Showing posts with label LOWASSA. Show all posts
Showing posts with label LOWASSA. Show all posts

16 Apr 2009

Mke wa Lowassa azindua kitabu

Na Mwandishi Wetu,
MTANZANIA, Aprili 15, 2009.

Watu mbali mbali jana jioni walimiminika nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kushuhudia uzinduzi wa kitabu kilichotungwa na mkewe Regina, uliofanywa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Regina aliandika kitabu hicho wakati akiwa katika matembezi binafsi inchini Israel, siku chache baada ya mumewe kujiuzulu uwaziri mkuu Februari mwaka jana kutokana na sakata la Richmond.

Kitabu hicho kilichoandikwa kwa lugha ya Kiingereza kiitwacho “Walk The Path With Diary in Israel, The Holy Land” kina kurasa 15 na dibaji yake imeandikwa na Monsinyori Julian Kangalawe kutoka Kanisa la Mtakatifu Joseph la Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Kardinali Pengo, bila kufafanua, aliwataka Watanzania waache tabia ya kusulubiana. “Yesu alikuja duniani, akasulubiwa na hadi leo watu wanaendelea kusulubiana. Tuache mchezo huo,” alisema.

Mhubiri maarufu mwenye makazi yake mjini Arusha, Christopher Mwakasege, ambaye pia alihudhuria hafla hiyo, alisema ni yeye aliyetoa wazo kwa Lowassa na mkewe kutembelea Israel baada ya matatizo yaliyowakuta.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa, ambaye pia alihudhuria hafla hiyo, aliwahimiza watu kujenga moyo wa kupendana ili kujenga nchi yenye maelewano.

Mbali na Mlasasusa, Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ni Pwani, Elinaza Sendoro, pia alihudhuria hafla hiyo, na akatumia nafasi hiyo kuwashawishi watu kutembelea Israel kujionea namna watu wa dini tofauti wanavyoishi.

Akizunmgumza katika hafla hiyo, Lowassa mwenyewe alisema baada ya kupata matatizo nayo, yeye na familia yake waliamua kumgeukia Mungu na kwamba ndio maana wakaamua kwenda Israel kutembelea maeneo takatifu.

LET'S BE HONEST.LOWASSA ALIJIUZULU KUTOKANA NA UFISADI WA RICHMOND.HILO HALINA MJADALA.SINA TATIZO NA HIYO ZIARA YAKE YA KUTEMBELEA ISRAEL.KAMA KWELI ALIENDA KUTUBU AU LA,ANAJUA YEYE NA MUNGU WAKE .LAKINI NASHINDWA KUWAELEWA HAO MAASKOFU WALIOJITOKEZA KATIKA SHUGHULI HIYO.NAELEWA KUWA DINI INAHUBIRI UPENDO NA KUSAMEHE WAKOSAJI LAKINI SIDHANI KAMA HIYO INAMAANISHA VIONGOZI WA DINI KUWA KARIBU NA WATUHUMIWA WA UFISADI.
NA MHASHAMU PENGO ANAPOTOA MFANO WA YESU KUSULUBIWA ANATAKA KUTUELEZA NINI?KWAMBA LOWASSA NAE ALISULUBIWA KAMA YESU?HIVI SIO RICHMOND NA BINAMU YAKE DOWANS ILIYOWASULUBU WALALAHOI WA TANZANIA KWA MAMILIONI YA SHILINGI!YESU ALISULUBIWA MSALABANI ILI KUWANUSUBURU WANYONGE,MASIKINI,WAJANE,YATIMA,NK KUTOKA KWA MINYORORO WANAYOFUNGWA NA MAFISADI.

JAPO NINA HESHIMA KUBWA KWA VIONGOZI HAO WA DINI LAKINI YAYUMKINIKA KUELEZA KWAMBA UHUDHURIAJI WAO HUO KATIKA HAFLA YA MTUHUMIWA WA UFISADI UNAWEZA KUTAFSIRIWA NA WAUMINI WAO KUWA NAO WANASAPOTI UFISADI.
IN A WIDER CONTEXT,UFISADI NI MATOKEO YA KUMOMONYOKA KWA MAADILI YA KIROHO.KITACHOTUPA IMANI KUWA WATUHUMIWA WA UFISADI WAMEAMUA KUMREJEA MUNGU SIO PUBLICITY STUNTS BALI FIRM COMMITMENT KATIKA KUHURUMIA NAFSI NA ROHO ZINAZOANGAMIA KUTOKANA NA MATENDO YA MAFISADI HAO.

2 Mar 2008

MTANZANIA UGHAIBUNI

Sakata la mkataba wa Kampuni ya Richmond linaelekea kuchukua mwelekeo mpya kila kukicha. Ni rahisi kutafsiri kwamba suala hili lisipopatiwa ufumbuzi wa kudumu linaweza kuwa na madhara makubwa kwa nchi na kwa chama tawala, CCM.

Tangu ripoti ya “Tume ya Mwakyembe” ilipowekwa hadharani katika kikao kilichopita cha Bunge la Jamhuri ya Muungano, kumejitokeza kauli kadhaa za utatanishi ambazo japo zinaweza kuwa ni za kawaida tu, tafsiri ya ndani inaashiria matatizo makubwa huko tuendako.

Naomba niwe muwazi zaidi katika makala hii, na ningependa kutamka bayana kwamba sina nia ya kumshushia heshima yeyote nitakayemtaja. Lengo kuu la makala hii ni kuikumbusha kila pande inayoguswa na sakata hilo kutambua kwamba taifa letu ni muhimu zaidi kuliko maslahi ya mtu mmoja.

Naikumbuka sana siku taifa lilipotangaziwa kifo cha Baba wa Taifa.Watanzania wengi walitokwa na machozi sio tu kwa vile hawangemwona tena Mwalimu bali pia ni ile hali ya kutokuwa na uhakika taifa letu lingekuwaje bila Nyerere.Naamini kwamba laiti Mwalimu angekuwepo, baadhi ya upuuzi kama huo wa mkataba wa Richmond wala usingetokea, lakini ndio hivyo tena, hatuko naye duniani.

Wanaoilaumu “Tume ya Mwakyembe” kuwa imewaonea wanasahau kwamba tume hiyo haikuundwa baada ya Mwakyembe na wenzake kutuma maombi ya kuwa kwenye tume hiyo.Inashangaza wanaolalamika sasa kwamba ripoti ya tume hiyo ilikuwa na ajenda za kumalizana kisiasa,ilhali hawakuipinga wakati inaundwa na pale ilipokuwa ikitimiza majukumu yake.Ina maana ajenda hizo za kisiasa zilianza baada ya akina Mwakyembe kuwa wajumbe wa tume au zilikuwapo kabla.Kama zilikuwapo kabla,kwanini basi waliotajwa kuhusika na kuliingiza taifa katika hasara kubwa kwa mkataba huo wa kizembe hawakulalamika?

Na iwapo ajenda hizo zilianza baada baada ya wajumbe hao kuingia kwenye tume,kwanini basi watajwa walikimbilia kujiuzulu (huku wengine wakigoma waziwazi kujiuzulu kwa kuendelea kung’ang’ania madaraka) badala ya kudai haki itendeke?Ni rahisi kuhitimisha kuwa kelele zinazoendelea hivi sasa ni za mfa maji.

Nakumbuka kwenye miaka ya tisini nilipokuwa mwanafunzi wa sekondari ya wavulana ya Tabora (Tabora Boys) tulibahatika kutembelewa na Komandoo Salmin Amour.Nayakumbuka baadhi ya maneno yake ambayo kimsingi yalikuwa na lengo la kutupa changamoto ya mafanikio ya kielimu na hatimaye kufanikiwa maishani (japo sio kila mara kufanikiwa kielimu ni tiketi ya moja kwa moja ya kufanikiwa kimaisha).Alitueleza kwamba madaraka ni mazuri na kutupa mifano ya namna yeye kama rais alivyokuwa na wasaidizi kibao wa kuhakikisha kila kitu kinakwenda vema.

Nilikubaliana na Komando wakati huo,na nakubaliana nae sasa,kwamba madaraka ni mazuri na matamu,na ndio maana tunashuhudia hizi kelele zinazoendelea kutoka kwa waliokumbwa na zahma ya kisiasa baada ya skandali ya mkataba wa kampeni ya Richmond.Hakuna dhambi kwa madaraka kuwa matamu kwani hata njia ya kuyafikia sio nyepesi.Inahitaji jitihada na juhudi za kutosha kufikia hatua ya kuongoza watu wenye akili timamu.Na inatarajiwa kwamba mtu akishapata bahati ya kuwa kiongozi atatambua kwamba wengi,kama sio wote,wa aliokuwa akiwaongoza ni watu wenye akili timamu,uwezo wa kufanya maamuzi na wanaostahili heshima.

Waziri Mkuu aliyepita,Edward Lowassa,ameendelea kuonyesha kwamba japo aliamua kubwaga manyanga kwa hiari yake,alifanya hivyo huku roho ikimuuma.Nasema hivyo kwa sababu kauli zake za hivi karibuni zinaashiria wazi kwamba bado ana kinyongo kikubwa na matokeo ya uchunguzi wa “Tume ya Mwakyembe.”

Lowassa anaamini kwamba atarejea tena kwenye ulingo wa juu wa kisiasa kama Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye alipokuwa Waziri alilazimika kujiuzulu kutokana na skandali iliyoikumba Wizara yake.Tofauti ya msingi kati ya Mwinyi na Lowassa ni ukweli kwamba wakati Mwinyi alijiuzulu kutokana na tukio lililotokea mbali kabisa na mahala alipokuwa akifanyia kazi (lilitokea Shinyanga wakati ofisi ya Mwinyi ilikuwa Dar es Salaam),Lowassa alijikuta akikumbwa na shutuma kuhusu mkataba huo kwa vile katika hatua flani ulipita machoni mwake na akaamua “kusikiliza maamuzi ya wataalamu.”

Uongozi ni pamoja na kuwa na maamuzi ya haraka na yanayoangalia athari zinazoweza kujitokeza mbeleni iwapo yatafanyika maamuzi potofu.Haiyumkiniki kwamba Waziri Mkuu mzima anaweza kusikiliza ushauri mbovu na kuafikiana nao pasipo kujiridhisha iwapo ushauri huo ni wa manufaa kwa taifa.Hilo pekee linamvua sifa ya uongozi mtu yeyote aliye katika nafasi ya juu kitaifa.

Hivi kama mkataba wa Richmond ungekuwa na madhara ya moja kwa moja kwa familia ya Lowassa,kiongozi huyo angeendelea kusikiliza ushauri asio na uhakika na matokeo yake au angetaka kujiridhisha kwamba kilichokuwa kikifanyika hakingekuwa na madhara kwa familia yake?

Tukimweka kando Lowassa kwa muda,tumeshuhudia vituko vingine kutoka kwa Mkurugenzi wa TIC Emmanuel Ole Naiko ambaye anadai kuna dalili za “mauaji ya halaiki” dhidi ya watu wenye asili ya wilaya ya Monduli.Hizi ni hoja mufilisi ambazo kama zitaachwa bila kudhibitiwa zinaweza kuliingiza taifa kwenye matatizo yasiyo na msingi.


Hivi Ole Naiko amefanya utafiti wa kutosha kiasi gani kuthibitisha kwamba kuna mpango wa “ethnic cleansing” dhidi ya watu wa Monduli?Kwa hakika serikali inapswa kumhoji kwa undani mtu huyu mwenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi kutokana na matamshi hayo ambayo yanaweza kabisa kuathiri hata utendaji wa ofisi yake (hakuna mwekezaji aliye tayari kuwekeza kwenye nchi inayoelekea kwenye “ethnic cleansing.”)

Kuna tetesi kwamba upo mkakati mkubwa wa “kujibu mashambulizi” dhidi ya ripoti ya “Tume ya Mwakyembe.” CCM imekuwa ikituaminisha kila siku kwamba vikao nje ya chama ni majungu,sasa basi inapaswa kuhakikisha kwamba wote wenye kudhani hawakutendewa haki wawasilishe malalamiko yao kwa ngazi hsuika katika chama hicho au hata bungeni.

Kama taarifa tunazozisoma katika vyanzo mbalimbali kwamba kuna mgawanyiko mkubwa ndani ya CCM kutokana na skandali la Richmond zina ukweli, basi ni muhimu kwa uongozi wa juu wa chama hicho kuachana na itifaki zake za kawaida za kuwasifia hata wanaostahili kukemewa na badala yake kuwawekwa “kiti moto” waeleze malalamiko yao mbele ya vikao halali badala ya kuendeleza mbinu za chini chini ambazo zinaweza kabisa kuathiri hali ya usalama wa nchi yetu.

Tusirejee makosa yaliyojitokeza katika mkataba wa Richmond ambapo baadhi ya watu walitahadharisha mapema kuhusu uhalali wa kampuni hiyo lakini wakapuuzwa.Kuna watu wanataka urais kwa kutimia njia yoyote ile hata kama kwa kufanya hivyo wanahatarisha uhai wa chama.

Lakini wakati tunawalaumu wanaolalamika kwamba wameonewa na “Tume ya Mwakyembe” tunapaswa pia kujiuliza kama hawapati jeuri hiyo kutokana na uzembe unaendelea wa kutowachukulia hatua wahusika.Pengine jeuri waliyonayo inatokana na ukweli kwamba wanaamini kuwa hakuna mwenye jeuri ya kuwachukulia hatua hasa ikizingatiwa kuwa baadhi yao wameishia kupongezwa kwa “ushujaa wao” badala ya kushutumiwa kwa hasara waliyoisababisha kwa taifa.

Nadhani anachopaswa kufanya Lowassa,Ole Naiko na wengine wote waliohusishwa na mkataba wa Richmond ni kutafuta msaada wa kisheria kuona haki inatendeka upande wao iwapo wanaamini kuwa hawakutendewa haki,badala ya kuendeleza hizi porojo ambazo kwa hakika zinaweza kuua kabisa ndoto zao za kurejea kwenye ulingo wa juu wa siasa za nchi yetu.Mahakama zipo,vikao vya chama vipo,sasa kwanini kelele za kuonewa zisipelekwe huko?TANZANIA NI MUHIMU ZAIDI KULIKO MASLAHI YA MTU BINAFSI.

BAADA YA KUMALIZA KUSOMA MAKALA HII,UNAWEZA KUANGALIA VITUKO VYA SIASA ZA URUSI AMBAVYO VIMEZAA TERM MPYA YA NANO PRESIDENT (as in iPod Nano).BONYEZA HAPA

HALAFU KWA WALE AKINA DADA "WENYE ULIMI MZITO",CLIP IFUATAYO INAWEZA KUWA YA MSAADA WA INA FLANI



27 Feb 2008

Makala yangu ndani ya toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema inazungumzia UNAFIKI: Ule wa Profesa Mwandosya kuitaka Dawasco isiwataje hadharani mawaziri wanaodaiwa maji na Mamlaka hiyo;ule wa Askofu Thomas Laizer wa KKKT Dayosisi ya Arusha kutumia neno la Bwana kuwapiga vijembe wanamwandama Lowassa,na ule wa "mabilioni ya EPA yanayorejeshwa kwa kasi."Makala hiyo imeanza kwa stori za hapa na pale,mambo ya muziki wa kufokafoka na albamu ya Jay-Z ya American Gangster ilivyosahau matatizo ya Black Americans.Stori hizo ni zinaunganishwa katika namna ile ile ya conversational style,napenda sana makala iwe mithili ya kupiga stori na msomaji,iwe kijiweni,kwenye pub,au hata barazani.Pamoja na habari na makala zilizokwenda shule,bingirika na makala hiyo kwa KUBONYEZA HAPA

14 Feb 2008





KATIKA TOLEO LA WIKI HII LA GAZETI LA RAIA MWEMA,MAKALA YANGU INAZUNGUMZIA YALIYOJIRI KUTOKANA NA SAKATA LA RICHMOND.KWA SABABU ZILIZO NJE YA UWEZO WANGU,MAKALA HIYO HAIKO KWENYE ONLINE VERSION YA GAZETI HILO.PIA KWA VILE VICHWA VYA MAKALA ZANGU HUWEKWA NA MHARIRI KUNA UWEZEKANO KICHWA CHA HABARI KILICHOPO KWENYE PRINTED VERSION YA GAZETI NI TOFAUTI NA CHA HAPO JUU.

Nianze makala hii kwa kutoa pongezi tatu muhimu. Kwanza, kwa Mheshimiwa Mizengo Pinda kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.CV yake katika utumishi wa umma “imetulia”.

Pili, nampongeza “mwana wa pakaya” ("mtoto wa nyumbani" kwa Kindamba), Jaji Kiongozi mpya Salum Masati, mzaliwa wa Ifakara, ambaye kuteuliwa kwake kumeuweka mji huo katika ramani ya uongozi wa kitaifa (angalau sasa Ifakara inaweza kujulikana kitaifa kwa jambo zaidi ya mchele na mafuriko ya Mto Kilombero.) 

Tatu, ni pongezi kwa mashujaa wote “walioshikia bango” suala la Richmond.Mungu awazidishie ujasiri zaidi na kuwapa ulinzi wake dhidi ya hujuma za mafisadi. Kwa kelele za kizalendo kama za akina Mheshimiwa Anne Kilango, tunaamini kuwa maslahi ya taifa yatawekwa mbele katika mjadala wa ufisadi wa BoT

Binafsi, sakata la Richmond liliniingiza kwenye msukosuko mkubwa baada ya “kupiga ngumi chini ya mkanda”. Novemba mwaka 2006,niliandika makala katika gazeti flani la huko nyumbani. Makala hiyo ilitokana na habari kwamba aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, angefanya kikao na wabunge wa CCM kuandaa mkakati wa kuzima mjadala bungeni kuhusu suala la Richmond. 

Katika makala yangu, nilikosoa utaratibu uliozoeleka wa viongozi wa CCM kuitisha vikao “vya kuwaziba midomo” wabunge wake kila linapojiri jambo linalogusa hisia za wengi. Sikuona mantiki ya Lowassa kuwaita wabunge wa chama chake kuwaweka sawa kwani tatizo la umeme lilikuwa mwiba mkali kwa Watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa. Kikao kilifanyika na agizo la kuweka mbele maslahi ya chama lilizingatiwa,na hatimaye ishu ya Richmond haikujadiliwa.

Kilichopuuzwa wakati huo ni hekima kwamba kuficha ugonjwa hakusaidii kuponya maradhi. Pengine suala hilo lingejadiliwa muda huo wala tusingefika hapa tulipo sasa. Waingereza wana msemo “sehemu mbaya ya uamuzi mbovu ni pale inapofika hatua ya kuujutia”. 

Pamoja na kushutumu mtindo huo wa kuwekana sawa ambao naamini unatumiwa kuficha maovu, makala yangu pia iligusia staili ya uongozi wa Lowassa ya kuwaumbua hadharani baadhi ya watendaji kwa madai ya utendaji wao mbovu wa kazi. 

Japo alikuwa sahihi kukemea viongozi wasiowajibika ipasavyo, kuwaumbua hadharani ulikuwa mkakati dhaifu wa kujitafutia umaarufu wa kisiasa. Nilieleza kwamba zilikuwapo fursa mbalimbali kwa Lowassa kuwakaripia, kuwakosoa au hata kuwaumbua viongozi hao (kwa mfano kuwaita ofisini kwake, kuwaandikia maonyo au hata kuwapigia simu) pasipo haja ya kufanya hivyo kwenye mikutano ya hadhara. Nilihofia kwamba licha ya kuwashushia hadhi watendaji walioumbuliwa hadharani, staili hiyo ya Lowassa ingeweza kutafsiriwa kuwa ni mbinu ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa machoni mwa wananchi ilhali tatizo liko kwenye mfumo wa uongozi. 

Siku chache baadaye, Mwandishi wa Habari wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Saidi Nguba, alijibu makala yangu gazetini (na baadaye kunitumia barua pepe na comments kwenye blogu yangu) kumtetea bosi wake huku akidai suala la CCM kuitisha vikao vya ndani ni utaratibu walijiwekea wao wenyewe na haulengi kuwaziba midomo wabunge kwa vile “wabunge tulionao si watu wa kuzibwa midomo.” 

Mwanahabari huyo alitoa orodha ndefu ya “mafanikio” ya Lowassa ikiwa ni pamoja na idadi ya wanafunzi waliopata nafasi za kuendelea na masomo (japo hakugusia upungufu wa walimu, madawati, nk.) Alimalizia kwa kunikumbusha kuwa kama mwanafunzi niliyeko nje ya nchi nikisomeshwa kwa fedha za Watanzania masikini ninapaswa kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kukosoa “mambo nisiyoyajua.”

Nilimjibu kwa kumfahamisha kwamba kuwa mwanafunzi ninayesomeshwa kwa fedha za walipa kodi masikini ni sababu tosha ya kukemea mambo mabovu ili kuhalalisha kwamba fedha inayotumika kunisomesha haipotei bure.

Pia nilimfahamisha kwamba wazazi wangu ni miongoni mwa Watanzania hao walipa kodi masikini, na kama masikini na walipa kodi wengine, wana haki ya kufahamu na kukosoa utendaji wa serikali waliyoiweka madarakani. Kuhoji utendaji wa serikali sio upinzani, na hata kama ungekuwa ni upinzani basi ni kwa manufaa ya Taifa letu.

Kusomeshwa kwa fedha za masikini haimaanishi anayesomeshwa asitoe mawazo yake (usahihi au upotofu wa mawazo hayo ni suala jingine). Nilipingana na utetezi wake kuhusu “mafanikio” ya staili ya Lowassa kuwaumbua baadhi ya watendaji hadharani na kumkumbusha kuwa hata Rais akitaka kumkosoa Waziri Mkuu wake hatofanya hivyo hadharani bali atamwita chemba. 

Mwandishi huyo mkongwe atakubaliana nami kwamba wakati Lowassa alituaminisha majukwaani kuwa ni “Sokoine mpya” (kwa kuwabana viongozi wazembe papo kwa hapo), “nyuma ya pazia” hakuwa tofauti na hao aliokuwa akiwaumbua hadharani kwani uoza wa Richmond umetokea ofisini kwake.

Naamini (mwandishi huyo) alikuwa akitekeleza tu majukumu yake ya kazi. Pengine moyoni aliafikiana na hoja zangu lakini ulikuwa ni wajibu wake kumtetea bosi wake. Natamani kusikia maoni yake sasa yake kuhusu sakata zima la Richmond.Naamini kwamba wengi wa watetezi wa mkataba huo sasa wataona mantiki za makelele yetu.

Hatimaye Lowassa amejiuzulu huku akijitetea kwamba suala zima la Richmond lilikuwa njama za watu waliokuwa wanataka Uwaziri Mkuu. Kuna msemo wa kiingereza kwamba “hukumu ya umma ni mbaya zaidi ya ile inayotolewa mahakamani.”

Wakati Lowassa anailamu Kamati ya “Kamati ya Mwakyembe” kwa kutompatia nafasi ya kujitetea, kelele zilizosikika mitaani kusherehekea kujiuzulu kwake ndio “hukumu ya umma” huku wengine wakidai kuwa Mzimu wa Nyerere “umemrudi.” 

Hivi mwongozo wa Bunge unasemaje pindi Mbunge anapoituhumu Tume Teule ya Bunge kuwa imesema uongo (kama alivyodai Lowassa)? Wakati nakerwa na UNAFIKI wa kupongeza “ushujaa wa Lowassa kujiuzulu”, ni muhimu Lowassa athibitishe uongo wa tuhuma dhidi yake kwani kama hoja ni kutoitwa kujitetea basi hata Zitto Kabwe alisimamishwa ubunge bila kupewa fursa ya kujitetea. 

Na kwanini alikimbilia kujiuzulu badala ya kudai haki yake, kama kweli aliamini ameonewa? Iweje Kazaura na Msabaha na wengineo wakati walipohojiwa nje ya kiapo waashirie mhusika ni Lowassa na sio mtu mwingine katika kabineti lenye mawaziri 60?Naamini kilio cha Lowassa kimesikika kwa vyombo vya dola. Niandike kwa herufi kubwa: LOWASSA ANAHITAJI KUHOJIWA.

Apewe haki hiyo anayodai kunyimwa na Kamati ya Bunge, lakini pia umma pia unahitaji hivyo kuhusu hizo shs milioni 152 kwa siku za Richmond. Wote waliohusika katika skandali hilo wana uhaba mkubwa wa uzalendo. Walithamini zaidi matumbo yao (na pengine “nyumba ndogo” zao) kuliko maisha ya Watanzania wenzao.

Hakuna haja ya kuwapeleka jela kwani watatuongezea tu gharama ya kuwahudumia chakula gerezani. La muhimu ni kuwafilisi kila walichovuna kwenye “dili” hilo. Katika hili, tuweke pembeni sheria za mapatano (laws of reconciliation) za Agano Jipya na kurejea kwenye sheria za kisasi (laws of retaliation) za Agano la Kale, yaani jino kwa jino na jicho kwa jicho. Wametufilisi nasi lazima tuwafilisi.

KUNA MWANANCHI AMENITUMIA E-MAIL YENYE UJUMBE WA KUFURAHISHA KWA NAMNA FLANI.IKO KWENYE POWERPOINT FORMAT.

9 Feb 2008

AMA KWA HAKIKA MAISHA HAYATABIRIKI.MAISHA SIO KAMA FUMBO LA HESABU AMBAPO MBILI KUJUMLISHA MBILI JIBU LAZIMA LIWE NNE.KATIKA MAISHA,JIBU LA FUMBO HILO LINAWEZA KUWA HAMSINI,AU KWA KUKATISHA TAMAA ZAIDI,JIBU LAWEZA KUWA SIFURI.

HAPO CHINI,NI PICHA YA REGINA LOWASSA,AKIFUTA CHOZI KUFUATIA MUMEWE,EDWARD LOWASSA, KUBWAGA MANYANGA YA UWAZIRI MKUU.HII NI NIGHTMARE AMBAYO KILA MKE ANAOMBA ISITOKEE KATIKA MAISHA YA NDOA YAKE






















KATIKA PICHA YA CHINI,KUSHOTO NI DADA TUNU,MKE WA WAZIRI MKUU MPYA MIZENGO PINDA.NI NDOTO AMBAYO KILA MKE ANGEPENDA IWE KWELI KATIKA MAISHA YAKE YA NDOA.HAPA NDIPO UAMUZI WA KUSEMA I DO UNAPOONEKANA WA BUSARA KULIKO MAAMUZI YOTE MAISHANI




















Picha ya juu kwa hisani ya Mjengwa,na ya chini kwa hisani ya Michuzi

8 Feb 2008

Mwezi Novemba mwaka 2006,niliandika makala moja iliyotoka katika gazeti la KULIKONI (toleo la tarehe Novemba 3-9, 2006 2006).Katika makala hiyo (BONYEZA HAPA KUISOMA),nilizungumzia kusikitishwa kwangu na habari kwamba ex-PM Edward Lowassa alikuwa akifanya jitihada za kuwanyamazisha wabunge wa CCM kuhusu shinikizo la kujadili mkataba wa Richmond.Pia katika makala hiyo nililaumu staili ya uongozi wa Lowassa ya kuwaumbua hadharani watendaji walio chini yake badala ya kufanya hivyo kimaandishi au ofisini.Nilieleza kwamba japo dhamira ya Lowassa kukosoa utendaji wa subordinates ni njema,njia anazotumia sio mwafaka.Nilihoji kiongozi angejisikiaje iwapo Bosi wake,JK,akitokea kumkosoa hadharani badala ya kufanya hivyo faraghani.Nilipoandika makala hiyo,sikujua kuwa kuna siku,Lowassa atakumbana na fedheha ileile aliyokuwa akiwapatia ma-DC,RAS,Katibu Kata,nk kwa kuwaumbua hadharani (pengine kwa kujitafutia tu umaarufu wa kisiasa).Leo siku hiyo imetimia.Siku chache baada ya makala hiyo kuchapishwa,Mwandishi wa Habari wa Lowassa,aliandika makala kupinga hoja zangu,kabla ya kunitumia barua-pepe ya shutuma na hatimaye aliweka comments kwenye blog hii.Contents za makala,barua-pepe na comments za muungwana huyo zilikuwa na ujumbe unaolingana,ambapo pamoja na mambo mengine alipingana na hoja zangu huku akishutumu kwamba sie wanafunzi tulio nje tukisomeshwa kwa kodi za masikini hatupaswi kukosoa mambo tusiyoyajua (BONYEZA HAPA KUSOMA COMMENTS HIZO.)Nami nimjibu kwa barua-pepe kusisitiza kwamba nilichoandika kilikuwa sahihi,na imani yangu kwamba utetezi wake kwa Lowassa ilikuwa sehemu tu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kazi (SOMA BARUA-PEPE HIYO KWA KUBONYEZA HAPA)

18 Jun 2006

KULIKONI UGHAIBUNI

Mambo yakoje huko nyumbani?Natumaini kila mmoja anawajibika kwa namna yake katika ujenzi wa Taifa.

Kuna jamaa mmoja hapa anaitwa David Cameron.Huyu ni kiongozi wa chama cha wahafidhina (Conservative Party).Nia yangu si kuzungumzia wasifu wake,bali nataka nimlinganishe na mwanasiasa nyota wa huko nyumbani kwa muda huu,au kwa lugha ya “kwa mama” tunaweza kumuita “a man of the moment.” (kwa tafsiri ya haraka, “staa wa muda huu”).Nadhani msomaji mpendwa umeshajua ni nani ninayemzungumzia.Lakini hapa namuweka kando kidogo ili nikupashe kuhusu huyo Bwana Cameron na chama chake cha Conservatives (au Torry,kama kinavyojulikana hapa).Kwa tafsiri nyepesi hawa Conservatives ni watu wenye mrengo wa kulia na ndio wapiga kelele wakubwa kuhusu sera za uhamiaji na nyinginezo ambazo zinawagusa makabwela hususan wale ambao si wazawa wa hapa.Pengine jeuri kubwa ya wahafidhina hawa inatokana na uwezo wao wa kifedha.Fedha wakati mwingine huwa na tabia ya kumfanya binadamu asiwafikirie wenzie aliowazidi kiuwezo,na aghalabu anapowafikiria basi huwa ni kwa manufaa yake binafsi.

Kuibuka kwa Cameron kulichochewa zaidi na mwelekeo usioridhisha wa chama chake katika chaguzi mbalimbali.Wachambuzi wengi wa mambo ya siasa walikuwa wanahusisha mwenendo mbaya wa chama hicho na kile kinachoitwa kuwa “out of touch.”Nitafafanua.Chama kilicho “out of touch” ni kile ambacho machoni mwa watu wa kawaida kinaonekana kama hakijihusishi na maslahi ya walio wengi.Kwa mfano,hawa wahafidhina kwa miaka kadhaa wamekuwa wakikumbatia zaidi Waingereza weupe hasa wale wa tabaka la juu na la kati huku wakiwasahau wale wa tabaka la chini pamoja na Waingereza wengine ambao ni “wakuja” (kwa mfano wale wenye asili ya Asia,Caribbean,Afrika,n.k).Pia wamekuwa wakiwaona wageni (ikiwa ni pamoja na wanafunzi wanaochangia mamilioni ya paundi kwenye uchumi wa nchi hii) kama watu wanaokuja kuharibu uchumi,utamaduni na mazingira ya hapa.

Baada ya Waziri Mkuu wa mwisho kutoka Conservative kushika wadhifa huo,John Major,alipoangushwa na Tony Blair mwaka 1997,chama hicho kimebadilisha viongozi kadhaa lakini bila mabadiliko hayo kuwanufaisha kwenye chaguzi mbalimbali.Ndipo katika mchakato huo alipoibuka Bwana Cameron,kijana (ana miaka 40 tu),ana mvuto na haiba ya kutosha.Huyo bwana aliamua kuwapa wenzake kitu “laivu” kwamba chama chao hakina mvuto kwa wapiga kura,kinaonekana kuwa kiko zaidi kwa maslahi ya mabwanyenye kuliko makabwela,na hakizungumzi “lugha ya mtu wa kawaida mtaani.”Kuna mengi ya kumzungumzia huyo bwana lakini kilichonisukuma kuandika makala hii ni jinsi navyomuona anafanana na Jakaya Kikwete.Ukiachilia ukweli kwamba wote ni handsome lugha wanayoongea inafanana:lugha inayomgusha mtu wa kawaida na sio makundi flani tu katika jamii hususan wale wenye nguvu za kiuchumi.

Jakaya amenukuliwa mara kadhaa akiwausia viongozi wenzie kwamba wako madarakani kuwahudumia hao waliowaweka madarakani.Sio dhambi kuwa karibu na matajiri lakini ukaribu huo usiwe kwa ajili ya kuwaumiza wasio nacho.Utajiri sio dhambi,na kuna matajiri kadhaa (mfano Mzee Mengi huko nyumbani au Bill Gates huko Marekani) ambao utajiri wao umekuwa faraja kwa mamilioni ya wale wasio nacho.Matajiri wa aina hii ni muhimu kwao kuwa karibu na viongozi wa serikali,vyama vya siasa na taasisi nyingine kwa vile ni kwa ukaribu huo ndio miradi mbalimbali wanayoifadhilia inaweza kuwa na manufaa kwa wananchi.

Juzijuzi nilimwona Bwana Cameron kwenye luninga akiwa kwenye mtaani wakati wa kampeni za chama chake kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwa upande wa England.Jinsi alivyokuwa akijichanganya na watu ilitosha kabisa kumfanya hata mtu aliyekuwa akikichukia chama cha wahafidhina afikirie upya.Siku chache baadae nikasoma kwenye mtandao kuwa Jakaya ameweka historia kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kutembelea wafungwa magerezani.Yalipotokea mauaji ya kutatanisha ya wale wachimba madini wa Mahenge hakukawia kuunda tume,na kinyume ya ilivyozoeleka mara baada ya kupewa ripoti na tume akaweka matokeo hadharani.Aliporejea tu kutoka Kusini mwa Afrika hakukawia kwenda kuwaona majeruhi wa tukio la uporaji wa fedha za NMB pale Ubungo,na kutoa maagizo papo hapo.Lakini si Jakaya pekee bali hata “luteni” wake Lowassa.Ghorofa lilipoanguka Keko hakusubiri kuletewa taarifa bali alikwenda kujionea mwenyewe na kuchukua hatua hapohapo, “mafuriko” yalipoielemea Sinza hakukawia kwenda kushuhudia hali ilivyo na kuwaamuru wahusika wachukue hatua za haraka.

Laiti kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya aliyokuja nayo Kikwete itaweza kufikia hatua ya kuigwa na viongozi kuanzia ngazi ya serikali ya mtaa,kata,tarafa,wilaya na mkoa,basi muda si mrefu Bongo itakuwa sehemu ya neema.Na mwenyewe Jakaya amekuwa akisema kuwa Tanzania yenye neema inawezekana.Enyi viongozi mliolala hebu amkeni,msisubiri kuamshwa.Jisikieni aibu pale mnapokwenda kinyume na spidi ya kiongozi wenu mkuu.

Alamsiki

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.