10 Jun 2010

Uandishi wa blogu si jambo rahisi kama inavyodhaniwa na wengi.Na ni jambo gumu zaidi kwa akina sie tunaoelemea zaidi katika kuandisha mambo yanayogusa maslahi ya mafisadi na vibaraka wao.Kwa mfano mara kadhaa nimekuwa nikipata comments zenye matusi ya kila aina kutoka kwa baadhi ya wasomaji.Huwa siyachapishi matusi hayo kwa vile naamini wanaotukana wana mtindio wa mawazo na tafakuri.Hoja hujibiwa kwa hoja na wala si matusi.

Ninafahamu matusi hayo yanatoka wapi,na pia natambua kwanini badala ya hoja zangu kujibiwa kwa hoja zao wanakimbilia kutukana.Ni hivi,ukiona mtu anakusema vibaya au kukutukana wakati hujamkosoea lolote ujue mtu huyo hana zuri upande wake,na maneno mabaya au matusi dhidi yako inakuwa kama njia ya mkato ya kupunguza matatizo yake.Watu wa aina hii wanahitaji ushauri nasaha badala ya kuwatukana.Na kibaya zaidi ni kwamba ukimtukana chizi,basi watu watashindwa kutofautisha kati ya nani mzima au mwenye busara na nani chizi.

Lakini wapenda matusi hawa wananipa faraja moja kubwa.Kwamba hadi kufikia hatua ya kutukana kwa njia ya comment kwenye blogu hii inamaanisha walitumia muda wao kusoma nachoandika.Hiyo ni faraja kubwa kwangu kwani walengwa wangu wakuu ni watu makini na sio vichwa panzi kama hao mabingwa wa matusi.

Ujumbe wangu mfupi kwa wazembe hao wa kufikiri ni huu: kasheshe nilizokumbana nazo huko nyuma kutokana na mtizamo wangu ni mara alfu ya hivyo vijimatusi mnavyotuma kama comments.Kwahiyo endeleeni kupoteza muda wenu kutukana lakini mkae mkifahamu kuwa mnachofanya ni sawa na kutegemea damu kutoka kwenye jiwe.

Anyway,nasikitika kupoteza muda wangu muhimu kuwazungumzia wazushi hawa.Lakini yote katika yote,hivi ni vijimambo tu ambavyo once ukiingia kwenye fani ya kublogu lazima utakumbana navyo.

Bring it on!

9 Jun 2010

WAKATI bajeti ya Serikali inasuasua kutokana na uhaba wa fedha za ndani, familia moja ya Dar es Salaam inayomiliki kampuni inayojihusisha na biashara ya bidhaa za nyumbani imejiingiza katika uwakala wa forodha kwa staili ya aina yake ikiwa ni pamoja na kujikita katika kuwasaidia wafanyabiashara wengine kukwepa kodi; huku wahusika wakijiwekea kinga kwa wanasiasa, Raia Mwema imeelezwa.


Biashara hiyo ya aina yake ya uwakala wa ukwepaji kodi, imeelezwa kuipotezea serikali mabilioni ya shilingi ambazo zilistahili kukusanywa kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wanaoingiza bidhaa mbalimbali kutoka China na Dubai; huku baadhi ya wanasiasa wenye nguvu serikalini na familia zao wakiwa nyuma ya uhalifu huo.


Vyanzo vya habari ndani ya serikali vimelieleza Raia Mwema kwamba familia hiyo yenye vijana watatu wenye asili ya kiasia ilirithi biashara ya wazazi wao ya kuuza plastic carpets (mazulia ya plastiki), door mats (mikeka ya milangoni), taulo, mapazia na mashuka na baadaye kuamua kuingia katika “uwakala wa ukwepaji kodi”.

Habari za ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zimeeleza kwamba mamlaka hiyo imekuwa ikifuatilia kwa makini suala hilo pamoja na kuwapo taarifa za uhakika kwamba maofisa waandamizi wa mamlaka hiyo wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara hao kukwepa kodi.

Mbali ya kuwahusisha watumishi wazito ndani ya TRA, vijana hao wameelezwa kuingizwa katika orodha ya “wachangiaji wakubwa” wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwa karibu na wanasiasa binafsi ndani ya chama hicho tawala.

Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba hayuko katika nafasi ya kufahamu kila kitu kinachoendelea ndani ya mamlaka hiyo kwa nafasi yake kwa kuwa kila eneo linaongozwa na kamishna wake na “kwa suala hilo anayepaswa kuzungungumzia ni Kamishna wa Forodha.”

Pamoja na kuelezwa kwamba TRA wanazo taarifa za ukwepaji kodi huo na kwamba wamekwisha kuanza uchunguzi, Kitilya alisema: “hilo suala liko chini ya Kamishna wa Forodha na mwenzake Kamishna wa Uchunguzi ambao ndio wanapaswa kulitolea ufafanuzi.”

Raia Mwema ilipomweleza Kitilya kwamba habari za kampuni hiyo kukwepa kodi zimeshawahi kumfikia na ofisi yake kuzitolea maelekezo, alisema, “Ndio kwanza leo unanieleza kuhusu kampuni hiyo, mimi sina taarifa kabisa labda uwatafute Kamishna wa Forodha na wa uchunguzi.”

Hata hivyo, maofisa wa ndani ya TRA wamelieleza Raia Mwema kwamba wafanyabiashara hao vijana wakiongozwa na kaka yao (jina tunalihifadhi kwa sasa), walikuwa wakiagiza bidhaa hizo kutoka nje kupitia bandari ya Tanga kati ya mwaka 2000 hadi 2004 mahali ambako walianza kuwa “mawakala wa ukwepaji kodi”.

“Kutokana na kuzoeleka kwao kwa maofisa wa forodha katika bandari ya Tanga wakati huo, walianza pia kupokea nyaraka za waingizaji wengine wa mizigo tofauti, na kuwasaidia kuivusha kwenye ofisi za Forodha kwa njia za ujanja ujanja.

“Wakati huo hawakuwa na kampuni ya uwakala, walitumia kampuni mbalimbali za kukodi na kutokana na kukua kwa biashara yao na ‘uwakala wao pori’, walijizatiti wakaanzisha mtandao wa kazi kwa kunyoosha au kusafisha njia tangu mizigo inapotoka Tanga hadi kwa wateja Dar es Salaam,” anasema mtoa habari wetu ambaye anafahamu kwa kina mitandao ya ukwepaji kodi.

Imeelezwa kwamba katika ‘kusafisha njia’ walitumia fedha kujitambulisha kwa maofisa forodha na polisi waliokuwa barabarani kudhibiti magendo kwenye vituo muhimu vya udhibiti kama Segera na Kabuku mkoani Tanga; Chalinze na Kibaha mkoani Pwani na kuendelea hadi wakaguzi wengine ndani ya jiji la Dar es Salaam.

“Lakini mwaka 2004 hali ya hewa ya bandari ya Tanga ilibadilika kwa Idara ya Forodha kuziba mianya ya rushwa lakini kwa kuwa vijana hawa walikwisha kuzoea kudanganya katika ulipaji ushuru, ilibidi wahamishie shughuli zao kwingine. Wakaelekeza nguvu zao zote Holili, Kilimanjaro, wakifanya yaleyale waliyokuwa wakiyafanya bandarini Tanga,” anasema mtoa habari wetu.

Imeelezwa kwamba wafanyabiashara hao waliendelea kutoa mizigo Holili kwa muda kati ya mwaka 2004 na 2006 mwishoni walipohamia rasmi bandari ya Dar es Salaam ambako sasa wamekita mizizi.

“Mtandao wao wa Dar es Salaam ni mkubwa wakiwa wameteka mamlaka zote zinazohusika na kodi. Ni mtandao ulioenea kutoka Dar es Salaam hadi nje ya nchi. Zimefunguliwa ofisi Hong Kong na Guanzhou, China na Dubai. Ofisi za nje hutumika kupokea mizigo inayoingia nchini.

“Mwagizaji wa mali yoyote kama nguo, hardware au vifa vya umeme hufanya manunuzi kwenye maeneo hayo na hupewa gharama zote za kufikisha mzigo Dar es Salaam pamoja na ushuru wa forodha na gharama nyinginezo hadi kweye bohari yao iliyopo Dar es Salaam,” kinaeleza chanzo kingine ndani ya serikali.

Imeelezwa kwamba mwagizaji anakabidhi mzigo ofisini China na anakabidhiwa mali yake Dar es Salaam baada ya siku kadhaa kati ya wiki tano hadi sita.

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini viwango vya gharama zao kwa baadhi ya mali ni kama ifuatavyo:

Kusafirisha na kutoa bandarini vifaa vya ujenzi hutoza Dola za Marekani 350.00 kwa meta moja ya ujazo(1 cbm).
Kusafirisha na kutoa bandarini bidhaa za nguo ni Dola za Marekani 450.00 kwa meta moja ya ujazo (1 cbm).
Kusafirisha na kutoa bandarini bidhaa za umeme kama swichi, circuit breakers na viginevyo ni usd Dola za Marekani 500.00 kwa meta moja ya ujazo (1 cbm).
Mizigo maalumu kama vitenge-mazungumzo hufanyika na bei maalumu hukubaliwa.
“Kinachotisha katika utaratibu huu ni kwamba wakati gharama za usafiri wa meli hupatikana kutegemea uzito na ujazo wa mali, wao wamefika mbali zaidi kwa kukadiria ushuru na kodi za Serikali kwa ujazo (yaani cubic measurements). Kwa kawaida ushuru wa forodha hutozwa kwenye Thamani halisi ya Manunuzi, Bima na Gharama za Usafiri hadi nchini (Cost, Insurane and Freight) na si vinginevyo,” anasema mtumishi mmoja wa TRA mwenye ufahamu wa biashara hiyo akidai kwamba biashara hiyo huwa na ulinzi wa ‘wakubwa’.

Ofisa huyo wa TRA ameendelea kwa kusema, “(wafanyabiashara hao vijana)... hutoza kwa kukadiria na kwa ajili hii wanapata faida kubwa kwa kuwa mfumo mzima umewabeba kuanzia mashirika kama Tiscan ambako nyaraka hupelekwa kuthamishwa (jukumu walilopewa Tiscan kwa mujibu wa mkataba na TRA) hadi bandarini ambako mizigo huruhusiwa kutoka baada ya taratibu zote kukamilika.”

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kwamba waagizaji wanaopitia mkondo wa vijana hao wamekuwa wakishangaa jinsi mizigo yao inavyoweza kutolewa bandarini bila wao kudaiwa ankara za manunuzi (invoices) wanazokabidhi katika ofisi za China na Dubai.

Wanachoulizwa China na Dubai ni orodha ya mali (packing list) jambo linaloashiria uhalifu wa kutisha kutokana na kudhihirika kwamba ankara za mizigo zinazopelekwa Idara ya Forodha ni za kughushi na hazina uhalisi wowote.

“Kwa kawaida mali au mizigo ya thamani ya manunuzi ya Dola za Marekani 10,000.00 na zaidi (FOB Cost) huwa inauliziwa bei na ubora wake kwenye nchi ilikotoka. Kwa hiyo kwa mteja anayepata huduma kwa hawa watu, nyaraka zake zikifikishwa Tiscan ambayo ni kampuni tanzu ya Cotecna International, wanaulizia kwenye hiyo nchi iliyouza mali hiyo kuja kwetu! Kwa vile hawa watu wamesajili kampuni China na Dubai na nyaraka (invoices) wamezitoa wao, hivyo Tiscan inapata majibu kutoka kwa watu walewale. Mapato ya Serikali yanahujimiwa kuanzia hapa,” anasema ofisa mwingine wa serikali ambaye amewahi kukwama kudhibiti uhalifu huo.

Habari za ndani ya sekta ya forodha zinaeleza kwamba kutokana na mafanikio yao katika kukwepa kodi, wamefikia hatua ya kuhodhi utoaji bandarini wa aina fulani ya bidhaa.

“Sasa ni vigumu sana, na kwa kweli hakuna wakala mwigine anayethubutu kutoa bandarini bidhaa za nguo kwa kuwa nyaraka za kampuni nyingine zifikapo Tiscan au Longroom huwekewa bei za juu ambazo hazilipiki ili kuwakatisha tamaa waagizaji ambao kwa sasa wamechoshwa na huduma za vijana hawa zilizojaa kiburi na dharau.

“Hali hiyo imewafanya waagizaji kukosa pa kwenda bali kwa vijana hao na wakabaki wakisikitika jinsi vyombo vya dola vinavyowekwa mfukoni kwa hasara ya jumla ya Taifa. Waagizaji wanalalamika kwamba hawana tena uhuru kwa kuwa wanalazimika kutumia kampuni moja tu ambayo bei zake hazina majadiliano. Ukienda kubembeleza unaambiwa katafute wakala mwingine ambaye hata hivyo huwezi kumpata kwa kuwa hawa wamehodhi kila kitu,” anaeleza mtoa habari wetu ndani ya sekta ya kodi.

Mfanyabiashara mmoja mzalendo ameliambia Raia Mwema kwamba vijana hao wamewakatisha tamaa wafanyabiashara wengi huku wao wakiwa na uwezo wa kutoa bandarini mizigo siku na wakati wanaotaka wao.

“Wanatoa inapofika fleet ya magari kama 20 kwa wakati mmoja. Wanafanya hivyo baada ya kusafisha njia au kusubiri siku ambayo hakuna ‘wanoko’ kwenye shift fulani huko Forodha. Inawasaidia pia katika mambo ya rushwa kwani fungu moja linatolewa kwa ajili ya makontena mengi zaidi. Hii ina athari kwa sisi waagizaji ambao kontena zetu nne au tano zinaweza kuwa zimefika mapema, lakini ikabidi zisubiri nyingine kwa wiki nne au tano ili nyaraka ziende pamoja na gharama (rushwa) iwe ndogo,” anaeleza mfanyabiashara huyo mwenye ofisi zake maeneo ya Kariakoo.

Mfanyabiashara huyo anaeleza kwamba kwa hali halisi iliyopo kwenye mfumo wa ukusanyaji kodi, ni vugumu kukwepa ushuru kwa kudanganya kiasi (idadi) cha mali kilichomo kwenye kontena (false declaration) au kuweka bei ndogo au ya chini ya ile bei halisi (under invoicing), lakini kwa kampuni hiyo hilo linawezekana kwa kuwa mfumo mzima tangu serikalini, Tiscan na TRA umekuwa nyuma yao kutokana na nguvu kubwa waliyonayo vijana hao.

Imeelezwa kwmaba kwenye kampeni za mwaka 2005 kampuni hiyo ilichangia chama tawala Sh. Milioni 200 na kwamba katika mwaka huu wameahidi kuchangia milioni 500 huku ofisini kwao zikiwa zimejaa picha walizopata kupiga na viongozi wa juu wa chama tawala na Serikali katika hafla za uchangiaji kampeni.

Ili kufahamu kiasi cha mapato ya Serikali yanayopotea angalia hesabu hizi:

Kontena la nguo za kawaida lenye urefu wa futi 20 laweza kuwa na thamani ya Dola za Marekani 60,000.00 hadi Dola za Marekani 80,000.00 kutegemeana na aina, ubora na idadi ya nguo zenyewe. Ushuru wa jumla ni 48% ya thamani halisi (cif value). Kwa hiyo kama thamani ni Dola za Marekani 60,000.00 x 48% = Dola za Marekani 28,000. Kwa thamani ya Dola 1 ya Marekani = Sh.1400, ushuru kwa kontena hili katika shilingi ni 40,320,000.
Kama kontena ni la thamani ya USD 80,000, ushuru ni 80,000.00 x 48% ambazo ni sawa na Dola za Marekani 38,000.00 na kwa Sh ni 53,760,000.

Kwa mujibu wa habari za ndani ya TRA, vijana hao wanakadiria gharama zote kwa meta za ujazo kutoka China hadi Dar es Salaam, na hivyo kontena la futi 20 ambalo lina meta za ujazo 36, ina maana gharama zote ni Dola za Marekani 450 x 36 = Dola za Marekani Dola za Marekani 16,200 ambazo ni sawa na Sh. milioni 22.68.

Ikiwa utaondoa gharama halisi za kusafirisha kontena hadi Dar es Salaam ambazo ni Dola za Marekani 2,500, basi kinachobaki ni Dola za Marekani 16,200 – 2500 = Dola za Marekani 13,700.00 au Sh. 19,180,000.

Uchunguzi wa Raia Mwema umeonyesha kwamba sehemu kubwa ya fedha hutumika katika kulipia ushuru kidogo, rushwa kwa maofisa sehemu mbalimbali husika, gharama za bandari na usafiri wa bandarini kwenda kwenye maghala yao.

“Kwa uzoefu wangu hawa jamaa kontena la nguo la futi 20 hawalipi zaidi ya Sh. milioni 10. Hii ina maana ya kuwa badala ya kulipia gharama halisi ya zaidi ya Sh. milioni 40 wao wanalipa milioni 10 tu. Kwa hiyo, kwa mfano mmoja tu, Serikali hupoteza Sh. milioni 30 kwa kila kontena la nguo la futi 20 linalotoka bandarini. Ikiwa makontena 100 yanaweza kutoka bandarini kwa wiki moja, ina maana serikali hupoteza milioni 30 x 100 = bilioni 3 kwa wiki. Kwa mwaka mmoja hii ni sawa na shilingi bilioni 156,” anaeleza mtaalamu wa kodi ambaye kwa sasa ni mstaafu.

.
CHANZO: Raia Mwema

8 Jun 2010

Rais Kikwete akikabidhi zawadi ya kinyago kwa mchezaji wa Brazil,Kaka,huku mtoto wa Rais,Ridhiwani Kikwete (kulia kwa Rais),akishuhudia na "tabasamu la haja" (Picha kwa hisani ya Ankal Michuzi)

Niite mzandiki,mkosoaji wa kila kitu,au hata mpuuzi.Yote sawa.Lakini haihitaji upeo hata wa mtoto mchanga kutambua kuwa uamuzi wa "kununua" kipigo cha mabao matano kutoka kwa Wabrazili ilhali tumegubikwa na matatizo lukuki ya kiuchumi ni,well,upuuzi.

Nilishabashiri awali kuwa baada ya mechi kati ya Taifa Stars na Wabrazili itakuja mechi kali zaidi kuhusu faida au hasara za mechi hiyo.Na hapa nazungumzia fedha.Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),mechi hiyo ilifanikishwa na mkopo wa benki flani kwa Shirikisho letu la Soka chini ya uongozi wa Leodgar Tenga.Inaelezwa kuwa TFF walitarajia mpambano huo ungeingiza takriban dola milioni tatu ambazo zingerejesha gharama zinazokisiwa kuwa dola milioni mbili unusu (zaidi ya shilingi bilioni tatu)walizotumia "kununua" mechi hiyo.Kwa akili ya Tenga na wenzake,walitarajia uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 ungefurika na pengine kuzalisha faida kubwa zaidi ya hizo dola milioni tatu zilizokisiwa.Sijui ni kufumbia macho umasikini unaowakabili Watanzania wengi au ni ubishi tu,TFF wakaweka viingilio vya juu na vitakavyoingia kwenye vitabu vya historia ya soka la Tanzania.

Sidhani kama tutafahamisha gharama halisi za mechi hiyo wala kuelezwa hasara kamili.Na si kwamba tutafichwa kwa sababu ya aibu ya waandaaji bali kuna "wajanja" (isomeke MAFISADI) watakaoongeza ukubwa wa hasara hiyo kwa kujirejeshea gharama wasizostahili.Lakini pamoja na usiri huo,tovuti ya BBC imemnukuu Waziri wa Habari na Michezo George Mkuchika akisema kuwa serikali haikuchangia chochote katika "ununuzi" wa mechi hiyo,na akatupa "kigongo" kingine kwa kudai TFF walikopa fedha kutoka benki kumudu gharama hizo.

Lakini kauli ya Mkuchika inakinzana na kauli ya awali iliyotolewa na Tenga,ambapo kwa mujibu wa tovuti ya gazeti la Daily Nation,alinukuliwa akieleza kuwa (nanukuu) "Tuliongea na Rais wetu (Jakaya Kikwete),na ni yeye ndiye aliyewezesha mechi hii kuwezekana".Tenga alisema (nanukuu tena) "(Rais) alivutiwa tangu mwanzo na kuhakikisha kila uwezo wa dola (serikali) unawezesha mechi hiyo".

Sasa sijui nani anasema ukweli kati ya Mkuchika na Tenga.Na pengine swali la muhimu zaidi ni nani atayebeba mzigo wa deni hilo kama si mlipakodi wa Tanzania.Na ni mzigo kweli kwani dalili za wazi za uzembe wa waandaaji wa pambano hilo tunaloaminishwa kuwa litaitangaza Tanzania ni matangazo mengi ya makampuni ya kigeni badala ya vivutio vya taifa letu.Well,unatarajia nini kutoka kwa wazembe walioshindwa hata kuwa na CD  ya uhakika ya wimbo wa taifa letu?

Kuna nyakati napata shida kuzielewa kauli za Rais Jakaya Kikwete.Nafahamu kuwa yeye ni mwanadamu kama mwingine,kwahiyo anaweza kufanya makosa ya kibinadamu.Lakini kwa vile nyingi ya hotuba zake huandaliwa na wasaidizi wake,nafasi ya makosa ya kibinadamu inapaswa kuwa ndogo.

Huko nyuma tumeshasikia kauli kadhaa tata kutoka kwa Kikwete,ikiwa ni pamoja na ile maarufu ya aliyotoa Mkoani Rukwa mwaka 2006 kwamba "anawajua kwa majina wala rushwa katika wizara na kwamba nguvu anayokwenda nayo siyo ya soda"(na ameishia kutoa indefinite deadline),kisha ile ya Bandarini Dar kuwa "ana orodha ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi kwenye Bandari ya Dar es Salaam" (lakini licha ya kuahidi kukabidhi orodha hiyo kwa Kamishna wa TRA hajafanya hivyo hadi leo) ,sambamba na ile ya "sijui kwanini Tanzania ni masikini" (kama hajui atawezaje kuleta maisha bora).Kauli nyingine tata ni hii ya majuzi kuwa "takrima haikwepeki" (ambapo tafsiri ya jumla ni sawa na kuruhusu rushwa),na jana nimeona mahali akisema "Haiwezekani kuua albino halafu utajirike, ingekuwa hivyo albino wenyewe wangekuwa matajiri wakubwa mno,”.Na sasa amekuja na kauli nyingine tata kuwa "matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe".Kadhalika,sambamba na kauli hiyo Mkuu wetu wa nchi alinukuliwa akisema "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe na wengine ni viherehere vyao; kwa mfano watoto wa shule"




Tukiweka kando hizo kauli tata za huko nyuma,hii ya mimba za wanafunzi imenisukuma kuandika makala hii.Hivi ina maana Rais hafahamu kuwa baadhi ya mimba za wanafunzi zinachochewa na mabazazi wa kiume au mafisadi wa ngono wanaotumia fedha zao za kifisadi kuwarubuni mabinti hawa?Sawa,tunaweza kuwalaumu mabinti hawa wanaorubuniwa lakini ni muhimu kuangalia suala hili kwa undani zaidi kwani wengi wa wanafunzi wa kike wanaoishia kutundikwa mimba na mafisadi wa ngono wanatoka familia masikini na inawawia vigumu kukabiliana na vishawishi vya mabazazi hao.

Kwa kudai kuwa sababu kuu ni kiherehere cha mabinti hao,Rais anatupa lawama kwa asilimia 100 kwa wanafunzi hao wa kika kana kwamba wanajidunga mimba wao wenyewe.Kwanini,yeye kama mwanaume,asiangalie upande wa pili wa shilingi?Kwanini,kwa mfano,sambamba na kudai kuwa tatizo ni kiherehere cha wanafunzi hao angewashutumu pia wakware wanaowinda wanafunzi?Kwa tunaofahamu siasa za mtaani,licha ya kuwa ni uzinzi pekee,wakati mwingine tamaa ya wanaume wakware kwa wanafunzi au mabinti wadogo inakuzwa na imani potofu kuwa "dogodogo hawana ukimwi" au "hawana gharama kuwatunza",na ushenzi mwingine kama huo.Na hii yote ni mitazamo ya wanaume ambao wamesalimika katika shutuma hizo za Kikwete.

Tukija kwenye kauli yake kuwa "Kila anayepata Ukimwi anaufuata mwenyewe..." ni dhahiri kuwa aidha Rais hajui namna ukimwi unavyoambukizwa au anapuuza njia nyingine za maambukizo.Japo ni kweli kuwa njia kuu ya maambukizo ya ugonjwa huo hatari ni tendo la zinaa,lakini licha tu kuwa hiyo sio njia pekee bali pia si kila anayeambukizwa "anaufuata mwenyewe".Vipi kuhusu akinamama au akinababa wanaoletewa ukimwi na wenza wao wasio waaminifu?Takwimu kadhaa zimekuwa zikutuonyesha kuwa asilimia ya wanandoa walioathirikia kwa ukimwi ni kubwa kama ilivyo kwa wasio wanandoa,na hiyo ilipaswa kumfahamisha Rais kuwa "kuna wanaoletewa ukimwi" na sio "kuufuata wenyewe" kama anavyoamini yeye.

Tukienda mbali zaidi,kauli hiyo ya Rais inaweza kutafsiriwa kama kuwanyanyapaa waathirika wa ukimwi,hususan wale walioambukizwa na wenza wao,au walioupata kwa njia nyingine kama tohara na chanjo za kienyeji ambapo nyembe moja hutumika kwa watu mbalimbali na hivyo kujenga uwezekano mkubwa wa maambukizo.Na kwa vile taasisi nyingi za afya zina vifaa duni,ni dhahiri kuna wauguzi mbalimbali wanaoambukizwa ukimwi kutokana na na nyenzo hizo duni makazini mwao.Lakini kuna kundi jingine la muhimu-watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa wameshaambukizwa ukimwi.Je Kikwete anaweza kudiriki kudai hata hawa nao wameufuata ukimwi wenyewe?

Kiongozi makini anapaswa kuepuka generalisation,yaani kutoa kauli za jumla jumla pasipo kuangalia exceptions katika anachozungumzia.Na ifahamike kuwa kauli ya Mkuu wa Nchi ni sawa na mtizamo wa nchi husika,hivyo hitaji la umakini kabla ya kutoa kauli zinazoweza kuwaathiri baadhi ya wananchi.

Anyway,pengine alikuwa anatania tu wakati akisema hayo kwenye sherehe za kimila huko Mwanza ambapo miongoni mwa walikuwa kwenye msafara wake ni mtuhumiwa wa ufisadi wa rada,Mzee wa Vijisenti Andrew Chenge.

5 Jun 2010

Mwezi Februari mwaka huu,Rais wa Kampuni ya Toyota (ya Japan) Akio Toyoda aliomba rasmi msamaha kwa wateja wa kampuni hiyo nchini Marekani ambao walikumbwa na matatizo ya kiufundi kwenye magari yao.Mwezi kama huo mwaka jana,mabosi wa mabenki ya RBS na HBOS ya hapa Uingereza nao waliomba msamaha kwa wateja wao na umma kwa ujumla kutokana na uzembe uliopelekea benki hizo kukwamuliwa na serikali kwa pauni bilioni 37 fedha za walipakodi wa hapa. Na hivi majuzi,Waziri Mkuu wa Japan,Yakio Hatoyama, ametangaza kuwa atajiuzulu kufuatia kutotimiza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni zake za uchaguzi kuwa angeondoa vikosi vya jeshi la majini la Marekani katika visiwa vya Okinawa.


Lakini wakati hayo yakitokea,serikali ya CCM imewaamuru mawaziri wake kuzunguka mikoani kueleza mafanikio ya Awamu ya Nne katika harakati za wazi kuelekea Uchaguzi Mkuu.Tuweke ushabiki pembeni,hivi kweli mawaziri hawa hawakustahili kuzunguka huku na huko kuomba msamaha kwa mlolongo wa madudu tunayoendelea kuyashuhudia tangu mwaka 2005 (na pengine madudu zaidi yanayoendelea kufanywa na CCM miaka nenda miaka rudi)?


Msanii mkongwe wa hapa Uingereza (na duniani kwa ujumla),Sir Elton John aliwahi kuimba wimbo wenye jina SORRY SEEMS THE HARDEST WORD (yaani 'samahani inaelekea kuwa ni neno gumu').Na hakukosea,japo hakuwa analenga siasa za nchi zetu za Dunia ya Tatu,hususan Afrika,na hasa Tanzania.Watawala wetu ni wepesi sana katika kugeuza lawama kuwa pongezi,na wakibanwa katika hilo hugeuka mbogo na kuja na vitisho lukuki.

Labda nikukumbushe kidogo kwanini naamini ziara za mawaziri zingekuwa na maana zaidi kama zingetumika kuomba msamaha kwa wananchi badala ya kuelezea mafanikio ambayo kimsingi yanabaki kwenye takwimu zaidi kuliko uhalisia.Kwanza,Awamu ya Nne ilitufahamisha kuwa inafahamu kilio cha Watanzania,na ikaja na kauli mbiu ya kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya.Naamini mie si pekee niliyesahau kuhusu kauli mbiu hiyo kwa vile wala haisikiki tena.Lakini kama hiyo haitoshi,kukaongezwa kibwagizo cha Maisha Bora kwa Kila Mtanzania (Yanawezekana).Japo sote tunatambua kuwa watawala wetu wanaishi kama wako peponi lakini hiyo sio excuse ya kuwafanya wasielewe kuwa maisha bora yamewezekana zaidi kwa mafisadi kuliko kwa wananchi walalahoi wa kawaida.Kwahiyo kama viongozi hawa wangekuwa na nidhamu kwa wapiga kura waliowaweka madarakani hapo 2005 basi angalau wangetuambia nini kinachopelekea maisha bora kubaki haki ya mafisadi wachache huku walalahoi wakizi kuwa walalawima.

Baada ya kuingia madarakani,Awamu ya nne ilitueleza kuwa ili kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kunahitajika baraza kuuuubwa la mawaziri.Binafsi niliona kuna mantiki katika hoja hiyo japo sikuwa na uhakika kuwa "mwalimu anaweza kumudu darasa lenye wanafunzi wengi" kama ilivyokuwa kwenye kabineti ya JK.Bila kuuma uma maneno,kwa kifupi ukubwa wa baraza la mawaziri haujafanikiwa kwa chochote katika ku-meet matarajio ya Watanzania.Sanasana wengine walilazimika kujiuzulu baada ya kutuingiza mkenge kwenye ishu kama za utapeli wa Richmond.Ungetegemea kujiuzulu huko kungeandamana na hatua za kisheria lakini waliojiuzulu waliishia kupongezwa huku wakikumbushwa kuwa yaliyowakumba ni ajali tu za kisiasa na si ajabu siku moja wakarejea madarakani.

Mkuu wetu wa nchi akatuambia kuwa anawafahamu wala rushwa ila anawapa muda wa kujirekebisha.Binafsi,hapo ndipo nilipoanza kuhisi kuwa sikuwa sahihi kuamini kwamba tumepata mrithi halisi wa Mwalimu (Nyerere) in the form of JK.Tangu lini mwizi akapewa deadline?Kama wala rushwa walikuwa wanajulikana kwa Rais kilichopaswa kufanywa ni yeye kukabidhi orodha hiyo kwa taasisi husika ili wachukuliwe hatua stahili.Unajua,laiti JK angekabidhi orodha ya wala rushwa anaowajua kwa vyombo vya usalama kisha wakakamatwa na kuepwa deadline,pengine by now tusingekuwa tunajiuliza wenye Kagoda ni akina nani.Ni muhimu wak Watanzania kumhoji Rais wetu mpendwa kuhusu hao wala riushwa anaowafahamu,na lini hiyo deadline ita-expire.Tunachohitaji ni majina na sio idadi,na hata kama ni idadi basi tuambiwe lini watashughulikiwa.

Tuaambiwa kuwa matatizo ya umeme yangepatiwa ufumbuzi wa kudumu only miezi michache baadaye kufahamu kuwa ufumbuzi wenyewe unahusisha matapeli wenye kampuni ya briefcase (Richmond).Shahidi muhimu katika sakata la EPA akahifadhiwa mpaka Maulana akachukua uhai wake (kuna wanaodai kuwa bado yuko hai au huenda kafanyiwa plastic surgery) halafu wenye nchi wakagoma katakata kutuambia mwizi mkubwa wa fedha za EPA (Kagoda ni nani).

Tuaaambiwa kuwa ziara za mara kwa mara za Rais wetu huko nje ni muhimu kuitangaza nchi yetu na yeye kujitambulisha,kabla ya kuaminishwa kuwa Mkutano wa Sullivan na huu wa majuzi wa Economic Forum utalinufaisha taifa hasa katika sekta ya utalii,only for tuliorogwa sie kulipa mabilioni ya shilingi kuialika timu ya taifa ya Brazil huku kukiwa na ngonjera zilezile za "ziara hii itasaidia kuitangaza Tanzania".Kama ziara za Rais huko nje na rundo la wafanyabiashara (plus mikutano kama ya Sullivan na huo wa Economic Forum) imeshindwa kuzaa matunda,dakika 90 za mechi na Wabrazili zitaweza?

Majuzi wafadhili wametangaza kupunguza misaada yao kwa sababu ya ufisadi (putting it straightforward) na Waziri wetu wa Fedha Mustapha Mkulo bila aibu anasema hiyo isitupe hofu kwa vile serikali itakopa benki ya Stanbic!Nasema "bila aibu" kwa vile sio tu kukopa sio sifa hususan kwa serikali iliyoingia madarakani na mkwara wa maisha bora kwa kila Mtanzania bali pia deni hilo litabebwa na walalahoi haohao wanaoendelea kubebeshwa mzigo wa mahela yanayokwibwa na mafisadi kila kukicha.

Haya,tukaambiwa tena kuwa kwa vile kuna mtikisiko wa uchumi wa dunia basi na hohehahe sie lazima tuyanusuru makampuni yetu katika kile kinachofahamika ki-uchumi kama "stimulus package".Hivi kwa mwenye akili timamu,ukitangaza kuwa kuna hela za bure somewhere unatagemea nini kama sio vigogo kuunda kampuni hewa na kuiba fedha hizo?Hadi leo hatujaambiwa mafanikio ya stimulus package hiyo, na kama ilivyokuwa kwenye ripoti ya mabomu ya Mbagala usitarajie kuambiwa lolote la maana zaidi ya takwimu za kizushi.

Halafu Mkuu wetu wa nchi akatupa presha kwa kuamua kuhutubia Bunge kuhusu sakata la EPA (pamoja na mambo mengine).Tunaloweza kukumbuka zaidi kwenye hotuba hiyo ni kauli yake kuwa anathamini sana haki za binadamu ikiwa ni pamoja na za mafisadi.Kumbukumbu nyingine ni angalizo kutoka kwa Spika wa Bunge,Samweli Sitta,kuwa haki za binadamu za walalahoi ni muhimu zaidi kuliko za hao mafisadi.

Nimejitahidi kuorodhesha machache yanayopaswa kuombewa radhi na mawaziri wa serikali ya Awamu ya Nne badala ya "kueleza mafanikio".Unless wanataka kutuaminisha kuwa kukua kwa ufisadi ni sehemu muhimu ya mafanikio yao.Natambua kuwa "SAMAHANI" ni neno gumu kama alivyosema Elton John lakini uungwana ni kitu cha bure.Hizo fedha za walipa kodi wanazotumia kuzunguka huku na kule zingeweza kutumika vizuri zaidi kwa kila Waziri kuomba msamaha kwa madudu aliyofanya katika miaka hii mitano.Kaulimbiu kuwa "mlitutuma, tumetekeleza, tumerudi kuwaelezeni tulivyotekeleza na kuwasikiliza" ni matusi ya nguoni kwa vile hakuna Mtanzania mwenye akili timamu aliyeituma serikali kuingia mikataba ya kitapeli na wazushi wa EPA,au kukomalia kutotaja Kagoda ni mdudu gani,plus madumu mengineyo.Tulichowatuma ni kutukomboa kutoka katika lindi hili la umasikini sambamba na kuboresha hali za maisha yetu.Hatukuwatuma kuuza kila kilichopo kwa bei ya kutupa wala hatukuwatuma kung'ang'ania kununua samani kutoka nje na hatimaye kukumbuka dakika za majeruhi kuwa ununuzi huo hauendani na umasikini wetu.

Japo nakerwa na ziara hizi za mawaziri zinazozidi kuwabebesha mzigo walipa kodi walalahoi lakini nakereka zaidi napoona watu hawa wanapotufanya wajinga kiasi cha kutuzushia kuwa TULIWATUMA KULEA UFISADI.

Tumia kura yako vizuri,ukiendekeza ushabiki utazidi kuumia.Hakuna miujiza inayoweza kuondoa ufisadi hata kama watu watakesha kwenye nyumba za ibada (na huko wanakutana na "wabishi" kama Askofu Kilaini ambao wanaendelea kung'angania mtizamo wao finyu kuwa JK bado ni chaguo la Mungu.Askofu muogope Mungu wako unayemtumikia,please!).Nia pekee ya kuondokana na ufisadi ni kuwaondoa mafisadi.Kumbuka kuwa ufisadi ni kitendo kinachofanywa na mafisadi,na as long as wanaendelea kuwepo basi inakuwa mithili ya kupe au mbung'o na damu.Watanyonya hadi tone la mwisho.

AMKA!

4 Jun 2010




Well,well...I'm not that good when it comes to fashion,but poor as I might be,the Japanese Prime Minister's sense of fashion is SIFURI,ZILCH,ZERO...Oh,no.He doesn't even deserve a zero.Let's rephrase the sentence...his sense of fashion is non-existent.He doesn't have any.Candy has voluntarily offered help to the likes of the PM (READ IT HERE).Check the video report below and then click the following links to see how fashion police have their knives out for the Premier Yukio Hatoyama 

AFP: Japan PM's threads are final straw for fashion critic

THE WEEK: Japan's prime minister undone by the world's ugliest shirt?

STYLEITE: Japan’s Prime Minister Forced To Answer For His Checkered Shirt
.
JEZEBEL: Fashion Police Condemn Japanese Prime Minister's Fashion, Poll Numbers Fall

2 Jun 2010

A come back to the Industry after almost 25 years, Anna Luks, a mother of two boys, is now revealing to us, a glimpse of her collection called Colour Explosion. Anna will have much to talk about her work very soon. Luks will show her debut collection in July, date to be confirmed.

This photo shoot was taken recently at the Middlesex University Cat Hill studios, and was modelled by Jestina George.

Designer/Stylist: Anna Luks

Photographer: Sonia Marabet

Hair & Makeup: Brenda

Kwa mujibu wa imani zetu za Kiswahili,aliyekuroga akifariki basi uwezekano wa kupona nao unakuwa kama umefariki.Na msemo huu unaonekana kurandana na hali halisi ya baadhi ya matendo yetu viumbe tunaojulikana kama Watanzania.Nafahamu kuwa si wote "tuliorogwa" lakini hiyo si sababu ya "kutowatolea macho" wenzetu "waliorogwa kisha aliyewaroga akafariki".

Mwishoni mwa wiki hii,timu yetu ya taifa inakabiliwa na mpambano muhimu dhidi ya timu ya taifa ya Rwanda katika kusaka nafasi ya kushiriki kwenye michuano ya CHAN.Taifa Stars inatarajiwa kucheza siku ya Jumapili kisha Jumatatu wanatarajiwa kuingia tena uwanjani kupambana na timu ya Taifa ya Brazil katika pambano lililonunuliwa kwa mamilioni ya dola na chama chetu cha soka.

Na kwa takriban wiki nzima sasa,uongozi wa FA umekuwa bize zaidi na maandalizi ya pambano hilo walilonunua kuliko kuelekeza akili zao kwa mpambano dhidi ya Rwanda.Japo natambua kuwa kila mpenzi wa soka duniani angependa kuiona Brazil ikicheza uwanjani lakini sio kwa kununua mechi ya mamilioni ya fedha ambazo hakuna uhakika kama zitarudi.FA hawajaweka bayana gharama za kununua mechi hiyo lakini taarifa zinasema wamelipa dola za kimarekani milioni mbili unusu  (zaidi ya shilingi bilioni 3 unusu).Na hiyo ni ada (fee) tu lakini kuna uwezekano wa kiwango hicho kuwa kikubwa zaidi tukichanganya na gharama za kumudu ziara hiyo.

Kuna hoja kuwa ziara hiyo itasaidia kutangaza utalii.Well,lakini tuwe wakweli,yaani kutangaza utalii kwa dakika tisini kwa gharama ya shilingi bilioni tatu!?Na kama tujuavyo tatizo sugu la wizi wa mapato kuanzia TRA hadi kwa watendaji ngazi ya kata,si ajabu muda huu mafisadi wameshapiga mahesabu ya pasenti ngapi watakwiba kwenye chochote kitakachpatikana kwenye mechi hiyo.

Na kuna hoja ya rankings za FIFA.Hivi mechi moja ya kununua kwa mabilioni itatupandisha kwa kiwango gani ukilinganisha na menchi dhidi ya Rwanda ambayo kama "tukikaza misuli" na kufanikiwa kucheza CHAN tutapata nafasi kubwa zaidi ya kupandisha ranking yetu huko FIFA?

Ukitaka kufahamu namna ubabaishaji na ufisadi unavyozidi kutafuna mfumo wa jamii yetu subiri mechi iishe kisha vianze visingizio vya namna FA walivyoshindwa kufikia lengo la mapato.Binafsi nisingekuwa na tatizo laiti FA wangeafikiana na wenzao wa Brazil kisha kuuza tiketi kabla ya mechi na hivyo kufahamu faida au hasara itakayopatikana.Lakini kwa hali yasasa ni sawa na kucheza bahati nasibu.Na si ajabu visingizio vimeshaandaliwa as to kwanini "mechi hiyo haikuweza kurejesha faida iliyotarajiwa".

Ndio maana nashawishika kusema kuwa inawezekana ALIYETUROGA KESHAFARIKI.

1 Jun 2010

Crew ya £OVELY GAMBLE
BARAKA BARAKA, Managing Director wa Urban Pulse,akitoa hotuba
 BARAKA, DAISY,TIM, RENNY na FRANK
FRANK EYEMBE na BARAKA BARAKA
MC wa Show,Miss TINA GEORGE wa AILTV
MECKY,RAHMA CLASSIC,TINA,BARAKA,HALIMA,FRANCIA na FRANK
Msanii ANN-LYNN,AMOS MASANJILA na TINA
Producer wa £ovely Gamble,FRANK EYEMBE,akitoa hotuba
Urban Pulse CEO akiwa na MECKY
£OVELY GAMBLE

31 May 2010


Nafahamu unaweza usinielewe kwenye post hii lakini naomba niweke bayana kuwa niko radhi kutofautiana nawe msomaji wangu mpendwa.Kwa tutakaoafikiana,all I can say is POA.Nimeguswa na habari kuwa jana Makamu wa Rais,Dkt Shein, amezindua mbio za mwenge.Lengo la makala hii ni kuibua mjadala kuhusu suala hili la MWENGE WA UHURU.

Zamani hizo,mwenge ulikuwa na maana kubwa kwa kila mahali ulipopita.Lakini ni dhahiri kwamba mbio za mwenge kwa sasa hazina tofauti na ngonjera kuwa "Tanzania ni nchi ya Kijamaa" au kaulimbiu kwamba "Maisha Bora kwa Kila Mtanzania Yanawezekana".

Hili dude linalokula mamilioni ya shilingi katika gharama za kununua mafuta ili liendelee kuwaka,sambamba na posho kwa wanaolizungusha nchi nzima lina umuhimu gani kwa sasa?Maana zamani hizo mwenge ulikuwa na madhumuni ya KUMULIKA lakini sote tunafahamu kuwa kwa muda mrefu sasa mwanga wa mwenge huo unamulika vichochoroni tu huku ukishindwa kuwaangazia macho mafisadi wanaotafuna nchi yetu kama mchwa.Natambua kuwa kuna miradi mbalimbali inayozinduliwa wakati wa mbio za mwenge lakini hilo linafanyika hata wakati mwenge umezimika.Kwa maana nyingine,mwenge uwake usiwake bado wananchi wataendelea kujikusanya (pamoja na uchovu wao) kujitafutia maendeleo yao wenyewe.

Tatizo kubwa la sie Waafrika ni kuendeleza "mila na desturi" hata pale zilipopitwa na wakati.Hivi fedha zinazotumika kuzungusha mwenge nchi nzima zinaweza kujenga zahanati,shule na barabara ngapi?Kwa hakika ni nyingi tu.

To cut the story short,mie nina mtizamo kuwa mbio za mwenge zimepitwa na wakati.Naamini kuwa gharama zinazotumika katika mbio za mwenge zinaweza kutumika vizuri zaidi kwenye maeneo mengine ya msingi.Mwenge unakimbizwa kila mwaka lakini umasikini wa Watanzania unazidi kuongezeka (puuza kauli za Mkulo kuwa uchumi unazidi kukua kwani analipwa mshahara kusema 'lolote'),ujambazi ndio usiseme,na mafisadi wanazidi kulindwa na chama tawala.Sasa hili dude linalokula mafuta kama halina akili nzuri bado lina umuhimu kweli kwa mazingira ya Tanzania ya sasa?

Karibu uchangie

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.