Showing posts with label LOWASSA. Show all posts
Showing posts with label LOWASSA. Show all posts

23 Sept 2015

BAADA ya harakati na pilika lukuki za vyama vyetu na wanasiasa kusaka fursa ya kumrithi Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, hatimaye tumefikia takriban mwezi mmoja tu kabla ya ‘siku ya hukumu’ kutimia.
Kufikia Septemba 23, tumebakiwa na mwezi mmoja na siku mbili kabla Watanzania hawajapiga kura kumchagua rais mpya, sambamba na kuwachagua wabunge na madiwani katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 25, 2015.
Pengine ni mapema mno kufanya tathmini inayoweza kutoa mwelekeo wa chama kipi kitaibuka kidedea au mgombea gani wa urais atashinda, lakini angalau sote twatambua kuwa kwa upande wa urais, mshindi atakuwa aidha Dk. John Magufuli, mgombea kwa tiketi ya chama tawala CCM au Edward Lowassa, mgombea wa Ukawa kupitia Chadema.
Pamoja na changamoto nyingine zitakazomkabili mshindi katika uchaguzi huo, moja kubwa ni kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja baada ya uchaguzi. Sio siri kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umetugawa mno. Na sio kati ya wafuasi wa vyama pinzani tu bali hata walio ndani ya vyama husika na sie wengine tunaojitambulisha kama tusio na vyama.
Kwa upande wa CCM, mchakato wa kumpata mgombea wake umeacha makovu kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizotangulia maara baada ya chama hicho kuruhusu ushindani katika kumpata mgombea wake. Wakati CCM ilipompitisha Rais Benjamin Mkapa mwaka 1995 kulikuwa na manung’uniko kwamba kada huyo ‘alibebwa’ na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na ‘kuwawekea ngumu’ makada wengine Kikwete na Edward Lowassa waliokuwa wakiwania fursa hiyo pia.
Mchakato wa CCM kumpata mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 uliacha majeraha makubwa zaidi, hasa kwa vile Mwalimu hakuwepo kusimamia mchakato huo, na kwa upande mwingine, Rais aliyekuwa madarakani, Mkapa, ni kama alizidiwa nguvu na kundi la mtandao wa Kikwete. Uchaguzi huo uliacha mpasuko mkubwa zaidi ambao umeigubika CCM hadi muda huu.
Lakini kilichojiri katika uchaguzi wa mwaka huu ni kikubwa zaidi kiasi kwamba kwa mara ya kwanza kabisa, chama hicho tawala kinakabiliwa na upinzani mkali ambao kimsingi ni matokeo ya mpasuko uliokigubika chama hicho tangu mwaka 2005. Kwa mara ya kwanza, CCM sio tu kinakabiliwa na upinzani uliotokana na ushirikiano wa vyama mbalimbali lakini pia mpinzani wake katika nafasi ya urais ni kada wake wa zamani, Lowassa, ambaye hadi anaondoka CCM alikuwa na nguvu kubwa kabisa katika chama hicho.
Kwa upande wa vyama vikuu vya upinzani, hali kwao pia ni tofauti kwa kiasi kikubwa. Kwa mara ya kwanza vyama vikuu vitatu, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, vikishirikiana na NLD, vimeweza kuruka kihunzi kilichowakwaza katika kila uchaguzi, yaani kuafikiana kusimamisha mgombea mmoja. Awali, wazo zima la umoja wa vyama hivyo unaojulikana kama Ukawa, kumsimamisha mgombea mmoja lilionekana kama ndoto ya alinacha, hasa kwa kuzingatia historia. Kwamba kila jitihada iliyofanyika huko nyuma kujenga ushirikiano miongoni mwa vyama vya upinzani haukuweza kufanikia.
Lakini kadri siku zilivyokwenda, taratibu wazo la ushirikiano wa vyama hivyo likaanza kujenga picha kamili kuwa safari hii wamedhamiria kuwa kitu kimoja. Hata hivyo, kosa la msingi na ambalo pengine litawagharimu katikia uchaguzi wa mwaka huu ni kutotumia vema fursa kubwa waliokuwa nayo kukamilisha mchakato wa kumpata mgombea wao na kumnadi kabla CCM hawajafanya hivyo. Ninachomanisha hapa ni kwamba, kwa vile vyama vya upinzani vinauelewa vema mchakato wa CCM kupata mgombea wake- ni kama vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo waweza kudhani itakipasua chama hicho kikongwe- wangetumia fursa hiyo wao kujimmarisha na mgombea wao kiasi kwamba CCM baada ya kumpata mgombea wao wangekutana na mgombea wa Ukawa ambaye sio tu amejiandaa vya kutosha lakini pia anatambulika kwa wapigakura.
Hatimaye, kitendawili cha kwa nini Ukawa walikuwa wakisuasua kumtangaza mgombea wao kiliteguliwa baada ya Lowassa kukatwa CCM na hatimaye kujiunga na Chadema na baadaye kupitishwa kuwa mgombea urais. Kumbe muda wote tulipokuwa tunahoji kwanini Ukawa hawatangazi mgombea wao, wenzetu walikuwa wanamsubiri kitakachodondoka kutoka CCM.
Licha ya ujio wa Lowassa huko Ukawa kuonekana umeleta msisimko na matumaini makubwa kwamba angalau upinzani mwaka huu una mgombea ‘anayeweza kuisumbua CCM,’ kisichoongelewa sana ni mpasuko wa kawaida tu kati ya wanaodhani ni sahihi kumtumia Lowassa katika azma ya kuing’oa CCM madarakani na wale wanaoona kuwa suala hilo sio tu ni usaliti lakini pia linaonyesha mapungufu ya vyama hivyo vya upinzani, kwa maana ya kwamba ilivibidi visubiri mtu kutoka CCM ili kufanikisha azma yao ya kuingiza Ikulu.
Tukiweka kando mazingira ambayo CCM na Ukawa wamepitia hadi tulipo sasa, kuna mambo kadhaa yanaanza kujitokeza ambayo yanaweza kutoa taswira ya matokeo ya uchaguzi huo japo ni muhimu kutambua kuwa, kwanza, si rahisi kubashiri kwa usahihi kabisa matokeo ya uchaguzi wenye ushindani kama wa mwaka huu, na pili, kama wiki moja katika siasa ni sawa na takriban mwaka (kwa maana ya lolote laweza kutokea) muda uliosalia kabla ya uchaguzi ni kipindi kirefu kinachoweza kuathiri ubashiri wowote utakaofanyika muda huu.
Miongoni mwa mambo ya msingi yaliyojitokeza katika kampeni zinazoendelea ni pamoja na lile ambalo wana-Ukawa hawataki kabisa kulisikia, nalo ni mapungufu ya mgombea wao, yaani Lowassa. Sote twaifahamu CCM, na japo mgombea wake, Magufuli ni mgombea kama Lowassa, lakini kimsingi kwa huko Ukawa Lowassa si mgombea tu lakini yeye ndio kama Ukawa yenyewe. Kwa lugha nyingine, uchaguzi huu unakuwa kama vita kati ya CCM na Lowassa, hasa kwa sababu mgombea wa CCM anajinadi kichama zaidi ilhali Lowassa anajinadi na kunadiwa kama Lowassa zaidi.
Moja ya madhara ya wazi ya suala hilo ni uwezekano wa Ukawa kupoteza viti vingi vya ubunge kwa gharama ya kumnadi zaidi Lowassa. Niliwahi kuandika kwenye mtandao wa kijamii wa twitter kuwa nina wasiwasi kuwa mmoja au hata wawili wa viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa kwa upande wa Bara, yaani Freeman Mbowe wa Chadema, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Emmanuel Makaidi wa NLD, anaweza kushindwa katika uchaguzi huo. Pamoja nao ni viongozi wengine wakuu wa vyama hivyo ambao pia ni wabunge, hususan kwa upande wa Chadema.
Iwapo hilo litamtokea, na iwapo Ukawa watashindwa, basi hatma ya vyama hivyo itakuwa mbaya. Kwa Chadema, yayumkinika kuhisi kuwa salama yake pekee ni kufanikiwa kwa jaribio (experiment) la kumtumia Lowassa kuiong’a CCM. Ikishindwa, kuna uwezekano mkubwa chama hicho kikaingia katika mgogoro wa ‘kumsaka mchawi’ ambao waweza kutishia uhai wa chama hicho kilichokubali kutelekeza ajenda yake ya kupambana na ufisadi ili kumtengenezea mazingira mazuri Lowassa.
Kwa NCCR-Mageuzi, ili Mbatia aendelee kubaki kiongozi wa chama hicho itambidi lazima ashinde ubunge anaowania huku akitegemea Lowassa kushinda urais. Kinyume cha hapo yeye na chama chake watakuwa matatani, na hatma ya uhai wa chama hicho kuwa tete. Angalau kwa NLD, Makaidi anaweza kuendelea kuwa kiongozi wa chama hicho hasa ikizingatiwa kuwa kwa muda mrefu ‘chama hicho kimekuwa ni yeye na yeye ndio chama hicho,’ angalau kwa mwonekano.
Lakini kubwa zaidi ni upungufu wa Lowassa kisera na kujinadi. Ajenda ya mabadiliko imekuwa shaghala baghala kiasi kwamba watu wanaimba na kuhubiri mabadiliko pasipo hata kubainisha yatakuwaje. Ukiuliza unaambiwa la muhimu ni kuiondoa CCM kwanza, mengine baadaye. Baadaye lini? Hakuna mwenye jibu.
Kwa upande mwingine, Lowassa ameshindwa kabisa kujinadi. Haiingii akilini kuona umati mkubwa unaojitokeza kwenye mikutano yake ya kampeni ukiishia kuambulia hotuba ya dakika chache tu. Sawa, tumeshasikia hotuba nyingi za wanasiasa na nyingi zimebaki kuwa hotuba tu pasi kubadilisha chochote, lakini huu ni wakati wa uchaguzi, na hotuba ya mgombea ni fursa nzuri ya kubainisha nini atawafanyia wapiga kura na wananchi kwa ujumla pindi wakimchagua. Laiti Lowassa angetumia vema ‘mafuriko’ ya wanaojitokeza kumsikiliza, basi hata hiyo utata kuhusu ajenda ya mabadiliko isingekuwepo kwani angeweza kuwaeleza Watanzania kwa undani kuhusu suala hilo.
Kwa upande wa CCM, licha ya mgombea wake kusimama kama mgombea anayewakilisha chama na si ‘mtu binafsi,’ mtihani mkubwa umekuwa ni jinsi ya kumshambulia Lowassa pasipo kumjengea huruma kwa wapigakura. Lakini mtihani mwingine umekuwa ni kipi hasa cha kukizungumzia kuhusu Lowassa na Ukawa ambao kwa kiasi kikubwa wananadi ajenda ya mabadiliko pasi kuielezea kwa undani. Kwa kutambua hilo, Magufuli amekuwa akijinadi kwa kutumia rekodi yake mwenyewe na zile za chama chake badala ya kuelekeza mashambulizi kwa mpinzani wake. Ni wazi, ili umshambulie mpinzani wako basi angalau awe na cha maana cha kukishambulia, vinginevyo yaweza kutafsiriwa kama uonevu.
Nimalizie makala hii kwa ahadi ya kuendelea na uchambuzi zaidi kuhusu Uchaguzi Mkuu, kwa matarajio ya kuwa na nafasi nzuri ya kufanya ubashiri wa matokeo angalau siku chache kabla ya uchaguzi huo, sambamba na kukumbushana wajibu wetu kijamii kuutumia uchaguzi huo kama fursa ya kuboresha mustakabali wa Tanzania yetu.

13 Aug 2015

MAKALA hii ni mwendelezo wa ile iliyochapishwa katika gazeti hili katika toleo la wiki iliyopita. Katika makala hiyo nilijadili kwa kirefu kuhusu kile nilichokiyumkinisha kuwa usaliti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), si tu kumpokea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa (aliyelazimika kujiuzulu Uwaziri Mkuu kufuatia skandali ya ufisadi wa Richmond), bali pia kumteua kuwa mgombea wake urais kupitia UKAWA.
Kadhalika, pamoja na mambo mengine, nilieleza kusikitishwa kwangu na kile nilichokitafsiri kama mwelekeo wa siasa za Tanzania yetu kutoka mfumo wa awali wa chama kimoja hatimaye vyama vingi na hiki tunachoshuhudia baada ya Lowassa kujiunga na Chadema, ninachokiita ‘chama cha mtu mmoja.’
Katika makala hii nitajadili nafasi za kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu ujao kwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt John Magufuli, na huyo wa Chadema/UKAWA, yaani Lowassa, sambamba na vikwazo vinavyowakabili kila mmoja wao.
Nianze na Magufuli. Kwa kada huyo, binafsi ninaona kuwa ana nafasi nzuri ya kushinda hasa kwa sababu, kama alivyotamka Rais Jakaya Kikwete hivi majuzi, CCM ina uwezo na nyenzo kumwezesha mgombea wao kufanya vizuri. Vyote viwili – uwezo na nyenzo – vimeshathibitika kuwa na ufanisi mkubwa katika chaguzi zilizopita.
Na vyote viwili vipo katika pande mbili; halali na isivyo halali. Uwezo halali wa CCM unatokana zaidi na mitandao wake mpana hasa vijijini. Kwa bahati mbaya au makusudi, licha ya maeneo mengi ya vijijini katika nchi yetu kukabiliwa na umasikini mkubwa, pia yana uhaba wa ‘wasomi,’ huku wachache waliopo wakiwa aidha wamekumbatiwa na ‘mfumo unaoilinda CCM’ au wameukumbatia kwa minajili ya kulinda nafasi zao.
Ninaposema ‘wasomi’ simaanishi maprofesa au watu wenye elimu ya juu bali hata wale wenye elimu ya wastani tu ambao ni muhimu sana katika kuhamasisha na kuleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali.
Katika mazingira ya kawaida, mtumishi wa umma kijijini anaweza kuwa na chaguo rahisi ‘kuitumikia CCM’ badala ya chama cha upinzani kwa vile hasa kwa vile katika maeneo mengi ya vijijini, ni vigumu kuitofautisha CCM na serikali.
Kuna tatizo la ziada kuhusu ‘wasomi’ wetu. Wakati katika stadi za matabaka, wasomi wanatarajiwa kuwa sio tu kiungo katika ya tabaka la walalahoi na tabaka tawala, wasomi wetu wengi sio tu hawamtaki kujihusisha na tabaka la walahoi bali pia wanajibidiisha – hata kwa kuiga tu – kuwa sehemu ya tabaka tawala. Na Wasomi wachache tulionao vijijini wanaotaka waonekane kama ‘vigogo’ au ‘vingunge’ badala ya wananchi wa kawaida au walalahoi. CCM inatambua udhaifu huu na kutumia ipasavyo.
Ikumbukwe pia kuwa wengi wa ‘wasomi’ hao ndio watumishi muhimu katika shughuli nzima ya uchaguzi, na yayumkinika kuamini kuwa wamekuwa na ‘msaada’ mkubwa kwa CCM katika chaguzi zilizopita, na wanaweza kuendelea kuwa nyenzo muhimu kwa chama hicho tawala.
Lakini pengine kubwa zaidi ni turufu ya CCM hasa katika maeneo ya vijijini kuwa ‘inaweza kuonyesha jinsi ilivyowatumikia wananchi’ tofauti na ‘vyama vya upinzani vinavyokuja kufanya majaribio ya kuongoza nchi.’ Ni hoja isiyo na msingi kwa wenye uelewa wa kuchanganua mambo, lakini kwa huko vijijini, kuipinga kwahitaji kazi kubwa na sio takriban miezi mawili iliyosalia kabla ya uchaguzi mkuu.

CCM inabaki kuwa ‘zimwi likujualo’ ilhali kwa vyama vya upinzani, tegemeo lao kubwa ni kuonyesha mapungufu ya chama hicho tawala, na kutegemea wananchi watawaelewa na kuwaamini, na ‘kucheza bahati nasibu’ ya kuwakabidhi madaraka.
Ukichanganya na ukweli usio rasmi kuwa CCM ni mnufaika mkubwa wa uhusiano wake na taasisi za serikali – Tume ya Uchaguzi, vyombo vya dola, nk – chama hicho tawala kitaingia katika uchaguzi kikiwa na nyenzo na uwezo wa kushindwa hata kama ni kwa tabu.
Kwa kifupi, mazingira yaliyoiwezesha CCM kushindwa chaguzi kuu zilizopita bado yapo na mfumo wa uchaguzi bado unakitengenezea chama hicho tawala nafasi ya kufanya vizuri.
Hata hivyo, ili Magufuli ashinde, inategemea zaidi mshikamano ndani ya CCM. Na nikiongelea mshikamano simaanishi matukio yanayoanza kujitokeza ya makundi ya wana-CCM kadhaa kuhama chama hicho na kujiunga na vyama vya upinzani. Ninamaanisha wanasiasa wenye nguvu na ushawishi katika chama hicho kumuunga mkono mgombea wa chama chao au kumsaliti.

Lakini tangu Lowassa ajiunga na Chadema/UKAWA, sijaona kile kilichotarajiwa kuwa ‘mafuriko’ ya viongozi muhimu wa CCM na maelfu ya wanachama kukiasi chama hicho tawala na kujiunga na wapinzani. Kwahiyo, yayumkinika kuhisi kuwa hadi muda huu Magufuli bado ana sapoti ya kutosha ndani ya chama chake.
Kanuni isiyo rasmi ya siasa za uchaguzi Barani Afrika ni kwamba ‘chama tawala hakishindwi uchaguzi, na kikishindwa basi si kwa sababu wapinzani wana nguvu kubwa bali migongano ndani ya chama tawala inayotoa fursa kwa wapinzani.’ Sawa, labda CCM kumkata jina la Lowassa wakati wa mchujo wa wagombea wake kumesababisha mpasuko wa aina flani, lakini kama nilivyobainisha hapo juu, mpasuko huo sio mkubwa kama ilivyotarajiwa, na sidhani kama unaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM.
Kwahiyo, kwa upande wa Magufuli, takriban mazingira yote yaliyowawezewezesha wagombea wenzake wa nafasi ya urais huko nyuma kufanya vizuri bado yapo ilhali vikwazo dhidi ya yeye kufanya vizuri ni hafifu, na pengine vya kufikirika zaidi kuliko uhalisia.
Twende kwa Lowassa. Mtaji mkubwa wa mwanasiasa huyo ni umaarufu wake. Iwapo umaarufu huo unachangiwa na kinachoelezwa kuwa ni uwezo wake mkubwa wa kifedha au ‘uchapakazi’ wake, hilo ni suala linalohitaji mjadala katika makala tofauti. Lakini kilicho bayana ni ukweli kwamba umaarufu ni turufu muhimu kwa mgombea yeyote yule katika uchaguzi.

Turufu nyingine kwa Lowassa ni hali halisi ilivyo katika mahusiano kati ya CCM na Watanzania wengi. Kwa muda mrefu chama hicho tawala kimekuwa kikichukulia chaguzi mbalimbali, kuu na ndogo, kama utaratibu tu wa kukipatia nafasi za uongozi. Hakijawahi kupigania ‘kufa na kupona’ kubaki madarakani. Kwa sababu nilizozitoa hapo juu, ukichanganya na udhaifu wa wapinzani wake, bila kusahau hujuma mbalimbali dhidi yao, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, chama hicho tawala kimekuwa kikiingia kwenye chaguzi kikiwa na uhakika mkubwa wa kushindwa.
Hata hivyo, safari hii kinaweza kukumbana na ushindani mkubwa (japo hadi muda huu ni suala la kufikirika zaidi) baada ya kada wake maarufu kabisa, Lowassa, kujiunga na wapinzani. Sasa kwa vile CCM haijawahi na haijazowea kuwa katika mazingira yaliyopo sasa, yayumkinika kuhisi kuwa inaweza ‘kupaniki’ na hivyo kutoa mwanya kwa Lowassa na Chadema/UKAWA yake kufanya vizuri.
Lowassa na Chadema/UKAWA wanatambua bayana kuwa kuna mamilioni ya Watanzania waliokwishaichoka CCM na pengine wangependa kuoina iking’oka madarakani. Ni rahisi kwa wapinzani hao kubainisha ‘maovu’ ya chama hicho tawala kwa sababu mengi yanaonekana waziwazi. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa kuna ‘mazuri’ kadhaa ya utawala wa CCM, na uzoefuwaonyesha kuwa chama hicho tawala ni mahiri katika kuyanadi ‘mazuri’ hayo, ambayo pia si vigumu kuyaona.
Kikwazo kwa Chadema/UKAWA ni jinsi ya kubadili maelezo waliyoyasimamia kwa muda mrefu kuwa ‘Lowassa ni fisadi.’ Kwa mitizamo wangu, muda uliosalia haitoshi kwa vyama hivyo vinavyounda UKAWA kuwashawishi Watanzania kuwa ‘Lowassa sasa si fisadi kwa vile amejiunga nasi tuliokuwa tunapambana na ufisadi.’ Na kwa bahati mbaya, hasa kwa Chadema ambayo ilikuwa mahiri kukemea ufisadi, Watanzania wengi tu wanaonekana kutafsiri Lowassa kukubaliwa kujiunga na chama hicho ni usaliti kwa wengi waliokiamini.
Hoja kwamba ili ukiondoa CCM kuna haja ya kushirikiana na watu kama Lowassa inakabiliwa na hoja mbadala kuwa ‘kwanini tuwaamini watu msio na uwezo wa kuleta mabadiliko wenyewe hadi mtegemee makapi ya CCM?’ Hoja hiyo mbadala inapewa nguvu na ukweli kuwa UKAWA ‘walisuasua’ kwa muda mrefu kutangaza mgombea wao, na sasa twajua kuwa walikuwa wanamsubiri mwana-CCM kama Lowassa awasaidie.
Lakini mtihani mwingine kwa UKAWA na Lowassa ni huu: Magufuli anagombea urais kwa tiketi ya CCM, ambayo sio tu ni chama tawala na ambacho kipo madarakani hata kabla ya ujio wa mfumo wa vyama vingi, lakini pia kinafahamika kwa wengi. Kwa UKAWA, na hili ni kosa lao kwa kuchelewa kupata mgombea wao wa kiti cha urais, inaonekana kama ni chama ‘kipya’ cha siasa. Laiti muungano huo wa vyama vinne vya siasa (Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD) ungepata mgombea wake mapema, na kumnadi kwa nguvu wakati CCM inahangaika kupata mgombea wake, basi muda huu wangekuwa na kazi moja tu ya kupambana na Magufuli na CCM kwani wao tayari wangeshakuwa wanajulikana kwa wengi.
Vilevile, kuna suala nililozungumzia katika makala iliyopita ambapo, dalili zilizopo zinaashiria uchaguzi wa rais ni katika ya CCM na Magufuli wake dhidi ya Lowassa. Hapa ninamaanisha kwamba ni rahisi kumwona mgombea huyo wa CCM kama anayewakilisha chama chake ilhali kwa Lowassa ni kama ‘mgombea binafsi.’ Utafiti kidogo tu katika vyombo vya habari waweza kukuonyesha msomaji kuwa wakati ‘kampeni’ za CCM zimeelemea zaidi katika kumnadi Magufuli na CCM, kwa Chadema/UKAWA ni suala la kumnadi Lowassa pekee kana kwamba ni mgombea binafsi.
Na hilo linachangiwa na ukweli kuwa UKAWA si chama bali ushirikiano wa vyma ambavyo awali lengo lao lilikuwa suala la mabadiliko ya Katiba. Vyama hivyo vina sera tofauti, na japo vyawezxa kutengeneza ilani moja ya uchaguzi, muda hauko upande wao. Kwa CCM, ni mwendelezo tu wa walichokifanya mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010.
Kadhalika, wakati nimetaja kuwa umaarufu wa Lowassa ni mtaji wake mkubwa huko Chadema/UKAWA, pengine ni mapema mno kuhitimisha kuwa umaarufu huo alioupata akiwa CCM, utaendelea kuwa juu wakati huu amejiunga na Chadema/UKAWA. Ikumbukwe kuwa wapinzani wakubwa wa Lowassa alipokuwa CCM hawakuwa ndani ya CCM bali katika vyama hivyohivyo ambavyo leo vimemfanya mgombea wao wa urais. Hilo laweza kuirahisishia CCM jukumu la kumbomoa kwani ‘wanamjua vilivyo.’
Kikwazo kikubwa lakini kisicho wazi ni nafasi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika uchaguzi huo, kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita. Hata tukiweka kando kile kwenye Baiolojia wanakiita ‘symbiotic relationship’ (uhusiano wa kutegemeana kati ya kiumbe kimoja na kingine) ambapo ustawi wa taasisi hiyo na wa CCM na serikali zake ni wa kutegemeana, Idara hiyo yaweza kutumia ‘kisingizio’ kama ‘Lowassa ni tishio kwa usalama wa taifa letu,’ ambapo kwa taratibu zisizo rasmi za Usalama wa taifa sehemu nyingi duniani, anaweza ‘kudhibitiwa.’ Hili ni gumu kulieleza kwa undani kutokana na sababu za kimaadili.
Nihitimishe makala hii ndefu kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi zaidi kuhusu uchaguzi mkuu kwa ujumla, hususan katika nafasi ya urais, hasa ikitarajiwa kuwa tunaweza kushuhudia mengi zaidi ya tukio lililogusa hisia za wengi la aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba kujiuzulu ghafla, sambamba na ‘sintofahamu’ kuhusu hatma ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt Willibrord Slaa.

6 Aug 2015

NINAANDIKA makala hii nikiwa na masikitiko makubwa mno. Siku zote maishani, twajikuta katika kipindi kigumu sana pale mtu tuliyemwamini kwa dhati anapotugeuka. Wanasema, inachukua muda mwingi na jitihada kubwa kujenga uaminifu japo kosa au tukio moja tu laweza kuondoa kabisa uaminifu huo.
Na hicho ndicho walichofanya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kukubali kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowaasa, sio tu kuwa mwanachama wao bali pia mgombea wao katika nafasi ya urais.
Kama ambavyo tetesi kuwa Lowassa angechukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya CCM zilivyozagaa kwa muda mrefu, ndivyo suala la Lowassa kujiunga na Chadema/ UKAWA lilivyokuwa.
Mara baada ya mwanasiasa huyo kukatwa katika mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa Urais, zilisikika tetesi nyingi kuwa kuna uwezekano angejiunga na moja ya vyama vinavyounda UKAWA, na hatimaye kuwa mgombea urais.
Lakini kwa vile Tanzania yetu haina uhaba wa tetesi, baadhi yetu tulidhani kuna ugumu kwa Lowassa kujiunga na UKAWA ni Chadema, kwa vile chama hicho kimejijengea umaarufu mkubwa kwa msimamo wake tuliodhani ni thabiti kupambana na ufisadi na mafisadi.
Na sio msimamo tu dhidi ya ufisadi na mafisadi, Chadema wamelipa gharama kubwa katika harakati zake ambapo baadhi ya wanachama wake walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya, huku wengine wakiishia rumande au magerezani kufuatia maandamano mbalimbali ya kutetea maslahi ya taifa na wanyonge.
Hata nilipoona picha zilizodaiwa kuwa ni za Lowassa akihudhuria moja ya vikao vya UKAWA nilijipa moyo kuwa huenda picha hizo zimefanyiwa ‘ufundi,’ wenyewe wanaita ‘photoshop,’ ambapo picha ya mtu inapandikizwa kwenye picha nyingine.
Faraja iliongezeka baada ya akaunti ya habari za Chadema katika mtandao wa Twitter, Chadema Media, kukanusha uwepo wa Lowassa katika kikao hicho. Hata hivyo muda mfupi baadaye, watu wa karibu na Lowassa walibandika picha zaidi katika mtandao huo kuthibitisha kuwa kweli Lowassa alihudhuria kikao hicho.
Na siku moja baadaye,’bomu lililipuka.’ Kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ambayo sie tulio mbali tuliweza kuyaona mtandaoni, viongozi wakuu wa UKAWA walionekana na Lowassa, na baadaye mwanasiasa huyo kutangaza bayana kuwa amejiunga na umoja huo kupitia Chadema.
Ninachoweza kusema kwa kifupi ni kwamba walichofanya Chadema ni usaliti wa hali ya juu, na hakuna maelezo ya aina yoyote yanayoweza kuhalalisha kitendo hicho. Ndio, ni muhimu kwao kuingia Ikulu, lakini ni muhimu zaidi kwa Chadema kutambua imefikaje ilipo leo.
Jibu la wazi ni kama nilivyotanabaisha hapo juu; msimamo wao imara wa kuuchukia ufisadi na kupambana nao kwa nguvu zote, hatimaye ulifanikiwa kuwafumbua macho Watanzania wengi, sio tu kuhusu kansa ya ufisadi bali pia kujenga hisia kwamba chama hicho ni kwa ajili ya maslahi ya mamilioni ya Watanzania wanyonge na wahanga wakuu wa ufisadi.

Kwahiyo, kwa kumpokea Lowassa, mwanasiasa aliyelazimika kujiuzulu kwa tuhuma za ufisadi wa Richmond, Chadema wametelekeza nguzo muhimu iliyokuwa ikikitambulisha chama hicho. Na kama tunavyoina CCM, chama chochote cha siasa kinachotelekeza nguzo zake, sio tu kinapoteza uaminifu wake kwa jamii bali pia chajichimbia kaburi.
Sawa, labda Lowassa anaweza kushinda urais (hili lahitaji mjadala wa pepe yake) lakini haihitaji kuwa na ujuzi wa uchambuzi wa siasa zetu kubaini kwamba mwanasiasa huyo hakujiunga na Chadema kwa vile anakipenda chama hicho au anaafiki sera zao bali amekitumia kama ngazi ya kuwania urais baada ya kukwamishwa na CCM.
Hilo tu lilipaswa kuifumbua macho Chadema. Lowassa huyohuyo aliyejigamba kwamba jina lake halitakatwa akijivunia ‘uchapakazi’ wake, na utumishi wake wa muda mrefu katika CCM, leo hii kaitelekeza CCM licha ya kudai asiyemtaka ndani ya chama hicho aondoke lakini yeye si wa kuondoka.
Ni wazi kuwa Lowassa ni mwanasiasa mwenye tamaa ya madaraka. Sawa, Katiba yetu yamruhusu kugombea uaongozi kupitia chama chochote kile, lakini moja ya sifa nzuri kwa mwanasiasa ni msimamo na kutokuwa na tamaa ya madaraka.
Leo kaitosa CCM kwa kutaka urais, je ataitendaje Chadema katika kutaka mengineyo?
Lakini pia ni ukweli usiofichika kuwa umaarufu wa Lowassa unatokana na ‘sifa’ kuu mbili: uwezo mkubwa wa kifedha ‘zisizo na maelezo ya kutosha’ na skandali ya Richmond. Katika mazingira ya kawaida, na hasa katika zama hizi za ufisadi, ni vigumu mno kumnadi mwanasiasa wa aina hiyo.

Tayari kuna hisia kuwa ‘fedha zilibadilishana mikono’ hadi akina Freeman Mbowe kukubali kumpokea mwanasiasa huyo ambaye walikuwa wakimwandama kila kukicha kwa kumuita fisadi.
Kama ni fedha kweli au ‘umaarufu,’ tayari Lowassa ndio mnufaika maana kwa muda mfupi tu ndani ya chama hicho, mambo kadhaa yameshabadilika.
Mie nazifuatilia kwa karibu zaidi harakati za Chadema kupitia mitandao ya kijamii au tovuti za vyombo vya habari mbalimbali vya huko nyumbani. Nilichobaini katika siku chache hizi baada ya Lowasaa kujiunga na Chadema, ghafla wanachama na mashabiki wa chama hicho wamegeuka ‘mabubu’ kuhusu masuala ya ufisadi.
Na hilo si la kushangaza kwa sababu watamudu vipi kukemea ufisadi ilhali mgombea wao wa urais ni mtuhumiwa wa ufisadi?
Kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa viongozi wa Chadema, Tundu Lissu, chama hicho na UKAWA kwa ujumla walikuwa wakifuatilia kwa karibu mchakato wa CCM kupata mgombea wake, na wao walitaka kuitumia ‘sintofahamu’ hiyo ndani ya CCM kufanikisha malengo yao ya kuingia Ikulu.
Huu ni udhaifu wa hali ya juu. Lakini angalau hii imesaidia kutufahamisha kwanini chama hicho kilikuwa kinasuasua kumtangaza mgombea wake: kilikuwa kinasubiri ‘makombo’ ya CCM.
Watu hawa wanajifanya kusahau kabisa mafanikio makubwa tu waliyoyapata katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo walisimama wenyewe, wakapata wabunge wa kutosha na madiwani wa kutosha tu, licha ya mgombea wao, Dkt Willbrord Slaa, kushindwa katika mazingira ambayo baadhi yetu tunaamini yalichangiwa na hujuma.
Na ni katika mazingira hayo, baadhi yetu tunaunga mkono Dk. Slaa kujitenga na Chadema. Ni matarajio yangu kuwa hatokubali kuwa sehemu ya usaliti huu hasa kwa kuzingatia gharama kubwa waliyoingia Chadema, kwa maana ya muda na jitihada, sio tu kukitambulisha chama hicho kuwa ni mtetezi wa wanyonge na kiongozi wa mapambano dhidi ya ufisadi bali pia kukiwezesha kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania.
Awali, nilipopata uthibitisho kuwa Lowassa amejiunga na Chadema nilitamka bayana kuwa ‘impact’ ya tukio hilo yapaswa kuonekana angalau ndani ya siku 7. Na siku hizo saba zimeisha juzi. Tuliambiwa tusubiri ‘mafuriko’ ya wana-CCM kumfuata Lowasaa huko Chadema/UKAWA.
Hadi sasa, hakuna dalili yoyote ya mafuriko hayo. Jina kubwa pekee lililojitokeza kumfuata Lowassa ni Naibu wa Kazi na Ajira, Dkt Makongoro Mahanga, ambaye hata hivyo amechukua uamuzi huo baada ya kubwagwa kwenye kura za maoni. Labda kuna wengine watakaomfuata Lowassa lakini sidhani kama watu hao watakuwa na mafuriko yanayotarajiwa.
Kikwazo kikubwa kwa makada wa CCM waliokuwa wakimsapoti mwanasiasa huyo kumfuata kwenye ‘chama chake kipya’ ni ukweli kwamba tayari vyama vinavyounda UKAWA vilishagawana majimbo.
Sasa sidhani kama kuna mwana-CCM mwenye akili zake atakikimbia chama hicho tawala na kujiunga na vyama vinavyounda UKAWA ilhali anatambua kuwa hata akishindwa ubunge au udiwani katika CCM bado ana fursa ya kuteuliwa kwenye nyadhifa nyingine serikalini.
Na ujio wa wafuasi wa Lowassa ndani ya Chadema na UKAWA unaweza kuvibadili vyama hivyo na kuunda makundi ya, kwa mfano, Chadema- asilia na Chadema-Lowassa. Busara za kisiasa zatuonya kuwa chama chenye mgawanyiko hakiwezi kushinda uchaguzi, na hata kikifanikiwa kushinda, hakitoweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Wakati kwa kumpokea Lowassa Chadema italazimika kutowekeza nguvu za kutosha katika mtaji wake mkuu katika uchaguzi mkuu uliopita – vita dhidi ya ufisadi (hawawezi kupigia kelele ufisadi huko mgombea wao akiwa mtuhumiwa wa ufisadi) – ni vigumu kubashiri watamnadi Lowassa kwa lipi hasa.
Wao ndio walikuwa vinara wa kumwita Lowassa fisadi, sasa muda haupo upande wao kubadilisha maelezo na kumnadi kama mtu safi.
Na hata maelezo ya Lowassa kuwa ‘alipata maagizo ya juu’ katika suala la Richmond hayana uzito kwa sababu kwanini aongee sasa na si wakati alipobanwa hadi kujiuzulu? Sawa, wengi twafahamu kuwa skandali hiyo iliwahusisha watu wengine pia, lakini ukweli unakuwa na nguvu pale tu unapowekwa hadharani wakati mwafaka.
Ni rahisi kwa CCM kuipangua hoja ya Lowaasa kuwa ‘alitumwa’ kwa kumuuliza ‘ulikuwa wapi siku zote hizi usiyaseme hayo hadi sasa ulipoamua kuingia upinzani kwa tamaa yako ya madaraka?’
Nimalizie makala hii endelevu kwa kurejea kuwakumbusha Chadema kuwa dhambi yao ya usaliti itawaandama milele. Hoja kuwa Lowassa ‘anauzika’ na atawasaidia kuingia Ikulu sio tu haina msingi bali pia yaweza kuwagharimu huko mbeleni hasa kwa vile, kama nilivyoandika hapo juu, mwanasiasa huyo hajajiunga na chama hicho kwa vile anakipenda bali kwa ajili ya maslahi yake binafsi.
Nachungulia kidogo tu ‘marafiki zake’ kisha utaelewa nini kinaisuburi Chadema huko mbeleni. Mie si nabii wa majanga (prophet of doom) lakini ninabashiri kuwa ujio wa Lowassa huko Chadema ni mwanzo wa mwisho wa chama hicho.
Inasikitisha kuona ‘People’s Power’ (nguvu ya watu) iliyowavutia wapenda mabadiliko wengi ikiishia kuwa ‘Money’s Power’ (kwa maana ya nguvu ya Lowassa kifedha).Pia inaumiza kuona demokrasia yetu ikipitia mlolongo huu usiopendeza wa ‘chama kimoja→ vyama vingi → chama cha mtu mmoja’ (one party→multiparty→one man’s party)
ITAENDELEA

28 Jul 2015

Ninaipenda siasa...kama stadi  (study, yaani kuisoma), lakini kwa hakika ninapata shida sana na jinsi mengi ya ninayosoma katika stadi za siasa (political studies) yanavyogeuka inapokuja kwenye matendo au shughuli za kisiasa an zinazohusiana na siasa. 

Stori kidogo. Fani niliyotamani sana kuisoma na pengine kubobea ni utabibu. Nilitamani mno kuwa daktari. Lakini ndoto yangu ya udaktari ilipata kikwazo baada ya kupata matokeo ya mtihani wa kumaliza kidato cha nne. Japo nilipata A kwenye Kemia na C kwenye Baiolojia, niliambulia D kwenye Hisabati na kufeli kabisa Fizikia ambapo nilipata F. Na japo nilipata Division One, uwezekano wa kuchukua 'combination ya udaktari' yaani PCB (Fizikia, Kemia na Baiolojia) kidato cha tano uliathiriwa na hiyo F ya Fizikia. Uwezekano pekee ulibaki kwenye kujaribu combination ya CBG (Fizikia, Kemia na Jiografia) ambayo ingeniwezesha kuikwepa Fizikia.

Nilipojiunga na kidato cha tano katika sekondari ya wavulana ya Tabora (Tabora Boys') nikakumbana na vikwazo vingine. Kwanza, Kemia ya kidato cha kwanza mpaka cha nne ni tofauti kwa kiasi kikubwa na ile ya kidato cha tano na cha sita. Kuna kitu inaitwa Physical Chemistry ambayo kimsingi ni kama mchanganyiko wa Kemia, Hisabati na Fizikia. Sasa kama nilivyotanabaisha hapo awali, udhaifu wangu katika Fizikia na Hisabati ulimaanisha kuwa nisingeweza kuimudu Kemia ya High School.

Pili, shule yetu ilikuwa haina mwalimu ya Jiografia, na ilibidi tuwe tunakwenda shule ya jirani ya Tabora Girls' kuhudhuria vipindi vya somo hilo. Angalau Baiolojia haikuwa tatizo japo kiukweli ilihitaji uwezo mkubwa wa kukariri na kuelewa majina ya sampuli za viumbe ambayo mengi yana asili ya Kilatini au Kigiriki. Kwahiyo kwa kifupi, dhamira yangu ya kusoma combination ya CBG ilikufa kifo cha asili.

Hivyo nikaamua kusoma combination yenye masomo ya Historia, Jiografia na Kiingereza. Hii ilikuwa mteremko kwa kiasi kikubwa, lakini ndoto yangu ya kuwa daktari ndio ikayeyuka. Lakini wanasema kile unachotaka sio lazima ndio unachopata (what you wish for is not always what you get).

Sukuma miaka kadhaa baadaye, nikajiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam na hapo nikajikuta nina uchaguzi wa ama kuzamia kwenye sayansi za siasa na utawala wa umma (pilitical science and public administration au sosholijia, elimu inayohusu masuala yya jamii. Mwaka wa pili, nikafanya uamuzi wa kuchukua hiyo choice ya pili, yaani Sosholojia. Kwa hakika niliipenda sana sosholojia. Yaani ilinisaidia mno kuielewa jamii. Miongoni mwa masomo ya kupendeza sana yalikuwa lile lilifundisha kuhusu uhusiano wa jamii, utamaduni na afya; somo la jinsia na uhusiano wa kijinsia, na zaidi ya yote ni sosholojia ya dini ambapo pamoja na mambo mengine tulifundishwa kuhusu Ukristo, Uislamu na Imani za Asili. 

Sukuma miaka kadhaa zaidi mbele, nikapata skolashipu ya kuja hapa Uingereza kusoma Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (Politics and International Relations), mkazo ukiwa kwenye masuala ya usalama. Kwa vile skolashipu ni kama zawadi, mwanafunzi anakuwa hana uchaguzi. Nilitamani sana kuendelea na Sosholojia lakini sikupewa fursa ya kuchagua. Na hivyo ndivyo nilivyojikuta nikiingia kwenye stadi za siasa. Tuishie hapo/

Kwanini nimeelezea stori hiyo? Ni kwa sababu kama nilivyosema awali, ninaipenda siasa kama stadi. Yaani baada ya kutokuwa na choice ya kusoma sosholojia, na 'kulazimishwa' kusoma Siasa, ikabidi niipende tu. Niliipenda pia kwa sababu siasa za kimataifa zina 'raha' yake kuzielewa, ukichanganya na maeneo kama diplomasia, amani na 'ugomvi' (peace and conflicts) na masuala ya usalama wa kimataifa (international security).

Lakini tatizo la siasa kama stadi ni ukweli mchungu kwamba kile unachosoma darasani mara nyingi hakiakisi hali halisi mtaani. Siasa kama fani au stadi sio mbaya, ina mafunzo mengi, inafundisha miongozo mingi na kanuni nyingit muhimu kwa maisha ya mwandamu, lakini mtaani hali ni tofauti.  Sihitaji kuelezea kwa undani kwanini watu wengi wanaichukia siasa. Lakini mfano mwepesi ni kwenye kampeni za uchaguzi ambapo utasikia chama kikitanabaisha sera nzuri kabisa lakini baada ya kuingia madarakani kikaishia kufanya kinyume kabisa na kilichoyaahidi. Na kwa Tanzania yetu tuna mfano hai wa jinsi sera tamu za CCM zinavyoishia kuwanufaisha matajiri na mafisadi huku zikiwadidimiza walalahoi.

Na mfano mchungu zaidi, uliopelekea niandike makala hii, ni jinsi Chadema katika mwavuli wa UKAWA inavyoelekea kuwasaliti mamilioni ya Watanzania kwa uwezekano wa kumpokea fisadi Edward Lowassa kuwa mgombea wa urais.

Jana niliumia mno nilipoona picha kadhaa zinazomwonyesha Lowassa akiwa na viongozi wa UKAWA. Baadaye, mwenyekiti wa NCCR, moja ya vyama vinavyounda UKAWA pamoja na Chadema, CUF na NLD, alitamka bayana kuwa wanamkaribisha Lowassa kujiunga nao.

Lakini baadaye kidogo nikapata ahueni baada ya kupatikana taarifa zilizothibitishwa na akaunti ya Twitter ya Chadema Media kuwa picha zilizokuwa zinamwonyesha Lowassa na viongozi wa UKAWA ni feki, yaani zilikuwa photoshopped. Hata hivyo furaha hiyo haikudumu muda mrefu baada ya Mbatia na wenzake kutangaza bayana kuwa wanamkaribisha Lowassa . Na kuna uwezekano leo Jumanne, aidha UKAWA wakamtangaza Lowassa kuwa mgombea wao wa Urais au Lowassa mwenyewe akatangaza kujiunga nao.
Huu ni usaliti mkubwa mno hasa upande wa Chadema, chama kilichojidhihirisha kuwa kinauchukia ufisadi kwa dhati. Sote twakumbuka jinsi Chadema ilivyojipatia umaarufu kwa kupambana na ufisadi, hasa baada ya kutangaza hadharani 'orodha ya aibu' (list of shame) pale Mwembeyanga jijini Dar ambapo walitaja orodha ya mafisadi akiwemo Lowassa. Kadhalika Chadema ilifanya jitihada kubwa kuibua ufisadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na skandali ya Richmond iliyopelekea Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu. Vilevile chama hicho kilitufumbua macho kuhusu ufisadi wa EPA, Meremeta, Dowans, Buzwagi, TanGold, Kiwira, nk. Kwa kifupi, ilikuwa haiwezekani kuzungumzia mapambano ya  ufisadi Tanzania bila kuitaja Chadema.

Na katika harakati zake za kupambana na ufisadi, kuna Watanzania wenzetu waliopoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa vibaya na kuachiwa ulemavu kwa kukiunga mkono chama hicho. 


Na kwa kuonyesha kuwa Chadema ilikuwa mwarobaini kwa CCM na mafisadi kwa ujumla, chama hicho kilifanyiwa kila aina ya hujuma. Mara kiliitwa chama cha kidini, baadaye kikaitwa cha kikabila, na hadi hivi majuzi kiliitwa chama cha kigaidi. Lakini taratibu Watanzania walifumbuka macho na kubaini kuwa sababu kubwa ya CCM na serikali yake kuiandama Chadema ni kwa vile chama hicho cha upinzani kilichofanya vizuri tu katika uchaguzi mkuu uliopita kinasimamia maslahi ya wanyonge ilhali CCM inatetea mafisadi na ufisadi.
Japo mie binafsi sikuwa mwanachama wa Chadema, nilikiunga mkono kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi kulingana na msimamo wangu kwenye suala hilo. Nilikuwa nina imani kuwa laiti Chadema ikifanikiwa kuingia Ikulu basi kwa hakika safari ya kuipeleka Tanzania yetu mahali inapostahili kuwa inawezekana. 
Sasa hili la kumpokea Lowassa ni pigo kubwa mno na ni usaliti wa hali ya juu kabisa. Ndio, Lowassa anaweza kuwasaidia Chadema na UKAWA kuingia Ikulu. Lakini kwa kuangalia tu maswahiba wa Lowassa utaweza kujua tutakuwa na serikali ya aina gani. Sipati shida kubashiri kuwa tutaishia kuikumbuka CCM. 

Embedded image permalink

Na huo ndio ubaya wa siasa katika vitendo, tofauti na ilivyo nzuri na mwafaka katika stadi. Kwamba kistadi za siasa, Chadema ilijijenga na kupata umaarufu kwa kuzingatia kanuni ilizojiwekea na ikajitambulisha kama chama kilichopo kwa maslahi ya wanyonge, tofauti na CCM iliyokimbia kanuni zake na kuwakumbatia matajiri na mafisadi. Lakini ghafla bin vup, Chadema inaelekea kwenda kulekule ilipo CCM. 

Nimalizie makala hii kwa kuahidi kufanya uchambuzi wa kina kuhusu suala hili katika makala yangu ya wiki ijayo katika gazeti la Raia Mwema. Spoiler alert, wiki hii katika toleo litakalokuwa mtaani kesho ninamjadili Magufuli. 

Asanteni kwa kuchukua muda wenu kunisoma.

19 Jan 2012







Kwa nini Lowassa na mabilioni yake makanisani ahofie nguvu ya umma?

NIANZE makala hii kwa kuwasilisha salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Regia Mtema. Nilishitushwa sana nilipopata taarifa za kifo chake kupitia mtandao wa Twitter hasa kwa vile siku chache tu zilizopita nilisoma bandiko lake moja katika ukumbi wa majadiliano wa mtandao wa Jamii Forums.
Japo nilikuwa sifahamiani naye lakini nilijisikia faraja sana kuona “mwana wa pakaya” (mtoto wa nyumbani) mwenzangu anavyofanya sie wazaliwa wa Wilaya ya Kilombero tujisikie ufahari.
Moja ya mambo magumu kabisa maishani ni kusema maneno yanayojitosheleza kwa wafiwa. Lakini hiyo si sababu ya kutosema japo machache yanayoweza kuifariji familia ya marehemu Regia, wana Kilombero, viongozi na wanachama wa CHADEMA na Watanzania kwa ujumla.
Tulimpenda Regia lakini Mwenyezi Mungu alimpenda zaidi na kwa vile ndiye aliyemuumba basi ameamua kumchukua. Kwa waumini, tunachoweza kufanya ni kuiombea roho ya marehemu, na sote kwa ujumla tunaweza kumuenzi vizuri zaidi mbunge huyo shupavu kwa kutekeleza yale yote aliyosimamia na kupigania.
Pengine mwenye changamoto zaidi kutokana na kifo hiki cha ghafla ni Mbunge wa Jimbo la Kilombero kupitia CCM, Abdul Mteketa. Kuna mengi ambayo dada yetu Regia alikuwa akipigania kwa ajili ya ustawi wa Jimbo la Kilombero (sambamba na maeneo mengine nchini kutokana na ubunge wa viti maalumu kumfanya kuwa mithili ya ‘mbunge wa kila jimbo’).
Kama Rais Jakaya Kikwete alivyoonyesha mfano kwa kuweka pembeni itikadi za kisiasa wakati anatoa salamu za rambirambi za kifo cha mbunge huyo, Mteketa naye anaweza kuweka kando tofauti kati ya chama chake CCM na CHADEMA na kuendeleza yale yote yaliyoanzishwa na mbunge mwenzie (ambaye walipambana kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010).
Hiyo si tu itakuwa namna bora zaidi ya kuomboleza kifo hicho bali pia kuwasaidia wana-Kilombero ambao kwa hakika wamepoteza tunu na lulu muhimu kwa jimbo hilo.
Baada ya salamu hizo naomba kugeukia kauli ya hivi karibuni ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambaye alizungumzia kuhusu matumizi ya nguvu za umma kuishinikiza mambo mbalimbali.
Kasoro ya kwanza katika kauli hiyo ya Lowassa aliyoitoa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya sekondari ya kanisa la FCTP huko Bigabiro, mkoani Kigoma, ni kuyaeleza matumizi hayo ya nguvu za umma kuwa yanaendeshwa na baadhi ya vyama fulani. Japo hakutaja jina la chama lakini ni wazi alikuwa anailenga CHADEMA.
Kwa nini Lowassa hayuko sahihi katika hili? Hivi chama kisicho na dola kama CHADEMA kinawezaje kulazimisha utashi wa wananchi kushiriki kwenye harakati hizo? Kumshawishi mlalahoi akatishe siku yake shambani akahudhurie maandamano yanayokihusisha chama cha siasa ni suala gumu mara kadhaa ya urahisi alionao Lowassa kuwakusanya marafiki zake matajiri kumwaga fedha kwenye harambee zao.
Binafsi, ninaitafsiri kauli hiyo ya Lowassa kama dharau kubwa kwa wanyonge wanaolazimika kutumia nguvu ya sauti yao kudai stahili zao.
Hivi Lowassa anadhani wananchi wanaojitokeza kwenye maandamano au harakati nyingine kushinikiza masuala mbalimbali wanafanya hivyo kama anasa, hasa ikizingatiwa kuwa wanafahamu fika uwezekano wa kulala rumande kama si kufunguliwa mashtaka pindi Jeshi la Polisi likijisikia kuwanyanyasa?
Tunaweza kumhurumia Lowassa katika hili kwa vile sidhani kama ameshawahi kulazimika kutumia nguvu kudai haki yake. Yeye ni miongoni mwa kikundi kidogo cha wateule wachache ambao miaka nenda miaka rudi wapo madarakani, huku mahitaji yake yakishughulikiwa na wasaidizi wake.
Raha ya kuwa na wasaidizi, wapambe na watoa huduma ni kwamba kwa kiasi kikubwa jukumu la kuhakikisha kila jambo lipo sawa kwa ‘bosi’ linakuwa mikononi mwa watu hao.
Katika hotuba yake kwenye harambee hiyo Lowassa alikaririwa akidai (namnukuu) “Nguvu ya umma tunayoshuhudia kwenye maandamano ya baadhi ya vyama vyetu, ingekuwa inatumika kwa kiwango kile kile kufanya kazi za kujitolea kwenye miradi ya maendeleo kama ujenzi wa sekondari zetu, hakika taifa lingepiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini linapokuja suala la kufanya kazi nguvu ya umma hutoweka.”
Kwa lugha nyingine Lowassa anahitimisha kuwa mahala pekee ambapo nguvu ya umma inatumika ni kwenye maandamano ya baadhi ya vyama vyetu. Huyu ndiye ambaye licha ya kuwa Waziri Mkuu huko nyuma ameshika nafasi kadhaa za uongozi serikalini na ndani ya CCM kwa miaka kadhaa.
Je, ni kweli hajawahi kuona nguvu inayotumika na Watanzania kujiletea maendeleo yao licha ya kukwazwa na majambazi wanaotumia fursa zao kuwafisadi?
Moja ya mambo yanayotufanya Watanzania tuendelee kumlilia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni jinsi alivyotuunganisha bila kutumia dini au urafiki na matajiri kuhamasisha maendeleo ya jamii na nchi yetu kwa ujumla.
Nyerere alitambua umuhimu wa nguvu ya umma katika kuleta mabadiliko yanayokusudiwa hususan kukiwa na usimamizi mzuri usioambatana na maslahi binafsi.
Uhuru wetu kutoka kwa mkoloni ulipatikana kutokana na wanyonge wa Tanganyika kuchoshwa kunyanyaswa na kukandamizwa na wakoloni na kuunganisha nguvu zao wakihamasishwa na Nyerere na wapigania uhuru wenzie na hatimaye tukapata uhuru wetu. Leo hii Lowassa anabeza harakati zenye mwelekeo kama huo.
Historia imetuonyesha jinsi nguvu ya umma ilivyoweza kuangusha tawala mbalimbali za kidhalimu, mifano mizuri ikiwa ni huko Afrika Kusini walivyopambana na utawala wa makaburu na Ulaya ya Mashariki walivyokabiliana na udikteta wa kikomunisti.
Na hivi karibuni tumeshuhudia nguvu ya umma ikiwang’oa madikteta Hosni Mubarak wa Misri, Ben Ali wa Tunisia na Muammar Gaddafi wa Libya.
Lakini kwa kile kinachoweza kutafsiriwa kama unafiki wa Lowassa ni ukweli kwamba yeye alikuwa miongoni mwa waliopongeza nguvu za umma nchini Misri huku akishauri watawala wetu kujifunza katika kilichojiri nchini humo. Ikumbukwe kuwa harakati za Misri zililenga zaidi kuutokomeza utawala wa kidikteta wa Mubarak ilhali nguvu ya umma huko nyumbani imeelemea zaidi kwenye kudai haki za msingi sambamba na kukemea maovu, hususan ufisadi. Sijawahi kusikia kuwepo kwa maandamano yenye wito wa kumng’oa Rais Kikwete madarakani kwani kwa mujibu wa sheria zetu kufanya hivyo ni uhaini pasipo mjadala.
Lakini licha ya kupongeza nguvu za umma huko Misri, ingekuwa miujiza kwa Lowassa kuunga mkono harakati kama hizo huko nyumbani kwani yeye ni miongoni mwa waathirika wake. Nguvu ya umma ikihamasishwa na CHADEMA ilimtaja mwanasiasa huyo kwenye orodha ya mafisadi (list of shame) na hadi leo hajachukua hatua za kisheria kudai amekashifiwa.
Tukiweka kando kauli hiyo ya Lowassa, labda tujiulize kidogo kuhusu hayo mamilioni yanayochangwa na marafiki zake kwenye hafla mbalimbali makanisani. Hivi Watanzania wenzetu hao wenye uwezo wa kutoa sadaka za mamilioni wanatoa wapi fedha hizo?
Na katika hili ninayalaumu sana makanisa yanayoweka mbele fedha pasipo kujiuliza fedha hizo zinazomwagwa kwao zinatoka wapi.
Wakati wa uhai wake, Baba wa Taifa alionyesha upinzani mkubwa kwa wanasiasa wenye utajiri wa kupindukia lakini usio na maelezo ya kutosheleza. Ifahamike kuwa utajiri si dhambi iwapo umepatikana kihalali.
Lakini kila mwenye uelewa anaweza kupatwa na wasiwasi kuona mwanasiasa mmoja akizunguka huku na kule kumwaga mamilioni ya shilingi makanisani. Huyu mtu ana fedha kiasi gani? Amepata wapi?
Jingine ambalo pengine ni muhimu zaidi kwa Watanzania hasa wakati tunaelekea kwenye mchakato wa Uchaguzi ujao mwaka 2015 ni hadhari iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuhusu wanasiasa wanaotumia nyumba za ibada kujisafisha.
Waziri Membe alisema amani ya taifa imo shakani kama viongozi wa kidini wataruhusu nyumba za ibada kuwa kimbilio la wanasiasa na wao kutumika katika kuwasafisha, hali hiyo inaweza kusababisha mgawanyiko katika jamii.
Lowassa kama muumini yeyote yule ana uhuru wa kutoa michango ya fedha nyingi na marafiki zake matajiri. Kadhalika, ni haki yake ya kikatiba kuongea lolote lile alimradi havunji sheria za nchi. Sasa kama yeye ana uhuru wa kumwaga mamilioni makanisani na kukemea walalahoi wanaotumia nguvu ya umma kushinikiza mambo mbalimbali, kwa nini basi asitambue kuwa walalahoi hao wanaotumia haki hiyo hiyo anayotumia yeye?
Wanasema uhuru bila nidhamu ni uhuni, na kwa msingi huo japo ninatambua uhuru alionao Lowassa kuzungumzia masuala ya kisiasa kwenye nyumba za ibada, uhuru huo unaweza kuwa na madhara makubwa katika taifa letu. Kama walalahoi anaowakemea Lowassa ni werevu na wanafanya harakati zao nje ya nyumba za ibada basi ni vema wanasiasa wetu nao wakaepuka kugeuza sehemu hizo takatifu kuwa majukwaa ya kisiasa.
Nimalizie kwa nukuu hii kutoka kwa Waziri Membe; “Kuweni macho na wanasiasa wanaokimbilia kwenu (viongozi wa dini), msikubali kutumiwa kwa kulinda maslahi ya wanasiasa, fanyeni kazi zenu za kuwajenga waumini wenu kwa mujibu wa mafundisho ya imani zenu, mkiruhusu kutumiwa na wanasiasa amani ya nchi mtaivuruga.”


8 Jun 2011






Mafisadi CCM wageuka mbogo

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 June 2011

SASA ni piga ni kupige ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wanakataa kujiuzulu, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema walipoitwa mbele ya viongozi wakuu wa chama hicho – makamu mwenyekiti Pius Msekwa na katibu mkuu, Wilson Mukama - wanaoitwa na CCM kuwa “watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini,” walishikilia msimamo kuwa hawawezi kujiuzulu kwa kuwa hawana hatia.

Wanaotakiwa kujiuzulu na viongozi wakuu wa CCM ni Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge. Mkutano wa kuwashawishi wajiuzulu, ulifanyika Alhamisi na Ijumaa wiki iliyopita katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba, Dar es Salaam.
Taarifa zinasema katika mkutano huo, Msekwa na Mukama waliomba Lowasa ajiuzulu ili kukiokoa chama hicho, lakini yeye alipinga kwa hoja kuwa hana hatia.

MwanaHALISI lilipowasiliana na Msekwa kutaka kufahamu kilichojadiliwa katika mkutano wake na viongozi hao, haraka alisema, “…Umetoa wapi habari hizo?”

Alipoelewa ni vyanzo vya ndani ya chama na serikali, Msekwa alisema, “Hayo ni mambo ya ndani ya chama. Hatuwezi kuyaleta magazetini.”
Lowassa alipoulizwa juu ya kuwapo kwa kikao hicho, alisema ni kweli wamekutana. Hata hivyo, alisema hawezi kueleza walichojadili kwenye vyombo vya habari.

Rostam hakupatikana kueleza upande wake. Hata hivyo, MwanaHALISI limeelezwa na mtoa taarifa wake kuwa mbunge huyo wa Ingunga alitoka kwenye ukumbi wa mkutano akiwa amenuna na kuvurumisha “maneno makali.”

Anasema Rostam alitoka pale akiwa amenuna na kusema yeye hana hatia yoyote na kwa hiyo hastahili kushambuliwa. Amesema yote yanayotokea sasa yanatokana na uadui wa siasa za urais wa mwaka 2005 na ule wa 2015.


Hili linatokea wakati uongozi wa juu wa chama hicho ukishindwa kukabidhi barua ya kuwataka watuhumiwa hao wajiuzulu.
Kuchelewa kwa utekelezaji wa maazimio ya kuwawajibisha Lowassa, Rostam na Chenge kumezaa majungu na umbeya. Hivi sasa taarifa zinasema, Mukama anadaiwa kugoma kuandika barua ya kuwataka watuhumiwa hao kuachia nafasi zao za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) wanazozishikilia.

Baada ya Mukama kugoma kuandika barua hizo kwa hoja kuwa kilichoamuriwa na NEC hakifahamu kwa kuwa alikuwa hajateuliwa, ndipo Nape Nnauye, katibu wa itikadi na uenezi alipoandika barua hizo na kuzipeleka kwa Msekwa.

Naye Msekwa alizipokea barua na kuzirekebisha. Akazirejesha kwa Nape ili azipeleke kwa Mukama kuzisaini. Mukama akagoma. Zikapelekwa kwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, ambaye taarifa zinasema, “amezifungia kabatini.”

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya kikao hicho, Lowassa alifika Lumumba saa nne asubuhi. Mazungumzo kati yake, Msekwa na Mukama inakadiriwa yalichukua takribani saa moja.

Katika mazungumzo hayo, Msekwa ananukuliwa akimweleza Lowassa “unatakiwa ujiuzulu nyadhifa zako za uongozi katika chama ili kutekeleza maagizo ya NEC na falsafa ya chama ya kujivua gamba.”

Akijibu hoja hiyo, mtoa taarifa anasema Lowassa alijibu, “Kuhusu Richmond (kampuni feki ya kufua umeme wa dahurula), ukweli unafahamika…Katika hili, mimi sina makosa. Rais anafahamu hilo na kila mmoja anajua hivyo.”

Anasema Lowassa alisema kama kuwajibika kwa makosa yaliyotokana na Richmond tayari amefanya hivyo kwa niaba ya chama chake na serikali pale alipoamua kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu.
Anasema mbali na kueleza hilo, Lowassa alisikika akisema, “nilikutana na Rais Kikwete. Aliyonieleza si haya.”

Alisema Rais Kikwete alimweleza kuwa hakuna maazimio yoyote ya NEC yaliyomtaka kujiuzulu. Akahoji, “Sasa nimwamini nani, ninyi mnaotaka nijiuzulu au rais aliyesema hakuna azimio kama hilo?”

Habari zinasema mara baada ya Lowassa kuwaeleza viongozi wake msimamo juu ya mazungumzo yake na Kikwete, ndipo Msekwa aliposikika akisema, “Lowassa acha mbio za urais.”

Naye Lowassa hakumkawiza Msekwa. Alijibu, “Lini nimetangaza kugombea urais? Lakini hata kama ninataka kufanya hivyo, ni haramu kugombea nafasi hiyo? Je, kuna mliowaandaa?”

Ni kauli hiyo ya Lowassa, iliyomshutua Msekwa na kusema, “Hapana. Hapana. Hakuna tuliyemuandaa…Haya mambo ya urais yatatuvuruga.”
Akihitimisha hoja zake kabla ya kumalizika kwa mkutano huo, mtoa taarifa anasema Lowassa alikitaka chama chake kuisaidia serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi, badala ya kufanyia kazi kile alichoita, “majungu ya wanasiasa.”

Naye Chenge taarifa zinasema aliwaambia viongozi aliokutana nao kuwa yeye si fisadi na hafahamu maana ya ufisadi. Akataka kama tuhuma wanazomtuhumu wanaweza kuzithibitisha wamfikishe mahakamani ili aweze kujitetea. Hakuna maelezo ya ziada.

Hata hivyo, watu waliokaribu na kiongozi huyo wanasema, Chenge amejipanga kuhakisha kwamba hang’oki katika kiti chake cha NEC; ikibidi kuondolewa kwa nguvu ametishia kuondoka CCM na kujiunga na upinzani.

Kwa upande wa Rostam Aziz, taarifa zinasema alitakiwa kujiuzulu ujumbe wa NEC kwa tuhuma za kuingiza nchini kampuni feki ya Richmond na baadaye Dowans.

Mtoa taarifa anasema, mara baada ya kuelezwa tuhuma hizo, Rostam alihoji, “Haya ni maamuzi ya NEC?” Naye Msekwa akajibu, “NEC imetaka chama kijivue gamba kuanzia ngazi ya taifa hadi chini kwa kuondoa watu wote wanaotuhumiwa ufisadi.”

Habari zinasema, katika mazungumzo kati ya viongozi hao na Rostam, hakuna mahali popote ambapo Msekwa na Mukama walitaja ushiriki wa mbunge huyo wa Igunga, katika wizi wa fedha za umma kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Kampuni ya Kagoda ni miongoni mwa makampuni 22 yaliyothibitika kuchota mabilioni ya shilingi kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Gazeti hili limeshindwa kufahamu mara moja kilichosababisha Msekwa na wenzake kushindwa kumweleza Rostam ushiriki wake katika Kagoda. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka minne sasa, CCM imekuwa ikituhumiwa kunufaika na fedha za EPA hasa Sh. 40 bilioni zilizoibwa na Kagoda.

Wakati suala hilo likichukua sura hiyo, taarifa zilizofikia gazeti hili zinasema baadhi ya vigogo wa chama hicho wamepanga kupeleka hoja katika vikao vijavyo vya (CC) na (NEC) kushinikiza kufukuzwa ndani ya chama hicho wanaoitwa, “wasaliti ndani ya chama.”

Wanaopangiwa mkakati wa kufukuzwa ni spika wa zamani wa Bunge, Samwel Sitta na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe wanaotuhumiwa kuanzisha Chama cha Jamii (CCJ) wakati wakiwa bado wanachama na viongozi wa CCM.

Wengine ni Nape Nnauye, Victor Mwambalaswa na Daniel Porokwa.
Habari kutoka ndani ya CCM zinawanukuu makada mawili; rais mstaafu, na mjumbe mmoja wa NEC wakitaka chama chao kuwafukuza waasisi wa CCJ kwa kukosa uaminifu.

MwanaHALISI limeelezwa na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa CCJ, Dickson Ng’hily kwamba Sitta na Mwakyembe waliokuwa waanzilishi wa chama hicho, walimkatiza masomo yake nchini Afrika Kusini ili kusaidia kupatikana usajili wa chama hicho.

Ng’hily ambaye mahojiano yake yatachapishwa kikamilifu katika toleo lijalo amesema, aliyemwingiza yeye CCJ ni Sitta na Dk. Mwakyembe na anasikitishwa na hatua ya viongozi hao kutaka kuficha ukweli.

“Hawa watu ndio waanzilishi hasa wa CCJ. Mimi na Makonda tulipewa jukumu la kutafuta usajili wa chama. Lakini naona wenzangu wameamua kuficha ukweli kwa maslahi binafsi. Hii si sahihi,” ameeleza.

Ng’hily anaonyesha nyaraka za muhtasari wa vikao walivyoshiriki viongozi wakuu wa CHADEMA, John Mnyika, Anthony Komu na Tundu Lissu kuwa ni miongoni mwa watu walioshiriki katika majadiliano ya kuunganisha nguvu kati ya CCJ ya Sitta na CHADEMA.

“Tulikubaliana kama CCJ itakosa usajili, basi mheshimiwa Sitta atagombvea urais kupitia CHADEMA. Lakini kama tutafanikiwa kusajili chama chetu, basi Sitta angegombea urais kupitia CCJ na CHADEMA wangetuunga mkono,” anaeleza Ng’hily.

Kuibuka kwa Ng’hily kuelezea ushiriki wa Sitta na Dk. Mwakyembe katika kuanzisha na kusimamia usajili wa CCJ kumekuja wiki tatu baada ya Fred Mpendazoe kumtaja Nape Nnauye kuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa kwanza wa CCJ.

Mpendazoe aliuambia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Njombe kuwa yeye, Sitta na Mwakyembe ndio walianzisha CCJ; bali yeye alitangulia kutoka CCM ili kurahisisha usajili wa chama hicho. Wenzake walikuwa wamfuate baadaye.

CHANZO: Mwanahalisi

16 Feb 2010


Pamoja na kuwa moja ya nchi maskini kabisa duniani, Tanzania yetu bado inaendelea kusifika kwa mambo kadhaa. Ukiachia mbali vivutio vya asili kama Mlima Kilimanjaro, utitiri wa wanyama huko Selous, Mikumi na kwingineko, na “utajiri” wa madini kama Tanzanite,dhahabu, almasi na madini mengineyo,nchi yetu pia inasifika kwa watu wenye uwezo wa kuongea.

Ndio maana jirani zetu wanapenda kututania kuwa “nyie Watanzania iko maneno mingi” wakimaanisha tunaongea sana. Na pengine mahala mwafaka pa kuthibitisha uwezo wetu wa kuongea ni katika vikao vya bunge letu tukufu. Laiti yote yanayoongewa katika vikao hivyo yangekuwa yanatafsiriwa kwa vitendo, basi kwa hakika tungekuwa mbali sana.

Lakini licha ya sifa hiyo ya kuongea sana, Watanzania tuna sifa nyingine ya usikivu na kuamini kirahisi kila tusikiacho hata kama ni “wizi mtupu”. Ndio maana basi watu wenye akili na busara zao walidanganyika kwamba miongoni mwa wabunge wa CCM kuna kundi la WAPIGANAJI DHIDI YA UFISADI.Kundi hilo lililojipatia umaarufu usiostahili linadaiwa kuwa chini ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

Na kwa katika kile kinachoweza kutafsiriwa kwamba ni jitihada za kujiongezea sifa za “upambanaji” , Spika Sitta na wabunge wawili kutoka vyama vya upinzani,Dr Wilbroad Slaa (Chadema) na John Cheyo (UDP) walichapisha kitabu walichokipa jina “BUNGE LENYE MENO”. Si lengo la makala haya kurejea yaliyomo katika kitabu hicho, lakini kwa kifupi ni mwendelezo wa sifa tulizonazo Watanzania: maneno meeeengi lakini vitendo SIFURI.

Sijui Sitta wa “wapiganaji” wenzie walikuwa na mawazo gani kurefusha mjadala wa ujambazi wa Richmond kwa takriban miaka miwili lakini tukashuhudia wakilamba matapishi yao walipounga mkono kile kinachoitwa “utekelezaji wa serikali wa maazimio ya bunge kuhusu suala la Richmond”.Kwanini hawakuiunga mono serikali tangu siku ya kwanza badala ya kuwazuga Watanzania kwa muda wote huu?

Binafsi siamini kabisa kuwa Spika Sitta ni mpambanaji dhidi ya ufisadi.Ni usanii tu ambao unaelekea kuwa moja ya sifa muhimu za wanasiasa wetu.Sitta atakuwaje kamanda wa vita dhidi ya ufisadi ilhali ndiye aliyemfungia Zitto Kabwe alipohoji ufisadi wa Buzwagi?Je sio Sitta huyohuyo aliyetishia kumpeleka Dr Slaa kwenye vyombo vya sheria pale (Slaa) alipoibua ufisadi wa EPA?

Spika Sitta,akisaidiwa na vyombo vyetu vya habari vinavyosifika kwa umahiri wa kukariri kikasuku kila kinachosemwa na wanasiasa (badala ya kwenda mbali zaidi na kuchambua kauli hizo), alitambua vema kuwa Watanzania wengi wanahitaji wanasiasa watakaoungana nao kupambana na ufisadi.Kwa lugha nyingine,alifahamu fika kuwa mapambano dhidi ya ufisadi ni mtaji maridhawa kisiasa na ungeweza kuimarisha nafasi yake.

Na kwa vile anafahamu kuwa Watanzania ni wasikivu sana hata kama wanadanganywa,akawa anapita huku na kule akijigamba kwamba “kamwe hatatishwa na wanaomwandama kisiasa kutokana na msimamo wake thabiti wa kupiga vita ufisadi”. Sitta, na wasanii wenzake waliotuhadaa kuwa ni “wapiganaji dhidi ya ufisadi” walibinafsisha ajenda ya vita dhidi ya ufisadi kiasi kwamba “kila aliyeonyesha dalili ya kutamani MAJIMBO YAO alionekana anasukumwa na umahiri ya akina Sitta katika kupambana na ufisadi”.Yaani hawakubinafisha tu hoja ya ufisadi bali wamegeuza majimbo yao kuwa mali zao za urithi ambazo hazipaswi kuguswa na Mtanzani mwengine yeyote yule.

Na Sitta anadai atawania tena kiti cha Uspika katika bunge lijalo.Kuna dalili kuwa anaweza kurejea bungeni kwa vile ametumia vema nafasi yake ya uspika kujiimariusha jimboni kwake Urambo.Lakini kama bunge lijalo litakuwa na wabunge wanaowajali wapiga kura wao basi ni dhahiri Sitta atabaki kuwa historia tu.Hatastahili hata unaibu Spika,pamoja na naibu wake wa sasa Anne Makinda,viumbe wawili waliotumia vibaya sana madaraka yao na kuendesha taasisi hiyo kwa utashi wao huku wakitumia kanuni zilizopitwa na wakati kuwaokoa mawaziri wazembe walioshindwa kutoa majibu sahihi kwenye mijadala bungeni.

“Wapiganaji feki wa ufisadi” wametuchezea shere.Upande mmoja wao ni sehemu ya mfumo wa kifisadi unaoshamiri kwa kulindana,na hawana jeuri ya kujitenga nao kwa vile ni wabinafsi.Lakini kwa upande mwingine wanataka tuwaone wao ni wenzetu,wanaguswa na matatizo yetu na wana uchungu wa dhati na nchi yetu.Wasanii hawa wanatuona sie wajinga tusiojua kuwa mishahara yao minono ni ushahidi tosha kuwa wanaishi dunia nyingine kulinganisha na walimu,madaktari,manesi,wakulima na walalahoi wengine.Wanarefusha vikao vya bunge ili posho zao nonoi ziendelee kutunisha akaunti zao.

Spika Sitta na wasanii wengine waliotudanganya kuwa wao ni wapiganaji dhidi ya ufisadi hawana sababu hata moja ya kuwaacha majambazi wa Richmond wakisafishwa na pasipo kuchukuliwa hatua yoyote.Kuna baadhi yetu tulikuwa tukifahamu tangu mwanzo kuwa hakutakuwa na hatua yoyote dhidi ya Lowassa,Karamagi,Msabaha,Mwanyika ,Hoseah na wengineo waliohishwa na ufisadi huo.Tulifahamu hivyo kwa vile kimsingi,ufisadi huo-kama ilivyo kwenye ishu za EPA,Kiwira,na kwingineko-ni matokeo ya ushirika wa kijambazi uliobuniwa na kufanikishwa kwenye korido za utawala za CCM.Kuwachukulia hatua watuhumiwa hawa kungeweza kabisa kupelekea vigogo wengine kuadhiriwa hadharani.

Hiyo haimaanishi kuwa kuadhirishwa kwa vigogo hao ni kosa,bali ni muhimu kwetu kuelewa kuwa mtandao huu wa kifisadi uliundwa kwa madhumuni ambayo mpaka sasa bado yana umuhimu kwa wahusika.Kwa lugha nyepesi.mfumo wa kifisadi ni matokeo ya moja kwa moja ya kundi la WANAMTANDAO.Na kama walivyoshirikiana kuingizana madarakani,wanaendelea kulindana ili Mtandao huu uendelee kututawala.

Na Watanzania tuna sifa nyingine ya ziada:UPOLE. Ungetarajia kusikia wananchi wakiandamana kupinga majambazi wa Richmond “kuachiwa huru na Bunge” huku wakihakikishiwa kuwa “kuna siku watarejea madarakani”. Yaani tumetapeliwa,tukachezewa akili kwa zaidi ya miaka miwili na sasa tunashuhudia majambazi wakisafishwa bungeni lakini hakuna tumetulia kana kwamba Katiba inatuelekeza tufanye hivyo!Ama kweli hiyo ndio amani na utulivu-sio kwako na kwangu bali AMANI KWA WANAOTAFUNA NCHI YETU NA UTULIVU KWA AKAUNTI ZAO ZILIZESHEHENI MAMILIONI YA FEDHA ZA KIFISADI.

Habari njema kwa mafisadi ni dalili kuwa wengi wao watarejea tena madarakani baada ya uchaguzi mkuu hapo Oktoba.Na habari njema zaidi kwao,ni kuwepo kwa kila ishara kuwa chama kinacholea ufisadi,CCM,kitaunda serikali ya awamu ya tano huku kikilindwa na idadi kubwa ya wabunge.Japo baadhi yetu tungependa kuona mabadiliko lakini ni muhimu kwetu kuwa wakweli kwa nafsi zetu.Hakuna dalili ya CCM kushindwa uchaguzi mkuu ujao kwa vile mazingira yaliyopo yanakwaza mabadiliko ya aina yoyote ile.

Hata hivyo,kama wewe Mtanzania umechoshwa na ufisadi,kulindana,ahadi hewa na ubabaishaji mwingine,una nafasi ya pekee ya kutimiza hasira zako kwa kuinyima kura CCM.Vinginevyo,hali sio tu itaendelea kuwa mbaya bali tunaweza kufika mahala watu wakalazimisha mabadiliko yatakayopelekea kutuathiri sote.Ni muhimu kwako mpiga kura kujisuta kwa makosa uliyofanya 2005 na huko nyuma,lakini kufanya kosa si kosa bali kurejea kosa.Ni mwaka huu au ndio tumeumia milele.Timiza wajibu wako.


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.