2 Oct 2014

Bado ninakumbuka vizuri maongezi yangu ya mwaka 2005 na mtu mmoja jijini Dar, ambaye sio tu ni mwajiriwa katika taasisi moja nyeti lakini pia ana uelewa mkubwa wa masuala yanayojiri 'nyuma ya pazia' (yaani masuala mbalimbali mazito ambayo kamwe huwezi kuyasikia au kuyaona kwenye vyombo vya habari). Nikiwa huko nyumbani kwa likizo katika kipindi ambacho Tanzania yetu ilikuwa katika harakati za uchaguzi mkuu ambao hatimaye ulimwingiza madarakani Rasi Jakaya Kikwete, mwandamizi huyo alinieleza kwa undani kwanini aliamini JK angeshinda uchaguzi huo kwa ushindi wa kishindo.

Kadhalika, mtu huyo alibashiri kuwa Watanzania watajuta kumwingiza Kikwete Ikulu kwa kile alichokieleza kuwa "mtu huyu hayupo serious kiasi cha kumkabidhi dhamana ya kuongoza nchi hii yenye matatizo kibao." Alikwenda mbali zaidi na kunisimulia masuala kadhaa yaliyojiri katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa (ambapo mie nilikuwa nje ya nchi kwa zaidi ya nusu ya awamu ya pili ya utawala wa Mkapa). Alieleza kuwa hali ilikuwa mbaya wakati huo, na laiti JK akiingia madarakani itakuwa mbaya zaidi.

Mtu huyo ameendelea kunijulisha mengi yanayojiri 'nyuma ya pazia,' na hivi karibuni aliniambia kuwa ana uhakika Watzanai wengi watapatwa na mshtuko mkubwa baada ya JK kuondoka madarakani hapo mwakani, pindi watakapopata fursa ya kufahamu jinsi nchi yao ilivyoendeshwa katika kipindi hiki cha miaka 10 (2005-2015). Alidai kwamba kinachofahamika kwa umma ni tone tu la maji kwenye bahari kwani kuna mlolongo wa 'madudu' yanayoendelea lakini nguvu iliyojengwa na mtandao wa JK 1995-2005 inafanya jitihada kubwa kuyadhibiti yasijulikane hadharani.

Lakini sidhani kama kuna Mtanzania anayehitaji kuwa na 'mjuzi wa mambo' kama  huyo jamaa yangu, kufahamu kwamba mwelekeo wa nchi yetu ni shaghalabaghala. Kwa wenye uelewa wa 'kusoma kati ya mistari' (reading between the lines) watabaini kuwa mengi ya yanayojiri huko nyumbani katika medani ya uongozi wa taifa letu ni matokeo ya ombwe kubwa la uongozi wa JK.

Wengi twakumbuka kauli ya Mbunge wa Ubungu kwa tiketi ya Chadema, Mheshimiwa John Mnyika, kuwa 'JK ni dhaifu.' Na kwa hakika watendaji wengi wa serikali ikiwa ni pamoja na mawaziri wake wanautumia vyema udhaifu huo wa bosi wao.

Hebu angalia mfano huu rahisi. Wakati lawama nyingi kuhusu sintofahamu ya hatma ya Katiba Mpya inaelekezwa kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katika, Samuel Sitta, mtu ambaye hawezi kukwepa lawama katika kuukoroga mchakato huo ni JK mwenyewe. Kana kwamba alilazimishwa kuteua Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba (Tume ya Warioba), JK pasi kujali athri za matendo yake alianzisha upizani wa waziwazi dhidi ya mapendekezo ya Tume hiyo ya Warioba. Mara kadhaa akiwa kama Mweneykiti wa Taifa wa CCM aliweka bayana upinzani wa chama tawala kwa mapendekezo ya Tume hiyo. Lakini yote tisa, kumi ni siku ya uzinduzi wa Bunge Maalum la Katiba ambapo badala ya kuwaunganisha Watanzania, hotuba yake ilipandikiza mbegu ambazo kwa hakika ndizo tunavyna matuonda yake sasa.

Ilipotokea baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuunda umoja wao wa UKAWA, na hatimaye kususia vikao vya bunge hilo, kauli za kujikanganya za JK hazikusaidia kuleta mwafaka, kwani mara aonekane anayetaka suluhu mara awatupie lawama UKAWA, mara awaombe viongozi wa dini wasaidie kuokoa mchakato huo, mara atumie ubabe kuzima hoja za UKAWA. Kwa kifupi, ukosefu wake wa msimamo wenye kulinda maslahi ya taifa ulitoa fursa kwa kila 'Dick, Toim na Harry' kujiropokea chochote kilichomuijia akilini.

Fast foward hadi hapa tulipo sasa, katika mazingira ya kawaida tu usingetegemea JK aende Marekani TENA kwa wiki mbili ilhali hatma ya Katiba mpya na Bunge Maalum la Katiba ni tata. Tumeshazungumza vya kutosha kuhusu jinsi JK anavyopenda kuzurura nje ya nchi, hususan ziara za Marekani. Kwa wanaofuatilia safari zake watafahamu kuwa alikuwa Marekani hivi majuzi tu kwa siku kibao, lakini hiyo haikumzuwia kwenda tena huko kwa wiki mbili kwa kisingizio cha kuhudhuria kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Je isingewezekana kwenda siku moja kabla ya siku yake ya kutoa hotuba na kisha kurejea nyumbani kushughulikia hatma ya Katiba mpya?

Kituko ni kwamba wakati akiwa ziarani Marekani, alifanya 'safari ndani ya safari' na kuja hapa Uingereza, kabla ya kurejea tena Marekani. Kwa hakika ni vigumu kubashiri maisha ya Rais wetu huyu atakapostaafu mwakani kwani ni wazi kuwa moja ya vitu atakavyovi-miss sana ni hizo safari mfululizo za nje ya nchi. Japo kuwa Rais mstaafu hakutomzuwia kusafiri mfululizo, lakini angalau kwa wakati huo 'hatokuwa na jeuri' ya kuambatana na lundo la watu kwenye misafara yake. Na hatuwezi kujua, huenda Rais ajaye akadhibiti safari za viongozi au viongozi wastaafu nje ya nchi pasipo sababu za msingi.

Ombwe la uongozi wa JK, ukichanganya na mchango wake katika kuukoroga mchakato wa Katiba mpya, ndio moja ya fursa zilizotumiwa kikamilifu na Sitta katika kufanikisha uhuni wa kisiasa/ mzaha wa kidemokrasia unaoendelea huko Dodoma. Kwa lugha nyingine, kiburi, ubishi, nyodo, na kila kisichopendeza kutoka kwa Sitta na uendeshaji wake wa Bunge Maalum la Katiba ni dalili tu za ugonjwa, ilhali chanzo cha ugonjwa huo ni ombwe hilo linalouandama utawala wa JK.

Hivi tuwe wakweli. Laiti JK angemkalisha Sitta kitako kama Waziri wake na ' kumpa darasa la kiutu-uzima' Mwenyekiti huyo wa BMK angeendeleza kufanya madudu tunayoshuhudia? Ni suala jepesi tu la bosi kukaa chini na anayemwongoza, kisha kumwambia bayana kuwa , "No, Mr Sitta, this is wrong." Na hata kama kuna watakaodhani huo ni sawa na udikteta, basi na bora iwe hivyo kwani udikteta kwa maslahi ya umma ni suala linalokubalika.Uzoefu unaonyesha kuwa kumpa mtu uhuru usio na mipaka unaweza kuufanya uhuru huo kuleta madhara yasiyokusudiwa. Rais asipokuwa na uwezo wa kumkaripia Waziri wake, au hata kumshauri tu abadili mwelekeo basi ana ,udhaifu mkubwa.

Twafahamu kuwa JK aliafikiana na Kituo cha Demokrasia kuhusu njia mwafaka za kukamilisha mchakato wa Katiba mpya kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuliendesha zoezi hilo taratibu badala ya kuliharakisha kama Sitta anavyofanya sasa. Kwa makusudi kabisa, Sitta akaamua kupuuza ushauri wa JK, na kuendesha BMK atakavyo. Si vigumu kufahamu kuwa kilichompa jeuri Sitta ni ufahamu mzuri kwamba bosi wake, yaani JK, ni dhaifu asiyeweza kumwajibisha kwa kiburi hicho. Na muda wa kumshughulikia Sitta ataupata wapi ilhali yupo bize na safari zake za kuzunguka dunia?

Uongozi katika zama hizi za JK umekuwa kama mzaha flani, mchezo wa kuingiza usiopendeza, yaani a bad comedy, Hebu angalia picha hizi hapa chini kupata uthibitisho wa ninachoandika





Pichani juu ni vimemo vya Sitta akilazimisha matakwa yake.

Lakini tukiangalia kwa upana zaidi kuhusu ombwe lililosababishwa na udhaifu wa JK, tunakutana na kituko hiki hapa chini. Kimsingi, moja ya kumbukumbu za muda mrefu kuhusu utawala wa JK itabaki kuwa kuibuka kwa wanasiasa/viongozi ambao pengine sifa pekee waliyonayo katika uanasiasa/ uongozi wao ni vituko, kashfa, mazingaombwe, na mambo mengine yasiyopendeza. Kama nilivyotanabaisha hapo awali, ombwe hilo liletoa fursa kwa kila Dick, Tom na Harry kufanya atakavyo. Hebu angalia kioja hiki


Nimalizie makala hii kwa kutoa wito kwa Watanzania wenzangu kukazani katika dua/sala ili JK amalize muda wake kwa amani, maana mustakabali wa taifa letu upo hatarini. Ni muhimu kufahamu kuwa amani na utulivu tuliyonayo yahitaji vitendo vya wapuuzi wachache tu kabla haijatokomea. Na uzoefu waonyesha kuwa amani ikipotea ni ngumu sana kuirejesha. Na kubwa tunalohitaji ni kukoma mara moja kwa vitendo vya watawala wetu kuwaona Watanzania kama 'hamnazo' kama tunavyoshuhudia katika BMK huko Dodoma.

Tumtegemee Mungu katika hili, sambamba na jitihada zetu wenyewe kukabiliana na tabia inayozidi kukota mizizi ya kugeuza uongozi kuwa uhuni flani.

MUNGU IBARIKI TANZANIA 


1 Oct 2014


Big up ndugu yangu mpendwa Sintah, a true definition of beauty and brain. Wanasema eduaction is sexy but being more educated is even sexier. 

Napenda kukupongeza sana ndugu yangu kwa kuanza kozi yako ya Postgraduate Diploma in Management of Foreign Relations. Hiyo ni on top ya Shahada yako ya Kwanza (Bachelor of Arts in Public Administration and Management) na Shahada ya Uzamili (Masters of Arts in International Relations and Diplomacy) ulizonazo. 
Ninaamini vipaji kadhaa ulivyonavyo ukichanganya na elimu yako ya kiwango cha juu vinakufanya uwe role model kwa wengi.

Keep it up ndugu yangu, sky is the limit and the world is all yours for grabbing kwani ninaamini muda si mrefu tutakuskia ukituwakilisha katika medani za diplomasia kimataifa. 

Keep it up, Sintah, I am so proud of you!

Nakutakia kila la heri na baraka.

30 Sept 2014

Rais Jakaya Kikwete amezilaumu sera za uchumi za Tanzania baada ya nchi yetu kupata uhuru akidai zimepelekea hali duni ya kiuchumi.

Alieleza kuwa sera hizo ni moja ya sababu zinazoifanya Tanzania kuwa katika kundi la Nchi Masikini Zaidi Duniani (The Least Developed Countries - LCD) tangu utaratibu huo wa kuzigawanya nchi kutokana na viwango vyake vya kiuchumi na maendeleo uanze miaka ya 70.

Akihutubia Alhamisi iliyopita jijini Washington DC, nchini Marekani katika Kongamano la Shirika la Misaada la nchi hiyo (USAid Forum) kuhusu vikwazo vya maendeleo na jinsi ya kutokomeza umasikini uliokithiri, Rasi Kikwete alisema kwamba itikadi iliyoongozwa na kuaminiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere imeshindwa kuzaa matunda.

Akieleza kwanini nchi 33 kati ya 48 masikini zaidi duniani zipo Afrika, Rais alieleza kuwa nyingi ya nchi hizo (25) ni wahanga wa migogoro, lakini baadhi kama Tanzania zimekuwa na amani na utulivu lakini zimeendelea kuwa katika kundi hilo, akiamini kuwa ni matokeo ya sera mbovu za kiuchumi katika miongo miwli unusu baada ya uhuru.

"Nchi yangu pendwa Tanzania ni mfano hai wa nchi iliyojaaliwa amani na utulivu tangu ipate uhuru lakini ni moja ya nchi masikini zaidi duniani tangu mwaka 1971wakati mgawanyo wa nchi kutokana na hali yake ya kiuchumi na maendeleo uanze.Licha ya mazingira yasiyo mwafaka kimataifa, sera za  kiuchumi baada ya uhuru ambazo hazikufanikiwa zina mchango mkubwa (katika umasikini wa Tanzania," alisema.

Rasi kikwete aliwaeleza washiriki wa Kongamano hilo akiwamo Makamu wa Rasi wa Benki ya Dunia, Mark Diop, na Mtawala wa USAid Dr Rajiv Shah, kwamba mwelekeo wa kiuchumi ulianza kubadilika baada ya mageuzi ya kiuchumi kuanzia  miaka ya 80.

"Tumebaki katika barabara ya mageuzi tangu wakati huo na tumekuwa na mafanikio mazuri. Nchi yetu sasa inafanya vizuri kiuchumi, na muongo uliopita ulikuwa wa mafanikio zaidi.Kwa ujumla, uchumi ulikuwa kwa wastani wa asilimia 3.5 katika miaka ya 90 hadi wastani wa asilimia 7 katika muongo uliopita," alieleza.

Rais Kikwete, hatahivyo, alikiri kwamba kukua kwa uchumi hakujaendana sawia na kupunguza umasikini. Katika miongo miwili iliyopita, umasikini wa kipato ulipungua kutoka asilimia 39 mwaka 1990 hadi asilimia 28.2 mwaka 2012, ikiwa ni kupungua kwa takriban asilimia 11.

"Hii inaeleza kwanini hatutomudu kufikia kiwango cha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millenium Development Goals - MDG) ya kupunguza umasikini uliokithiri kwa nusu ya kipimo kilichowekwa mwaka 1990."

"Hata hivyo, tumekuwa na mafanikio katika kupunguza maradufu idadi ya watu wanaoishi chini ya kiwango cha umasikini wa chakula. Punguzo hilo ni kutoka asilimia 21.6 mwaka 1990 hadi asilimia 9.7 mwaka 2012, ikiwa ni kupungua kwa takriban asilimia 12."

CHANZO: Habari hii imetafsiriwa kutoka gazeti la The Citizen

MAONI YANGU: Huko nyuma, Rais Kikwete, kama ilivyo kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliwahi kutamka bayana kuwa hajui kwanini Tanzania ni masikini. Labda hizo safari za mfululizo huku ughaibuni zimempata mwangaza mpya, na sasa anashutumu sera za kiuchumi za Mwalimu Nyerere.

Japo kuna hoja za kitaalum zinazosapoti hoja yake kuhusu mchango wa mapungufu ya sera za kichumi katika umasikini wa Tanzania yetu, alichokwepa kuzungumzia ni mchango wa ufisadi unavyorutubisha kukua kwa umasikini wa nchi yetu. 

Japo baadhi ya wasomi wana mtizamo kama huo wa Kikwete kwamba sera za uchumi za Nyerere zilifeli, na kwamba hata kung'atuka kwake kulitokana na sababu hiyo - huku wengine wakienda mbali zaidi na kudai Nyerere alipaswa kuwaomba msamaha Watanzania baada ya experiement yake ya Ujamaa kufeli - ukweli unabaki kuwa jithada za kurekebisha mapungufu hayo zimekwazwa mno na ufisadi. 

Tanzania yetu imekuwa miongoni mwa mataifa yanayopokea lundo la misaada lakini kwa kiasi kikubwa misaada hiyo imeishia katika kutunisha akaunti za vigogo, sambamba na kuongeza idadi ya mahekalu yao, misururu ya magari yao ya thamani na hata kuongeza idadi ya 'nyumba ndogo' zao.

Kila ukimsikia JK anapozungumzia umasikini wa nchi yetu au kuzorota kwa uchumi wetu, jambo moja la wazi ni kukwepa kwake kutaja rushwa/ufisadi kama moja ya sababu kuu. Pengine nafsi inamsuta kwa vile kila anayefahamu siasa za nchi yetu anatambua mchango wa awamu zake mbili katika kustawisha ufisadi.

Kadhalika, JK amekuwa muumini wa kasumba ya 'kitaalamu' ya kuangalia takwimu kama tarakimu tu na kupuuzia kuwa tarakimu hizo zinamaanisha watu. Ni rahisi kwa Rais wetu kudai kuwa tumepiga hatua zaidi ya ilivyokuwa katika zama za Ujamaa kwa kuangalia takwimu na kupuuzia hali halisi huko mtaani.

Kwa wenye uwezo wa kutafsiri, anachofanya JK kwa sasa ni kujaribu kutengeneza kinachoitwa LEGACY ya utawala wake, kujitenga na ukweli kuwa yeye ni sehemu ya tatizo  - kama ambavyo utitiri wa safari zake huko nje unavyokwangua kipato chetu kiduchu - na kutupia lawama wengine, sambamba na kujaribu kuonyesha kuwa amekuwa akifanya jithada kubwa kuikomboa Tanzania yetu kutoka katika lindi la umasikini. Muda utaongea, na mengi kuhusu utawala wa JK yatazungumzwa baada ya kumaliza miaka yake 10 hapo mwakani. 

26 Sept 2014

Mahojiano na dadangu Fina Mango katika kipindi chake cha Makutano Show kinachorushwa na kituo cha redio cha Magic FM, Dar es Salaam. Masahihisho: Katika mhojiano hayo nimeeleza kwa makosa kuwa Great Britain inaundwa na England yenye mji mkuu London, Wales yenye mji mkuu Cardiff, na GLASGOW yenye mji mkuu Edinburgh. Niliitaja Galsgow kimakosa badala ya Scotland. Kadhalika, katika mahojiano hayo kuna sehemu nimesema kimakosa kwamba moja ya ugumu ulioikabili kambi ya NO ni jinsi ya kuitetea hoja ya mafuta. Nililenga kusema 'kambi ya YES na sio NO. Naomba samahani sana kwa makosa hayo yaliyotokana na kile Waingereza wanaita 'heat of the moment.'

24 Sept 2014

Scotland's First Minister and leader of the Scottish National Party (SNP) Alex Salmond (C). (Reuters/David Moir)
Chama tawala hapa Uskochi cha Scottish Nationalist Party (SNP) kimekuwa chama cha tatu kwa ukubwa kwa Uingereza nzima baada ya kuvuna wanachama wapya kwa asilimia 66% katika muda wa siku nne tu baada ya kushindwa katika kura ya uhuru wa Uskochi.

Jumla ya wanachama wapya 26,000 wamejiunga na chama hicho tangu Alhamisi iliyopita, na hivyo kutunisha idadi ya wanachama wake hadi kufikia zaidi ya 51,000, takriban maradufu ya idadi ya awali ya wanachama wake.

Takwimu hizo zimeleta mshangao mkubwa kufuatia kambi ya 'Ndiyo' iliyokuwa ikiongozwa na chama hicho tawala kushindwa katika kura ya uhuru kwa asilimia 45 kwa 55, na hatimaye kiongozi wake, Waziri Mkuu wa Uskochi, Alex Slmaond, kutangaz aanaachia ngazi mwezi Novemba mwaka huu.

Takwimu hizo pia zinamaanisha kuwa SNP imefanikiwa kuvuta asilimia 10 ya ya wakazi wa Uingereza nzima, na kuipiga kikipiga kikumbo chama cha Liberal Democrats kwa idadi ya wanachama wenye kadi za uanachama.

Wabunge wa chama hicho waliokutana Hollyrood, katika mji mkuu Edinburgh, walionyesha kuridhishwa na takwimu hizo mpya na mwelekeo wa jumla wa Uskochi kufuatia kura ya aidha Uskochi iwe huru au iendelee kubaki sehemu ya muunganowa Uingereza.

"Devolution (kuipatia Uskochi mamlaka zaidi badala ya uhuru) ililenga kuua utaifa (wa Uskochi)," alisema mbunge mmoja wa SNP. "Kisha matokeo ya kura ya uhuru na kujiuzulu kwa Salmond. Lakini matokeo yamekuwa kinyume kabisa."

Inadaiwa pia kuwa wanachama wapya 3000 wamejiunga chama cha Scottish Greens huku chama kingine cha Scottish Socialist Party kikivuatia wanachama wapya. Vyama vyote hivyo viwili vilikuwa vikisapoti uhuru wa Uskochi.

Jumla mpya ya idadi ya wanachama wa SNP ilikuwa 50000 mnamo saa 6 na dakika 40 jana, kulinganisha na wanachama 25642 Alhamisi iliyopita siku ya upigaji kura ya uhuru.

CHANZO: Imetafsiriwa kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni

21 Sept 2014

Scotland
Kura ya kuamua hatma ya Uskochi kama ibaki kuwa sehemu ya United Kingdom au iwe nchi huru imekwisha, wak asilimia 55 ya wapigakura kusema HAPANA na 45 kusema NDIYO.Kwa matokeo hayo, muungano unaounda UK, wenye umri wa miaka 307 umesalimika.

Wakati nitaielezea kwa undani zaidi kura hiyo ya uhuru wa Uskochi katika makala yangu ya Jumatano ijayo ndani ya jarida la RAI MWEMA,katika post hii nitazungumzia kinachoanza kuonekana kama 'Uskochi kuingizwa mkenge' kufatia kuanza kuparaganyika kwa baadhi ya ahadi za msingi zilizopelekea ushindi wa kundi lililotaka Uskochi iendelee kuwa sehemu ya Muunganowa UK.

Mmoja wa wanasiasa wanaotajwa kama waliofanikisha kuunusuru Muunganowa UK ni Waziri Mkuu wa zamani, Gordon Brown, ambaye kama Waziri Mkuu wa sasa, David Cameron, kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Ed Milliband, Naibu Waziri Mkuu na kiongozi wa chama cha Liberal Democrats, Nick Clegg, na kiongozi wa 'kampeni ya Better Together' ya kuunga mkono muungano ambaye pia alikuwa 'Waziri wa Fedha' wa serikali ya Labour, Alistair Darling, kwa pamoja waliwaahidi wapigakura ya uhuru wa Uskochi kuwa wakikataa uhuru 'watazawadiwa' kwa nchi hiyo kupatiwa mamlaka zaidi ya kiutawala na kimaamuzi.

Mamlaka hizo zinafahamika kama 'Devo Max.'Kimsingi Devo Max, kifupisho cha Maximum Devolution,  inamaanisha Bunge la Uskochi kuwa na nguvu katika kila kitu ispokuwa ulinzi na mambo ya nje. Hata hivyo licha ya ahadi kuwa Uskochi itapatiwa mamlaka zaidi, uwezekano wa kupatia Devo Max kwa maana halisi ya nguvu zote kabisa zinazohitajiwa ni kama haupo.

Kwa sasa, na hadi wakati inapigwa kura ya uhuru au la, Uskochi imepewa mamlaka ya kujiamulia mambo yake yenyewe katika sekta za elimu, afya, huduma za jamii, makazi, utalii, mazingira, uvuvi, misitu, kilimo, sheria na usalama wa raia, na baadhi ya maeneo katika sekta ya usafiri. Kwa upande mwingine, serikali kuu ya Uingereza (Westminster) ina mamlaka katika sekta ya ulinzi, hifadhi ya jamii (social security), mafao kwa jamii (benefits)- kwa hapa Uingereza, watu wasio na kazi wanalipwa fedha ya kujikimu na kodi ya nyumba na serikali,gesi na mafuta, nishati ya nyuklia, uhamiaji, ajira, mawasiliano ya radio na runinga, biashara na viwanda sera za nje, masuala ya walaji (cunsumer affairs) na Katiba. 

Sasa kilichoahidiwa na Cameron na wenzake kushawishi Waskochi wakatae uhuru kuhusiana na Devo Max hakipo bayana sana. Miongoni ya yaliyomo kwenye ajenda ni Uskochi kuwa na mamlaka zaidi ya ukusanyaji kodi na mafao ya makazi kwa wasio na ajira. Suala la gesi na mafuta na kodi za mashirika (corporation tax) hayapo kabisa katika makubaliano hayo ambayo kimsingi bado hayajafikiwa.

Lakini hata kabla shamrashamra za kusherehekea kusalimika kwa Muungano wa UK hazijaisha, kizaazaa kimeibuka katika jinsi ya kutekeleza ahadi hiyo ya kutoa mamlaka zaidi kwa Uskochi. Kwa upande mmoja, ahadi hiyo iumevutia madai ya mamlaka zaidi kutoka Wales na Northern Ireland kama nchi ambazo pamoja na Uskochi na England zinaunda muunganowa UK. Kwa upande mwingine, baadhi ya 'mikoa' yenye wakazi wengi, kama vile Manchester, Yorkshire, Cornwall, nk nayo imeanza kudai kupatiwa mamlaka zaidi ya kiutawala.

Ttatizo kubwa zaidi lipo katika kupata mwafaka kati ya chama tawala Conservatives na wapinzani wao wa Labour. Ili Uskochi iweze kupatiwa mamlaka iliyoahidiwa, Bunge la Muungano huko Westminster litalazimika kufanya mabadiliko ya katiba. Hilo tu ni tatizo pia, kwani kwa mujibu wa taratibu za hapa UK, mabadiliko ya katiba ya nchi hii ni zoezi linalohitaji muda mrefu. Lakini muda haupo upande wa Serikali Kuu kwa vile kuna matarajio makubwa kutoka kwa Waskochi waliokataa uhuru.

Hata urasimu wa mabadiliko ya Katiba ukiwekwa kando, bado kuna tatizo linalowakabili Cameron na Conservatives wenzie na Milliband na Labour yake. Kwa Cameron, ile kuahidi tu kuwa ataipatia Uskochi mamlaka zaidi, wabunge wengi tu katika chama hicho nao wameanza kudai mamlaka zaidi kwa majimbo yao. Kwa Milliband, tatizo ni kubwa zaidi. Kwa sasa, chama cha Labour kina wabunge 49 kutoka Uskochi katika Bunge Kuu la Muungano, ambao pia wanapiga kura katika maamuzi yanayoihusu England pekee. Hii imerejesha kinachoitwa 'swali la Lothian ya Magharibi' (the West Lothian Question), yaani kuhoji kwanini wabunge kutoka Uskochi katika Bunge la Muungano waruhusiwe kupigia kura masuala yanayoihusu England pekee ilhali wabunge kutoka England hawana fursa hiyo. Hii inalingana na 'kilio' cha baadhi ya wanasiasa wa Tanzania Bara wanaodhani si sawia kwa wabunge kutoka Zanzibar katika Bunge la Muungano kuhusika katika maamuzi ya masuala yanayohusu Bara pekee ilhali hakuna mbunge wa Bara mwenye mamlaka kama hiyo katika Bunge la Zanzibar. Kama ilivyo huko nyumbani, hakuna mbunge wa England katika Bunge la Uskochi, kama ambavyo hakuna mbunge kutoka Bara katika Bunge la Zanzibar.

Wakati chama cha Labour kitaanza Mkutano wake Mkuu hapo kesho na ajenda kuu ya Milliband ilipangwa kuwa kuzungumzia taasisi muhimu ya huduma za afya (National Health Service-NHS) sasa anaweza kulazimika kuzungumzia uwezekano wa chama hicho kupunguziwa nguvu katika Bunge Kuu la Uingereza iwapo mpango wa kuwanyima malaka ya kimaamuzi wabunge kutoka Uskochi katika Bunge la Muungano utatekelezwa.

Na siku hiyohiyo ambapo Labour wanaanza mkutano wao mkuu, Cameron anatarajiwa kutoa hotuba kuhusu kinachoiwa 'kura za Waengland kwa sheria za England' (English votes for English laws), kwa maana ya kura zinazopigwa katika Bunge Kuu katika masuala yanayohusu England zipigwe na wabunge wa England pekee, na wale wa kutoka Uskochi wasiruhusiwe kupiga kura hizo.

Tayari Cameron ameanza kumlaumu Milliband kwa upinzani wake dhidi ya mpango huo, akidai kuwa kiongozi huyo wa Labour anaisaliti England. Kwa upande wake, Labour inamshutumu Cameron na chama chake kwa kile inachokiona kama jitihada za kupinguzia Labour nguvu katika Bunge la Muungano.

Mhanga wa 'mgogoro' huo ni Uskochi kwani pasi kufikiwa mwafaka kati ya vyama hivyo viwili, uwezekano wa Uskochi kutekelezewa ahadi ya kuongezewa mamlaka ya kiutawala sio tu utachukua muda mrefu bali pia unaweza kukwama kabisa.

Na Waziri Mkuu wa Uskochi, Alex Salmond, aliyetangaza kuachia ngazi mwezi Novemba tayari ameingilia kati suala hilo na kuwakumbusha Cameron na Milliband kwamba tofauti zao zitapelekea waliopiga kura ya kukataa uhuru wa Uskochi kujiona kama 'wameingizwa mkenge' kwa kupewa ahadi za hadaa.

Kwa mtizamo wangu ninadhani mwamuzi ni muda (time will tell) lakini kama nilivyosapoti kambi iliyotaka uhuru wa Uskochi, imani yangu kutoka kwa Cameron, Milliband na wanasiasa wengine wa Westminster ni ndogo. Na hoja hii ilijitokeza wakati wa kampeni za kampeni za uhuru ambao kuna waliohoji, kama tupo 'Better Together' hivi sasa, kwanini basi mambo hayaendi sawia-kwa maana ya wanasiasa wa Westminster kuahidi mengi lakini kutekeleza machache. Kadhalika, kwa kukataa uhuru wa Uskochi kwa ahadi kutoka kwa wanasiasa, Waskochi wanaweza kuwa wamerudi kulekule kwa kurejea hatma yao mikononi mwa wanasiasa, tofauti na suala zima la kura ya uhuru lilivyoendeshwa  kwa kiasi kikubwa na wananchi wenyewe kwa mustakabali wao





20 Sept 2014


Kwanza ninaomba kukiri bayana kuwa nimehuzunishwa na matokeo ya kura ya maoni kuhusu uhuru wa Uskochi. Hiyo inatokana na ukweli kwamba sio tu nilikuwa naunga mkono kambi ya 'Yes' iliyokuwa inataka uhuru wa taifa hili bali pia nilipiga kura ya 'Ndiyo.'

Lakini kwa vile uamuzi wa iwapo Uskochi iwe nchi huru au iendelee kubaki sehemu ya United Kingdom ulipaswa kuamuliwa kwa wingi wa kura-hata ingekuwa moja tu- sina budi kuafiki matokeo na kukubaliana na ukweli. Ukweli kwamba asilimia 55 ya wapiga kura wametaka Uskochi iendelee kuwa sehemu ya UK huku waliotaka uhuru wakiwa asilimia 45 inamaanisha wengi wa Waskochi wanataka iwe hivyo. Na ukweli unabaki kuwa ukweli hata kama ni mchungu.

Hata hivyo, wakati ninatambua umuhimu wa sie kama Watanzania kujifunza kuhusu kura hiyo ya uhuru wa Uskochi, binafsi ninaona kuna unafiki mkubwa katika suala hili zima la 'tujifunze kutoka Uskochi.' Naomba nieleweke. Ni vema tujifunze kutoka kwa hawa wenzetu kuhusu hatma ya Muungano wetu lakini ninadhani ni unafiki kuamua kuchagua jema moja na kupuuzi mema mengine lukuki ya kujifunza kutoka kwa hawa wenzetu.

Eneo la kwanza la unafiki huo ni katika suala la uraia pacha. Moja ya hoja kuu iliyouwa wazo la uraia pacha kwa Watanzania walio nje ya nchi hiyo ni dhana fyongo kwamba uraia pacha ni tishio kwa usalama wa Tanzania. Si wanasema 'tujifunze kutoka Uskochi'? Sasa kwa taarifa tu ni kwamba katika kupiga kura hiyo ya uhuru wa Uskochi, baadhi ya wakazi wa taifa hili ambao japo si wazaliwa wala raia wa hapa waliruhusiwa kupiga kura. Kila mkazi wa Uskochi ambaye anatoka nchi za Jumuiya ya Madola aliruhusiwa kupiga kura. Na mie- hata kama ningekuwa sina sababu nyingine zilizoniruhusu kupiga kura- ningeweza kupiga kura kwa kigezo cha kuzaliwa Tanzania ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola.


Ni muhimu sana kutambua kuwa haki ya kupiga kura ni moja ya haki muhimu mno kwa mwananchi kwa sababu inachangia upatikanaji wa uongozi wa mahala husika, sambamba na ushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa taifa husika, kama ilivyo kwa suala la kura ya uhuru wa Uskochi.

Je Waskochi ni wendawazimu kuruhusu hata watu wasio na urai wa nchi hii kupiga kura? Hapana. Wenzetu wanathamini na kutambua mchango wa kila mwenye uhusiano na nchi hii, iwe wa kuzaliwa, asili au makazi. 

Na je kwa Waskochi kuruhusu  wakazi wa nchi hii ambao sio wazaliwa wa hapa, au wasio na uraia wa hapa, kupiga kura imehatarisha usalama wake? 

Naomba ieleweke kuwa haki ya kupiga kura haimfanyi mhusika kupewa uraia wa hapa bali ni moja ya vitambulisho muhimu sana. Kwa mfano, daftari la wapiga kura ni moja ya nyenzo muhimu katika uchunguzi unaofanywa na taasisi za fedha (credit check) kabla ya kutoa mkopo au hata kufungua akaunti ya benki. Kimsingi, kuwemo kwenye daftari hilo kunampatia mkazi wa hapa haki flani ambazo japo si sawa na uraia zinamsaidia katika maeneo mbalimbali.

Oh yes, tujifunze kutoka taifa tajiri la Uskochi linalowaenzi wageni wasio raia wa taifa hili ilhali masikini sie tunawahofia Watanzania wenzetu ambao kwa sababu moja au nyingine wamelazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine. Hapo kuna neno sahihi zaidi ya unafiki?

Twende katika maeneo mengine. Moja ya kumbukumbu muhimu kwenye runinga wakati matokeo ya kura hiyo yanatangazwa ni kuonekana kwa mkimbizi wa kisiasa kutoka Papua New Guinea, Benny Wanda, (pichani) akielezea anachojifunza kutoka kwa zoezi hilo la kidemokrasia 
Benny Wenda from West Papua, Indonesia

Wanda alikuja Uskochi kama mgeni wa kikundi kinachoitwa Radical Independence kujifunza jinsi kura ya maoni kuhusu uhuru inavyoandaliwa na kufanyika. Katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha BBC, kiongozi huyo alieleza jinsi alivyoguswa mno na jinsi uhuru ulivyokuwa ukitafutwa kwa uhuru mkubwa, akitolea mfano kutokuwepo kwa wanajeshi au polisi au vifaru mitaani tofauti na hali ilivyo nchi kwake wakati wa harakati za kudai uhuru kutoka Indonesia. Naam, tunasema tujiefunze kutoka Uskochi, lakini kimatendo ni kama picha hii hapa chini inavyoonyesha, na hapa sio katika harakati za wananchi kudai uhuru bali kutumia tu haki yao ya kikatiba kupinga uhuni unaofanywa dhidi ya upatikanaji wa Katiba mpya huko Dodoma 




Hebu tuache unafiki. Hivi kama hiyo haki 'kidogo' tu ya kuandamana kwa amani kwa minajili ya kutetea upatikanaji wa Katiba yenye maslahi kwa Watanzania wote, sambamba na kuokoa mabilioni ya fedha yanayotafunwa kwa Bunge 'feki' la Katiba huko Dodoma linazua haya, je tunaweza kukaribia japo kiduchu walipofika Waskochi kupiga kura kwa amani na utulivu kuhusu hatma ya nchi yao?

Na hata tukiweka kando hilo la matumizi makubwa ya nguvu za dola kunyamazisha sauti za wananchi, sambamba na kulazimisha matakwa ya watawala, bado kuna unafiki mwngi ne mwingi tu kama unavyotanabaishwa na picha zifuatazo


Picha hiyo juu inapigia mstari hoja yangu kuhusu unafiki. Naam, gazeti la serikali Daily News latoa rai kuwa tujifunze kutoka Uskochi, lakini picha iliyopo katika ukurasa huo inakinzana kabisa na hali ilivyo hapa Uskochi. Picha hiyo ni ya Rais Jakaya Kikwete akihutubia nchini Marekani ambapo amekwenda TENA kwa ziara ya WIKI MBI. Ni majuzi tu alikuwepo huko kwa siku kibao, lakini katika kuendeleza spirit ya 'safari ni safari' ameenda tena nchi humo.Ni hivi, ni nadra mno kusikia Waziri Mkuu wa Uskochi Alex Salmond akizurura huku na kule, au Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron akiwa kiguu na jia hapa na pale, au hata Malkia Elizabeti kuwa msafiri wa kila kukicha. Na hawa ni viongozi wa taifa hili tajiri kabisa lakini sio wazururaji kama Rais wetu.

Ndio rais lazima asafiri lakini sio kila baada ya wiki kadhaa, tena kurejea sehemu zilezile alizokwishatembelea. Hivi tangu 2014 hii ianze Kikwete ameshakwenda Marekani mara ngapi? Ndio, tujifunze kutoka Uskochi kuhusu kura ya uhuru wao lakini pia tujifunze kuhusu umuhimu wa viongozi kama Kikwete kutambua kuwa Tanzania yetu ni maskini isiyoweza kubeba gharama zisizo za lazima za Rais wake kusafiri kila anapojiskia.

Natambua ukweli kuwa kutokana na umasikini wetu, kuna haja ya viongozi wetu kwenda nje kusaka misaada. Lakini ni nani asiyejua kuwa asilimia kubwa ya misaada hiyo inaishia kwenye akaunti za mafisadi? Kadhalika, busara kidogo tu inaweza kutufundisha kwamba safari hizo za mara kwa mara za Kikwete zinatafuna sehemu ya fedha zinazosakwa kama misaada kwa nchi yetu.


Katika gazeti hili hapo juu tunakutana tena na wito wa kujifunza kutoka kwa kura ya uhuru wa Uskochi, lakini chini yake kuna habari kwamba deni la taifa limepaa hadi kufikia shilingi TRILIONI 42, kwa tarakimu ni shilingi  42,000,000,000,000 Na wakati hali yetu ikiwa mbaya kiasi hicho, bado twashuhudia serikali yetu ikifanya matumizi ya kitajiri kwa mfano kuruhusu uhuni unaoendelea huko Dodoma kwa jina la Bunge la Katiba, huku Kikwete akiendlea na safari zake za uuvumbuzi wa dunia.


Na picha ya hapo juu inathibiths unafiki wa kauli ya 'tujifunze kutoka Uskochi.' Kwa kifupi, zoezi zima la hadi kufikia kupigwa kura ya maoni liliambatana na uwazi na haki kwa kiwango cha juu kabisa. Japo ajenda ya uhuru ilikuwa katika manifesto ya chama tawala hapa Uskochi cha SNP, suala la uhuru lilibaki kuwa mikononi mwa Waskochi wote. Sasa kama mnavyoona hapo kwenye picha, kichwa kikuu cha habari kinahusu mwanasiasa wa upinzani Lema kupigwa marufuku na wafuasi wake kuandamana. Hivi haiwezekani wakaruhusiwa kuandamana huku wakisindikizwa na polisi? Na uzoefu umeonyesha kuwa mara nyingi polisi wakiridhia, maandamano hufanyika na kumalizika kwa amani. Mara nyingi pia, uamuzi wa polisi kulazimisha wananchi wasiandamane hupelekea vurugu na maafa yasiyo ya lazima


Pichani juu ni maandamano ya wanauonga mkono Uskochi kubaki sehemu ya UK, yaliyofanyika jana jioni hapa Glasgow, na polisi walikuwepo kwa minajili ya kuhakikisha hakuna uvunjifu wa amani lakini sio kuyazuwia maandamano hayo.

Nimalizie makala hii ndefu kidogo kwa kutilia mkazo kuwa tuna mengi ya kujifunza kutoka Uskochi na sio suala hilo la kura ya maoni pekee. Wanasiasa wa Uskochi na pengine Uingereza kwa ujumla wametoa darasa zuri kwa wababaishaji wetu huko nyumbani ambao licha ya kuwalipa mamilioni ya shilingi kwa mwezi kama mishahara na posho lakini tunachoishia kushuhudia ni matusi, vijembe, malumbano na upuuzi mwingine kwenye vikao vya Bunge la kawaida na hili la Katiba.

Ndiyo, umoja ni nguvu, na kura ya maoni ya uhuru wa Uskochi kumalizika kwa nchi hiyo kubaki sehemu ya United Kingdom kunatukumbusha sie wana-Muungano wa Tanganyika na Zanzibar juu ya umuhimu wa mshikamano lakini ni muhimu kutambua kuwa mazingira waliyopitia Waskochi kufikia hapa yameletwa heshima na utambuzi wa haki za kibinadamu, kidemokrasia sambamba na kuangalia mustakabali wa nchi hii sio kwa leo na kesho tu bali pia miaka mingi ijayo.





19 Sept 2014

Alex Salmond
Waziri Mkuu wa Uskochi Alex Salmond amejiuzulu wadhifa huo kufuatia kushindwa kwa kura ya maoni ya 'uhuru wa Uskochi.'

Salmond, mwanasiasa machachari, ameeleza kuwa ataondoka madarakani rasmi mwezi Novemba. Alieleza kuwa amemwandikia barua Katibu Mkuu wa chama anachokiongoza cha Scottish National Party (SNP) kuwa hatogombea uongozi.

"Baada ya kura ya uongozi ndani ya SNP hapo Novemba, nitaondoka madarakani kama Waziri Mkuu ili kuruhusu kiongozi atakayechaguliwa katika mkutano huo kuchukua wadhifa huo kwa mujibu wa kanuni za Bunge."

Alipoulizwa na mwandishi wa Shirika la Utangazaji wa Uingereza (BBC) kwa atafanya shughuli gani baada ya kung'atuka Uwaziri Mkuu, ikizingatiwa kuwa 'unri haujamtupa mkono,' Salmond alitanabaisha kuwa ataendelea kujihusisha na shughuli za siasa. "Sintojitoa moja kwa moja katika siasa." Alisema kuwa anaweza kushiriki chaguzi zijazo kwa minajili ya kuwa mwanasiasa wa kawaida. "Huhitaji kuwa kiongozi wa SNP au Waziri Mkuu ili uweze kushiriki katika siasa."

Waziri Mkuu wa Uingereza 'nzima' David Cameron alimpongeza Salmond, na kumwelezea kama mwanasiasa nguli, hata kama walitofautiana kimsimamo kuhusu Muungano wa Uingereza."

CHANZO: Habari hii imetafsiriwa kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni

ALHAMISI, Septemba 18, 2014, mamilioni ya Waskochi watapiga kura ya kuamua hatma ya taifa lao, aidha liwe taifa huru au liendelee kuwa ndani ya ‘Muungano wa Falme ya Uingereza.’
Pengine kabla ya kuelezea kwa undani kuhusu kura hiyo, ni muhimu kutoa ufafanuzi kuhusu nchi hii ambayo kwa wengi inaitwa tu Uingereza japo ina ‘mkanganyiko’ fulani katika majina yake halisi kwa Kiingereza. Jina halisi la nchi hii kama ilivyo sasa ni the United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland. Hivyo ndivyo ilivyo kwenye hati za kusafiria za nchi hii.
Great Britain ni muungano wa mataifa matatu: England ambayo mji mkuu wake ni London, Wales ambayo mji mkuu wake ni Cardiff na Scotland ambayo mji mkuu wake ni Edinburgh (ambao Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipata elimu yake ya chuo kikuu). Ukiunganisha Great Britain na Ireland ya Kaskazini (ambayo mji mkuu wake ni Belfast), ndio tunapata kitu kiitwacho The United Kingdom (of Great Britain and Northern Ireland) au kwa kifupi UK.
Ni muhimu kubainisha pia kwamba ‘kuna Ireland mbili,’ Ireland ya Kaskazini ambayo ni sehemu ya United Kingdom, na Jamhuri ya Ireland (Republic of Ireland), yenye mji mkuu wake Dublin, ambayo ni taifa linalojitegemea na sio sehemu ya UK.
Baada ya ufafanuzi huo, turejee kwenye ‘kura ya uhuru’ Alhamisi. Baada ya kipindi kirefu cha majadiliano na makubaliano, hatimaye wakazi wa Uskochi watapiga kura yenye jibu la ‘ndio’ au ‘hapana’ kwa swali ‘Je, unataka Uskochi kuwa nchi huru?’
Hadi wakati ninaandika makala hii kura za maoni zinaashiria mchuano mkali kabisa, ambapo moja ya kura hizo ilionyesha ‘wanaotaka uhuru’ (kambi inayojulikana kama ‘Yes’ inayoongozwa na Waziri Mkuu- hapa anaitwa First Minister- Alex Salmond, na chama chake cha Scottish Nationalist Party-SNP) inaongoza kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya kambi ya ‘No’ ya wanaotaka Uskochi iendelee kuwa sehemu ya UK, inayoongozwa na ‘Waziri wa Fedha’ (Chancellor of the Exchequer) wa zamani, Alistair Darling. Hata hivyo, kura nyingine ya maoni inaonyesha kambi ya No inaongoza kwa idadi hiyo hiyo ya pointi.
Binafsi nitakuwa miongoni mwa wapiga kura hao. Na pengine suala hili linapaswa kuwasuta wanasiasa wetu walioamua kwa makusudi kuwanyima Watanzania wenzao kadhaa haki ya uraia, kwa kukataa suala la uraia pacha. Ni hivi, kwa hapa, haki ya kupiga kura inawapa haki raia wa nchi za Jumuiya ya Madola, ikiwemo Tanzania, kupiga kura. Kwa hiyo, pamoja na ‘sababu nyingine,’ kinachonipa haki ya kupiga kura hiyo ni asili yangu kama Mtanzania, nchi iliyowahi kuwa koloni la Uingereza.
Japo ningetamani sana kubashiri matokeo ya kura hiyo ya kesho, matukio kadhaa ya hivi karibuni yananifanya nishindwe kufanya hivyo. Awali, kwa uelewa wangu wa stadi za siasa na chaguzi, nilitarajia matokeo kuwa ‘Uskochi kuendelea kubaki sehemu ya UK,’ wazo lililopewa nguvu na kura mbalimbali za maoni hadi wiki chache zilizopita.
Na pengine mtizamo huo, ambao wachambuzi wengi wa siasa walikuwa nao pia, ulichangia viongozi wa vyama vikuu vya siasa hapa Uingereza, wanaounga mkono Uskochi kuendelea kuwa sehemu ya UK, chama tawala cha Conservative na washiriki wake wa Liberal Democrats na chama cha upinzani cha Labour, wasihangaike kuhamasisha kura ya ‘hapana.’ Hata hivyo, wiki iliyopita ilishuhudia ujio wa Waziri Mkuu David Cameron (akiwakilisha Conservatives), Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg (akiwakilisha Liberal Democrats) na Ed Milliband (kiongozi wa Labour) hapa Uskochi kupiga kampeni dhidi ya kura ya ‘ndiyo.’
Ujio huo ulichangiwa zaidi na kura ya maoni ya taasisi ya kura za maoni inayoheshimika hapa Uingereza, ya YouGov, iliyoonyesha kambi ya ‘Ndiyo’ ikiwa mbele kwa asilimia 51 na kambi ya ‘hapana’ ikiwa na asilimia 49. Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kabisa kwa kambi ya ‘ndiyo’ kuongoza katika kura za maoni. Na pengine kuashiria kuwa uwezekano wa ‘uhuru wa Uskochi’ si suala la kufikirika tu bali linawezekana, asilimia hiyo 51 katika kura za maoni ilikuwa imepanda kwa takriban asilimia 30 ndani ya mwezi mmoja.
Ningependa kutumia nafasi hii kukiri kwamba kamwe sijawahi kushuhudia siasa ikifanya kazi kama ilivyo sasa tunapoelekea kwenye ‘siku ya hukumu’ hapo kesho (Alhamisi). Wenyewe wanasema ‘siasa imerejea kwenye siku zake za nyuma’ au kwa kimombo ‘old school politics.’ Wanasiasa wameonekana mitaani wakijumuika na wanaounga mkono au kupinga ‘uhuru wa Uskochi,’ huku mijadala mbalimbali ikifanyika katika hali unayoweza tu kulinganisha na mijadala ya maisha yetu ya kila siku, ila kwa umuhimu mkubwa kabisa.
Japo nina furaha ya kuwa miongoni mwa watakaopiga kura kuamua hatma ya taifa hili, ninajisikia uchungu kuona hali ikiwa tofauti kabisa huko nyumbani, ambapo sasa tunashuhudia Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, akitumia ubabe dhidi ya ushauri wa Rais Jakaya Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania kuwa mchakato wa kupata Katiba mpya usogezwe mbele. Sitta ameziba kabisa masikio yake dhidi ya kelele kutoka kila kona kuwa Bunge la Katiba lisitishwe na taifa lijipe muda kujipanga vizuri kushughulikia suala hilo muhimu kwa mustakabali wa taifa letu.
Ndiyo, pengine Sitta anataka kuchapa kazi kwa kinachoitwa ‘kasi na viwango,’ lakini japo kasi kwa mwendesha gari la mashindano ya Formula One ni mkakati mzuri wa ushindi, kwa barabara za mtaani ni sawa na kuikaribisha ajali. Kichwani mwangu ni kama namsikia Sitta akijigamba siku moja, ‘mie ni mtu wa viwango na kasi, na mmeshuhudia wenyewe jinsi nilivyoweza kuhakikisha Bunge la Katiba linakamilisha kazi yake ndani ya muda tuliojipangia.’ Japo ninashindwa kutabiri matokeo ya kura ya kesho, sipati tabu kubashiri kuwa ‘kiburi cha Sitta’ sio tu kitaharibu mchakato mzima wa kupata Katiba mpya bali pia chaweza kuwa ndio anguko lake kisiasa.
Nikiangalia jinsi ajenda ya ‘uhuru wa Uskochi’ ilivyoanza hadi kufikia leo siku moja kabla ya kupiga kura, nadhani sitaonekana mtu wa ajabu nikiyumkinisha kuwa ‘kuna kitu fulani walichojaaliwa hawa wenzetu lakini sisi tumenyimwa...au tumejinyima.’ Nikisikiliza hoja za kambi zote mbili- wanaotaka uhuru na wanaopinga- mkazo unawekwa zaidi kuhusu hatma ya taifa hili (Uskochi au UK kwa ujumla) na vizazi vijavyo. Kwa kiasi kikubwa, japo kura zitapigwa kesho, lakini mtizamo wa wengi ni wa muda mrefu kabisa.
Ningetamani sana Sitta asome makala hii na ajifunze jinsi mwafaka wa kitaifa unavyopatikana kwa njia za demokrasia halisi, kwa maana ya wanaotaka uhuru wa Uskochi na wanaopinga kujadiliana kistaarabu na hatimaye kupewa fursa ya kuhitimisha mjadala huo kwa sanduku la kura. Mchakato huu umechukua muda mrefu, japo si kwa gharama kubwa kulinganisha na ‘vurugu-mechi’ yetu ya kusaka Katiba mpya.
Na japo hoja ya ‘uhuru wa Uskochi’ imekuwa ajenda ya muda mrefu ya chama cha SNP, kampeni ya ‘kudai uhuru’ imeendeshwa kwa utaifa badala ya itikadi za kichama. Na wengi wanaounga mkono suala hilo wametamka bayana kuwa wanafanya hivyo kwa mustakabali wa Uskochi na sio kuiunga mkono SNP. Kadhalika, wanaopinga suala la ‘uhuru’ wamekuwa wakieleza bayana kwamba hawafanyi hivyo kwa minajili ya kuviunga mkono vyama vya Conservatives, Labour au Liberal Democrats.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanadai kuwa hata kama kambi ya ‘hapana’ itashinda na Uskochi kuendelea kuwa sehemu ya UK, wazo la kudai uhuru halitokufa, huku baadhi wakitabiri kuwa Uskochi inaweza kuwa huru ndani ya miaka 10 ijayo. Sababu ni nyingi lakini kubwa zaidi ni utawala wa chama cha kihafidhina cha Conservatives ambao sera zake zimeonekana kuwachukiza Waingereza wengi.
Lakini kama ilivyo huko nyumbani ambapo kila Rais baada ya Mwalimu Julius Nyerere anahofia kuvunjikiwa na Muungano wetu wakati wa utawala wake- kinachoitwa ‘kuogopa mzimu wa Nyerere’- kwa hapa pia mtihani unaomkabili Waziri Mkuu Cameron ni kutoingia katika historia kama mtu aliyeongoza Uingereza na kushuhudia Uskochi ikijitenga.
Laiti Uskochi ikipata uhuru wake, kuna dalili kuwa ‘moto’ huo ukasambaa sehemu nyinginezo duniani, ambapo tayari kumesikika ‘kelele kama hizo’ huko Hispania na kwingineko. Lakini pengine la muhimu zaidi kwa hatma ya Muungano wetu ni ukweli kwamba Uskochi ni makazi ya Wazanzibari wengi (na kwa ufahamu wangu wengi wao kesho watapiga kura ya ‘ndiyo’ kama ilivyo kwa wapiga kura wengine wengi wenye asili ya nje ya Uskochi). Je, kwa kuona ‘mchango wao’ katika kupatikana uhuru wa Uskochi hawawezi kuhamasika kuchochea Wazanzibari wenzao huko Zanzibar kuhusu ‘uhuru wa nchi yao’?
Nimalizie makala hii kwa kukiri kwamba nina msisimko kama ilivyo kwa Waskochi wengine kuhusu siku ya kesho na umuhimu wake kwa hatma ya taifa hili ambalo kwangu limekuwa ‘nyumbani mbali na nyumbani’ (home away from home) kwa zaidi ya miaka 12 sasa. Yawezekana makala hii ikawa ya mwisho kuiandika nikiwa katika Uskochi iliyo sehemu ya UK. Lakini kubwa zaidi ni kupata fursa adimu ya kushuhudia historia ikijiandika- iwe kwa Uskochi kujitenga au kubaki sehemu ya UK. Na kubwa zaidi kama mwana-stadi za siasa, ni kushuhudia jinsi siasa inayofanya kazi katika hali ambayo nimekuwa nikiisoma vitabuni tu.
Japo kura ni siri, kesho nitapiga kura ya 'ndiyo’ ili Uskochi iwe nchi huru, hasa kutokana na imani yangu kwamba ina uwezo na sababu za kuwa huru. Kwa hiyo basi, nihitimishe kwa kusema kwa ki-Skochi ‘AYE FOR ALBA’ yaani ‘Yes for Scotland’ au ‘Ndiyo kwa (uhuru wa) Uskochi’

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.