Showing posts with label BENKI KUU. Show all posts
Showing posts with label BENKI KUU. Show all posts

26 Jul 2014

Tanzania yetu haina uhaba wa vituko, na si vituko vya kupendeza bali vya kukera.Kuna baadhi ya taasisi,ile ukiskia tu jina unatambua nini kinafuata.Kwa mfano Tanesco: kila ninaposkia kuhusu Tanesco ninatambua ni aidha ishu ya ulaji wa fedha za miradi hewa ya uzalishaji umeme usipo,au ni mgao wa umeme.

Benki Kuu ya Tanzania nayo ni miongoni mwa taasisi zilizojipatia umaarufu mkubwa katika ufisadi.Ni nani amesahau kuhusu moja ya skandali kubwa kabisa katika historia ya ufisadi Tanzania, yaani EPA? Nani amesahau mazingaombwe yaliyozunguka ishu ya EPA, kuanzia kufichwa jina la mmiliki wa jambazi mkubwa zaidi katika skandali hiyo, yaani Kampuni ya Kagoda hadi 'kifo' cha aliyekuwa Gavana wa Benki hiyo, Daudi Ballali (kama kweli alikufa basi ni vema mwili wake ukatumika kama kuni za kuchoma watenda maovu huko motoni).

Lakini Benki Kuu pia inajijengea sifa nyingine ya ubabaishaji, pengine kutokana na ukweli kwamba ubabaishaji ni moja ya kumbukumbu muhimu katika utendaji wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete. Katikia 'toleo jipya' la ubabaishaji wa Benki Kuu, taasisi hiyo nyeti 'imelamba matapishi yake' baada ya kutoa taarifa za kujikanganya ndani ya wiki moja kuhusu hatma ya benki ya FBME. Angali mtiririko wa matukio:

Jumapili Julai 20,2014: Benki Kuu yasambaza taarifa kwamba tetesi kuhusu benki ya FBME kufungwa' na uendeshaji wake kuwekwa mikononi mwa Benki Kuu si sahihi, ni uzushi tu. Tamko hilo lipo hapa


Lakini katika hali inayoweza kuelezwa tu kama UBABAISHAJI,Benki Kuu hiyo hiyo, jana Ijumaa,iltoa tangazo linalokinzania kwa asilimia zaidi ya  100 na hilo hapo juu, ambapo sasa ilieleza kuwa FBME imewekwa chini ya uangalizi wake (Benki Kuu). 


Sidhani kama kuna neno sahihi la kuelezea sintofahamu hii zaidi ya UBABAISHAJI uliokithiri. Lakini nani anajali? Kama ambavyo Tanesco wanaweza kukata umeme kila wanapowashwa na vidole na Watanzania wakaishia kuitukana matusi ya nguoni kana kwamba matusi yatasaidia kumaliza mgao wa umeme, ndivyo habari hii ya ubabaishaji wa BoT ilivyopita kimyakimya kana kwamba walichofanya ni sawia.

TUMEROGWA?



14 Jun 2009


Majuzi,Watanzania wametahadharishwa kuhusu athari za mdodoro wa uchumi wa dunia na madhara yake kwa nchi yetu.Kadhalika,bajeti ya mwaka ujao wa fedha imeandaliwa kwa kuzingatia tahadhari hiyo huku kukitangazwa mpango wa kuchochea uchumi (economic stimulus plan).

Hata hivyo,kama nilivyojadili HAPA,uwezekano wa bajeti na stimulus plan hiyo kufanikiwa,sambamba na umuhimu wa tahadhari iliyotolewa,utategemea zaidi hatua kali na za makusudi dhidi ya ufisadi na mafisadi.Yayumkinika kubashiri kwamba pamoja na imani kwamba mipango hiyo inalenga kulinusuru taifa,wanaufaika wakubwa wanweza kuwa mafisadi wanaojua vema namna ya kubuni mikakati ya ulaji huku wakiwa hawana hofu ya kuchukuliwa hatua yoyote kutokana na siasa za kulindana na kishkaji.

Hebu soma kwanza habari ifuatayo,kisha tujadili kidogo mwishoni.

Wingu zito fedha za EPA
• Chegeni: Zimekwenda kusikojulikana

na Mwandishi Wetu

UTATA umegubika mahali zilipo na matumizi ya fedha zilizorejeshwa na kampuni zilizoshiriki katika wizi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akilihutubia Bunge mjini Dodoma Agosti mwaka jana, alibainisha fedha hizo zilizorejeshwa na baadhi ya kampuni si mali ya serikali lakini zitawekwa kwenye akaunti maalumu kabla ya kupelekwa katika Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kwa ajili ya kufungua dirisha dogo la kuwakopesha wakulima wakati nchi ikielekea katika mchakato wa kuanzisha Benki ya Kilimo.

Ingawa Rais Kikwete na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kwa nyakati tofauti walieleza kuwapo kwa fedha hizo katika akaunti maalumu, taarifa ambazo Tanzania Daima Jumapili imezipata zinasema hadi sasa fedha hizo hazijaingia katika Benki ya TIB, licha ya kuwapo kwa taarifa kuwa fedha hizo zimetumika kununulia mbolea iliyotolewa kwa mfumo wa vocha kwa baadhi ya wakulima hapa nchini.

Chanzo kimoja cha habari kilichomo ndani ya TIB kimedai fedha hizo wamekuwa wakizisikia kupitia katika vyombo mbalimbali vya habari kutoka kwa wanasiasa, ambao wamekuwa wakijinadi kuwa fedha hizo zitatumika kunyanyua kilimo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Chanzo hicho kilibainisha kuwa hadi sasa dirisha la kilimo lililosemwa bado halijaanza kufanya kazi iliyotarajiwa, ingawa maneno ya watu mbalimbali yamekuwa yakibainisha kuanza kazi kwake ambako kungetarajiwa kuwasaidia wakulima kupata mikopo ya muda mrefu, baada ya kuikosa fursa hiyo kwa kipindi kirefu kutokana na kutokopeshwa na taasisi za fedha za hapa nchini.

“Haya mambo huwa tunayasoma, kuyasikia na kuyaona kwenye hivyo vyombo vyenu vya habari, lakini kwenye makaratasi hali ni tofauti, sasa sijui niseme siasa inatawala au muda bado haujafika,” kilisema chanzo hicho.

Tanzania Daima Jumapili, ilifanya juhudi za kumtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Peter Noni, ambaye ameteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo na Rais Jakaya Kikwete, lakini Ofisa Mwanadamizi wa Mambo ya Uhusiano wa benki hiyo,Catherine Magambo, alisema mkurugenzi wake hawezi kutoa ufafanuzi hivi sasa, kwa kuwa ameanza kazi siku si nyingi na ni busara akapewa wiki moja ili aweze kujipanga.

Catherine, alipotakiwa kueleza kama ana taarifa zozote za kutokuwapo kwa fedha zilizoahidiwa na rais kupelekwa katika benki hiyo, alisema anachokifahamu ni kile kilichoelezwa wakati fulani na Mkurugenzi aliyestaafu, William Mlaki, kuwa hawajapokea fedha hizo na kama kungekuwa na mabadiliko vyombo vya habari vingejua kama walivyofanya hapo awali.

“Nyinyi Tanzania Daima Jumapili, habari kama hii unayoniuliza au unayotaka mkurugenzi wangu akujibu, najuakwamba hakuna kitu ambacho kimebadilika lakini kama mnataka habari zaidi msubiri mkurugenzi mpya azoee ofisi kwa muda wa wiki, halafu ndipo uje kumuuliza maswali yako,” alisema Magambo.

Pia alibainisha kuwa hajaona mabadiliko yoyote juu ya ahadi iliyotolewa pia na Rais Kikwete ya kutoa kiasi cha sh bilioni 15 kwa ajili ya kuendeleza benki hiyo ili iweze kutoa mikopo kwa wakulima.

“Jamani maswali yenu mbona yamezidi, si nimewaambia hakuna mabadiliko na hayo maswali yenu msubirini mkuu? Mbona mnanibana kwa mambo nisiyo na uwezo wa kutoa majibu? Kwani kila ofisi ina utaratibu wake,” alisema Magambo.

Wakati fedha hizo zikionekana kugubikwa na utata, baadhi ya watu wamekuwa wakiiona hatua ya serikali kutangaza kurejeshwa kwa fedha hizo ni kiini macho au zimetumika katika matumizi mengine badala ya kupelekwa katika kilimo kama ilivyoahidiwa, kwa kuwa viwanda vingi vya mbolea kwa mwaka huuvimejikuta vikishindwa kujiendesha baada ya kuzalisha bidhaa hiyo na kukosa wanunuaji.

Dhana hiyo inachagizwa na baadhi ya wakulima ambao wamekuwa wakilalamikia kutokupata mbolea hiyo, licha ya serikali kutangaza kutenga fungula fedha kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kukuza kilimo na kuleta mapinduzi ya kijani.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa na wanasiasa mbalimbali wa hapa nchini walikuwa wakihusisha wizi huo wa fedha na mkakati maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwaagiza baadhi ya makada wake na wanachama wakwapue fedha hizo kwa ajili ya matumizi ya kampeni za uchaguzimkuu wa mwaka 2005 uliokiwezesha chama hicho kuibuka na ushindi wa ‘kishindo.’

Hisia hizo zilipata nguvu baada ya kuwapo tetesi kuwa kampuni iliyochota kiasi cha sh bilioni 40 ya Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, inadaiwa kumilikiwa na baadhi ya vigogo wa chama hicho, jambo lililochangia ugumu wa kukamatwa kwa wamiliki wa kampuni hiyo ambayo inaaminika ndiyo iliyosuka mpango wa uchotaji wa fedha hizo.

Tuhuma hizo mara kadhaa zimekuwa zikikanushwa na viongozi waandamizi wa chama hicho, akiwamo Katibu Mkuu wake, YusufMakamba, ambaye aliweka bayana kuwa CCM haijamtuma mwanachama wake afanye wizi huo na kama kuna mwanachama amehusika na wizi huo apewe lawama hizo binafsi na si chama.

Naye Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni, katikati ya wiki alinukuliwa na vyombo vya habari mjini Dodoma akisema kuwa fedha za EPA zinaonekana kwenda sehemu zisizoonekana kirahisi kwa wananchi, ingekuwabusara kama zingetumika katika ujenzi wa barabara ambayo ingepewa jina la EPA, ili kila
mwananchi aweze kuamini kinachosemwa na viongozi wa serikali.

Alisema mazingira ya fedha hizo tangu awali yalionyesha utata, hivyo ingekuwa busara hata matumizi yake yakafanyika bila kuwapo kwa usiri, ili kuondoa fikra potofu kuwa hakuna fedha iliyorejeshwa.

“Hizi fedha za EPA mimi nafikiri zingetumika kujengea barabara na tukaziita barabara za EPA, ili yeyote anayetaka kuzusha lake ashindwe kufanya hivyo au tumuonyeshe vithibitisho,” alisema Chegeni.

Alisema sekta ya kilimo ni pana na hata fedha zinazotumbukizwa huko ni lazima ziandaliwe mipango mizuri na mapema ili ziweze kufikia walengwa na zilete tija inayotakiwa kuliko inavyoonekana sasa ambapo serikali inasema imetoa mbolea ya ruzuku kwa wingi, lakini wakulima wanalalamika kutoipata mbolea hiyo kwa kiwango kinachohitajika.

Wizi wa fedha za EPA ulibainika baada ya Kampuni ya ukaguzi ya kimatifa ya Ernst &Young kubaini wizi wa sh bilioni 133, ambapo baada ya uchunguzi huo, Rais Kikwete aliamua kumfukuza kazi aliyekuwa Gavana wa benki hiyo, marehemu Daudi Ballali na kuagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi kwa maofisa wa benki hiyo ili kufikishwa mbele ya vyombo vyasheria.


CHANZO: Tanzania Daima.

Katika mazingira kama haya,itakuwa kosa kweli kuyamkinisha kwamba hiyo stimulus plan inaweza kuishia kutengeneza dili ya kuifanya EPA ionekane "cha mtoto"?

Halafu,habari hiyo hapo juu ina kitu kingine cha ziada,nacho ni kuhusu PETER NONI.Huyu jamaa anahusishwa kwa karibu na skandali la EPA.Awali wasiwasi wangu ulikuwa kwenye kuteuliwa kwake kuwa Mkurugenzi wa TIB.Kilichonifumbua macho katika habari hii ni ukweli kwamba marejesho ya fedha za EPA yalipangwa kupelekwa TIB.You see the connection?NONI anahusishwa na ishu ya EPA kwa wadhifa aliokuwa nao BoT.Sasa anapokwenda TIB ambako tunaambiwa ndiko zitakapopelekwa marejesho ya fedha za EPA ni mithili ya "kula denge" kuelekea lilipo fungu hilo.

Ndio Tanzania yetu hiyo!

21 Feb 2009

ULE MCHEZO WA KUIGIZA KUHUSU "KUTOWEKA" KWA LIYUMBA BADO UNAENDELEA.LATEST EPISODE INAHUSU TAKUKURU KUTANGAZA DONGE NONO KWA ATAYEFANIKISHA KUKAMATWA KWA NDUGU LIYUMBA.

Na Boniface Meena

TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini(Takukuru) imetangaza kutoa donge nono kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi (DPA) wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba ambaye hadi hivi sasa hajulikani halipo.

Wakati Takukuru ikifikia hatua hiyo, tayari kuna wananchi ambao wametoa taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuwa wanaweza kutoa taarifa za alipo Liyumba. Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana Afisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani alisema wameamua kutangaza doge nono ambalo hakulitaja ni kiasi gani cha fedha ili wananchi wasaidie kupatikana kwa Liyumba. Alisema Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Dk Edward Hoseah ,anakaribisha watu ambao wanaweza kutoa taarifa au kusaidia alipo Liyumba ili aweze kukamatwa.

"Kuna wananchi tumesikia wako tayari kuisaidia Takukuru, tunawakaribisha na Dk Hoseah anawakaribisha ili waweze kutusaidia na donge nono litatolewa kwa atakayesaidia kukamatwa kwa Liyumba," alisema Kapwani.

Wakati Takukuru ikifikia maamuzi hayo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema kama Takukuru itahitaji msaada wa Wizara hiyo kumtafuta Liyumba iko tayari kutoa msaada huo.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili Waziri wa Wizara hiyo, Lawrance Masha alisema wakipewa maombi ya kumtafuta Liyumba, watasaidia kumtafuta kwa kuwa wote ni Serikali. "Juzi nilitoa tamko kuwa hatujaletewa maombi ya kumtafuta, lakini Takukuru wakituletea tutafanya hivyo, kwa kuwa sisi ni Serikali," alisema Masha.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifuta dhamana ya Liyumba Februari 19 na kutoa amri ya kuwakamata wadhamini wake ambao walikamatwa siku hiyohiyo na baadaye kuachiwa. Wadhamini hao ni wafanyakazi wa BoT Benjamin Nduguru (mhasibu wa benki hiyo) na Agaterus Oto (Afisa Usalama wa ndani wa benki hiyo).

Hata hivyo, licha ya mahakama kufuta dhamana kuwakamata wadhamini hao, ilitoa amri ya kumtafuta na kumkamatwa Liyumba.Liyumba pamoja na aliyekuwa Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka wameshitakiwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka yao katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo na kuisababishia hasara serikali jumla ya Sh221 bilioni.

Liyumba alipewa dhamana na Hakimu Mkaazi wa Kisutu, Hadija Msongo kwa kutumia hati ya nyumba yake iliyoko Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam yenye thamani ya Sh800 milioni, ambayo hata hivyo ililalamikiwa na upande wa mashitaka kwamba imetolewa katika mazingira tata kwa kuwa haijafikisha kiwango cha Sh50 bilioni walizotakiwa kutoa

Juzi Wakili wa serikali, Prosper Mwangumila aliileza mahakama kwamba, Liyumba bado hajapatikana. Hakimu alisema amri ya kumkamata Liyumba bado inaendelea na ya kuwakamata wadhamini imesitishwa hadi kesi itakapotajwa Februari 24, mwaka huu.

Katika hatua nyingine Mawakili wanaomtetea mtuhumiwa huyo waliulalamikia upande wa mashitaka kwa kitendo chake cha kuwanyanyasa ndugu wa mtuhumiwa huyo ambapo walidai kuwa uliwanyang’anya baadhi ya mali zao.

Mmoja wa mawakili hao wa utetezi, Majura Magafu aliiomba mahakama kutoa amri ya kuutaka upande wa mashitaka kuacha kuinyanyasa familia ya Liyumba na kwamba warudishe gari ya mmoja wa wadhamini ambayo waliikamata. Akijibu hoja hiyo, Hakimu Msongo aliutaka upande wa utetezi kama una maombi yoyote kuyapeleka kwa utaratibu wa mahakama kwa kuwa juzi haikuwa tarehe ya kesi.

Wakati akitoa dhamana hiyo Februari 17, mwaka huu, Hakimu Msongo alisema mshitakiwa huyo, atakuwa nje kwa dhamana ya Sh882 milioni wakati mahakama inajiridhisha na hati nyingine zilizopingwa na upande wa mashitaka. Alisema mshitakiwa atatakiwa kutimiza masharti ya dhamana ya kiasi kilichobaki cha Sh54,417,344,800.23 endapo mahakama itabaini kuwa hati hizo zina kasoro.

Hata hivyo baada ya kutolewa maamuzi hayo Wakili wa serikali Justus Mulokozi alisema hawajaridhika na maamuzi yaliyotolewa na kwamba watakaa kuyajadili na kuyatolea maamuzi. Upande wa mashitaka ulipinga kupokelewa kwa hati 10 kati ya 11 zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi kwa madai kuwa zina kasoro, zikiwemo za kuwa na mali zisizokuwa za kudumu kama mbuzi, ng’ombe na kuku.

Siku mbili baada ya mtuhumiwa huyo kuachiwa huru na mahakama kutokana na kutimiza masharti, mahakama ilitoa amri ya kukamatwa tena jambo lilosababisha wadhamani wake kushikiliwa kwa muda na kisha kuachiwa.

Liyumba na Kweka walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza , Januari 27, mwaka huu kwa tuhuma za kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia hasara serikali kiasi cha Sh 221 bilioni. Kweka bado hajapata dhamana.



TATIZO KUBWA LA VYOMBO VYETU VYA HABARI NI KURIPOTI HABARI AU MATUKIO BADALA YA KWENDA NDANI ZAIDI NA KUCHUNGUZA YALIYOJIFICHA KATI YA MISTARI.KWA MFANO,KWANINI HATUJIULIZI SABABU WA WADHAMINI WA LIYUMBA KUKAMATWA KISHA KUACHIWA?JE WADHAMINI HAO NAO "WAKITOWEKA" SI ITAMAANISHA "KIFO CHA ASILI" CHA KESI HIYO?

HIVI HATUWEZI KUJIULIZA SABABU ZA HAKIMU KUTOA DHAMANA KWA MSHTAKIWA JAPO DHAMANA HIYO ILIKUWA NA MAPUNGUFU?NAFAHAMU NI HAKI KWA MSHTAKIWA KUPATIWA DHAMANA LAKINI SHARTI ATIMIZE MASHARTI YA DHAMANA HIYO.

WIZI MTUPU!

27 Jan 2009

Picha kwa hisani ya BongoPicha.JAPO KANUNI MUHIMU KATIKA SHERIA INATAMKA BAYANA KUWA MTUHUMIWA ANABAKI KUWA MTUHUMIWA HADI ATAPOTIWA HATIANI,LAKINI YAYUMKINIKA KUHISI KWAMBA HUKO MITAANI ISHU YA HUYU MHESHIMIWA LIUMBA ISHATOLEWA HUKUMU ZAMANI HIZO...NA WALA HAIHUSIANI NA HIZO GHOROFA PACHA ZA BENKI KUU.NAAMINI WANAOFATILIA VIMBWANGA VYA VIGOGO WATAKUWA WANAELEWA NAZUNGUMZIA NINI.KWA HABARI KAMILI KUHUSU KILICHOMPANDISHA KIZIMBANI LIUMBA BONYEZA HAPA.

11 Feb 2008

Uongozi wa kisiasa wa Tanzania,kama ilivyo sehemu mbalimbali duniani,umekuwa ukitegemea watu kutoka fani mbalimbali za maisha.Tuna viongozi wa dini (kama Mchungaji Lwakatware),Wasomi (kama Prof Mwandosya,Prof Msola,Prof Mwakyusa),wanajeshi (kama Kapteni John Komba,Kapteni Jaka Mwambi,Luteni Yusufu Makamba) na hata wasanii kama Khadija Kopa .Hivi karibuni,JK alielezea kutoridhishwa kwake na athari zinazoweza kutokana na kuwa na viongozi ambao pia ni wafanyabisahara.Ana hoja ya msingi hapo,lakini nadhani tatizo la msingi sio fani aliyotoka au anayoendela nayo kiongozi husika bali ni utashi alionao katika kuwahudumia Watanzania wenzake.Kadhalika,mkanganyiko uliopo kwenye kanuni za maadili ya uongozi ziko shaghala baghala,hasa baada ya kuuawa kwa Azimio la Arusha na kuzaliwa Azimio la Zanzibar.Endelea na makala yangu hii kwenye gazeti la Mtanzania.
MTANZANIA UGHAIBUNI-

Watanzania wengi wameipokea kwa furaha kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu umuhimu wa kutenganisha biashara na utumishi wa umma.Ni kauli mwafaka kwani hata katika Maandiko Mtakatifu tunafundishwa kwamba ni vigumu kutumikia mabwana wawili.

Naamini kwa mtazamo wa wengi,wafanyabiashara kama Watanzania wengine wana kila haki ya kushiriki katika shughuli za siasa ikiwa ni pamoja na kugombea ubunge au hata kuteuliwa mawaziri.Tatizo linakuja pale maslahi ya biashara zao yanapoingiliana na utekelezaji wa majukumu yao katika kuuhudumia umma.

Inaweza kuwa sio sahihi kuwalaumu wafanyabisahara wanaochanganya biashara na siasa pale ilhali hakuna miongozo maalumu (kama ya Marekani na Uingereza).Ndio maana wazo la kufanyika mchakato wa kuleta sheria na kanuni zitakazoweka bayana mazingira ambayo kwa upande mmoja hayatawanyima nafasi wafanyabiashara kushiriki kwenye siasa,na upande mwingine biashara zao kutoathiri majukumu waliyokabidhiwa na taifa,lina umuhimu mkubwa.

Pamoja na pongezi hizo ni muhimu kuangalia chanzo cha tatizo lililopo hivi sasa.Ni ukweli usiopingika kwamba wakati wanasiasa wengi wameendelea kuhubiri kwamba siasa ya Ujamaa na Kujitegemea bado ni mhimili wa taifa letu,hali halisi tuliyo nayo sasa inapingana kabisa na matamshi hayo.

Azimio la Arusha lilisaidia kuweka wazi mwelekeo wa taifa letu.Makala moja kama hii haiwezi kutosha kuelezea undani wa Azimio hilo lakini kilicho wazi ni kwamba Baba wa Taifa,ambaye kimsingi ndiye anayekubalika kama mwasisi wa itikadi hiyo,alikuwa na ndoto ya kuona jamii ya Watanzania inayoishi kwa usawa na haki.

Baadaye likaja Azimio la Zanzibar.Pengine mie ni mzembe wa kujua kilichomo katika Azimio hilo lakini naamini kwamba kuna Watanzania wengi ambao hadi leo hawajui kilichomo kwenye Azimio hilo.Labda ni kutokana na ufahamu mdogo uliopo miongoni mwa wananchi wengi kuhusu Azimio la Zanzibar ndio maana wengi wetu tunarahisisha majibu kwamba lilikuwa tamko rasmi la kifo cha Azimio la Arusha.Na katika hili,CCM inastahili kubeba lawama zote kwani haijafanya jitihada zozote za makusudi kuuelewesha umma kuhusu madhumuni na kulichomo kwenye Azimio hilo (la Zanzibar).

Kuna mapungufu makubwa katika suala zima la uwazi pindi yanapojiri masuala nyeti kwa taifa letu.Mfano mzuri ni kwamba wengi wetu tulikuwa hatufahamu kwamba hadi uteuzi wake unatenguliwa na Rais,aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu aliyeondolewa madarakani,Dkt Daudi Ballali,hakuwa mtumishi wa serikali.Pengine taratibu zinasema hivyo lakini kwa vile mtu anayekalia nafasi hiyo ndiye mwenye kushika dhamana ya fedha za Watanzania wote,nadhani kulikuwa na kila sababu ya wenye fedha zao (Watanzania) kufahamishwa kuhusu hilo badala ya kusubiri mpaka litokee tatizo la ufisadi kwenye taasisi hiyo muhimu kwa taifa.

Hadi muda huu,ukiwauliza viongozi wa CCM kwamba je Azimio la Arusha bado ni mwongozo muhimu kwa maendeleo na mwelekeo wa taifa,sanasana utachoambulia ni hadithi ndefu zisizotosha kutoa jibu moja la kueleweka.Ni dhahiri muuliza swali atakumbana na ugumu wa aina hiyohiyo pindi akiuliza iwapo nchi yetu bado inafuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.Na haiishii hapo kwani majibu yataendelea kuwa tete pindi mtu akiuliza iwapo CCM bado ni chama cha wakulima na wafanyakazi.

Na ni katika hilo la wakulima na wafanyakazi ndipo napoona kuna tatizo la msingi.Inasemekana Azimio la Zanzibar lilihalalisha watumishi wa umma (wafanyakazi) kumiliki mali kinyume na katazo lililowekwa na Azimio la Arusha.Laiti wakati wanasiasa wetu walipokutana Zanzibar kuua Azimio la Arusha wangeangalia mbali,ni dhahiri wangebaini uwezekano wa kutokea mgongano kati ya biashara na utumishi wa umma.Haraka ya kupitishwa Azimio hilo inaweza kuwa sababu muhimu ya wanasiasa hao kutoangalia mbali.Lakini pia haraka hiyo inaweza kuwa ilichochewa na ukweli kwamba wakati wanasiasa wengi walikuwa wakituimbia ngonjera za Ujamaa na Kujitegemea majukwaani,majumbani mwao walikuwa wakicheza ngoma za ubepari.

Dhana hapo ni kwamba Azimio la Zanzibar lilipitishwa chapchap ili wajamaa wa hadharani waliokuwa mabepari wa kificho waweze kuendesha maisha yao bila hofu na bughudha ya kuonekana wanatenda kinyume na imani ya taifa letu kwa wakati huo.Hawa ni pamoja na wale ambao walikuwa wakituaminisha kwamba ni watu wa karibu na Baba wa Taifa kumbe moyoni walikuwa wakiomba dua Mwalimu aondoke madarakani ili watumie vile walivyokuwa wakikusanya kwa kificho katika zama hizo za Ujamaa na Kujitegemea.Na wengine japo Mwalimu aliwasaidia kuwaingiza madarakani akidhani ni waumini wa siasa zake,wamestaafu wakiacha skandali lukuki.

Kama kuna madhara mabaya zaidi ya mfumo wa chama kimoja basi ni kule kutoruhusu mawazo tofauti na ya watawala,hata kama mawazo hayo ni ya kuchochea maendeleo ya taifa.Kinadharia kila Mtanzania ana uhuru wa kutoa mawazo yake alimradi asivunje sheria halali za nchi,lakini kiuhalisia bado kuna chembechembe zilizorithiwa kutoka katika mfumo wa chama kimoja ambapo mawazo tofauti ni sawa na uhaini.

Katika zama za chama kimoja,hoja kama ile ya “chama kushika hatamu” zilisaidia baadhi ya mafisadi wa wakati huo kupata kinga dhidi ya wale maovu yao.Sote tulikuwa ni Watanzania tusio na tofauti,tunaoamini kwamba ili nchi yetu iendelee tunahitaji ardhi,watu,siasa safi na uongozi bora.Mwalimu aliamini kuwa hiyo ni njia sahihi ya maendeleo kwani alishuhudia namna ilivyofanikiwa sehemu kama China na Cuba.Kosa lake ni kuamini kwamba walio karibu yake walikuwa na imani ya dhati kama yeye.Angalau leo tunawajuwa wanafiki hawa,lakini kwa sababu za “kulinda umoja wa kitaifa” na kutaka “wapumzike kwa amani” tunaendelea kuwaheshimu kwa kutowaumbua hadharani.

Kumkosoa mzazi ni kosa,na kwa mwananchi wa kawaida au hata kiongozi kumkosoa Rais inaweza kutafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu.Hata hivyo,kutoa ushauri kwa heshima na taadhima ni jambo linalokubalika.Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana naamini kwamba wakati Watanzania wengi wanakubaliana na mtizamo wa Rais Kikwete kuhusu kutenganisha siasa na biashara,ni vema katika utekelezaji wa dhamira yake hiyo akaweka maanani namna Baba wa Taifa alivyosalitiwa na baadhi ya watu wake wa karibu.

Nasema hivyo kwa sababu naamini hata zikiwekwa sheria nzuri namna gani za maadili ya uongozi,pasipo kutengeneza mazingira yatakayozuia wasimamizi wa sheria hizo kuzihujumu,itakuwa ni kazi bure.Mwanasiasa anaweza kabisa kutangaza kwamba biashara zake za awali zimekabidhiwa kwa wadhamini flani,lakini pasipo usimamizi mzuri mfanyabiashara huyo anaweza kuendelea kuendesha biashara zake huku akiwa mwanasiasa japo machoni mwa umma anaonekana ametekeleza sheria hiyo tarajiwa ya kutenganisha biashara na siasa.

Mfano mzuri wa ninachosema ni hili sakata linaloendelea la fedha za EPA huko Benki Kuu.Yayumkinika kubashiri kwamba kama itafikia hatua ya watu flani kupelekwa mbele ya vyombo vya sheria,kuna uwezekano watu hao wakawa ni wamiliki “hewa” ambao majina yao yalitumika tu kuficha wamiliki halali.Katika mazingira ambapo taasisi kama TAKUKURU ilikuwa ya kwanza kudai mradi wa Richmond haukuwa na harufu ya rushwa ilhali sasa tunaona suala hilo likiwaka moto huko bungeni,tutarajie nini pindi wakipewa jukumu la kuhakikisha mfanyabishara anayetaka kuingia kwenye siasa kweli amekabidhi biashara yake kwa wadhamini kama sheria itakavyokuwa inataka?

Mwisho,kikao kinachoendelea cha bunge kimeonyesha dalili kwamba baadhi ya wawakilishi wetu wamechoka kupiga mihuri kupitishwa miswada inayoonekana mizuri machoni lakini inaishia kwa mashirika kama ATC kununua ndege mbovu,TANESCO kujikuta hohehahe kwa kulipa madeni yaliyosababishwa na walafi flani wasio na uchungu na taifa au kuletewa umeme hewa ulioahidiwa na makampuni ya kisanii.Hoja hapa sio kuitupilia mbali miswada ya manufaa kwa taifa au kuchochea upinzani dhidi ya serikali bali kuwabana mafisadi wote wananaotumia nyadhifa zao kulikamua taifa letu.
BAADA YA POLITIKI ZA BONGO,HEBU ANGALIA HIZI ZA NAS KUHUSU THE N-WORD


20 Jan 2008

Makala hii ilitoka kwenye gazeti la Mtanzania siku ya Alhamisi 17Jan 2008.

Hatimaye ugavana wa Dkt Daudi Ballali katika Benki Kuu ya Tanzania umetenguliwa.Sijui kama utenguzi huo ni sawa na tunachosoma,kuona na kusikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwamba Balali amefukuzwa kazi.Pengine la muhimu kwa sasa ni kwamba mtu huyo ametolewa katika wadhifa huo japo la muhimu zaidi ni kuweka rekodi vizuri kwa minajili ya kuondoa utata uliojitokeza hasa katika neno “KUTENGUA”.

Kuna wanaosema kwamba Ballali ametolewa kafara hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba sio rahisi wizi mkubwa namna hiyo uwe umefanywa na mtu mmoja tu.Ni vigumu pia kuamini kwamba uamuzi wa gavana huyo wa zamani kuyazawadia makampuni yaliyotajwa kwenye ufujaji wa fedha hizo ulifanywa na mtu mmoja pekee (Balalli).

Sakata hili lilisabaisha,linasababisha na litaendela kusababisha maswali mengi zaidi kuliko majibu.Sijui kuna wazalendo wangapi hapo Benki Kuu, lakini nashawishika kuhoji uzalendo wao kwani japo si kila mtumishi angeweza kufahamu alichokuwa akifanya Balali na washirika wake,ni dhahiri wapo waliokuwa katika nafasi ya kutoa taarifa kwa vyombo husika lakini wakaamua kukaa kimya.

Nadhani kuna waliojua kinachoendela lakini wakaa kimya kwa vile nao walikuwa washiriki katika ufisadi huo.Hawa hawana cha kujitetea kwani hawana tofauti na Balalli na wanachostahili ni adhabu tu.Kikwazo kikubwa kinachojitokeza katika uwezekano wa kuwaadhibu waungwana hawa ni ukweli kuwa baadhi yao wamepewa nafasi ya kujichunguza wenyewe (kwa vile bado wako madarakani) na sote tunaelewa kwamba hawawezi kujihukumu.Sanasana wataishia kuharibu ushahidi muhimu katika uchunguzi mzima wa ufisadi huo.

Kundi la pili ni wale waliokuwa wakifahamu kinachoendelea lakini hawakuchukua hatua kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kauli za utetezi zilizokuwa zikitolewa na watu mbalimbali pindi tuhuma za ufisadi huo zilipoanza kuibuka.Tunakumbuka kwamba kuna wakati huko bungeni lilitolewa tishio la kumfikisha Dr Slaa mbele ya vyombo vya sheria akituhumiwa kwamba ameghushi nyaraka zinazohusiana na sakata hilo.Yayumkinika kusema kwamba kauli kama hizo zinaweza kuwa ziliwakwaza baadhi ya watumishi wa Benki Kuu (waliokuwa na ufahamu wa ufisadi huo) kuripoti kuhusu uhuni uliokuwa ukiendelea hapo.
Imeripotiwa pia kwamba moja ya makampuni ya ukaguzi wa mahesabu ya benki hiyo iliripoti kuhusu kasoro zilizokuwepo lakini ikaishia kuona mkataba wake na benki hiyo ukisitishwa.Ni rahisi kukubaliana na “busara” hii kwamba kama kampuni iliyolipwa kuchunguza mahesabu imepuuzwa je “nani atanisikiliza mie niliyeajiriwa kufanya majukumu mengine katika Benki Kuu”.

Miongoni mwa madhara ya kulea ubadhirifu ni kujengeka kwa imani (miongoni mwa wasiojihusisha na ubadhirifu huo) kwamba ubadhirifu sio dhambi kwani ingekuwa haukubaliki basi wahusika wasingeendelea nao pasipo kuchukuliwa hatua.Yeyote aliyehusika na skandali hiyo lakini bado yuko madarakani ni sawa na kansa ambayo isipodhibitiwa inasambaa katika mwili mzima.Ni kama katika familia yenye watoto kadhaa na baadhi yao wanajihusisha na tabia zisizofaa.Ni dhahiri wale wanaoepuka tabia hizo (ilhali wenzao wanaendelea nazo) wanaweza kushawishika kuiga tabia hizo hususan kama wanaona wenzao wananufaika kwa namna flani.

Nakumbuka hivi karibuni,mkongwe wa siasa Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alinukuliwa na gazeti moja akieleza masikitiko yake kuhusu namna uzalendo unavyopungua miongoni mwa Watanzania.Ni kweli uzalendo umepungua sana na tusipokuwa makini utapotea kabisa lakini kuwa na wasiwasi au kulalamika pekee hakuwezi kusaidia kurekebisha mambo.Ni dhahiri kwamba moja ya mambo yanayochangia kupungua uzalendo ni pamoja na ufisadi kama huo uliofanyika hapo Benki Kuu.

Hivi mtu atakuwaje mzalendo iwapo wakati yeye anahangaika kutafuta fedha za kumwezesha kupata angalau mlo mmoja wa siku kuna wajanja wanatumbukiziwa mamilioni ya shilingi kwenye makampuni yao pasipo kuvuja tone moja la jasho.Kibaya zaidi na pengine katika kuwaringia walipa kodi wanaoibiwa,mafisadi hawaogopi kuonyesha namna wizi wao “unavyolipa” kwa kuporomosha mahekalu ya gharama kubwa,magari ya thamani ya kutisha na vimbwanga vingine chungu mbovu.Ni kama mtu anakupora mke halafu kesho yake unamwona anatamba nae mtaani.Hii inaongeza chuki na hasira kwa aliyeibiwa.

Kila zinapojitokeza tuhuma za ufisadi huwa nashindwa kujizuia kuhoji uwezo wa TAKUKURU katika jukumu lake la kuzuia na kupambana na rushwa.Taasisi hii imekuwepo kwa muda mrefu sasa lakini bado ni legelege licha ya jitihada kadhaa zilizokwishafanywa iwe na ufanisi zaidi.Naafikiana na baadhi ya hoja kwamba matendo mengi ya ulaji fedha za umma hayafanyiki hadharani,hivyo kusababisha ugumu katika kuyabaini.Hata hivyo,katika sakata hili la ufisadi hapo BoT,tetesi zilikuwepo mtaani na magazetini kwa muda mrefu.Kama ilivyozeleka,kauli za TAKUKURU zilikuwa “taarifa hizo tunazo na tunazifanyia uchunguzi”.Ikumbukwe kwamba katika mazingira ambayo matatizo yanazaliana kila kukicha,kuchelewa kutatua tatizo moja ni sawa na kutengeneza mlima wa matatizo hayo ambapo mwisho wake itakuwa ni suala lisilowezekana kabisa kuyaondoa.

Pengine umefika wakati mwafaka kwa wawakilishi wetu huko bungeni kuhoji uhalali wa kuendelea kuwa na taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa.Kanuni ya haki katika sheria inatamka waziwazi kwamba haki sio tu itendeke bali pia ionekane imetendeka.Tunaweza kuitumia kanuni hiyo kwa TAKUKURU pia kwamba mapambano dhidi ya rushwa yasiishie tu kuwa ya dhamira bali yaonekane hadharani kuwa yapo na yana ufanisi unaotarajiwa.

Naweza kuonekana mtu wa ajabu iwapo nitashauri kuvunjwa kwa TAKUKURU lakini nina hoja ya msingi napofikiri hivyo.Mamilioni ya fedha yanayoelekezwa kwa taasisi hiyo kupambana na rushwa hayajasaidia lolote katika kupunguza tatizo hilo.Mabadiliko mbalimbali ya kisheria yaliyolenga kuipa meno taasisi hiyo nayo yameshindwa kuifanya iwajibike ipasavyo.Binafsi sioni cha ziada kinachoweza kubadili ulegelege wa taasisi hiyo zaidi ya kuivunjilia mbali na kasha majukumu yake kuhamishiwa kwenye taasisi nyingine kama vile kitengo cha upelelezi katika jeshi la polisi (CID).

Kwa kuzingatia rekodi ya TAKUKURU katika uendeshaji wa kesi inazopeleka mahakamani,sintoshangaa iwapo wanaotajwa kwenye sakata hilo wataishia kuibuka washindi kwenye kesi hizo.Tumeshuhudia namna taasisi hiyo ilivyokuwa “ikipelekeshwa” kwenye kesi dhidi ya Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia.Kama kesi ya mtu mmoja imekuwa ngoma nzito namna hiyo,tutarajie nini kwenye lundo la kesi linalowahusu watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha?

Wengi wanatafsiri vurugu zinazoendelea nchini Kenya kuwa ni matokeo ya ukabila.Lakini baadhi ya wachambuzi wa uchumi wananyumbulisha kwamba vurugu hizo ni sehemu tu ya mapambano ya kiuchumi kati ya wenye nacho na wasio nacho.Migongano ya kidini au kikabila hujichomoza zaidi kwenye jamii isiyo na uwiano wa kimapato kwani mara nyingi washiriki kwenye vurugu hizo huamini kwamba pindi zikifanikiwa zitarekebisha maisha yao ya kila siku.Tuna kila sababu ya kuzuia nchi yetu inayosifika kwa amani na utulivu isiingie kwenye machafuko yanayoweza kusababishwa na wengi wanaoona wachache wakinufaika kwa “ulafi wa kula keki ya taifa” huku wao (wengi hao) wakiendelea kutaabika.Kinachowezekana leo kisingoje kesho.

17 Jan 2008


Gavana mpya wa Benki Kuu,Profesa Benno Ndulu,amefanya mabadiliko kadhaa katika uongozi wa benki hiyo.Katika mabadiliko hayo,Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala (DAP) wa B.O.T,AMATUS LIYUMBA (pichani) ameondolewa katika wadhifa huo.Habari kamili soma hapa.
(Picha hii ya zamani ya Liyumba ni alipokuwa Mkuu wa Chuo cha BoT 1993-2000)

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.