26 Aug 2016

Msanii nguli wa Bongo Movies, Gabo Zigamba, anatoa tahadhari kuhusu matapeli mbalimbali wanaotumia jina lake. Awali, msanii huyo alipoteza simu mbili za mkononi, ambazo baadaye zilikuwa zikitumiwa na matapeli hao kuomba misaada kwa watu mbalimbali wakijifanya kuwa wao ndio Gabo.
Kadhalika, majuzi, akaunti ya Facebook ya msanii huyo ilidukuliwa na ikatumika kwa muda na matapeli hao kwa kujifanya wao ndio msanii huyo. Hatimaye alifanikiwa kuirejesha akaunti hiyo katika himaya yake.
Gabo ameeleza kuwa anahisi kuwa yeye ndio msanii anayeongoza kwa jina lake kutumiwa na matapeli kwa sababu amekuwa akipata taarifa mbalimbali kuhusu watu wanaotumia jina lake, kwa mfano binti mmoja aliyejifanya ndiye Gabo na amekuwa akitapeli kwa kudai anauza mabegi.


Msanii huyo ametoa wito kwa Watanzania kuwa makini na watu wanaotumia majina ya watu wengine, hususan watu maarufu, kwa minajili ya kutapeli. Amesema kuwa yupo katika mchakato wa uzinduzi mpya wa akaunti zake mbalimbali za mitandao ya kijamii ili, pamoja na sababu nyingine, iwe rahisi kwa watu kuwasiliana nae pindi wanapokumbana na matapeli hao wanaotumia jina lake.

20 Aug 2016



Kwanza kabla ya kuingia kwa undani katika uchambuzi huu, ni vema nikaweka bayana uhusiano wangu na watu wawili ninaowaongelea katika makala hii: Rais John Magufuli na aliyekuwa RC wa Arusha Felix Ntibenda. 

Oktoba mwaka 2006, nilianza kufuatilia kilichokuja kujulikana baadaye kama 'skandali ya Richmond' (rejea HAPA na HAPA  na hatma yake HAPA). Kwa kifupi, nilikuwa bloga pekee niliyelivalia njuga suala la Richmond, tangu mwanzo wake hadi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alipolazimika kujiuzulu.

Wasichoelewa watu wengi ni kwamba uamuzi wangu wa kufuatilia suala hilo ulinigharimu mno, kikazi, kimasomo na kimaisha kwa ujumla. Laiti ningelipa kisogo suala hilo basi leo hii ningeendelea kuwa mtumishi wa umma. Hata hivyo, sijilaumu wala kusikitika kwa sababu mabadiliko yanahitaji kujitoa mhanga.

Lakini niwe mkweli, yaliyonisibu kutokana na ufuatiliaji wangu wa suala hilo yameniachia kinyongo, na ni kinyongo hicho kilichopelekea uamuzi wa kumuunga mkono mpinzani mkuu wa Lowassa katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais mwaka jana. Pamoja na 'tofauti zangu na CCM' haikuwa vigumu kwangu 'kuungana nao dhidi ya our common enemy.' Waingereza wanasema 'chuki ya pamoja na mwanzo wa urafiki.'

Hiyo ndio iliyokuwa sababu ya kumpigia debe mgombea wa CCM, Dkt John Magufuli. Na kwa vile kabla ya hapo nilikuwa nikiunga mkono harakati za vyama vya upinzani, hususan Chadema, uamuzi huo wa kumsapoti mgombea wa CCM ulipelekea mie kuonekana 'msaliti,' nikamwagiwa idadi kubwa tu ya matusi, huku baadhi ya 'waungwana' wakidai kuwa nilikuwa najikomba kwa ajili ya kutaka u-DC.

Kufupisha stori, sio tu kuwa kama Mtanzania nina haki na uhuru wa kupongeza au kumkosoa Rais Magufuli bali pia ukweli kuwa nilikuwa miongoni wa waliompigia kampeni unaniongezea haki na uhuru huo.

Na katika makala hii ninatumia uhuru huo na haki hiyo kwa kumkosoa kidogo Rais wangu katika 'tumbua majipu' yake. Ninasema 'kumkosoa kidogo' kwa sababu kwa ninamuunga mkono kwa kiasi kikubwa katika jitihada zake za 'kuinyoosha Tanzania yetu,' ikiwa ni pamoja na umuhimu wa utumbuaji majipu.

Waingereza wana msemo kwamba sio kila jambo sahihi ni zuri na sio kila jambo zuri ni sahihi.Ntakupa mfano. Ukitembelewa na mtu mwenye njaa kali, waweza kukimbilia kumpa chakula kingi ili aondoe njaa hiyo. Kwa kufanya hivyo waweza kumpelekea akavimbiwa au hata akapoteza maisha (yes, mlo 'wa ghafla' waweza kuuwa mtu). Kinachopaswa kufanyika katika hali hiyo ni kwanza kumpatia mwenye njaa huyo kimiminika cha moto, kama vile uji au chai kabla ya kumpatia mlo kamili.

Mfano huo unaonyesha kuwa jambo sahihi la kumpatia mlo mwenye njaa lingeweza kuwa na matokeo yasiyo mazuri, yaani kuvumbiwa kwa mwenye njaa au hata kupoteza maisha.  Na laiti mwenye njaa huyo angepewa kwanza uji badala ya mlo mzito, angeweza kuhisi kuwa mwenyeji wake 'amepuuza njaa yake' kwa kumpa uji badala ya ugali/wali. Kwahiyo hapa jambo sahihi linatafsiriwa kuwa sio zuri.

Kwa mantiki hiyohiyo, utumbuaji majipu wa Rais Magufuli ni jambo sahihi kabisa, lakini kuna nyakati utekelezaji wake unaleta taswira isiyo nzuri.

Na hapa nitolee mfano wa tukio lililotokea juzi ambapo wadhifa wa aliyekuwa Mkuu wa Arusha Felix Ntibenda ulitenguliwa pasipo kutolewa maelezo yoyote.

Kwanza kitendo tu cha kutengua wadhifa wa mwakilishi mkuu wa Rais katika mkoa, bila kujali kuwajulisha wananchi ni kuwanyima haki na pia kutomtendea haki aliyetenguliwa. Ikumbukwe kuwa penye ukosefu wa taarifa sahihi, majungu au uzushu huziba pengo hilo.

Nilibainisha awali kuwa ninafahamiana na Ndugu Ntibenda. Ni mtu aliyewahi kuwa 'mwalimu' na kiongozi wangu wakati nikiwa mtumishi wa serikali huko nyuma. Misingi aliyonipatia wakati nikiwa chini yake ilipelekea nami kupewa promosheni ambayo ilidumu hadi wakati ninaondoka huko nyumbani kuja huku Uingereza kimasomo. Na sio mie pekee bali Ndugu Ntibenda 'aliwapika' lundo la maafisa ambao wengi leo hii ni watu muhimu kabisa kwa usalama wa taifa letu.


Kwa tunaomfahamu, licha ya uchapakazi wake usio na mfano, Ndugu Ntibenda ana utu wa kipekee. Na hicho ndio kilichmfanya awe kiongozi mzuri. Walio chini yake walikuwa kama sehemu ya familia yake.

Niwe mkweli, niliposikia kada fulani wa CCM ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya katika mkoa wa Arusha uliokuwa chini ya Ndugu Ntibenda nilipatwa na hofu kuhusu hatma ya bosi wangu huyo wa zamani. Na sababu kubwa ni kuwa Mkuu wa wilaya huyo anafahamika kwa majungu na fitna, mmoja wa mtaji mkubwa wa makada wa CCM hasa wale waliopo au waliopitia Umoja wa Vijana wa CCM .

Na kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, kuna kila dalili kuwa njama za kumhujumu Bwana Ntibenda zilichochewa na kada huyo wa CCM kwa kushirikiana na wenzie mkoani humo. Natambua kuwa ninaweza kuonekana mnafiki kwa 'kushikilia bango' suala la Bwana Ntibenda kwa vile tu ninafahamiana nae, lakini hiyo haina uzito kulinganisha na uzito wa suala lenyewe.



Ukiangalia jinsi wadhifa wake ulivyotenguliwa unaona bayana kuwa kuna hali kama ya kuumbuana makusudi.Kama Rais au Waziri Mkuu walikuwa wanafahamu 'makosa' ya RC Ntibenda, kwanini wamwondoe madarakani katika hali ya kumdhalilisha, na kwa uharaka kana kwamba ni gaidi or something? Isingewezekana kusubiri hadi mwisho wa siku ya kazi au baada ya kumaliza majukumu yake ya kazi katika siku hiyo? 




Na kubwa zaidi, kama tukiamini kuwa alifanya makosa yaliyopelekea wadhifa wake kutenguliwa, kwanini basi, kwanza, makosa hayo yafanywe siri, na pili, kwanini ahamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu? Akarudie tena makosa au ni kumdhalilisha tu?

Hii ni nje ya rekodi, lakini Bwana Ntibenda alifanya kazi kubwa sana katika uchaguzi mkuu uliopita.Siwezi kuandika hapa kwa sababu ni 'mambo yasiyoandikika hadharani' lakini 'wanaofahamu yanayoendelea behind the scene' wanafahamu fika mchango wa RC huyo wa zamani.

Nimalizie makala hii kwa kumshauri Rais Magufuli kuepuka kusikiliza majungu ya kisiasa, moja ya kansa inayoitafuna CCM kwa muda mrefu. Hao vijana wanaompelekea majungu, wakishamaliza kuwaharibia wengine watamgeukia yeye Rais. Kuna msemo wa kiswahili usemao: "Mchawi akimaliza kuroga mtaa mzima huigeukia familia yake."

Kilichojiri Arusha chaweza kuwa mwendelezo wa 'kuzadia uhuni,' kama ilivyokuwa kwa yule kijana aliyemfanyia vurugu Jaji Warioba akaishia kuzawadiwa ukuu wa wilaya,na leo ni Mkuu wa Mkoa. 



Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti jana kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akieleza kuwa Watanzania wanaruhusiwa kwenda jijini Dar es Salaam lakini LAZIMA WAWE NA SIFA MAALUM...na japo wanaruhusiwa kutembelea ndugu zao LAKINI WASIKAE SANA.

Hivi huyu mtu kalewa madaraka ama? Yeye ni nani hasa wa kuingilia HAKI YA WATANZANIA ILIYOWEKWA WAZI KWENYE IBARA YA 17 CHA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA inayotamka bayana 



Sasa huyu Makonda ni nani hasa kiasi cha kujiona yupo juu ya Katiba na kuingilia haki na uhuru wa Watanzania? 

Huyu bwana amekuwa mtu wa kukurupuka tu na amri, nyingi zikiwa zisizo na kichwa wala miguu kwa maana ya ugumu wa kutekelezeka kwake. 

Ninatumaini kuwa Rais Dkt John Magufuli hatoruhusu uhuni wa madaraka wa aina hii ambao kimsingi utapelekea hisia za 'Magufuli ni dikteta' kupata nguvu zaidi.

Tupo mwaka 2016 halafu anakurupuka mtu kuwarejesha Watanzania kwenye zama za ukoloni ambapo serikali ya mkoloni ilidhibiti uhuru wa wazawa kwenda watakako kama mbinu ya kudumisha ukoloni na kudhibiti upinzani dhidi ya mkoloni.

Mbinu hiyo ya kidhalimu ilitumika pia wakati wa utawala wa kinyama wa Makaburu huko Afrika Kusini ambapo Weusi walipaswa kuwa na ruhusa maalumu kutoka nje ya maeneo yao.

Huyu Bwana Makonda aendelee kufuatilia hao mashoga, ombaomba, wavuta shisha, nk ambao ni dhahiri wamemzidi akili na wanaendelea na maisha yao kama kawaida.

Wito wangu kwa Bwana Makonda ni kwamba yawezekana kabisa kuwa kiongozi mzuri bila kukurupuka na amri zisizo na mwelekeo. Ni muhimu kwa RC huyo kutofautisha maigizo na uongozi, na akitaka maigizo aende bongo movie.

Hizi ni jitihada za makusudi za kumkosanisha Rais Magufuli na Watanzania.



19 Aug 2016

Magufuli ni dikteta. Yeye ni nani hasa wa kutupangia mikutano ya kisiasa?” Ni kauli ya mtu mmoja kwenye mtandao wa kijamii wa twitter. Kama Magufuli ni dikteta, basi hamia Sudan ya Kusini…au Somalia,” lilikuwa jibu la mtumiaji mwingine wa mtandao huo.
Mada ya ‘Magufuli ni dikteta/Magufuli si dikteta’ ndiyo inayotawala zaidi kwenye mijadala mbalimbali, hususan, ya kijamii, ambako kwa uzoefu wangu, ni kati ya maeneo muafaka kupima maoni na mitazamo ya watu wa kada mbalimbali.
Kwa kiasi kikubwa, kambi inayodai kuwa ‘Magufuli ni dikteta,’ inajumuisha wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao sasa wanahamasishana kuhusu mkakati wao mpya uanaofahamika kama ‘UKUTA,’ yaani ‘Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania.’ Sina hakika neno ‘umoja’ limeingiaje hapo kwa sababu tofauti na ‘Umoja wa Katiba ya Wananchi’ (UKAWA) ulioijumisha Chadema na CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ‘umoja’ wa UKUTA unakihusisha Chadema pekee.
Kwa upande mwingine, kambi inayomtetea Dk. Magufuli kuwa si dikteta, inaundwa na wafuasi wa chama tawala CCM, na idadi kubwa tu ya Watanzania wengine wanaoamini kuwa si tu kwamba kiongozi huyo anafanya kazi nzuri bali pia kuna masuala ya muhimu zaidi kwa nchi yao kuliko mikutano/maandamano ya kisiasa.
Hoja ya Chadema, au UKUTA yao, ni kwamba agizo la serikali kuzuia mikutano na maandamano ya kisiasa ni la kidikteta, linakandamiza haki yao ya kikatiba ya kufanya shughuli za kisiasa, na hawahitaji ruhusa ya Rais katika utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa.
Sambamba na hilo, malalamiko dhidi ya Dk. Magufuli na serikali yake ni kamata-kamata inayoendelea dhidi ya viongozi na wanachama wa vyama vya Upinzani. Kwa wapinzani, huo si udikteta tu bali pia mkakati wa kuviua vyama hivyo.
Pengine katika hatua hii ni muhimu kuweka bayana maslahi yangu. Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, nilimuunga mkono na kumpigia kampeni Dk. Magufuli, kwa kutumia haki yangu ya kikatiba na utashi wangu.
Kwangu, uchaguzi ulishamalizika mwaka jana. Tumeshampata Rais na serikali yake. Ninaiangalia Tanzania kama nchi na si kwa ‘lensi’ ya u-CCM au u-Chadema. Uchambuzi huu mfupi unafanyika katika mantiki hiyo, kwamba Tanzania yetu ni muhimu zaidi kuliko vyama vya siasa, na maslahi ya taifa ni muhimu zaidi ya maslahi ya kiitikadi.
Baada ya angalizo hilo, nina hoja kuu mbili ambazo ndio mtazamo wangu rasmi kuhusu ‘Magufuli ni dikteta/si dikteta.’ 
Hoja ya kwanza ni kwamba sidhani kuwa uamuzi wa kuzuia shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani ni la busara. Katiba inaviruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli hizo alimradi zinazingatia sheria na hazisababishi uvunjifu wa amani.
Kwa kuazima busara za Kighoma Malima, “haki haitolewi kama zawadi. Haki hudaiwa, wakati mwingine kwa nguvu,”. Wapinzani wanaona ni sawia kwao kutumia nguvu kudai haki yao.
Hivi, vyama vya upinzani vikiachwa kufanya mikutano yao (kwa kuzingatia sheria za nchi) kutakuwa na madhara gani hasa? Katika hili, naona kama Rais Magufuli anashauriwa vibaya, hasa ikizingatiwa kuwa kwa kiasi kikubwa kabisa, amemudu kumiliki takriban hoja zote za muhimu za vyama vya upinzani, hususan, vita dhidi ya ufisadi. Binafsi, ninaona zuio hilo la shughuli za kisiasa za wapinzani ni sawa na “kuwapa wapinzani kitu cha kuongea.”
Hoja yangu ya pili ni kwamba ifike mahala vyama vya upinzani vitambue kuwa mikutano na maandamano si shughuli pekee za vyama vya siasa. Kuna masuala mengine mbalimbali yanayoweza kufanywa na vyama hivyo badala ya mikutano na maandamano tu.
Ndiyo, mikutano na maandamano ni haki ya vyama vya siasa, lakini si kipaumbele kikubwa cha Watanzania, hasa katika kipindi hiki ambacho Rais Magufuli anafanya kila jitihada kuiondoa Tanzania yetu kutoka katika lindi la ufisadi ambao kwa kiasi kikubwa umechangia umasikini unaoikabili nchi yetu.
Nimalizie makala hii kwa kukumbushia kuwa huko nyuma, takriban sote – ikiwa ni pamoja na vyama vya upinzani – tuliafikiana kuwa “ili Tanzania yetu iendelee, twahitaji Rais dikteta.” Na yayumkinika kuhisi kuwa kama udikteta wawezesha kuongeza pato la taifa, kuwaibua watumishi hewa, kuwadhibiti ‘wauza unga,’ na kurejesha nidhamu ya ‘asiyefanya kazi na asile,’ basi Dk. Magufuli aendelee tu kuwa ‘dikteta.’
Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

16 Aug 2016


NDOTO yangu ya muda mrefu utotoni ilikuwa utabibu. Moja ya sababu zilizonipa ndoto hiyo ni uuguzi (unesi) wa dada yangu, ambao ulinifanya nimtembelee kazini kwake (hospitalini) mara kwa mara. Kila nilipomtembelea, nilishuhudia wagonjwa mbalimbali wakiwa wamekabidhi afya na uhai wao mikononi mwa madaktari na manesi. Nikanuwia kuwa nitakapomaliza elimu ya msingi na kufanikiwa kuingia sekondari, nitasoma masomo ya sayansi ili baadaye niwe daktari.
Kwa bahati nzuri nilifaulu darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga sekondari ya kutwa ya Kilombero, Ifakara. Mimi na wanafunzi wenzangu tuliofaulu mwaka huo ndio tulikuwa wanafunzi waanzilishi wa shule hiyo maarufu kwa jina la Kilombero Day.
Kujiunga na shule hiyo kuliisogeza karibu ndoto yangu ya udaktari, sio tu kwa vile nilipata fursa ya kusoma masomo ambayo yangeweza kunisaidia kusomea udaktari lakini pia shule hiyo ilikuwa jirani tu na chuo cha waganga wasaidizi (MATC), kilichokuwa katika hospitali ya Mtakatifu Francis.
Hata hivyo, nilikabiliwa na vikwazo viwili. Kwanza, shule hiyo mpya ilikuwa na uhaba mkubwa wa nyenzo mbalimbali za kitaaluma, vitabu vya kiada na maabara. Kikwazo cha pili kilikuwa katika uwezo wangu binafsi. Somo la hisabati lilikuwa ‘mgogoro’ tangu siku ya kwanza, na somo la Fizikia likatokea kuwa gumu kuliko yote. Wakati huo, nilishafahamu kuwa mkondo wa udaktari ni Fizikia, Kemia na Baiolojia (PCB) na Hisabati kidogo.
Kufupisha simulizi, nilipohitimu kidato cha nne nilipata Daraja la Kwanza huku nikiwa na alama A ya Kemia, C ya Baiolojia na F ya Fizikia. Ukichanganya na D ya Hisabati, mkondo wa PCB uligoma.
Nilipochaguliwa kidato cha tano, nikataka kuikwepa Fizikia kwa kusoma Kemia, Baiolojia na Jiografia (CBG), ambayo ingeweza kunifikisha katika azma yangu ya kusomea udaktari. Nikakumbana na kikwazo cha kuchukua tena Hisabati (Basic Mathematics) kama somo la ziada na kumbe Kemia ya Kidato cha Tano na Sita haikuwa nyepesi kama ile niliyopata alama A kidato cha nne. Kipengele cha Physical Chemistry kilikuwa ni kama Fizikia zaidi kuliko Kemia na hisabati juu. Nikaamua kuzika ndoto yangu ya udaktari, nikachukua mkondo wa Historia, Jiografia na Kiingereza (HGL) na somo la ziada la Siasa.
Lengo la simulizi hiyo sio kuelezea safari yangu ya kitaaluma au ndoto yangu hiyo ya udaktari iliyokufa kifo cha asili bali kama kielelezo mwafaka cha kukosoa uamuzi wa serikali kulazimisha masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne.
Sitaki kujigamba kuhusu kiwango changu cha elimu, lakini ukweli ni kwamba licha ya kufanikiwa kuhitimu shahada tatu nikisaka ya nne kila ninapokutana na hata mhitimu wa kidato cha sita tu wa mkondo uliohusisha Fizikia na Hisabati (kwa mfano PCB au PGM), ninampa heshima zote. Sababu nyepesi ni kwamba ameweza kile kilichonishinda.
Na hadi muda huu, nikiwaona wanafunzi wa shahada ya kwanza katika masomo ya sayansi kama vile uhandisi, ninawaheshimu mno. Kwa kifupi tu, masomo ya sayansi yanahitaji mtu mwenye akili zaidi. Japo haimaanishi tunaosoma kozi zisizo za sayansi ni ‘patupu kichwani,’ ukweli ni kwamba angalau kozi zetu zina ahueni fulani.
Sasa serikali inapokurupuka na uamuzi wa kulazimisha masomo ya sayansi kwa wanafunzi wote, kinyume cha utaratibu uliopo ambapo wanafunzi wa sekondari wanaingia kidato cha tatu wanapewa uhuru wa kuchagua mkondo wanaotaka (hasa kwa kuzingatia ndoto zao kitaaluma na uwezo wao kimasomo).
Huu ni udikteta wa kitaaluma, kumlazimisha mwanafunzi kusoma kitu asichotaka. Na hapa suala sio kutaka tu bali pia kuna suala la uwezo wa kumudu masomo ya sayansi. Na kingine ni kuwabebesha wanafunzi mzigo wasiostahili.
Sababu iliyotolewa na serikali kupitia Waziri wa Elimu, Teknolojia, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kuwa hivi sasa Tanzania imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa kati ambao ni wa viwanda, na hivyo suala la sayansi haliwezi kuepukwa (kwa sababu ni wakati sasa wa kuwa na wataalamu wengi wa fani za sayansi watakaoweza kutosheleza mahitaji ya sekta ya viwanda nchini) haina mashiko.
Nihitimishe makala hii kwa kumshauri waziri huyo msomi kurejea mada kama ‘reactance’ na ‘boomerang effect’ kwenye saikolojia na kuzihusisha na uamuzi huo wa serikali na athari zake.
Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

13 Aug 2016

14026664_162506520845816_426045486_n
Leo ni siku ya kuzaliwa ya mwana-hiphop mahiri na lejendari nchini Tanzania, Fareed Kubanda a.k.a Fid-Q. Na katika kuadhmisha birthday yake, msanii huyu ambaye sio tu amedumu "kwenye fani" kitambo bali pia ni miongoni mwa waasisi wa Swahili Hip-Hop.

 Kwangu, Fid-Q sio tu ni msanii maarufu kabisa huko nyumbani Tanzania na katika Swahii hip-hop duniani, bali ni mmoja wa watu ambao wamkuwa wakinipatia sapoti kubwa katika kazi zangu za uandishi wa vitabu. Na ndio maana kwa kutambua mchango wake huo, alikuwa mtu wa kwanza kupata nakala dhahiri ya kitabu changu kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa (ushushushu) kama inavyoonyesha pichani chini.

 Jana niliuliza huko kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuhusu wimbo gani wa Fid-Q unawavutia zaidi mashabiki wake. 



Jibu jepesi lilikuwa "kila wimbo wake unavutia." Nimesikiliza hii track mpya ya 'SUMU.' Imesheheni kauli nyingi za busara. Nitamwomba Fid-Q anitumie mashairi ya wimbo hu ili kuwaletea ninyi wasomaji uchambuzi zaidi ya wimbo huo. Lakini hata bila uchambuzi, kwa kuusikia tu, utaafikiana nami kuwa umeshehenu busara tele.

 Na hiki ndio kinachomfanya Fareed aendelee kuwa mmoja wa wasanii wachache na adimu kabisa Tanzania sio tu kuwa waasisi wa fani bali pia wasiochuja: kuwa na nyimbo zenye ujumbe usiochuja. Kama ingekuwa ni muziki wa bendi basi tungelinganisha na timeless tunes za kina Mbaraka Mwinshehe, Marijan Rajabu, Bitchuka, Shaban Dede, nk ambao tungo zao zilituvutia tangu tukiwa utotoni (kwa tulozaliwa enzi hizo) na ni tamu hadi leo. Na utamu so wa ladha tu bali pia relevance ya ujumbe uliomo. 

 Basi nisiandike 'gazeti,' bali nimtakie Fareed heri ya siku yake ya kuzaliwa, na kumtakia kila la heri na fanaka maishani, na kumshukuru kwa sapoti yake kwa kazi zangu, na kumpongeza kwa kutupatia 'SUMU.' Isikilize hapa chini

11 Aug 2016

Makala hii maalum ya sauti inazungumzia kitabu changu kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa (ushushushu) ambacho sasa kinapatikana katika nakala dhahiri (hard copy). Makala hii inaeleza kuhusu nini kilichonisukuma kuandika kitabu hiki na pia inaeleza kwa undani yaliyomo kitabuni.




Check this out on Chirbit

9 Aug 2016

Kwa mujibu wa takwimu, asilimia 48 ya Waingereza wanajitambulisha kama wasio na dini.

Na hapa Uskochi ninapoishi ndio panapngoza kwa idadi ya 'waliovunja uhusiano na Mungu' kwa idadi ya asilimia 36.

Kwa upande mwingine, Ireland ya Kaskazini ndio sehemu ya UK inayoongoza kwa kuwa na idadi ndogo (asilimia 10 tu) ya wasiomtambua Mungu/wasio na dini/wapagani.

Ramani kamili ni hii hapa chini

Null

Je watambua ni nchi gani duniani ambazo 'upagani' ni kosa lenye adhabu ya kifo? Hebu chemsha bongo kidogo kwa kuzitambua nchi hizo kwenye ramani ifuatayo (kidokezo kipo chini ya picha)

1


·        Afghanistan
·        Iran
·        Malaysia
·        Maldives
·        Mauritania
·        Nigeria
·        Pakistan
·        Qatar
·        Saudi Arabia
·        Somalia
·        Sudan
·        United Arab Emirates

·        Yemen



5 Aug 2016


Kitabu kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa (ushushushu) kinapatikana kwenye maduka ya vitabu sehemu mbalimbali nchini Tanzania.

Kwa wanunuzi wa rejareja, kitabu hiki kinapatikana katika maduka ya vitabu yafuatayo


 Bei ya rejareja ni sh 15,000. 

Pia fursa hii ni kwa wenye vibanda vya kuuza magazeti au wachuuzi wa bidhaa za mkononi. Bei ya jumla kwa kila kitabu ni sh 8,400.

           KARIBUNI SANA


30 Jul 2016


Kwa rafiki zangu huko Facebook, nadhani mwakumbuka stori moja niliyowasimulia kitambo kuhusu rafiki yangu mmoja, Mtanzania, ambaye kitaalua ni mfamasia, lakini ameamua kuweka kando taaluma hiyo na kujikita katika kilimo.

Baadhi ya marafiki zangu waliomba mawasiliano nae, na takriban wote walinipa mrejesho kuwa wamevutiwa sana na jitihada za @d33dat, ambaye binafsi ninamchukulia kuwa ndio mwasisi wa falsafa ya "Kilimo kama Ajira."

Angalia mahojiano mafupi kati yake na kipindi cha Dira ya Dunia cha BBC Swahili yaliyofanyika jana Ijumaa Julai 29, 2016.



Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.