Kwa kumbukumbu tu,kwa hapa Uingereza msimu wa majira ya joto (summer) unaanza hapo saa 7 usiku.Kama ilivyo ada,inalazimu kusogeza muda kwa saa moja.
Tovuti hii inawatakia nyote Summer Time njema
Rombo kama LoliondoThursday, 17 March 2011 20:25
Daniel Mjema, Moshi
Ni siku za mwisho? Hili ndilo swali lililoanza kuumiza vichwa vya watu baada ya kijana mmoja kuibuka wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro na kudai ameoteshwa dawa ya ajabu na Bikira Maria inayotibu magonjwa sugu ukiwamo Ukimwi.Kama ilivyo kwa mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambikile Mwasapile wa Loliondo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi, kijana huyo naye amekuwa akitoa tiba kwa sh500.
Kwa imani ya waumini wa Kanisa Katoliki Duniani, Bikira Maria ni mama wa Yesu ambaye anaaminiwa na waumini wa Kanisa hilo na hata katika sala jina lake ndilo linalotumika zaidi huku wakiamini kuwa Yesu ni mtoto wa Mungu.Habari za uhakika kutoka eneo la Customs katika mji mdogo wa Tarakea, mpakani mwa Kenya na Tanzania, zilimtaja kijana huyo ambaye sasa anajiita Nabii, kuwa ni Hilary James Kitwai (28), kutoka wilayani Babati.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kutoka Tarakea, Kitwai alisisitiza kuwa dawa hiyo ameoteshwa na Bikira Maria na Yesu na kwamba inatibu Ukimwi, Saratani, Kisukari, Shinikizo la Damu, Figo, Pumu na maradhi ya maumivu.
"Walinitokea kwenye ndoto wakanionyesha huo mti na waliniambia kwa sasa tuko wawili tu Tanzania, lakini huyo mwenzangu simfahamu. Mimi natoza Sh500 lakini katika hiyo pesa yangu na familia yangu ni Sh300 tu,"alidai.
Kitwai ambaye amekuwa gumzo katika mji wa Tarakea, alisema anakabiliwa na changamoto kubwa katika kuwahudumia wenye mahitaji kwa kuwa hana msaada na kuomba serikali imsaidie kumpatia wahudumu.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka wilayani Rombo, tayari vyombo vya ulinzi na usalama vimemzuia kwa muda, kijana huyo kutoa tiba inayofanana na ya mchungaji Mwasapile na kuitisha sampuli za mizizi anayoitumia.
Kijana huyo ambaye ni fundi baiskeli kwa miaka mingi katika eneo hilo, aliibuka Jumatatu wiki hii na kuanza kutoa tiba kwa kutumia kikombe na tayari watu takribani 100 kutoka Kenya na Tanzania wamekunywa dawa yake.
"Anadai kuwa ameoteshwa na Bikira Maria na alielekezwa huo mti ambao una utomvu na kuanzia juzi (Jumatatu),watu kama 100 hivi walishakunywa dawa hiyo ambayo wenyeji wanadai mti wake ni sumu,"kilidai chanzo chetu.Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tarakea, Motamburu, Kimario, alilithibitishia Mwananchi kuwapo kwa kijana huyo.
Kimario alisema yeye binafsi, Ofisa Afya na Ofisa Usalama wa Taifa, walifika nyumbani kwa kijana huyo juzi na kumfanyia mahojiano."Tulimhoji akasema alitokewa na Bikira Maria na Yesu ambao walimwonyesha mti huo ambao upo katika Mto Tarakea na walimwambia yupo mmoja tayari anayetibu maradhi sugu na kwamba yeye atakuwa wa pili,"alisema mtendaji.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo, kijana huyo aliwaeleza kuwa baada ya Babu wa Loliondo na Yeye, bado atatokea mtu wa tatu ambaye naye ataoteshwa dawa za kutibu maradhi hayo na baada ya hapo Yesu mwenyewe atakuja duniani.
"Tulimuuliza kama ameshatoa dawa hiyo kwa watu mbalimbali akasema alianza kutoa Jumapili na watu kama 20 hivi walikunywa na alitupa vipande vya miti viwili vya dawa hiyo na tumevikabidhi kwa uongozi wa juu,"alisema Kimario.
Kwa mujibu wa Kimario aliyekuwa akimkariri kijana huyo, alisema 'nabii' huyo ameamua kutoendelea kutoa tiba hiyo hadi hapo serikali itakaporidhia na kwamba kwa sasa anamuomba Mungu ampe maono zaidi juu ya dawa hiyo.
Wananchi walioongea na Mwananchi baada ya kuzagaa kwa taarifa hizo, wameitahadharisha serikali kuwa makini na watu wanaojiita ni manabii vinginevyo wananchi wanaweza kukumbwa na maafa ya kunywa sumu bila kujua.
Wananchi hao wameitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuwajibika kikamilifu kwa kuzuia matumizi ya dawa ambazo hazijathibitishwa kutokuwa na madhara.Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Anthony Tesha ambaye pamoja na kukiri kusikia habari hizo lakini alisema anaviachia vyombo husika kufuatilia jambo hilo.
JK: Tutatumia mkongo kufundishia wanafunziThursday, 17 March 2011 20:27
Fredy AzzahRAIS Jakaya Kikwete, amesema serikali imebuni mpango maalumu wa kutumia mkongo wa mawasiliano, ili kukabiliana na upungufu wa walimu katika shule za sekondari nchini.Katika kufanikisha jambo hilo, shule zote za sekondari zitaunganishwa katika mtandao huo ambao utawawezesha mwalimu mmoja kufundisha shule hizo wakati mmoja.Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Januari mwaka 2006 na kutoa maagizo ya kuboresha elimu kwa miaka mitano ijayo.
"Pamoja na kuwa tuna tatizo la upungufu wa walimu kwa jumla, hali ni mbaya sana kwa walimu wa sayansi, mpaka sasa kuna upungufu wa walimu 34,000 na sisi kwa mwaka uwezo wetu ni kuzalisha walimu 10,000," alisema Rais Kikwete.
Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, serikali itaziunganisha shule za serikali katika mkonga wa taifa wakati ikiendelea pia kuzalisha walimu kadri itakavyoweza."Kutokana na idadi ya walimu wanaosoma, tatizo la walimu litaweza kwisha baada ya miaka mitatu, lakini sasa pamoja na walimu 10,000 kumaliza masomo yao kwa mwaka, unaweza kukuta bado tuna upungufu wa walimu 40,0000 kwa mwaka," alisema
"Tukiziunganisha shule zetu kwenye mkongo wa taifa ambao mpaka kufikia Juni mwaka huu utakuwa umekamilika, mwalimu mmoja akiwa hapa, anaweza kufundisha wanafunzi wa kemia nchi nzima kwa wakati mmoja." alisisitiza.
Alisema mpango huo ukifanikiwa mwalimu atakaye kuwa yupo kwenye darasa la shule husika, kazi yake itakuwa ni kusimamia wanafunzi kufanya mazoezi na yatakayotolewa na mwalimu aliyekuwa akifundisha kwa njia ya mtandano na kusahihisha kazi zao.
Alieleza kuwa, tayari serikali imeshafanya mazungumzo na kampuni moja ya Kimarekani ambayo itasaidia katika teknolojia hiyo."Wameshanionyesha jinsi tutakavyofanya kwenye maeneo ambayo yana umeme na hata yale yasiyokuwa na umeme," alisema Rais Rais pia aliitaka wizara kuweka bayana mipango yake kuhusu namna ya kuinua ubora wa elimu.
Rostam aponda tiba ya Mchungaji Loliondo
Tuesday, 15 March 2011 21:22
Shija Felician, Igunga
WAKATI Watanzania wengi wakimiminika kwenda wilayani Loliondo, mkoani Arusha kupata dawa inayodaiwa kutibu magonjwa sugu, Mbunge wa Igunga (CCM), Rostam Aziz ameibuka na kusema tiba hiyo haina lolote akidai kwamba ndugu zake watano wameitumia lakini hawajapona.
Akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wapigakura uliofanyika kwenye Viwanja vya CCM wilayani Igunga, Tabora mbunge huyo alisema haiamini dawa hiyo kwa kuwa ana ushahidi kwa ndugu zake hao ambao anadai kwamba wanaendelea kuugua kisukari licha ya kutumia dawa hiyo siku saba zilizopita.
Aliwataka wale watakaokwenda Loliondo ambao wanatumia dawa za hospitalini kuendelea kuzitumia badala ya kuzipuuza na kuzitupa... “Ndugu zangu wananchi wa Igunga, mimi mjomba wangu Hassan mnamfahamu karibu wote hapa mjini ni mgonjwa wa siku nyingi wa kisukari. Ameshakunywa dawa hiyo lakini mpaka sasa ni mgonjwa kama mnavyomuona sasa hiyo dawa inaponyesha nani?”
Hata hivyo, aliwataka wananchi wote wenye imani juu ya dawa hiyo waende huku akiwasisitizia kutopuuza ushauri wa madaktari kwani.
Wakati Rostam akipinga dawa hiyo, wilayani Kahama, mamia ya wafanyabiashara wamefunga shughuli zao na kukimbilia Loliondo kwa Mchungaji Mwasapile kunywa dawa hiyo huku baadhi ya waliorejea baada ya kuinywa wakidai kuwa hali zao sasa ni nzuri.
Wafanyabiashara hao wengi wao wanaondoka kwa siri wakidai wanakwenda Dar es Salaam katika shughuli zao, lakini siri imefichuka baada ya baadhi yao kuoneka katika runinga wakiwa katika foleni wakisubiri kupatiwa huduma hiyo.
Mbali ya kuzungumzia suala hilo la tiba ambalo limegusa hisia za wananchi wengi wa Afrika Mashariki, mbunge huyo aliwapa pole wananchi wa Igunga ambao nyumba zao zimeezuliwa na upepo uliosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha wiki iliyopita ambazo ziliathiri kaya 19. Aitoa msaada wa Sh500,000 kwa kila kaya iliyokumbwa na maafa hayo.
Lowassa apata kikombe Loliondo
Tuesday, 15 March 2011 23:47
Waandishi Wetu
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa juzi alipata tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile katika Kijiji cha Samunge, Tarafa ya Sale, Loliondo, mkoani Arusha.Lowassa alifika katika eneo hilo mchana akiwa na viongozi kadhaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Serikali kisha kupata kikombe kimoja chenye dawa kinachotolewa na mchungaji huyo kwa ajili ya tiba.
Tofauti na viongozi wengine, Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM), Jimbo linalopakana na Kijiji cha Samunge, alikwenda huko akiwa na viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na baadhi ya wapigakura wake.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Lowassa alithibitisha kwenda Loliondo na kuwataja viongozi wa dini alioambatana nao katika msafara wake kuwa ni Askofu Msaidizi wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Dk Frederick Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Dayosisi ya Kaskazini Kati (Arusha), Mchungaji John Nangole.
Katika ramani ya utendaji kazi ya KKKT, Jimbo la Masai Kaskazini ndipo kilipo Kijiji cha Samunge ambako ni makazi ya Mchungaji Mwasapile.“Ni kweli, nimekwenda pale na wapigakura wangu pamoja na viongozi wa dini, Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Mchungaji Nangole,” alisema Lowassa na kuuliza: “Kwani hiyo nayo ni habari jamani?”
Baada ya Lowassa kufika katika kijiji hicho akiwa na ujumbe wake, aliongoza moja kwa moja hadi kwa Mchungaji Mwasapile na kuzungumza naye kisha akapata kikombe cha tiba na kuondoka.
Kabla ya Lowassa kwenda kupata tiba, amekuwa akitoa msaada wa nauli kwa wagonjwa mbalimbali wa jimbo lake kwenda kwa mchungaji huyo ambaye dawa yake inadaiwa kutibu magonjwa ya saratani, kisukari, pumu, shinikizo la damu na Ukimwi.Lowassa ni miongoni mwa wanasiasa maarufu nchini ambao wameshafika kwa mchungaji huyo kupata tiba hiyo wakiwamo mawaziri, naibu mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya.
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Maponduzi (NEC) Itikadi na Uenezi, Bw. John Chiligati amesema licha ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kuwa na haki ya kutoa maoni, lakini hawana mamlaka ya kuiondoa sekretarieti madarakani.
Wakati Bw. Chiligati akitoa kauli hiyo, wajumbe wenzake wa sekretarieti waliotakiwa kuachia ngazi kwa kushindwa kutimiza wajibu wao wa 'kumsaidia' mwenyekiti wametofautina kuhusu kauli hiyo huku wakishindwa kuzungumzia kwa uwazi wito huo wa vijana.
Jana gazeti hili liliwakaririwa vuoa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ukiitaka sekretarieti ya chama hicho kujizulu kabla umoja huo haujachukua hatua za kuwaondoa kwa kuwa imeshindwa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo wa mkoani Pwani, Bw. Abdallah Ulega wakati akifungua Baraza la Umoja wa Vijana Mkoa humo, huku akisisitiza kuwa sekretaeti hiyo haifai kwa kuwa ilisababisha chama hicho kushinda kwa taabu katika uchaguzi mkuu uliopita, na kuwa ndiyo imekuwa ikitoa siri kwa chama cha upinzani cha CHADEMA.
Secreterieti inayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba, inajumuisha Manaibu Katibu Wakuu Bara, Kapteni George Mkuchika na Salehe Ramadhani Ferouz (Zanzibar), Katibu wa Itikadi na Uenenezi, Kapteni John Chiligati, Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha, Bw. Amos Makala na Katibu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe.
Akizungumza na Majira jana Bw. Chiligati alisema kimsingi vijana hao wametumia uhuru wao ndani ya chama kutoa maoni yao na kwamba haoni sababu ya hatua hiyo kusumbua vichwa vya watu kwa kuwa ni jambo la kawaida kikatiba.
"Ni haki yao kutoa maoni, sioni cha ajabu hapo, vijana wana haki ya kuzungumza na kutoa maoni yao kwa uhuru kabisa.
"Lakini Secretarieti inachaguliwa na NEC na tunawajibika kwa NEC kupitia Kamati Kuu, hao waliotuchagua ndio wana mamlaka ya kutuondoa, lakini hilo haliwakatazi vijana kutoa maoni," alisema Bw. Chiligati.
Alipoulizwa changamoto waliyopata na iwapo wanajiandaa kuwasilisha mapendekezo yao kwenye vikao vya juu kutokana na wito wa UVCCM hakuwa tayari kutoa majibu ya moja kwa moja badala yake alisisitiza kuwa hayo ni maoni ya vijana.
"Nimesema hayo ni maoni ya vijana na wana haki ya kuyatoa," alisistiza Bw. Chiligati bila kufafanua.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba alisema licha ya kuheshimu uhuru wa kutoa maoni lakini haamini kama yaliyoandikwa katika vyombo vya habari ndiyo yaliyozungumzwa na UVCCM mkoa wa Pwani.
"Hayo ndio maoni ya vijana, wamekaa kwenye baraza lao na wakaona hivyo. Hayo ndio maoni yao mimi sina cha kusema," alisema Bw. Makamba.
Alipotakiwa kujibu iwapo katiba, kanuni na taratibu za CCM zinatoa nafasi kwa umoja huo kuondoa secretarieti iwapo imeshindwa kutimiza wajibu wake alisema;
"Ni maoni yao, lakini pia sina hakika kama yaliyoandikwa yako sawa sawa," alisema Bw. Makamba bila kutoa ufafanuzi wa kina.
Alipoulizwa hatua atakazochukua kama Mtendaji Mkuu wa CCM kuhusu wito huo wa UVCCM alisema yeye hawezi kujitetea kupitia magazeti na kusisitiza kuwa hayo ni maoni ya vijana.
"Siwezi kufanya kazi ya kujitetea kwenye magazeti, wao ni vijana wa CCM, wamekaa kwenye baraza lao wakasema, sasa unataka nisema nini? alihoji Bw. Makamba na kuongeza, "Nasema hivyo ndivyo walivyoona. wajumbe wengine wa sekretarieti hiyo hawakupatikana kutoa maoni yao kwa simu zao zilikuwa zinaita bila majibu.
Mbali na sekretarieti, vijana hao waliwashambulia mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye wakisema kauli zao za kukikosoa chama hazina lengo zuri bali ni njia tu ya kutafuta urais 2015
Akizungumzia suala hilo, Bw. Lowassa ambaye pia alionywa na vijana hao kutoa maoni nje ya vikao wakati anayo nafasi ya kukutana na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Rais Jakaya Kikwete, alisema maoni yake kuhusu uchumi hayana sababu ya kusubiri vikao.
"Nilikuwa vijijini kwenye ziara sijasoma magazeti, lakini wewe nikikuuliza hali ya uchumi utasema kuwa ni nzuri?Nani asiyejua kuwa kuna hali ngumu ya uchumi! Hata bei ya nyanya imependa hilo nalo tusubiri vikao? alihoji Bw. Lowassa.
Alisema kama mtu anataka kuwania urais mwaka 2015 hawezi kuanza kampeni kwa sasa kwa kuwa kufanya hivyo ni kutoa nafasi ya kushughulikiwa na kuchafuliwa na maadui. Bw. Sumaye hakupatikana jana kwenye simu yake.
Majira ilipomtafuta Makamu Mwenyekiti Taifa wa CCM, Bw. Pius Msekwa ili kuzungumzia wito huo wa UVCCM, alisema hawezi kusema lolote kwa kuwa hayo ni maoni ya vijana na kila mmoja anayo haki ya kutoa maoni yake.
"Hayo ni maoni ya vijana, sasa unataka nitoe maoni gani?" alihoji Bw. Msekwa.




KIKOSI cha Kutuliza Ghasia cha Jeshi la Polisi (FFU) jana kilitawanya maandamano ya wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi na sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam waliokuwa wakielekea Ikulu kupinga ongezeko jipya la nauli za daladala.
Kundi la kwanza la wanafunzi hao lilijikusanya katika Viwanja vya Mnazi Mmoja majira ya mchana na kuanza maandamano hayo yaliyokuwa na lengo la kumfikishia ujumbe Rais Jakaya Kikwete wa kutoridhishwa na ongezeko hilo la nauli. Kundi jingine la wanafunzi lilianzia maandamano hayo katika Uwanja wa Karume.
Mwandishi wa habari hii alipofika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja aliwakuta wanafunzi hao wakijipanga kuanza maandamano hayo huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali. Baadhi ya mabango hayo yalisomeka: ‘Kama ni maji ya pilipili, hayawezi kuwa suluhisho la migomo.’
Baadhi ya wanafunzi walisema wameamua kupinga nauli hiyo mpya kwa maandamano ili kuishinikiza serikali iifute wakitaka kurejeshwa kwa ile ya zamani ya Sh100 ili kuwapunguzia mzigo wazazi wao kuwasomesha.
“Sisi wengine kwa siku tunapanda magari matatu hadi kufika shule na hapo bado hujala. Sasa kwa hali hii kweli tutasoma?" Alihoji mmoja wa wanafunzi hao.
Mwanafunzi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Habib Juma alisema nauli ya Sh150 kwa mwanafunzi ni kubwa mno kuimudu akisema kipato cha wazazi wengi ni duni na baadhi yao wanashindwa hata kutoa michango mbalimbali ya shule.
Hata hivyo, jitihada za wanafunzi hao kufikisha ujumbe wao Ikulu ziligonga mwamba baada ya kudhibitiwa na FFU muda mfupi tu baada ya kuingia barabarani.Askari hao waliokuwa na pikipiki walitanda barabarani na kuwatawanya wanafunzi hao na baadaye waliwashikilia wanafunzi wawili wa kiume baada ya wenzao kukimbia. Wanafunzi hao walipakiwa kwenye gari la polisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi.
Nauli hizo mpya za daladala zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), wiki iliyopita zilianza kutumika rasmi jana.Ofisa Mfawidhi wa Sumatra katika Kanda ya Dar es Salaam, Conrad Shio alisema nauli hizo zimegawanywa katika makundi matatu kwamba wanafunzi watatozwa Sh150 kwa safari, kundi la pili ni njia zenye nauli moja ya Sh300 na la tatu ni la njia zenye nauli zaidi ya moja na kwamba nauli hizo zimeongezeka kwa Sh50 katika nauli za awali, katika kila safari moja.
Shio alitoa mfano akisema kwa njia ambayo abiria wake walikuwa wanatozwa nauli ya Sh250 kwa safari, sasa watatozwa Sh300.Alisema katika Kanda ya Mashariki nauli ya juu zaidi itakuwa Sh1,700 kwa safari kati ya Kigamboni na Pembamnazi, eneo ambalo awali nauli yake ilikuwa Sh1,300.
Sumatra imeongeza nauli hizo baada ya kupokea maombi ya wamiliki wa mabasi mwishoni mwa mwaka jana wakilalamikia kupanda kwa gharama za uendeshaji.