuma mawasiliano ya kielektroniki kwa kutumia kompyuta kwa mtu mwingine kwa malengo ya 'kumsukuma kwa nguvu' (coerce), kumtisha, kumyanyasa au kumsababishia msongo wa mawazo, na mtu atakayekiuka kipengele hocho atakuwa anafanya kosa, na adhabu yake ni sio chini ya shilingi milioni tatu au kifungo cha sio chini ya mwaka mmoja au adhabu zote pamoja."  

Muswada kamili ni huu hapa chini (kwa bahati mbaya au makusudi, watawala wetu hawakuona umuhimu wa kuupatia tafsiri ya Kiswahili)



Wakati muswada huu ni habari njema kwa wahanga wa unyanyaswaji mtandaoni, unatarajiwa pia angalau kupunguza kushamiri kwa matusi na picha zisizofaa mtandaoni. Sio siri kwamba baadhi ya mitandao ya kijamii, hususan Instagram, imegeuka uwanja wa matusi.

Kibaya zaidi, umahiri wa matusi umegeuka moja ya vyanzo vya umaarufu mtandaoni. Kama nilivyobainisha hapo juu,mtandao unatoa fursa 'mbaya' kwa wenzetu  wasio  na cha kuelimisha, kujadili au hata kujivunia hadharani, na matokeo yake ni kuwabughudhi watu wengine au kubandika picha zisizofaa kama mbinu ya kusaka sifa za kipuuzi.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbushana kuwa Tanzania yetu haina uhaba wa sheria.Tatizo kubwa ni katika kuziheshimu na kuzitekeleza. Twaweza kuwa na sheria kali dhidi ya uhalifu wa mtandaoni lakini utekelezaji ukiwa hafifu basi sheria hizo zitabaki maandiko tu vitabuni.

Kadhalika, ni muhimu kutahadharisha kwamba sheria hii ya uhalifu wa mtandaoni isitumiwe vibaya na serikali kuwanyima wananchi uhuru wa mawasiliano, au kibaya zaidi, kuitumia kwa minajili ya kuficha maovu na kuwalinda waovu. Sitarajii kuona sheria hii ikitumika iwapo chombo cha habari kitaibua utovu wa maadili wa kiongozi, kwa mfano.

Mwisho, ni matarajio yangu kuwa vitendo vya uhalifu wa mtandaoni, ikiwa ni pamoja na cyberbullying, vitapungua kufuatia sheria hii, iwapo itapitishwa na bunge. Angalau sasa, cyberbullies watafikiria mara mbili kabla ya kumwaga sumu zao kuwanyanyasa watu wasio na hatia.

26 Mar 2015

The United States said on Wednesday it had information of “possible terrorist threats” to locations frequented by Westerners in Uganda’s capital, Kampala, and warned that an attack could take place soon.
The U.S. Embassy in Kampala issued the warning in a statement posted on its website.
"The U.S Embassy has received information of possible terrorist threats to locations where Westerners, including U.S. citizens, congregate in Kampala, and that an attack may take place soon," it said.
"Out of an abundance of caution, the U.S. mission has canceled some non-essential events scheduled at local hotels in the coming days," it added.
Uganda is a close security ally of the United States in East Africa. The embassy issued similar alerts last year about possible attacks in Uganda.
The embassy cautioned that foreigners staying in or visiting hotels should expect increased security sweeps.
Uganda is one of the countries that contributes forces to an African Union peacekeeping mission battling the Islamist militant group al Shabaab in Somalia.
Al Shabaab, which is aligned with al Qaeda, attacked a shopping mall in Nairobi, capital of neighboring Kenya, in 2013. In 2010, it bombed sports bars in Uganda where people were watching soccer’s World Cup on television. Dozens were killed in both attacks.
SOURCE: Matthew Aid



Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Mohamed Thabit Kombo akimpongeza Mwenyekiti wa Mfuko huo,Doris Mollel kwa kuona jukumu la kusaidia jamii katika kuokoa maisha ya watoto njiti.






Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Mohamed Thabit Kombo akizungumza wakati wa hafla ya kutambulisha Mfuko wa Doris Mollel,iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency,jijini Dar es salaam.




Mwenyekiti wa Mfuko huo,Doris Mollel akizungumza na wageni waalikwa waliofika kwenye hafla ya kutambulisha Mfuko wa Doris Mollel,uliofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency,jijini Dar es salaam.



Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Mohamed Thabit Kombo (pili kushoto),Balozi Mwanaid Maajar (kulia),Mwenyekiti wa Mfuko huo,Doris Mollel (katikati) pamoja na wadau wengine wa Mfuko huo wakishiriki kwa pamoja kukata keki,kuashiria uzinduzi rasmi wa Mfuko wa Doris Mollel,uliofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency,jijini Dar es salaam.



Sehemu ya Wageni waalikwa katika hafla ya kutambulisha Mfuko wa Doris Mollel,iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency,jijini Dar es salaam.



Picha ya pamoja na baadhi ya wadau waliohudhulia hafla hiyo.


Kutoka kulia ni HEENA ambaye ni mmoja kati ya washirika wakubwa wa mfuko huo, wakiwa wameshikana mikono na muanzilishi wa mfuko huo miss DORIS MOLLEL pamoja meneja wa mfuko huo RAHAB MBISE mara baada ya kuzindualiwa kwa mfuko huo jijini Dar es samaam


Meneja wa mfuko huo RAHAB MBISE akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jjini Dar es salaam




Mrembo wa singida aliyeshika nafasi ya tatu katika mashindano ya miss tanzania mwaka wa 2014 DORIS MOLEL leo amezindua rasmi rasmi DORIS MOLEL foundation ambayo ni mahususi kwa ajili ya kusaidia watoto ambao wamekuwa wanazaliwa wakiwa bado hawajatimia NJITI ambapo amewataka watu mbalimbali kujitokeza kumpa saport katika shighuli hiyo.

Uzinduzi huo ambao umefanyika leo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na wadau wanaohusika katika kuwasaidia watoto hao. wengi wamepongeza jitihada zinazoonyeshwa na mrembo huyo kwani watoto wanaozaliwa wakiwa na tatizo hilo wamekuwa wakusahaulika sana nchini tanzania jambo ambalo limetajwa kuwaadhiri watoto hao pamoja na wazazi wao.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mrembo DORIS ambaye ni mmoja  kati ya watu walioathiriwa na tatizo hilo (alizaliwa akiwa njiti) alisema kuwa ameamua kuwasaidia watoto na wazazi  wenye matatizo hayo baada ya yeye kupitia katika kipindi kama hicho ambapo alisema kunahitajika msaada mkubwa kutoka kwa watu wa mbalimbali.

Mimi nilizaliwa nikiwa njiti nilikuwa sijafikisha uzito halali wa kuzaliwa lakini nilizaliwa na mama akanisaidia hadi leo hii mnaniona hapa ni miss Tanzania na ni mtu nayekubalika na jamii,hivyo nimeona kuna haja ya kuwasaidia watoto kama mimi ambao wamezaliwa hivyo ili waweze kukua na afya njema na baadaye kutimiza malengo ya maisha yao,”alisema mrembo huyo.

Alisema kuwa baada ya kuchaguliwa kuwa mrembo namba tatu wa Tanzania alifikiria kitu cha kufanya ili arudishe shukrani kwa Watanzania na baada ya kutembea katika maeneo mbalimbali aligundua kuwa watoto wanaokumbwa na matatizo hayo bado wamekuwa hawapewi kipaumbele katika kusaidiwa jambo ambalo limemsukuma yeye kuanza kufanya mchakato huo.

Aidha alisema kuwa ipo haja ya serikali pamoja na wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo kwa lengo la kuokoa kizazi kikubwa ambacho kinazaliwa na matatizo kama hayo ambapo kwa takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto laki mbili wanazaliwa wakiwa njiti kwa mwaka nchini Tanzania.

Uzinduzi huo uliambatana na  uchangiaji wa mfuko huo kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao, ambapo watu mbalimbali wachangia na kuwaomba Watanzania wengine kuendelea kumsaidia mrembo huyo kuhakikisha kuwa anatimiza lengo lake.

Baadhi ya watu waliojitokeza kumpa nguvu katika shughuli hiyo leo ni pamoja na muandaaji wa mashindani ya miss tanzania ambapo ndiko mrembo huyo alikotokea bwana hashimu lundenga, Mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) Mzee Iddi Simba, Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mohamed Thabit Kombo pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Bara na Viusiwani




25 Mar 2015


Wiki mbili zilizopita niliandika makala iliyoonya tabia iliyoanza kuzoeleka kwa baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM kufanya mzaha kuhusu ugaidi. Kwa muda mrefu sasa, viongozi wa chama hicho hususan Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba wamekuwa wakiihusisha Chadema na ugaidi. Lakini tabia hiyo haikuanzia kwa Chadema pekee kwani huko nyumaCUF nayo ilikumbwa na tuhuma kama hizo kutoka kwa CCM.

Katika makala hiyo ambapo nileleza kwa kirefu kiasi kuhusu hatari inayoikabili dunia hivi sasa kutoka kwa vikundi vinavyoongoza kwa ugaidi kwa muda huu, yaani ISIS, Al-Qaeda, Boko Haram na Al-Shabaab, nilitahadharisha kwamba tabia ya CCM kuufanyia mzaha ugaidi, kwa maana ya kuzusha tu 'Chadema ni magaidi au CUF ni magaidi', inaweza kutugharimu huko mbeleni. Nilibainisha kuwa mzaha huo unaweza kuwarahisishia magaidi halisi dhima ya kushambulia nchi yetu, kwani 'tayari tuna magaidi wa ndani- kwa maana ya tuhuma za CCM dhidi ya Chadema na CUF.

Vilevile nilitanabaisha kwamba kuufanyia mzaha ugaidi kunaufanya uzoeleke, uonekane ni kama jambo la kawaida tu ambalo halikauki midomoni mwa akina Nape na Mwigulu.Lakini pengine baya zaidi ni vyombo vyetu vya dola kuwekeza nguvu kubwa kudhibiti 'magaidi hewa' hali inayoweza kuwapa upenyo magaidi halisi.

Kwa bahati mbaya, tahadhari niliyoitoa kwenye makala hiyo inelekea kubeba uzito, baada ya kupatikana taarifa kwamba kikundi hatari kabisa cha magaidi cha ISIS kina mpango wa kujienga na hatimaye kufanya mashambulizi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa za kituo cha televisheni cha Aljaazera, mawasiliano ya hivi karibuni ya kikundi hicho cha kigaidi yanaonyesha kuwa kinajaribu kujijenga Afrika Mashariki, eneo ambalo limekuwa likisumbuliwa na magaidi wa Al-Shabaab na Al-Qaeda kwa vipindi tofauti.

Hivi karibuni, kikundi cha kigaidi cha Boko Haram cha Nigeria kimetoa ahadi ya utiifu kwa ISIS, hatua iiliyotafsiriwa na wachunguzi wa masuala ya ugaidi kuwa inaweza kuongeza nguvu za ISIS katika maeneo mbalimbali ya bara la Afrika.

Hata hivyo, kitu ambacho hakikufahamika kwa wengi ni kwamba tukio hilo la Boko Haram kuonyesha utii wa ISIS lilitanguliwa wiki chache kabla ya ujumbe uliotumwa kwa kiongozi wa Al-Shabaab , Abu Ubaidah, kumwomba afanye kama walivyofanya Boko Haram (kutangaza utii kwa ISIS)

Ujumbe huo uliwasilishwa na  Hamil al-Bushra, jina linaloaminika kutumiwa na vyanzo viwili vya habari vinavyohusishwa na ISIS.

Katika ujumbe huo, Bushra aliwapongeza Al-Shabaab na kuwahamasisha wafanya mashambulizi Kenya, Ethiopia na TANZANIA.

Soma habari kamili HAPA

12 Mar 2015

SIKU chache zilizopita, kikundi hatari cha kigaidi cha Boko Haram cha nchini Nigeria kilitangaza utiifu wake kwa kikundi kingine hatari kabisa cha kigaidi cha ISIS.
Hizi si habari njema hata kidogo kwani ushirikiano wowote kati ya makundi ya kigaidi, hususan, yaliyopo maeneo tofauti, unamaanisha kusambaa kwa vitendo vya kigaidi.
Ujumbe ulitolewa na Boko Haram, ambao hata hivyo bado haujathibitishwa (ni nadra kuthibitisha ujumbe wao ), uliwekwa kwenye akaunti ya kikundi hicho katika mtandao wa kijamii wa twitter, ambayo inaaminika kuwa ya kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau.
Kikundi hicho kilianza mashambulizi ya kigaidi mwaka 2009 maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria, lengo kuu likiwa kuanzisha utawala unaoendeshwa kwa sheria za Kiislamu. Tayari kikundi hicho kimeshasababisha mauaji ya raia kadhaa, na hivi karibuni kimekuwa kikijaribu kusambaza unyama wake kwa nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.
Awali, ilifikiriwa kwamba Boko Haram ina mahusiano na kikundi kingine kikubwa na hatari cha Al-Qaeda, ambacho kilikuwa maarufu sana kabla ya kuibuka kwa ISIS.
Kwa upande wake, ISIS kimekuwa kikifanya unyama ambao pengine haujawahi kuonekana katika historia ya vikundi vya kigaidi, licha ya mashambulizi ya kujitoa mhanga, kikundi hicho kimeshawachinja mateka wake kadhaa na kuweka unyama huo hadharani.

Hivi karibuni, ilifahamika kuwa gaidi anayedaiwa kuwa ndiye ‘mchinjaji’ mkuu, anayejulikana kama Jihadi John, aliwahi kufika Tanzania na kuzuiliwa kuingia, kabla ya kuelekea Syria, ambako pamoja na Iraki, ni maeneo yanayosumbuliwa na kikundi hicho.
Lengo kuu la ISIS ni kuanzisha himaya (Caliphate) ya Kiislam, na kiongozi wake, Abu Bakr al-Baghdad, amejitangaza kuwa ndiye mkuu wa himaya hiyo ambayo wanalenga kuisambaza dunia nzima.

Kinachoifanya ISIS kuonekana hatari zaidi, licha ya unyama wake, ni uwezo wake mkubwa wa kifedha, sambamba na ufanisi wa kimuundo kana kwamba ni dola kamili yenye serikali.
Tangazo la Boko Haram kuahidi utiifu kwa ISIS si la kushangaza sana, japo wafuatiliaji wa masuala ya ugaidi walishangazwa kwanini hali hiyo haikutokea mapema zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa mbinu na malengo ya vikundi hivyo yanashabihiana.

Huu ni mtihani mkubwa kwa wana-intelijensia duniani hasa ikizingatiwa kuwa ISIS, kama ilivyokuwa Al-Qaida, si tu imefanikiwa kuwavutia ‘wapiganaji’ kutoka sehemu mbalimbali duniani, bali pia ina dhamira kubwa ya kusambaza unyama wake takriban kila kona ya dunia.
Kwa tafsiri ya haraka, Boko Haram wanaweza kunufaika na ushirikiano wake na ISIS na pengine kufanikiwa kusambaza kampeni yao ya kigaidi katika maeneo mengine ya Afrika.
Lengo la makala hii sio kujadili vikundi hivyo vya kigaidi. Kilichonishawishi kuandika makala hii yenye utangulizi unaohusu vikundi hivyo vya ugaidi ni tamko la hivi karibuni la Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye kuwa kikosi cha ulinzi cha Red Brigade cha Chadema ni kundi la kigaidi.

Lakini Nape si mwanasiasa wa kwanza wa CCM kutoa tamko zito kama hilo. Mwaka juzi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Mwigulu Nchemba, aliandika waraka mrefu katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums kuizungumzia Red Brigade ya Chadema, ambapo pamoja na mambo mengine alidai ina malengo ya “uhaini, ni ugaidi, ni maandalizi ya kupindua nchi au kuvuruga kabisa amani tuliyonayo.”
Kwa upande wake, Nape alidai makundi ya vijana wa ulinzi vya chama hicho (Red Brigade) yameandaliwa kwa ajili ya kuingia msituni kwa shughuli za ugaidi. Alitoa kauli hiyo wilayani Mpwapwa kwenye ziara ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, mkoani Dodoma.
“Chadema wanaandaa vijana kupitia Red Brigade ili kuingia msituni na kuchukua madaraka ya nchi kwa mabavu. Wanafanya hivyo kwa sababu wanajua hawawezi kuchaguliwa kwa njia ya kura wakati wa uchaguzi mkuu,” alidai mwanasiasa huyu muumini wa siasa za uhasama, na kuongeza kuwa, “Taarifa tulinazo ni kwamba Red Brigade ni vikosi vinavyoandaliwa kwa ajili ya vitendo vya ugaidi na shughuli nyingine za ovyo. Taarifa ni kwamba hili ni kundi la kigaidi, wataanzishaje kundi la usalama wakati tunavyo vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi yetu?”
Huu ni uhuni wa kisiasa. Na baya zaidi, ni mwendelezo wa kasumba ya muda mrefu kwa Nape na Mwigulu kuufanyia mzaha ugaidi kwa kuvihusisha vyama vya upinzani hususan Chadema.
Lakini kabla ya kuwajadili wanasiasa hawa wawili ‘wanaaombea uwepo wa ugaidi nchini mwetu,’ ni vema kutambua kuwa kamwe kauli zao hazijawahi kupingwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete au kiongozi mwingine yeyote yule wa chama hicho tawala. Wakati Julai mwaka, Rais Kikwete alisema si sahihi kwa vyama vya siasa kuanzisha vikundi vya mgambo kwani vitendo hivyo ni viashiria vya uvunjifu wa amani nchini, chama anachokiongoza (CCM) pia kina kikundi cha Green Guard, kama ilivyo Blue Guard kwa CUF.
Kwa maana hiyo, kwa Nape na Mwigulu kukemea Red Brigade ya Chadema ilhali CCM nayo ina Green Guard si tu ni unafiki bali pia wanaweza kuwa wanatumika kama ‘kipaza sauti’ cha Rais Kikwete na CCM kwa ujumla.

Lakini sote tunafahamu siasa zetu za upinzani zilivyo ambapo ‘kurushiana madongo’ ni sehemu ya kawaida. Hata hivyo, jaribio lolote la kuhusisha ugaidi na ‘madongo’ ya kawaida litatugharimu kama taifa. Ugaidi si jambo la kufanyia mzaha hata kidogo.
Moja ya madhara ya kuufanya ugaidi kama jambo la kawaida ni kuwarahisishia magaidi halisi fursa ya kutudhuru. Hivi, kwa mfano, magaidi tulio jirani nao zaidi kuliko Boko Haram, ISIS na Al-Qaeda, yaani Al-Shabaab wa Somalia, wakitaka kufanya ugaidi nchini mwetu (Mungu aepushie) hawawezi kutumia upenyo wa ‘Red Brigade wa Chadema ni magaidi’ kuficha dhamira yao ovu?
Vyombo vyetu vya usalama vinaweza kulazimika kuwekeza nguvu kubwa kuwadhibiti ‘magaidi wa kufikirika’ wa Red Brigade, na hiyo yaweza kutoa fursa kwa magaidi halisi kufanya unyama wao.
Tayari tumeshaona jinsi vyombo vya usalama vinavyotumia nguvu kubwa kulinda maslahi ya CCM, ikiwa ni pamoja na kuwakandamiza wapinzani wake, huku ufisadi, ujangili, biashara ya madawa ya kulevya, na sasa mauaji ya albino vikistawi kana kwamba ni shughuli halali.
Kichekesho, majuzi wakati Rais Kikwete anazindua studio za kituo cha Televisheni cha Azam jijini Dar alitoa karipio kali kwa vyombo vya habari akisema serikali haitavumilia vyombo vya habari visivyosimamia uadilifu, weledi pamoja na kutumika katika kuchochea ghasia. Kwanini ukali huo wa Rais wetu uwe kwa vyombo vya habari tu ilhali wahuni wa kisiasa wakiruhusiwa kufanyia mzaha tishio la ugaidi?

Nimalizie makala hii kwa kuwahamasisha Watanzania wenzangu kuwapuuza wanasiasa mufilisi wanaojaribu si tu kujenga chuki miongoni mwetu bali pia kufanyia mzaha tishio la ugaidi.
Sote ni mashuhuda wa unyama unaofanywa na Boko Haram, ISIS, Al-Qaeda, Al-Shabaab na makundi mengine ya kigaidi, na ninaamini hakuna mtu anayeweza kudiriki kutamani uharamia huo utokee katika nchi yetu. Siasa za chuki za kipuuzi ni hatari sana kwa mustakabali wa Tanzania yetu.
Inahitaji kauli chache tu za kupandikiza mbegu za chuki, lakini ni vigumu mno kung’oa chuki pindi mbegu hizo zikifanikiwa kuotesha chuki.

10 Mar 2015

Tafsiri: Mimi sishangazwi hata kidogo. Viongozi wa Kanisa na wanasiasa wakubwa wanashiriki katika mila hii ya kishetani. Kiongozi mmoja mkubwa wa kanisa mwenye usharika mkubwa jijini Dar es Salaam, anayemiliki benki, alikamatwa akiwa na albino amefungwa nyuma ya gari lake. Alitoroka eneo la tukio na kesi yake haikuripotiwa kwa sababu alitoa rushwa. Yeye pia ni muuza madawa ya kulevya mkubwa na mtakasaji fedha haramu. Kwahiyo tunatarajiwa Umoja wa Mataifa utaanza kuwafungulia watu hawa mashtaka ya ukatitili dhidi binadamu ili Watanzania walichukulie suala hili kwa makini.

Kwa umoja wetu na upendo wetu kwa ndugu zetu albino, tuunganishe kumsaka mwanaharamu huyu anayejiita mchungaji ilhali anafanya matendo ya kishetani. 

Mie ni muumini katika nguvu ya umma. Na nguvu ya umma si kuandamana tu bali hata katika kufichua maovu katika jamii. Ni na imani ya asilimia 100 kuwa kuna mtu au watu flani, sehemu flani wanamfahamu 'mchungaji' huyu. Kadhalika ninaamini kuna mtu au watu flani wanamfahamu mwanasiasa au mfanyabiashara au mganga au muuaji anayejihusisha na mauaji ya albino. Sasa pengine hofu ya kumripoti inachangiwa na kuchelea matokeo hasa ikizingatiwa kuwa polisi wetu hawaaminiki.

Tutumie nguvu ya umma. Kama una taarifa ya uhakika (ikiwa na uthibitisho itakuwa vema zaidi) basi ninaomba uwasiliane nami kwa barua-pepe CHAHALI at ABOUT dot ME au nitumie meseji Facebook https://www.facebook.com/evarist.chahali.1 au nenda kwenye tovuti hii http://swarmsecret.com/ kisha tweet kwa @chahali nami sio tu nitaweka hadharani suala hilo bali nitatumikia kila tone la nguvu zangu kuhakikisha mtu huyo anachukuliwa hatua za kisheria, ndani au nje ya Tanzania yetu.

Vinginevyo, ukifanikiwa kupata taarifa za mchungaji huyo au mtu yeyote anayejihusisha na unyama huo, 

Kwa pamoja tunaweza katika hili

SHUKRANI: Asante Ndugu Alfred Kiwuyo kwa kutufahamisha kuhusu habari husika

5 Mar 2015

"NI wajinga wa kisiasa pekee wanaoweza kudharau mchango wa Marehemu Komba katika siasa za Tanzania. Nimeona kuna watu wanabwabwaja sana!" Hii ni kauli ya Profesa Kitila Mkumbo aliyoitoa Jumapili iliyopita, katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
MSOMI huyo ambaye pia ni mwanasiasa alitamka hivyo kufuatia mpasuko mkubwa uliojitokeza (angalau katika mtandao wa intaneti) kufuatia taarifa za kifo cha mwanasiasa maarufu na Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM) Kapteni John Komba, kilichotokea Jumamosi jijini Dar es Salaam.
Japo inafahamika kwa idadi ya Watanzania wanaitumia mtandao wa intaneti ni ndogo sana kulinganisha na idadi ya Watanzania wote, kwa kiasi fulani mada zinazotawala mtandaoni huweza kuakisi hali halisi iliyopo 'mtaani.' Ni kwa mantiki hiyo, ninashawishika kuhisi kuwa mpasuko uliojitokeza mtandaoni kufutia kifo cha Kapteni Komba waweza pia upo mitaani pia.
Mpasuko huo ulichukua sura ya makundi mawili, moja likionekana kufurahia kifo cha mwanasiasa huyo huku likifanya marejeo ya kauli zake mbalimbali hasa ile ya wakati wa Bunge Maalum la Katiba kuwa angeingia msituni iwapo pendekezo la muundo wa Muungano wa serikali tatu lingepitishwa.
Kundi jingine lilikuwa la waombolezaji, wananchi walioguswa na kifo hicho, huku wakilaani vikali 'jaribio lolote la kumlaumu marehemu.' Katika kundi hili, kulijitokeza 'mapadri na mashehe' walionukuu Biblia Takatifu na Kuran Tukufu kukumbushia umuhimu wa kuenzi marehemu na kuheshimu kifo.
Lakini ndani ya makundi hayo kulijitokeza 'waliouma na kupuliza,' yaani kwa upande mmoja wakionyesha jinsi walivyokwazwa na baadhi ya kauli za marehemu Komba hususani zilizokua zinachochea chuki na uhasama wa kisiasa na kijamii, lakini upande mwingine wakidai kuwa 'si vizuri kumsema vibaya marehemu.'
Kama nilivyotanabaisha hapo juu, sina hakika hali ikoje huko mitaani lakini yayumkunika kuhisi kuwa idadi ya waombolezaji ni kubwa kuliko ya 'wanaomwandama marehemu.' Idadi kubwa ya waombolezaji yaweza kusababishwa zaidi na 'uoga wetu wa kawaida kwa kifo' kuliko kuguswa na kifo husika.
Japo sote twatambua kwa uhai wetu una kikomo kwa njia ya kifo, na japo hatuna la kufanya kubadili ukweli huo mchungu, twaendelea kukiogopa kifo huku vifo vya watu wa karibu au tunaowafahamu vikitukumbusha tena na tena kuwa kifo kipo.
Kwa namna flani ya kusikitisha, kuna nyakati vifo huwa nafasi ya kushuhudia unafiki wa baadhi yetu kama wanadamu. Ni mara ngapi tumeshuhudia, kwa mfano, baadhi ya vijana wakiteketeza uhai wao kwa matumizi ya madawa ya kulevya, lakini jamii ikiwatelekeza, na kisha kumwaga lundo la rambirambi pale wanapofariki? Sawa, rambirambi ni ishara ya kuguswa na kifo, lakini ina faida gani hasa pale upendo ungeweza kuepusha kifo hicho?
Kwa upana zaidi, kuna haja gani kumpenda mtu baada ya kufariki ilhali alipokuwa hai alichukiwa? Upendo huo wa ghafla ni nini zaidi ya unafiki kwani wakati mwafaka tunapohitaji upendo ni tunapokuwa hai.
Kilichojitokeza baada ya kifo cha marehemu Kapteni Komba, ambapo baadhi ya wenzetu wameonekana 'kufurahia,' ni mwendelezo wa chuki katika Tanzania yetu, huku baadhi ya wanasiasa wa CCM wakiwa ndio wahusika wakuu.
Sawa, sio vema kuzungumzia 'mabaya' ya marehemu Komba, kwa mfano, lakini kwa bahati mbaya au makusudi, ukiweka kando umahiri wake katika nyimbo za maombolezo ya kifo cha Baba wa Taifa, marehemu Julius Nyerere, kumbukumbu muhimu ya hivi karibuni ni lugha kali aliyoitumia wakati wa Bunge Maalum la Katiba.
Yeye, pamoja na 'waeneza chuki' wengine walifikia hatua inayoweza kutafsiriwa kama kumtakia kifo Jaji Joseph Warioba kwa vile tu Tume aliyoongoza kukusanya maoni ya Katiba ilipendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Lakini ishara kuwa chuki inazidi kutawala katika Tanzania yetu zilianza kujitokeza kwa wazi zaidi pale Rais Jakaya Kikwete alipolazwa nchini Marekani kwa matibabu ya tezi dume. Wakati idadi kubwa tu ya Watanzania ilijitokeza kumtakia Rais wetu uponyaji wa haraka, kulikuwa na kundi dogo ambalo halikuficha hisia zao, kiasi cha baadhi yao kutaka Rais asirudi akiwa hai. Kwa lugha nyingine, wenzetu hawa walikuwa wanamwombea kifo Rais wao.
Kwa bahati mbaya au makusudi, hakuna jitihada zilizofanyika japo kuanzisha mjadala tu kuhusu ustawi wa chuki katika nchi yetu. Na matokeo yake, leo hii twashuhudia baadhi ya wenzetu wanaoonekana kufurahia kifo cha mwanasiasa wetu mahiri.
Ni rahisi kuitazama chuki hii kama ujinga, kama alivyotanabaisha Profesa Kitila, lakini binafsi ninaamini hili ni swali gumu lisilostahili majibu rahisi. Kwa mtizamo wangu, moja ya sababu za chuki hiyo inaweza kuwa ni pengo la kitabaka kati ya watawala na watawaliwa, sambamba na pengo linalozidi kukua kati ya wenye nacho na wasio nacho.
Lakini chuki hiyo inachangiwa pia na jeuri ya watawala wetu, kusahau kuwa 'kesho kuna kifo,' kuropoka kila baya hasa kwa wapinzani wao kisiasa, na kuwadharau wananchi ambao kimsingi ndio waajiri wa watawala hao.
Kauli za baadhi ya wanasiasa mahiri kwa 'kusema ovyo' kama ile ya 'vijisenti' ya Mbunge wa Bariadi (CCM) Andrew Chenge, hii ya majuzi ya 'shilingi milioni 10 za kununulia mboga (labda ni tembo mzima)' ya Profesa Anna Tibaijuka, ile ya Profesa Muhongo kuwa 'Watanzania hawawezi kuendesha biashara ya gesi na mafuta bali wanamudu biashara ya matunda tu,' na nyinginezo nyingi, zinachangia kushamiri kwa hasira za baadhi ya wananchi kwa baadhi ya viongozi wao.
Tuna wanasiasa kama LivingstonLusinde, maarufu kama 'kibajaji’, Nape Nnauye, William Lukuvi, Stephen Wassira na Mwigulu Nchemba (japo huyu amekuwa na nafuu sasa), ambao wakizungumzia vyama vya upinzani wanaweza kumwaminisha msikilizaji kuwa wapinzani ni viumbe hatari kuliko magaidi wa Al-Shabaab, Boko Haram au ISIS.
Wanajitahidi sana kupamba mbegu za chuki, na kwa hakika wamefanikiwa kwa kiasi fulani. Lakini uongozi wa juu wa chama hicho tawala haujawahi kukemea kauli hizo za chuki, yayumkinika kuhisi kuwa ujenzi wa chuki ni miongozi wa sera zisizo rasmi kwa chama hicho, kama ilivyo ufisadi.
Ni muhimu kwa watawala wetu kujifunza kitu katika chuki hii inayolitafuna taifa letu. Kinachotufanya tuendelee kumlilia Baba ya Taifa hadi leo ni matendo yake ya kuigwa mfano wakati wa uhai wake.
Yawezekana kama binadamu mwingine, Mwalimu aliwahi kuwakwaza baadhi ya Watanzania, lakini 'hukumu ya jumla' kwa matendo yake wakati wa uhai wake ni kwamba aliweka mbele maslahi ya taifa kuliko maslahi yake binafsi. Tunamkumbuka na kumlilia kwa sababu tunaona ombwe kubwa lililotokana na kifo chake.
Sasa, japo 'marehemu hasemwi vibaya,' sidhani kama kuna atakayeshangaa sana kuona kifo cha mwanasiasa mahiri kwa matusi, vijembe, mipasho na mambo mengine mabaya kikipelekea furaha katika sehemu flani ya jamii. Ndio, dini zetu zinasisitiza kuwaenzi marehemu, lakini dini hizo pia zinasisitiza umuhimu wa heshima wakati wa uhai wetu.
Na pia licha ya ukweli si kila Mtanzania ni mcha-Mungu, wingi wa wacha-Mungu katika nchi yetu umeshindwa kuzuwia mauaji ya albino, ufisadi na 'dhambi'nyingine lukuki.
Nimalizie makala hii kwa kutoa salamu zangu za rambirambi kwa familia ya marehemu Kapteni Komba, ndugu, jamaa, marafiki na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.
Njia mwafaka ya kumwenzi marehemu ni kudumisha mema yake, na kujifunza katika mapungufu yake. Kadhalika, kifo hiki kinapaswa kutuamsha na kuanza mjadala wa kitaifa kuhusu kudidimia kwa upendo, umoja na mshikamano wetu.
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Kapteni Komba mahala pema peponi. Yeye ametangulia tu, sote twaelekea huko.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.