31 Dec 2010



Muda huu natoka Kanisani.Dada yangu mmoja wa Kizulu alinialika kanisani kwao.Ibada ilikuwa ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka huu 2010 salama,na kuomba baraka kwa ajili ya mwaka 2011 ambao tunatarajia kuuona takriban masaa 13 kutoka sasa (kwa mujibu wa masaa ya hapa-tuko nyuma masaa matatu kulinganisha na huko nyumbani Tanzania,na masaa sita mbele ya Houston kwa Mrs Chahali mtarajiwa.Lol!).

Cutting the story short,Mchungaji wa Kibrazili aliyeendesha ibada ya leo alitushtua aliposema,"Samahani,ningependa sana kuwatakia heri ya mwaka mpya lakini...".Kisha akafafanua kwanini amemalizia na LAKINI.Alitoa mfano huu ulionigusa mno.Alisema kwamba kuingia mwaka mpya ni mithili ya kwenda sehemu ambayo hujawahi kufika kamwe.Tuchukulie mfano wa mahala nilipozaliwa,Ifakara.Je haingekuwa jambo la busara kuwapata wadogo zangu Peter na Paul (Kulwa na Doto,respectively) wakakuelekeza ulipo Mto Lumemo au Mto Kilombero?Au wakakuelekeza shule ya msingi niliyosoma ya Mapinduzi au sekondari nilyosoma ya Kilombero Day?Au pengine ungetaka kwenda Hospitali ya Mtakatifu Fransis au kufika eneo la Viwanja Sitini.Au labda ungetaka kwenda mahala zilipo ofisi mbalimbali za serikali huko Kibaoni,na mapacha hao wakakupatia guidance.

Katika ufafanuzi wake,Mchungaji huyo alieleza kwamba kama ilivyo tunapoingia mwaka mpya ambao hatujui kinachotusubiri,ndivyo ilivyo tunapoingia sehemu ambayo hatujui lolote kuihusu.Hatujui maeneo yenye vibaka ambapo kuonyesha simu au saa ni sawa na kutangazwa mwaliko wa kupigwa roba ya mbao.Hatujui mitaa ambayo mtu wa heshima ukionekana unaweza kudhaniwa unasaka huduma ya dada poa.Na kwa uswahilini,huwezi kujua mitaa inayoaminika kuwa makazi ya majini,mashetani,vibwengo,wanga,na viumbe kama hao.Kumpata mwenyeji kutakuepusha na sintofahamu hiyo.

Basi,Mchungaji alieleza kuwa safari ya kwenda mji ambao hatujawahi kufika-yaani mwaka 2011- ina mwenyeji wake.Kuna akina Kulwa na Doto wa Ifakara katika safari hiyo.Na mwenyeji huyo si mwingine bali ni Muumba wetu,Mungu mweza wa yote.Yeye anajua kila litakalotokea kuanzia saa 6 na kamili na sekunde moja hadi saa tano usiku na sekunde hamsini na tisa ya tarehe 31.12.2011.Mungu ni mzaliwa na mwenyeji wa mji huo tusioujua wa MWAKA 2011.

Sasa kwanini tuhangaike kuuliza huku na kule,hapa na pale kuhusu mji huo wakati tuna mwenyeji ambaye sio tu anaufahamu vilivyo mji huo wa mwaka 2011,lakini pia yuko tayari kutupatia makazi na mlo wa bure buleshi?Sharti lake jepesi ni moja tu: KUMWAMINI YEYE KUWA NDIYE MWEZA WA YOTE.Kumkabidhi kila tulichonacho kwa maana na mwili na roho na kuamini kuwa atatupatia ulinzi na mwongozo.

Hebu rewind tarehe hii miezi 12 iliyopita.Ni watu wangapi walikutakia HAPPY NEW YEAR?Bila shaka ni wengi.Lakini hebu tutafakari.Je hizo best wishes zimetisaidia vipi kukwepa madeni,magonjwa,chuki,migongano ya kifamilia, na matatizo mengine tuliyokutana nayo mwaka huu tunaoumaliza leo?Ndio,napaswa kuwatakia heri ya mwaka mpya wasomaji wangu wapendwa wa blogu hii.Lakini je salamu hizo za heri pekee zitatosha kuifanya 2011 kuwa mwaka wa maana kwako na kwangu?

Basi,nami naomba nifuate mfano wa Mchungaji Mbrazil kwa kusema HERI YA MWAKA MPYA,LAKINI....(TUJIKABIDHI KWA MWENYEJI WA MJI HUU TUSIOJUA AMBAO TUTAUINGIA MUDA MFUPI UJAO-YAANI MWAKA 2011.NA KWA VILE MWENYEJI WETU HUYO NI MWENYE UPENDO,ATATUPATIA TOUR GUIDE YA BURE,MAKAZI NA MLO BURE).


Wanasema ukitaka kumjua Mswahili ni mtu wa aina gani subiri apate madaraka.Muda mfupi uliopita nikiwa Facebook nilikutana mtandaoni na Mheshimiwa flani aliyebahatika kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa wana nchi (Mbunge) katika uchaguzi mkuu uliopita.Kwa vile sikuwahi kumpatia pongezi zangu kwa ushindi wake wa kishindo dhidi ya mgombea wa chama tawala,nikaonelea si vibaya kutumia fursa hiyo kumwambia maneno haya (nanukuu)

MHESHIMIWA,NAOMBA KUKUPA HONGERA KWA USHINDI.KILA LA HERI KATIKA UJENZI WA TAIFA LETU.HAPPY NEW YEAR 2011.

Kwa vile ujumbe wangu huo ulishaashiria kuwa lengo langu ni pongezi na heri ya mwaka mpya tu,na sio kurefusha maongezi,nilitarajia japo "Thanks" au "Poa".Lakini,kama ilivyo kawaida kwa Waheshimiwa wengi,Mheshimiwa huyo ambaye nilijaribu kumsapoti yeye na chama chake wakati wa kampeni,akahisi labda nataka "kumpiga mzinga/kirungu" ( kuomba msaada).Hakujali pongezi za mie mwananchi (na sapota wake), "akauchuna",kisha akatoka nje ya chumba cha kuchati logged out of the chatroom).Nilifadhaika hasa kwa vile namchukulia mwanasiasa huyu kijana kama role model kwa makundi mbalimbali ya vijana katika jamii yetu (safari yake hadi kuwa Mheshimiwa is truly inspirational na inaweza kuzalisha changamoto na tumaini jipya kwa vijana mbalimbali).Zaidi,dadangu mmoja anayemfahamu fika Mheshimiwa huyo aliwahi kuniambia kuwa mwanasiasa huyo mpya ni mtu humble (poa) sana.Very down to earth licha ya umaarufu aliokuwa nao kabla ya kujitosa kwenye ulingo wa siasa.Na kilichonisukuma "kujikomba" kutoa salamu na pongezi ni ukweli kwamba ni nadra kukutana na kigogo kwenye chatroom ya Facebook,na uwepo wake niliutafsiri (wrongly?) kuwa dalili ya utu poa (humility) wake.How wrong!

Lakini kwa ujumla nadhani ni dharau tu,na kasumba iliyobobea miongoni mwa Waswahili waliokwaa madaraka kuwapuuza "wat wa kawaida (yaani tusio na umuhimu).Ila nachopata shida kuelewa ni je Waheshimiwa kama huyu ninayemzungumzia hapa wanapungukiwa na kitu gani wakiamua kuonyesha kuwa uheshimiwa wao hauondoi ubinadamu wao?Watavuliwa madaraka?Wataamvukizwa maradhi flani?Vitambi vyao vitasinyaa (na vitambi vyao vinatafsiriwa nao kama part and parcel of uheshimiwa wao just like kipara-au ualaza- na wasomi njaa).Yah,Uswahili unaambatana na imani za ajabu kabisa.Hakuna uthibitisho wa kisayansi kuwa upungufu wa nywele kichwani unamaanisha ufanisi wa ubongo.Na kwa namna hiyohiyo,ukubwa wa tumbo-ambao pengine ni matokeo ya kuelemewa na pombe kama sio dalili za kwashakoo- haupaswi kuwa kigezo cha uheshimiwa hususan pale Mheshimiwa anapokuwa mtovu wa heshima.

Pengine msomaji mpendwa unaweza kunishutumu kuwa nafanya ishu hii kuwa big deal.Well,nimekuwa mfuasi mzuri sana wa dadangu mmoja,bloga maarufu Dinahicious,ambaye huko Twitter anatoa elimu ya bure kwa mtindo wa "wape vidonge vyao".Mdada huyu ni kama mtambo wa kurekebisha tabia zinazokera,hususan za hao wanaojiona watu maarufu.Kwani mtu ukiwa maarufu-hata kama hisia hizo za umaarufu ni za ndotoni tu-kisha ukawa-treat wanadamu wenzio kama watu hai na sio mawe,umaarufu huo utadidimia?

Natumaini Mheshimiwa huyu nayemzungumzia atasoma makala hii (kama ana muda.Si unajua sifa mojawapo ya uheshimiwa wa Kiswahili ni kuwa bize?).Madaraka ni kitu cha kupita,ilhali utu wa mtu ni kitu cha kudumu.Waheshimiwa wetu wanapaswa kujifunza kwa kwa watu kama Nyerere,Mandela,Martin Luther King,Jr,Mahatma Ghandi,Mama Theresa na hata Mitume ambao waliishi maisha ya unyenyekevu huku wakitambua kuwa uongozi wao ni matokeo ya imani kutoka kwa wanaowaongoza.

Kuisha kwa uchaguzi na kukwaa madaraka kusiwe sababu ya kususa hata salamu za pongezi kutoka kwa watu wa kawaida kama sie.Biblia inatuasa kuwa wajikwezao watashushwa na wajishushao watakweza.

Naamini ujumbe umefika,loud and clear!

29 Dec 2010



Sijaamini macho yangu niliposoma habari kuhusu hukumu iliyotolewa na mahakama dhidi ya Mbunge wa Bariadi (CCM) Andrew Chenge a.k.a Mzee wa Vijisenti ambapo licha ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya watu wawili na makosa manne ya barabarani,amehukumiwa faini ya SHILINGI LAKI SABA!And as you would have expected,AMELIPA NA KESI KWISHNEY.

Pengine hakimu aliyetoa hukumu hiyo alikuwa hajatoa zawadi ya Krismas kwa bosi wake mpya,Jaji Mkuu Othman.Au pengine hakimu huyo aliona hukumu hiyo ni fursa nzuri ya kutoa salamu za mwaka mpya kwa Watanzania in form of a prank.Au labda hakimu huyo amezingatia kanuni isiyo rasmi inayotawala sheria za Tanzania kwamba wanaostahili kwenda jela ni walalahoi tu,vigogo wanapokutwa na hatia wanapaswa kunyenyekewa kwa kila hali.Na pale inapobidi kutoa hukumu ya "changa la macho",matokeo yake ndio hukumu kama hii aliyopewa Chenge.

Ungetegemea mtu kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Werema kukata rufaa dhidi ya hukumu hii ya mzaha.Lakini atapata wapi muda huo wakati yuko bize kuhakikisha majambazi wa Dowans wanalipwa mabilioni yao?Na ungetegemea makundi ya haki za binadamu yashikilie bango hukumu hii lakini you and I know better kuwa generally speaking civil society Tanzania ni imegeuka mradi kwa wajanja (wezi?) kuwaghilibu wafadhili waendelee kumwaga misaada,ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia kuongeza idadi ya mahekalu,magari ya kifahari na nyumba ndogo za wenye NGOs hizo.

Ukiwa Mtanzania,unapaswa kuielewa vema Tanzania.No,simaanishi utafute vitabu vya Jiografia,Historia au Elimu ya Uraia kuhusu Tanzania.Ninachomaanisha ni kwamba unapaswa kuishi katika uhalisia na kufahamu kwamba kuna Tanzania ya aina mbili: ile masikini ya kupindukia ya walalahoi,na ile ya wenye ma-Vogue,X8,Hummer,nk.Pia kuna Tanzania ya wezi wa kuku wanaozeekea jela wakati uchunguzi unaendelea,au wanaobambikiwa kesi kwa vile hawamudu kuwahonga polisi mafisadi,na Tanzania ya akina Chenge ambao hata wakigonga na kuua kwa magari yenye bima iliyoisha muda wake wanaishia kupewa faini ya kishkaji la shilingi laki saba!Pia tuna Tanzania ya wanausalama kuhaha huku na kule (huku wakitumia mamilioni ya fedha za walipa kodi) kuandama maisha binafsi ya wanasiasa kama Dokta Wilbroad Slaa,na ile Tanzania ya wanausalama wanaotweta kuhakikisha mmiliki wa Kagoda anaendelea kuwa SIRI KUU.Na tuna Tanzania ambayo ni haramu kuandamana kudai Katiba mpya au kumpongeza mbunge wa chama cha upinzani,na ile ambapo kauli yoyote ya kiongozi wa CCM (hata kama ameitoa ndotoni au akiwa chakari baa)inageuzwa wimbo wa Taifa.

Inachukiza kuona miaka 49 baada ya uhuru wetu,Tanzania inazidi kugeuzwa punching bag na shamba la bibi la mafisadi.Ufisadi unatapakaa kila kona.Na mahakama zetu hazitaki kuachwa nyuma katika mchezo huo mchafu.Ndio maana sikushangazwa na kauli ya kitoto ya Jaji Mkuu mstaafu Agostino Ramadhani kuwa baadhi ya hukumu za majaji zina walakini (na alisubiri astaafu kwanza kisha ndio atoe kilio.Nchi ya rambirambi!).Actually,Jaji Ramadhani alipata fursa adimu ya kuingizwa kwenye vitabu vya historia pale aliposhiriki katika hukumu ya mgombea binafsi.Lakini tungetarajia nini kuyoka kwa wateuliwa ambao utiifu wao uko zaidi kwa aliyewateua kuliko nchi wanayoitumikia?

Nimalize kwa maneno makali.Kuna roho mbili za Watanzania wasio na hatia zilizopelekwa kaburini na Chenge.Kwa lugha nyingine,Chenge alijikabidhi jukumu la Ziraili mtoa roho.Hakimu aliyetoa hukumu hii ya mzaha anafahamu fika kuwa haki haionekani kutendeka japo imetendeka katika hukumu hiyo ya kihuni.Mungu atawalaani washiriki wote katika suala hili.Atawaadhibu ipasavyo kwa kupuuza thamani ya maisha ya marehemu hao wawili.Yawezekana huko waliko wanateseka kusikia thamani ya uhai wao ni shilingi laki saba (inclusive of makosa mengine ya Chenge).Of course,hata kama Chenge angehukumiwa fedha zote za akaunti yake huko Jersey isingetosha kufidia maisha ya marehemu hao,lakini alistahili japo kifungo cha muda mfupi.Lengo la hukumu kali ni kutoa fundisho kwa wazembe na wahalifu.Huruma au mzaha kwa wavunja sheria inachangia sana kukomaza uvunjaji sheria.Ikumbukwe kuwa hukumu hiyo inaweza kutumika katika kesi nyingine kuepisha adhabu kali kwa dereva mwingine atakayegonga na kuua ( hususan kama anatoka Tanzania ya vigogo).

Ee Mola,wewe ni mwenye huruma na mtoa haki ya kweli.Blogu hii inakuomba utoe hukumu mbadala ambayo angalau itaweza kuonyesha kuwa haki sio tu imetendeka bali pia inaonekana imetendeka.Katika Wewe kila jambo linawezekana.Kwa Chenge na hakimu wako,kwa hakika ipo siku mtavuna mlichopanda katika mzaha wenu huu wa mwisho wa mwaka



Takriban kila jambo kinaweza kutizamwa kwa sura mbili,au zaidi,hasa kwa minajili ya kuangalia faida na hasara.Ni katika mantiki hiyo,baadhi yetu tunaweza kuthubutu kuangalia "upande wa pili wa shilingi" kuhusu umoja wa Watanzania.Naomba nisisitize kuwa hoja hapa sio kudharau jitihada za waasisi wa taifa letu waliofanya kazi kubwa kujenga mshikamano miongoni mwa makabila zaidi ya 120 na kuzaa Utanzania uliogubika ukabila,udini,nk (angalau kwa kipindi kirefu cha uhai wa Tanzania).

Lakini moja ya athari zinazosababishwa na umoja huo ni uwezekano wa watu wasio na damu ya Kitanzania kujificha kwenye kivuli hicho cha "umoja wetu".Na ukichanganya na udhaifu,let alone ufisadi uliokubuhu,wa Idara ya Uhamiaji,yayumkinika kuamini tuna "Watanzania wenzetu" kadhaa tu ambao kimsingi hawapaswi kuwepo nchini mwetu.Kadhalika,kwa vile teuzi zinazofanywa na Rais Jakaya Kikwete (kama ilivyokuwa enzi za Mwinyi na baadaye Mkapa) hazizingatii kujiridhisha kuhusu u-Tanzania halisi ( as opposed to u-Tanzania wa kufoji), baadhi ya viongozi wanaoteuliwa kushika nyadhifa nyeti wanaweza kabisa kuwa sio Watanzania.

Kuongeza ugumu katika suala hilo la u-Tanzania ni makabila ambayo yametapakaa zaidi ya mipaka ya nchi.Hapa nazungumzia makabila ambayo yapo zaidi ya nchi moja.Kwa mfano,Kenya kuna Wamasai,Wameru,Wajaluo,nk kama ilivyo Tanzania.Simaanishi kila Mtanzania anayetoka katika makabila ya aina hiyo anaweza kuwa na utata katika u-Tanzania wake bali kilicho wazi ni ukweli kwamba ni rahisi kwa asiye Mtanzania (lakini anatoka kabila kama la Kitanzania) kujificha nchini ndani ya kivuli cha umoja wetu.

Tutamtambuaje mtu wa aina hiyo?MATENDO YAKE (including KAULI zake).Na ni katika mstari huo wa fikra nimefika mahali nikalazimika kujiuliza iwapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Jaji Werema ni Mtanzania kweli au ni walewale wanaotumia umoja wa Tanzania (licha ya wingi wa makabila)+udhaifu na ufisadi Idara ya Uhamiaji,kuwepo Tanzania isivyo halali,na kupewa madaraka makubwa pasipo watoa madaraka hayo kujiridhisha kuhusu u-Tanzania wa mteuliwa.

Simtuhumu Werema kuwa si Mtanzania kwani sina nyaraka za kuthibitisha hilo.Hata hivyo,nalazimika kupata hisia za walakini katika u-Tanzania wake kutokana na mlolongo wa kauli zake za kihuni na zisizoendana na wadhifa mkubwa aliokabidhiwa.Wakati takriban kila Mtanzania halisi anazungumzia umuhimu wa Katiba mpya,mbabaishaji Werema akakurupuka na kudai hakuna haja ya Katiba mpya (kana kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyesema atashughulikia suala hilo ni mdogo kimadaraka kwa Werema).

Mpuuzi huyu ambaye ni dhahiri kuteuliwa kwake tena kuwa Mwanasheria Mkuu kunathibitisha matatizo makubwa ya kimaamuzi yanayomwathiri Rais Kikwete alifikia hatua ya kusifia rushwa ndani ya CCM kuwa ni sehemu ya demokrasia (rejea gazeti la Uhuru,Agosti 6,2010 habari yenye kichwa AG Asifu Demokrasia CCM).Yani kichwa maji huyu mwenye jukumu la usimamizi wa sheria ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa alijifanya kupofu kwenye rushwa za wazi zilizotawala mchakato wa CCM kupata wagombea wake katika uchaguzi mkuu uliopita.Basi bora angekaa kimya,lakini mropokaji huyu akaona ni vme atuthibitishie how good msema ovyo he is.

Tunakumbuka pia ubabaishaji wake kuhusu muswada wa kizushi wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi.Ofisi ya mbabaishaji huyu pasipo aibu iliwasilisha madudu huko Bungeni ambapo haikuchukua muda kwa watu makini kama Dr Wilbroad Slaa kubaini uhuni uliofanyika.Na kwa vile ni rahisi zaidi kwa Kikwete kufanya teuzi kuliko kutimua wababaishaji,Werema hakuguswa.In fact,amezawadiwa tena Uanasheria Mkuu.

Ilikuwa rahisi kwa Werema kupandwa na muku katika kipindi cha kampeni za uchaguzi na kutishia kuishtaki Chadema kwa sababu anazojua yeye lakini sasa badala ya kuungana na Watanzania halisi kuonyesha hasira zao kuhusu hukumu ya Dowans ambapo serikali inatakiwa kuwalipa matapeli hao shilingi BILIONI MIA MOJA THEMANINI NA TANO (Tshs185,000,000,000/=)!!!!Badala ya angalau kuonyesha uchungu kwa nchi yetu na kuelezea suala hilo kistaarabu,jitu hili linakurupuka na kudai "..The matter is as good as closed...let's use our resources on important issues..." (mjadala huo umefungwa,tuangalie mambo mengine ya msingi).Yaani kwa mzembe huyu wa kufikiri,malipo ya shilingi bilioni 185 kwa matapeli wa Dowans sio suala muhimu (ambao laiti Werema na ofisi yake wangewajibika ipasavyo mmiliki wa Dowans angekuwa jela muda huu).Je cha muhimu ni kipi Mista Jaji?

Kwanini Watanzania wabebeshwe mzigo uliosababishwa na ufisadi katika serikali ya Kikwete?Yes,Kikwete anahofia kumuudhi swahiba wake anayemiliki Dowans,na ataendelea kuwa mateka wa fisadi huyo mpaka anamaliza urais wake 2015.Ni katika mazingira haya ya kubebana na kulindana ndipo wababaishaji kama Werema wanapata nafasi za kupewa madaraka (kulinda maslahi ya mafisadi) na kwa vile anafahamu fika kuwa Kikwete hana ubavu wa kumtimua (Werema) anaropoka kadri misgipa ya mdomo wake inapowashwa.Huyu mtu ana kauli chafu na zilizojaa ngebe.Si mlevi wa madaraka (kama walivydai Chadema) bali ni teja la madaraka.Uanasheria wake Mkuu haukamiliki pasipo kuwadharau Watanzania wenye nchi yao.Hajioni mheshimiwa mpaka aongee maneno mawili matatu ya "kutunyooshea kidole cha kati" (middle finger in the air)

Ndio maana nimepatwa na wazo la kujiuliza kuhusu iwapo Werema ni Mtanzania kweli au ndio walewale wanaojificha kwenye umoja wetu licha ya wingi wa makabila yetu?Nimeeleza hapo awali kuwa katika mchanganyiko huu wa makabila ni rahisi kwa wasio Watanzania kujichanganya nasi kana kwamba ni wenzetu.Kuwatamvua si rahisi lakini kwa bahati nzuri baadhi ya watu hawa wanaweza kutambulika,sio kwa mwonekano wao,bali KAULI ZAO ZINAZOONYESHA BAYANA HAWANA UCHUNGU WALA UPENDO KWA TANZANIA.

Nimalize kwa kumlaumu tena Rais Kikwete kwa kuzidi kuipeleka Tanzania shimoni.Teuzi zake za rapid fire na zinazoelemea zaidi kwenye kulindana badala ya sifa na/au uzalendo ndio sababu ya kupata watu wa ajabu kama huyu Werema.Najua Chadema wamemtaka kichwa maji huyu ajiuzulu,lakini hiyo ni ndoto mbaya.Werema ajiuzulu achekwe?Na akishajiuzulu nani atasimamia maslahi ya mafisadi hapo kwa Mwanasheria Mkuu?Nani atasimamia malipo kwa mafisadi kama wa Dowans?Nani atahakikisha mikataba ya kiuendawazimu inaendelea kusainiwa na kulindwa kwa nguvu zote?Werema ajiuzulu ili Kikwete aonekane a total fraud katika uongozi na teuzi zake?



Waziri Mkulo afanya kufuru
•  Akodi ndege kwenda Dodoma, aagiza shangingi toka Dar

na Bakari Kimwanga

WAKATI serikali ikisisitiza kutaka kupunguza gharama za matumizi kwa kuacha kuendelea kununua magari ya kifahari 'mashangingi', baadhi ya matumizi ya mawaziri yanatisha na kuwa mzigo kwa serikali.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano kwa muda mrefu sasa, umebaini kuwa wapo mawaziri na watendaji wengine wa serikali, wanaofanya ziara mikoani na kusafiri kwa ndege za kukodi, lakini hulazimika kuyaagiza mashangingi yao aina ya G8 kutoka Dar es Salaam hadi katika mikoa wanayokwenda kufanya ziara hata kama yatatumika kwa siku moja.

Mmoja wa mawaziri hao ni Waziri wa Uchumi na Fedha, Mustafa Mkulo, ambaye wiki iliyopita alikodi ndege kwa fedha za serikali kwenda kuhudhuria mahafari ya Chuo cha Mipango mjini Dodoma, lakini bado aliliagiza gari lake la uwaziri limfuate kutoka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kulitumia katika mji huo wakati Wizara ya Fedha na Uchumi, ina ofisi na magari mjini Dodoma.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano, ulibaini kuwa Desemba 17, mwaka huu, Waziri Mkulo mwenye dhamana ya fedha nchini, alikodi ndege ya Shirika la Tanzania Air, yenye namba za usajili 5HTZC na kuwasili katika uwanja wa ndege wa mjini Dodoma, majira ya saa nane mchana.

Wakati Waziri Mkulo akipasua anga la Dodoma kwa ndege ya kukodi, siku hiyo hiyo, dereva wake alilazimika kujaza mafuta shangingi la waziri huyo na kuweka kibindoni posho yake kumfuata bosi wake mjini Dodoma.

Kwa mujibu wa habari hizo, ndege hiyo ilikodishwa kwa dola za Kimarekani 5,000, sawa na sh milioni 7.5.

'Mimi niko hazina, hivi sasa serikali haina fedha, kuna madeni mengi, kuna walimu zaidi ya 500,000 waliomaliza vyuo vya elimu ya juu tangu Mei mwaka huu wanasubiri ajira kutokana na ukosefu wa fedha, lakini hazina inafanya matumizi mabaya kila siku. Huku ni kulifilisi taifa bila sababu,' alisema mtoa habari wetu ambaye jina lake limehifadhiwa.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kuhusina na kashfa hiyo, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, John Haule, alikiri kuwa Desemba 17, mwaka huu, wizara yake ilikodi ndege kwa ajili ya kumuwahisha Waziri Mkulo kuwahi mahafali ya Chuo cha Mipango ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Haule ambaye alikuwa na wakati mgumu kutoa ufafanuzi huo, alisema walilazimika kufanya hivyo kutokana na umuhimu wa kazi alizokuwa nazo Waziri Mkulo siku hiyo kabla ya kuondoka kwenda Dodoma na kusisitiza kuwa ukodishwaji wa ndege ni jambo la kawaida kwa watendaji wa wizara hiyo.

'Hili ni suala la kawaida kabisa katika utendaji wa wizara yetu; siku hiyo ilikuwa lazima waziri aende Dodoma katika mahafali na kuzindua bodi ya chuo cha mipango, sasa kwa hili tulishirikiana na chuo chenyewe kulipia gharama za ndege kwa waziri,' alisema Haule bila kufafanua chuo kililipia kiasi gani na wizara kiasi gani.

Alisema gharama za kukodisha ndege hiyo ilikuwa dola za Kimarekani 350,000, sawa na sh milioni 5.2 na kusisitiza kuwa kiasi hicho kimelipwa na wizara kwa kushirikiana na Chuo cha Mipango.

Alipoulizwa sababu ya wizara kulituma shangingi la waziri huyo kutoka Dar es Salaam wakati Dodoma kuna magari ya wizara hiyo yenye hadhi ya waziri, Haule alisema walilazimika kufanya hivyo ili Waziri Mkulo aende na kurudi kuwahi majukumu mengine jijini Dar es Salaam.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Naibu Waziri wa wizara nyeti inayochangia sehemu kubwa ya pato la taifa (jina lake limehifadhiwa), ambayo iliwahi kuwa katika wakati mgumu kutokana na kugubikwa na hoja ya ufisadi, alikumbwa na kashfa ya aina hiyo ya matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Waziri huyo akiambatana na msaidizi wake, alifanya ziara mkoani Kilimanjaro kwa kutumia usafiri wa ndege ya kampuni ya Precision, lakini alilitanguliza gari lake la uwaziri kutoka jijini Dar es Salaam hadi mkoani humo siku mbili kabla ambapo alilitumia kwa takriban saa sita tu na jioni alirejea Dar es Salaam kwa ndege hiyo na kuliacha gari lake likirudi na dereva pekee.

Gari hilo lilifika mkoani humo siku moja kabla ya waziri huyo na msaidizi wake kufika na mara alipotua katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), majira ya saa 2.30 asubuhi, tayari dereva wa gari lake alikuwa akimsubiri na kumpeleka katika ofisi ya wizara hiyo mkoani humo kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi.

Ilipofika majira ya saa 12 jioni siku hiyo hiyo, Naibu Waziri huyo ambaye ni mmoja wa mawaziri vijana na mara yake ya kwanza kuwa waziri baada ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko madogo ya baraza lake, aliwasili tena KIA na msaidizi wake kwa ajili ya safari ya kurudi jijini Dar es Salaam kwa ndege na kuliacha shangingi lake lililorudi siku iliyofuata.

Kwa hali hiyo, serikali ililazimika kulipa posho ya siku tatu kwa dereva huyo na gharama za mafuta yaliyotumika kuliwezesha gari hilo kusafiri kwenda na kurudi mkoani Kilimanjaro.

Malalamiko ya matukio kama hayo, yaliwahi kutolewa bungeni na Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee (CHADEMA) wakati akichangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba kigogo mmoja mkoani Kigoma, alialikwa kwenye semina iliyofanyika mjini Bagamoyo na kusafiri kwa ndege, lakini alilitanguliza shangingi lake wiki moja kabla ya yeye kuwasili.

Halima ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kawe (CHADEMA), alisema gari hilo lilitumika kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na mwisho wa semina, alilitumia kumfikisha katika uwanja huo wa ndege na gari hilo lilisafari kurudi Kigoma baada ya kigogo huyo kuondoka.

Mbunge huyo alilalamikia kuwa hali hiyo imekuwa ikitumiwa na viongozi wengi wa serikali na kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa makini kudhibiti matumizi ya aina hiyo kwa watendaji wake.

Mawaziri hao pia wamekuwa wakilalamikiwa kwa matumizi binafsi ya magari ya serikali kama vile kuyatumia kuwapeleka watoto wao shule katika safari nyingine binafsi ambazo hutumia mafuta ya serikali.

Wakati yakitumika kwa shughuli hizo binafsi, magari hayo hung'olewa namba za uwaziri na kubandikwa zingine, jambo ambalo linaelezwa na duru za kisiasa kama ni aina nyingine ya ufisadi.

Chanzo: Tanzania Daima

26 Dec 2010





Kwa mara ya kwanza kabisa,nalazimika kumpongeza Mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM,Edward Lowassa.Tuweke kando ishu nyingine ambazo blogu hii zimepelekea kumshutumu kiongozi huyo mara kwa mara,hadi kufikia hatua ya aliyekuwa Mwandishi wake wa habari (Press Secretary),Bwana Said Nguba,kutoa comments bloguni hapa kumtetea bosi wake wa wakati huo (Lowassa).

Majuzi,Lowassa alitoa wito kwa chama chake cha CCM na Chadema wakae pamoja kutafuta mwafaka kuhusu sakata la umeya wa Arusha.Waziri Mkuu huyo wa zamani alifanya kile kiongozi yoyote anayejali maslahi ya umma anachopaswa kufanywa kwa kuweka kando itikadi za kisiasa na badala yake kutilia mkazo umuhimu wa kupata mwafaka katika sakata hilo la umeya wa Arusha.Lowassa alionya kwamba kama hatua za haraka na za makusudi hazitachukuliwa basi kuna hatari ya kuzalisha 'Ivory Coast nyingine ndani ya Tanzania yetu' akirejea hali tete inayozidi kusumbua katika taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya Rais aliyemaliza muda wake na kushindwa uchaguzi mkuu kugoma ''kuachia ngazi".

Lakini wakati baadhi yetu tukivutiwa na uzalendo wa Lowassa,akaibuka mmoja wa wanasiasa wenye rekodi nzuri ya kubwatuka na "kusema ovyo",Katibu Mkuu wa CCM,Yusuph Makamba.Kiongozi huyo mwenye rekodi ya uropokaji alimvaa Lowassa akidai amekosea kusema aliyosema kwani hayo yalipaswa kujadiliwa kwenye vikao vya chama hicho tawala.Sina hakika kama Makambaanatumia kilevi cha aina yoyote lakini mchemsho huu wa safari hii unapaswa kuwa "wake up call" kwa (Mwenyekiti wa Taifa wa CCM),Rais Jakaya Kikwete,kwamba Makamba anastahili kupatiwa msaada wa kuchunguzwa akili yake.Ni mpuuzi asiye na mfano ambaye kwake usalama wa wakazi wa Arusha una umuhimu mdogo kulinganisha na taratibu za chama hicho tawala.Angalizo aloloyoa Lowassa kuwa Arusha inaweza kugeuka Ivory Coast halikuweza kuingia kwenye ubongo wa Makamba,sio kwa vile haelewi umuhimu wa political consensus bali kwa vile kwa akili yake nayohisi ina mapungufu kitendo cha CCM kukaa kitako na Chadema ni sawa na kuvunja Amri ya Mungu.

Mpuuzi huyu amesahau kuwa mgogoro mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar ulimalizwa baada ya CCM na CUF kuweka mbele maslahi ya taifa na kukaa pamoja kutafuta mwafaka wa kudumu.Na kwa tunaokumbuka kauli za kitoto za Makamba katika nyakati tofauti za jitihada za CCM na CUF kutafuta mwafaka huko Zanzibar,yayumkinika kuamini kuwa suluhu hiyo isingepatikana laiti mwanasiasa huyo "angepewa rungu" la kupitisha maamuzi ya mwisho.

Kwa akili yenye mapungufu ya Makamba,vyama vya upinzani ni mithili ya wanyama wasiopaswa kuwepo nchini.Ni sahihi kusema kuwa laiti CCM ingekuwa ile ya Baba wa Taifa,basi Makamba asingepewa hata fursa ya kuwa Mjumbe wa Nyumba Kumi.Inakuwaje kiongozi wa kitaifa wa chama tawala haoni umuhimu wa kutafuta ufumbuzi wa haraka wa matatizo yanayoendelea huko Arusha?Haihitaji PhD ya Siasa kutambua kuwa anayemlea Makamba ni Kikwete ambaye anakiendesha chama hicho kwa mtindo wa "bora liende".Na Kikwete asipoamka kutambua kuwa CCM inazidi kujiweka mbali na wananchi,si ajabu chama hicho kichovu kikamvunjikia kabla hajamaliza muda wake hapo 2015.Mwenyekiti gani asiye na ujasiri wa kumwambia Katibu wake kuwa achunge mdomo wake?

Enewei,tuweke kando tofauti zetu na tusapoti mawazo ya busara ya Lowassa kuhusu umuhimu wa kutafuta suluhu huko Arusha.Sambamba na hilo,tumpuuze Makamba na pengine tumshauri aruhusu ubongo wake uwe na mawasiliano na mdomo wake kabla hajaropoka jambo lolote lile.

24 Dec 2010


Majuzi,msomaji mmoja wa blogu hii alinitumia maoni ambapo pamoja na mambo mengine aliashiria kuwa nina chuki dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.Msomaji huyo aliyejitambulisha kuwa mkazi wa hapa Glasgow alidai (namnukuu) "...I know you hate JK because whatever happens to him you have a negative view, even a tyre puncture...",yaani kwa Kiswahili,"najua unamchukia JK kwa vile chochote kinachotokea kwake wewe una mtizamo hasi,hata pancha ya tairi".Hii ndio mitizamo ya Watanzania wenzetu ambao licha ya kubahatika kuwa nje ya nchi,hususan nchi zilizoendelea kama hapa Uingereza,bado wana mitizamo mgando ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia kutufanya hata miaka 49 baada ya uhuru kutamani mkoloni arejee.

Yah,huwezi kuwalaumu wanaotama mkoloni arejee japo mie si mmoja wao.Hivi tunawezaje kuelezea namna Watanzania wanavypelekeshwa kama watoto wadogo tena yatima siku chache tu baada ya Kikwete na CCM yake kupita huku na kule kuahidi neema,only for madudu and more madudu kuibuka kila kukicha?Unajua,angalau mkoloni alipotupelekesha alikuwa na excuse (japo isiyokubalika) kwamba yeye hakuwa Mtanganyika,na hakuwa na uchungu na nchi yetu.Na kwa wanaokumbuka vizuri somo la historia wanafahamu bayana kuwa ujio wa mkoloni ulikuwa kwa minajili ya kuendeleza nchi zao za asili,yaani kukwapua raslimali zetu kwa ajili ya viwanda vyao,kupata masoko ya bidhaa zao na eneo la makazi kwa nguvukazi ya ziada katika nchi hizo za wakoloni.Sasa ondoa neno mkoloni kisha weka neno FISADI,na yayumkinika kuhitimisha kuwa angalau mkoloni alikuwa na ajenda ya maendeleo huko kwao japo at our expense.Mafisadi nao wana ajenda za maendeleo pia,ila ni katika kutunisha akaunti zao kwenye mabenki ya hukohuko kwa wakoloni,kuongeza idadi ya nyumba ndogo zao (isomeke ufuska au uzinzi),kuongeza idadi ya mahekalu yao na magari ya kifahari,na sasa ajenda mpya ya kuimarisha himaya zao kwa kutumbukiza kila mwanafamilia na ndugu wa karibu kwenye siasa ili pindi baba akiondoka madarakani basi mwana amrithi kuzuia uwezekano wa baba mtu kukaliwa kooni kwa madudu aliyofanya akiwa madarakani.

Nimelazimika kuandika makala hii sio kwa minajili ya kumjibu huyo msomaji wangu wa hapa Glasgow bali ni baada ya kusoma toleo la mtandaoni la gazeti la Mwananchi ambapo kuna habari kuwa Tanesco wametangaza tena mgao wa umeme nchi nzima.Hivi sio majuzi tu shirika hilo lilitangaza mwisho wa mgao wa umeme?Tuwe wakweli,hivi uhuni huu wa Tanesco,ambao mie natafsiri kuwa ni uhuni wa serikali iliyopo madarakani,utaendelea hadi lini?So far,hakuna taarifa za wazi kuhusu athari za mgao wa umeme lakini haihitaji sayansi ya roketi au dissertation ya quantum physics kumaizi kwamba mgao huo una madhara makubwa mno kwa uchumi wa taifa na kwa maisha ya walalahoi kwa ujumla (vigogo licha ya kunufaika na ufisadi unaowawezesha kuuza jenereta kila mgao unapotangazwa lakini pia hawaathiriki kwa vile majumbani na maofisini kwao kuna jenereta zinazoendeshwa na fedha za kodi za walalahoi).

Hatuwezi kuilaumu Tanesco pekee kuhusiana na uhuni huu kwani ni siri ya wazi kuwa shirika hilo na sekta ya nishati kwa ujumla vimegeuzwa kitegauchumi kizuri kwa mafisadi.Majuzi tu tumesikia majambazi wa Richmond wakijiandaa kurejeshewa fedha walizotuibia ambapo watalipwa fidia ya mabilioni kwa mgongo wa binamu zao wa Dowans.Hatuwezi kumwepusha Kikwete na CCM yake na ufisadi huu kwa vile licha ya madudu hayo kushika hatamu wakati wa utawala wake,sasa tunafahamu kuwa amekuwa akiwakingia kifua mafisadi wasichukuliwe hatua za kisheria (thanks to nyaraka za siri za kidiplomasia zilizovujishwa na mtandao wa WikiLeaks).Kwa wale ambao hawajabahatika kusoma habari hizo,kuna nyaraka kutoka ubalozi wa Marekani hapo Dar zilizobeba maongezi kati ya bosi wa Takukuru Edward Hoseah na afisa ubalozi wa Marekani ambapo Hoseah alinukuliwa akieleza bayana kwamba Kikwete alishinikiza baadhi ya mafisadi wasichukuliwe hatua.Japo bosi huyo wa Takukuru amejaribu kuruka kimanga na kukana tuhuma hizo,kila mwenye akili timamu anafahamu kuwa ufisadi unashamiri Tanzania kwa vile Kikwete ameshindwa kuwachukulia hatua mafisadi papa licha ya madaraka lukuki aliyorundikiwa na Katiba.

Baadhi yetu tuliwaasa Watanzania wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita majuzi kwamba kuirejesha tena madarakani serikali ya Kikwete ni sawa na kumwaga chumvi kwenye kidonda kibichi,na matokeo yake ndio haya.Wakati tunaelekea mwezi wa pili tangu Kikwete atangazwe mshindi,hakuna lolote la maana lililokwishafanyika kuashiria kuwa kiongozi huyo ana ajenda mpya tofauti na zile zilizotawala miaka mitano iliyopita,kubwa ikiwa na kushamiri kwa ufisadi na uimarishaji himaya za mafisadi huko nyumbani.

Sawa,makosa yameshafanyika kwa kumrejesha Kikwete na CCM yake madarakani lakini hiyo isiwe sababu ya kuendelea kunung'unika kimoyomoyo huku nchi yetu ikizidi kuteketea.Umefika wakati Watanzania wasikubali kupelekeshwa namna hii.Kwanini Kikwete asibanwe kuhusu tatizo la umeme licha ya ahadi zake za mara kwa mara kuwa tatizo hilo lingekuwa historia?Au alimaanisha kuwa tatizo hilo litaendelea kuwa la kihistoria?

Nimesikia taarifa za mpango wa Chadema kuandaa maandamano ya nchi nzima kupinga kuongezwa bei ya umeme.Yaani licha ya mgao wa kila kukicha bado Tanesco wanataka kuongeza bei?Yayumkinika kuhisi kuwa wazo hilo la ongezeko la bei ya umeme ni la kifisadi lenye lengo la kupata fedha za kuwafidia mafisadi wa Richmond/Dowans.Ni muhimu kwa kila Mtanzania mzalendo kuunga mkono mpango huo wa maandamano ya amani ili kufikisha ujumbe kwa Kikwete na serikali yake kuwa Watanzania wamechoka kupelekeshwa.Hata hivyo,kama maandamano ya kuwapongeza wabunge wa upinzani yalizuiliwa na polisi,sidhani kama serikali itaridhia maandamano hayo ya kupinga ongezeko la bei ya umeme.

Mwisho,tuna choices mbili tu:kuchukua hatua sasa kabla hatujafika mahala ambapo hata tukichukua hatua itakuwa sawa na kutwanga maji kwenye gunia,au tusubiri kusoma rambirambi kuhusu nchi yetu hapo 2015.

22 Dec 2010



Picha kwa Hisani ya Mjengwa

Japo haipendezi kuona jeshi la polisi likitumia nguvu kubwa kuzuwia haki ya kikatiba ya wananchi kuandamana au kugoma kwa amani,lakini nashawishika kutowaonea huruma wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kufuatia kichapo walichopewa na askari wa FFU.Hivi sio hawa wana UDOM waliochangisha fedha kwa ajili ya kampeni za Jakaya Kikwete?Na sio hawa waliotoa tamko la kukemea haki ya kikatiba ya wabunge wa Chadema kususisa hotuba ya Kikwete huko Bungeni?

Najua si vyema kutoa lawama za jumla kwani si kila mwana-UDOM aliafiki wazo la kujikomba kwa Kikwete lililopelekea wanafunzi hao kuchangia fedha zao za ngama ili kumwezesha mwanasiasa huyo aliyekuwa mgombea wa CCM arejee madarakani.

Na kama tulivyoandika baadhi yetu wakati wa kampeni za uchaguzi wakati tunaonya madhara ya kuirejesha CCM madarakani,haijachukua muda kwa  Kikwete na serikali yake kuwalipa fadhila wasomi hao wa Dodoma.

Majuzi nilimsuta mwanahabari mkongwe Dunstan Tido Mhando baada ya kupata taarifa kuwa serikali imemtosa ubosi wa TBC.Nilimsuta kwa vile naamini wakati Tido anaombwa na WALIOMUOMBA kuja kuendesha TBC alikuwa anafahamu fika kuwa aidha anapanda mchicha au bangi,na mavuno yangekuwa mchicha au bangi,respectively.Ukikubali kutumiwa lazima ukubali kitachotekea itapojiri "expiry date" yako.

Sasa tunashuhudia kundi jingine la walioingizwa mkenge.Hawa wasomi watarajiwa wa UDOM walijikomba kwa Kikwete na CCM na kuchangia kampeni zake,sijui wakitarajia kuwa pindi mwanasiasa huyo akirejea Ikulu angewapatia muujiza gani sijui!

MLIPANDA BANGI SASA MNATARAJIA KUVUNA MPUNGA?

17 Dec 2010



So the infamous Dunstan Tido Mhando is gone!I was a bit shocked to learn that,not because he did or did not deserbe the boot,but rather the fact the the guy had been running TBC as if it were an extension of the CCM-owned Radio Uhuru.You wouldn't blame him,would you?He had to serve his masters in the government who shamelessly disregard the fact that state-run bodies are funded by all Tanzanian taxpayers (minus mafisadi,of course) regardless of their politicwl affiliations.

Tido has simply been used and abused.I'm sorry to say this but anyone,journalists included,who allow themselves to be used by some unscrupulous politicians could find themselves deemed useless once their service is no longer required.We all are aware of how,for instance, our artists attract inexplicable attention from our politicians come elections,only to hear the same cries of "tumesahauliwa" after the elections.Our ever important politicians can't afford to be seen sorrounded by a bunch of wana bongoflava.They had afterall done their job and got paid,so no more reasons for them to hang around with such important people in our society.

Of course we could blame such selfish crooks who never shy away from taking for a long ride whoever willing to attend to their needs but I think the latter deserve a share of such blames simply because they wouldnt be on the receiving end of such dirty games had they resisted being manipulated in the first place.Njaa?kujikomba?Blind faith?or sheer stupidity?

Back to poor Tido,he just reaped what he had sewn.I simply don't get it when I hear some people suspecting that his removal would bring TBC back to the 'Radio Tanzania era'.What they overlook is the fact that before he took the TBC post,Tido was working with one of the best,and hugely transparent,media house in the world,The British Broadcasting Corporation (BBC).Some people.Some of us expected that Tido would have brought "the BBC effect" to Tanzanian media but you and I know how he fared.Of course,I understand it wouldn't have been easy for him to transform an exceedingly biased,pro-ruling party state-owned media into an independent,fair and balanced organisation but at least he could have tried.Praising him for allowing opposition parties candidates to take part in "Jimbo kwa Jimbo" is totally missing the point.Why?Because that's actually what a public funded media organisation is supposed to do.Let us not forget what TBC behaved when Chadema inaugurated their general election campaign.And who was TBC's top boss when that was happening?

Rumour has it that Tido was brought to TBC by a certain bigwig who's currently not in the government.If such rumours are true,then why should we feel sorry for someone who got the job not on merit but rather because someone out wanted Tido at the helm of TBC for the bigwig's personal interests to be realised?

I just hope Tido has learned a lesson that political conmen would never hesitate to use and abuse anyone who is willing to be manipulated.For these cons,any tesource is like a condom: needed before and during sex,but something to disposed of immediately after the act.It's my hope that a decorated professional like him would never again allow any politician to take him for a stepping stone.There were some rumours that a certain fisadi who's aspiring to vie for the presidency in 2015 was planning to recruit Tido as his proposed TV/radio chief.If the rumours eventually turn out to be true in the future,and Tido grabs the offer,then we surely haven't seen the end of saddening chapters in Tido's professional life.

16 Dec 2010

Soma stori yake HAPA

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.