![]() |
Makala yangu katika toleo la wiki hii la jarida mahiri la Raia Mwema inazungumzia suala lililokamata hisia za Watanzania wengi kwa sasa la CCM kujivua magamba
Makala yangu katika toleo la wiki hii la jarida la Raia Mwema inazungumzia namna watawala wetu wanavyoendekeza matumizi ya anasa huku wananchi wa kawaida wakizidi kuwa masikini
Makala yangu wiki hii inajadili changamoto zinazowakabili mashushushu wetu
![]() |
Babu aenda msibani chini ya ulinzi
MCHUNGAJI Ambilikile Mwasapila anayetoa tiba ya magonjwa sugu huko Samunge Loliondo, juzi jioni aliondoka hapa kwenda Babati, Manyara kuhudhuria mazishi ya mtoto wake huku safari yake hiyo ikiratibiwa na Serikali na akipewa ulinzi mkali wa maofisa usalama na polisi.
Aliondoka Samunge saa 12:20 jioni na gari la Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro akiwa na maofisa hao wa usalama, polisi na wasaidizi wake.Kabla ya kuondoka Samunge, watu mbalimbali walikuwa wamejitolea kumpatia usafiri mchungaji huyo lakini walizuiwa kutokana na sababu za kiusalama.
"Tulikaa kama kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, tukaona ni busara tuchukue jukumu la kumsafirisha Mchungaji hasa kutokana na sababu za kiusalama," alisema ofisa mmoja mwandamizi wa serikali wilayani hapa.Alisema mchungaji huyo atalindwa akiwa msibani na atakaporejea Samunge.
Mgodi wa dhahabu waibuka shuleni• Walimu, wanafunzi waacha masomo, wachimba madini
na Makunga Peter, Bukombe
MGODI mpya wa machimbo madogomadogo ya dhahabu umeibuka katika Shule ya Msingi Nganzo, wilayani Bukombe, mkoani Shinyanga na kufanya viongozi wa wilaya kwa kushirikiana na mwalimu mkuu wa shule hiyo kuufanya kuwa mradi wao wa kujiingizia fedha.
Machimbo hayo yaliyoibuka takriban miezi miwili iliyopita yamesababisha shughuli na masomo katika shule hiyo kusuasua kutokana na walimu na wanafunzi kujiingiza katika shughuli za uchimbaji huku wakisahau kuzingatia masomo hali ambayo imesababisha utoro mkubwa wa wanafunzi.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho yalipo machimbo hayo, Boniphace Mashebela, alisema kuwa machimbo hayo madogo kwa sasa yanamilikiwa na kamati ya shule na kijiji lakini yanaendeshwa kwa ridhaa ya Ofisa Elimu wa Shule za Msingi, Fides Munyogwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Kuruletera Majige, kwa kigezo kuwa machimbo hayo yapo katika eneo la shule.
Mmoja wa wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo, Masamaki Kambale, alisema wao wapo hapo kisheria na si wavamizi kwani wao hufika na kuripoti ofisini kwa mwalimu mkuu pamoja na mtendaji wa kijiji na wao hugawiwa viwanja kabla ya kuzamisha maduwara yao.
Masamaki alisema kuwa kila duara linasajiliwa kwa sh 40,000, ambapo fedha hizo hupewa mwalimu mkuu na mtendaji wa kijiji na pindi duara linapofikia kuanza uzalishaji kila utoapo mifuko 10 ya mawe kati ya hiyo miwili ni mali ya viongozi hao wa wilaya hiyo.
Alisema kuwa kwa upande wa kamati ya shule na mtendaiji wao hutoza ushuru wa sh 1,000.
Kwa upande wake Ofisa Madini wa Wilaya ya Kahama na Bukombe, Medard Msengi, alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya shutuma hizo alisema mgodi huo mpaka sasa ofisi yake haiutambui na kuomba kuongozana na waandishi wa habari hadi katika eneo hilo kujionea.
Ofisa huyo alipofika alijionea kuwa machimbo hayo yanaendeshwa kinyume cha sheria, kwani kipimo kutoka shimo hadi shimo kinatakiwa kiwe futi 10 kwa 10 lakini hayo yapo futi mbili hadi tatu, hali ambayo inaweza kusababisha maafa ya watu kufunikwa na kifusi wakati wowote wa uchimbaji.
Aidha, alitoa ushauri kuwa ni bora machimbo hayo yakafungwa kwa kuwa yapo katika eneo la shule, hali ambayo inachangia wanafunzi kutosoma vizuri na walimu kukimbilia kufanya biashara hiyo ya uchimbaji, hali ambayo itadhoofisha maendeleo ya elimu katika shule hiyo kwani hayana uataratibu wowote.
Alisema katika eneo hilo hakuna vyoo, hakuna mtaalamu anayetambulika katika ofisi yake ambaye anashughulikia madini katika eneo hilo maarufu kama waangalizi wa madini ili kufanya hali ya usimamizi katika eneo hilo kuwa rahisi na kudhibiti wanafunzi na walimu kufanya kazi hiyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe alipoulizwa kwa njia ya simu, alisema kuwa kweli machimbo hayo yapo katika eneo la shule na kuongeza kuwa tayari ameshatoa taarifa kwa mkuu wa wilaya ya maandishi, ila alikanusha kuwa yeye hahusiki katika kuchukua mifuko katika eneo hilo na kuiuza kama inavyosadikiwa
Barua za kuwang’oa kina Lowassa zakamilika• Yadaiwa ziko mezani kwa Msekwa
na Mwandishi wetu
Barua za makada watatu wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rostam Azizi, Edward Lowassa, na Andrew Chenge, za kuwataka wajiondoe katika nafasi za uongozi ndani ya chama hicho, ziko tayari.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano umethibitisha kwamba makada hao, waasisi wa mtandao uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani mwaka 2005, wanaweza kupokea barua zao wakati wowote kuanzia leo Jumatano.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, barua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) iliyomaliza kikao chake hivi karibuni mjini Dodoma.
Inadaiwa makada hao maarufu na wenye ushawishi mkubwa ndani ya nje ya chama hicho tawala, walipewa siku 90 tangu siku ya kikao, wapime wenyewe uzito wa kashfa zinazowakabili na wajiengue kwenye nafasi za uongozi, vinginevyo chama kitawaengua katika kikao kijacho cha NEC.
“Barua za Lowassa, Chenge na Rostam ziko tayari, na suala lao liko mikononi mwa Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chama. Wiki hii watakabidhiwa,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya CCM.
Pamoja na mambo mengine, barua hizo zimeorodhesha tuhuma zao na kurejea maazimio ya NEC yanayowahusu.
Alipohojiwa na Tanzania Daima Jumatano juu ya barua hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alithibitisha kwamba tayari barua hizo zimeshaandaliwa. Naye alisema watakabidhiwa barua hizo wakati wowote kuanzia leo Jumatano.
“Kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa maazimio ya NEC, si jambo geni. Ninachojua, tulikuwa tunasubiri mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka yapite, kila mtu ale Pasaka yake,” alisema Nape.
Wakati barua hizo zikisubiriwa kwa hamu, baadhi ya makada wajumbe wa NEC wamekaririwa na vyombo kadhaa vya habari na katika mazungumzo yasiyo rasmi wakisema hakukuwa na azimio lolote lililopitishwa la kuwataka makada hao wapewe siku 90 za kujiengua. Vilevile, wamekanusha kuwapo kwa azimio lolote la kuwaandikia barua.
Hata hivyo, Nape amekuwa akisema kwa waandishi na katika mikutano ya hadhara kwamba NEC ilitoa azimio hilo. Baadhi ya makada wasiokubaliana na kauli za Nape, katika hali ya kuwaonea huruma au kuwatetea watuhumiwa, wamekuwa wakidai kwamba kauli za Nape zimetoka nje, si ndani ya kikao cha NEC.
Lakini baadhi yao wamekuwa wakidokeza kuwa si rahisi Nape kujitungia maneno makali ya aina hii, huku wengine wakisema anatumwa na wakubwa “kuwashughulikia” kina Rostam.
Katika kujaribu kuthibitisha kwamba Nape anazungumza jambo lisilotokana na maazimio ya NEC, baadhi ya makada wanakumbushia kauli za hivi karibuni za mtangulizi wake, John Chiligati, ambaye amepata kutaja mara kadhaa taarifa zisizosahihi za maazimio ya vikao vya Kamati Kuu na NEC, tofauti na kilichojadiliwa ndani ya vikao hivyo.
Wanasema, kwa mfano, Chiligati alipata kulalamikiwa kwa kutoa taarifa potofu kuhusu maamuzi ya Kamati Kuu kuhusu uamuzi wa ama kuilipa au kutoilipa fidia kampuni ya uzalishaji umeme ya Dowans ambayo inaidai TANESCO shilingi bilioni 94.
Vilevile, wanasema Chiligati aliwahi kutoa maazimio ya kupotosha aliposoma maazimio ya NEC kuhusu utata ulioibuka baada ya kukatwa kwa jina la Hussein Bashe katika kinyang’anyiro cha uteuzi wa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM kwa jimbo la Nzega katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Hata hivyo, Nape anasisitiza kuwa kauli yake ni ya chama na inatokana na maazimio ya NEC. Katika mikutano ya hadhara inayodaiwa ni ya kujitambulisha, amekuwa akisisitiza kwamba Lowassa, Rostam na Chenge wametakiwa kujiondoa kwenye ujumbe wa NEC ndani ya siku 90, vinginevyo watang’olewa kwa nguvu.
Ndiye pia aliyesema kwamba wataandikiwa barua za kuwaorodheshea tuhuma zao na kuwataka waondoke kwenye uongozi wa chama. Hata hivyo, hakuna kiongozi hata mmoja aliyesema kama makada hao watavuliwa pia ubunge.
Lowassa ni Mbunge wa Monduli, Chenge anawakilisha jimbo la Bariadi Magharibi, na Rostam Azizi ni mwakilishi wa Igunga.
Wadadisi wa mambo ya siasa wanasema kilichotokea mjini Dodoma ni muendelezo wa minyukano ndani ya CCM na kwamba hoja kuu inayosababisha haya si ufisadi, bali urais katika uchaguzi wa mwaka 2015, hasa kwa kuwa baadhi yao wanasemekana wanatamani kugombea au kuunga mkono baadhi ya wagombea.
Nguvu yao ya kifedha na ushawishi wao ndani ya chama ni baadhi ya mambo yanayoogopwa na washindani wao ndani ya chama tawala. Ingawa wote watatu wamekuwa watu wa karibu sana na Rais Kikwete, habari zinasema kumekuwapo na taarifa za kuchongeana miongoni mwao, zikichochewa na makachero wanaomwaminisha Rais Kikwete kwamba sifa yake iliyopotea mbele ya jamii inaweza kurudi iwapo ataondokana na watatu hao.
Rais Kikwete naye anatumia ushauri huo kama fursa ya kurejesha matumaini ya wananchi kwake na CCM, akitumia kaulimbiu ya kujivua gamba.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wakosoaji wa Rais Kikwete wamesema kujivua gamba kunakofanywa naye ni unafiki mtupu, kwani kama lengo ni kupiga vita ufisadi, naye yu miongoni mwa waliotajwa kwa ufisadi pamoja na Chenge, Rostam na Lowassa.
Baadhi ya makada wamesema kwamba kama CCm inaazimia kuondoa mafisadi, basi kiwaondoe viongozi wote waliopatikana kwa pesa za kifisadi za EPA.
Katika orodha ya viongozi waliofaidika na ufisadi wa EPA, anatajwa pia Rais Kikwete, kwa maelezo kwamba pesa hizo zilitumika kununua kura ili ashinde.
Wanasema hata kuvunja Kamati Kuu na kuingiza wajumbe wengine hakukusaidia kuisafisha, kwani walioingia ni wachafu kama waliotoka, maana historia zao na wasifu wao vinafahamika.
Wengine wanakwenda mbali na kusema kwamba iwapo Rais Kikwete atatekeleza azima yake hii, atakuwa anaandaa anguko lake lisilotarajiwa, maana atakuwa anaongeza idadi ya maadui miongoni mwa watu wanaomjua vema, waliomjenga na kumsaidia hadi hapo alipo
Mafisadi CCM waandaa mamilioni kujisafisha*Wadaiwa kuandaa vijana kupinga hatua dhidi yao
Na John Daniel
KUNDI la mafisadi wanaokabiliwa na hatihati ya kuvuliwa uongozi na pengine uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamebuni mbinu mpyakujihami kwa kutumia haramu kwa kuandaa vijana kufanya maandamano kumpinga Rais Jakaya Kikwete na chama chake.
Kundi hilo linapinga vikali uamuzi wa CCM kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kuwapa muda wa kujiengua wenyewe kabla ya kufukuzwa baada ya siku 90.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu vimeeleza kuwa kundi hilo limepitisha bajeti ya mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwandaa vijana kufanya maandamano kupinga uamuzi wa kuondolewa NEC na hata CCM kwa ujumla, mara tu baada ya kukabidhiwa barua muda wowote kuanzia wiki hii.
"Tayari wameapa kuwa wakiondolewa ni lazima Rais Kikwete naye aondoke kwa kuwa ndiye aliyepitisha maamuzi ya kuwafukuza, wanapanga vijana kwa kuwarubuni kwa fedha haramu ili waandamane mara tu watakapopewa barua.
"Wiki iliyopita walikutana wakapitisha zaidi ya milioni 500 kumshughulikia Bwana mkubwa (Rais Kikwete), wanataka kumchafua ili kummaliza nguvu kuwashughulikia," kilisema chanzo kingine.
Habari hizo zilieleza kuwa mbali na Rais Kikwete anayeelezwa na kundi hilo kukabiliwa na tuhuma na ufisadi, akiwa miongoni mwa watu 11 waliotangazwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, na familia yake, akiwamo mwanawe Ridhiwan anayedaiwa kuwa mali kuliko kipato chake, pia kundi hilo linasaka kwa udi na uvumba majalada ya mawaziri wanne wa sasa kwa lengo la kuwaunganisha katika tuhuma za ufisadi, kwa kinachoelezwa kuwa ni kampeni ya 'tuchafuke wote'.
"Kati ya fedha hizo sh. milioni 18 zitatumwa katika mikoa 20 kugawiwa vijana ili wafanye maandamano ya kupinga kuondolewa na kuwapakazia wengine wanaotaka waondoke nao kama njia ya kujitakasa.
"Fedha zinazobaki zinatumika kununua mafaili ya watu wengine kutafuta makosa yao ya aina yoyote akiwamo Waziri wa Afrika Mashariki, Bw. Sitta (Samwel) Prof. Mwandosya, (Mark), Dkt. Mwakyembe (Harrison) na Membe au Magufuli," kilisema chanzo chetu.
Ilielezwa kuwa kundi hilo limekuwa likifanya vikao katika maeneo maeneo mbalimbali kwa lengo la kutaka kujisafisha na ufisadi, au kupunguza makali kwa kutaja wengine.
"Mmoja wao amejiandaa kuzungumza na waandishi wa habari kuwapa nyaraka za uongo ili kuwachafua watu wengine, walengwa wakuu ni Rais na familia yake, mawaziri wanne na wengine wadogo," kilisema chanzo kingine.
"Usifikiri hatujui hayo, mbinu zote wanazofanya tunazijua, hatuwezi kupambana na wajinga, tunasubiri tuone mwisho wao, lakini hata ninyi waandishi lazima mjue kuwa Watanzania wanaosoma vitu mnavyoandika wanajua yote," alisema kigogo mmoja wa serikali bila kutoa ufafanuzi.
Mbinu nyingine iliyotajwa mara baada ya uamuzi wa NEC Dodoma ni kuwatumia viongozi wa vyama vya siasa kutoa tuhuma mpya ili ionekane kwamba wameonewa na kupoteza lengo la kuwaondoa.
Pamoja na kwamba hakutaja jina, Chama cha demokrasia na Maendeleo ndicho kimetaja watuhumiwa wapya wa ufisadi, huku Katibu Mkuu wake, Dkt. Slaa akipinga madai ya kutumiwa kufanya hivyo kwa nia ya kuwachafua.
Katika tuhuma hizo, alizungumzia uuzaji wa nyumba za serikali bila kufuata utaratibu zilizoelekezwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na aliyekuwa waziri wake wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli; Kuhusu fedha za EPA na mahali zilipo zile zilizorejeshwa akielekeza tuhuma hizo kwa Rais Kikwete na John Malecela na Philip Mangula waliodaiwa kuhusika katika wizi wa fedha za EPA, hasa zile zilizoingia katika kampeni ya CCM mwaka 2005.
Katika hatua nyingine kundi hilo la mafisadi wa linadaiwa kuwalenga baadhi ya viongozi wa dini kuwasafisha kwa kutangaza msimamo kuwa wameonewa na hakuna mtakatifu au wao wametolewa kafara.
Majira ilipomtafuta Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye kujua kama wana taarifa hizo alikiri na kuongeza kuwa haziwasumbui kwa kuwa mfa maji hakosi kutapatapa.
"Kwanza nilishasema nilipokuwa uwanja wa Manzese, niliwaambia wananchi kuwa mafisadi wamejipanga kumchafua Mwenyekiti wetu na familia yake"
Diwani matatani kwa kumwita Chiligati fisadi
na Francis Godwin, Iringa
DIWANI wa kata ya Mgama, wilayani Iringa Vijijini, Denis Lupala (CCM), yuko matatani baada ya kumwita Naibu Katibu Mkuu CCM, Tanzania Bara, Kapteni John Chiligati, kuwa ni fisadi na anapaswa kuvuliwa gamba kama Katibu Mkuu aliyepita Luteni Yusuf Makamba na wenzake.
Diwani huyo anadaiwa kutoa kauli hiyo hivi karibuni mkoani Iringa wakati Chiligati na viongozi wengine wapya wa sekretarieti ya CCM taifa alipofanya ziara mkoani humo kwa ajili ya kujitambulisha.
Diwani hayu ambaye tayari ameitwa na sekretarieti ya wilaya na Kamati ya Maadili kujadiliwa kwa utovu kwa Chiligati na viongozi wengine waandamizi wa CCM ambao alipendekeza watimuliwe.
Akithibitisha kuitwa kwenye vikao hivyo, Lupala alisema alipewa barua ya kuitwa kuhusu tuhuma hizo, lakini hakuhojiwa.
‘Kweli waliniita na mwanzoni niliambiwa kikao kitanijadili kwa utovu wa nidhamu niliouonyesha badala yake tulijadili tukio la jukwaa kuanguka wakati Chiligati akihutubia,” alisema diwani huyo.
Hata hivyo alijigamba kuwa alikuwa amejiandaa kupangua hoja zao kwani hadi sasa binafsi hataki Chiligati abaki kwenye nafasi hiyo kwa madai kuwa anapaswa kuvuliwa gamba kama viongozi wenzake aliokuwa nao kwenye sekretarieti iliyopita.
“Nilijipanga vizuri kuwajibu viongozi wa wilaya iwapo wangejaribu kutaka kuniadhibu kwa kumwita Chiligati fisadi. Ni ukweli usiopingika kuwa kati ya watu wanaovuruga CCM Chiligati ni mmojawapo na hana sifa ya kuwa kiongozi ndani ya CC na nasema kuwa niko tayari kuwajibika kwa kusema ukweli dhidi ya Chiligati,” alisema diwani huyo.
Hata hivyo habari zaidi zinasema kuwa diwani huyo anatarajiwa kuitwa wakati wowote kuanzia sasa kujibu tuhuma alizozielekeza kwa Chiligati.
Wakati wa mkutano wa hadhara, diwani huyo wa CCM alipata nafasi ya kuuliza swali na kuanza kumrushia madongo Chiligati kwamba ni fisadi na ajiuzulu nafasi yake.
Pia alitaka Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, Andrew Chenge (Bariadi Mashariki) na Rostam Aziz (Igunga) na wengine kufilisiwa mali zao na kunyang’anywa kadi za uanachama.
Hata hivyo alishindwa kuendelea na hoja yake baada ya baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM kuingilia kati na kusitisha swali lake kwa Chiligati.
Wa-Tanzania wanalalamika sana kuhusu mikataba bomu ambayo inalisababishia Taifa hasara kubwa. Tafsiri yao, kwa ujumla, ni kwamba tunaingizwa katika janga hili na mafisadi ambao wanasaini kwa makusudi mikataba hii, kwamba hao ni wa-Tanzania wenye ubinafsi na uroho, na hawana uchungu na nchi, bali wanatafuta namna ya kunufaika wao. Mafisadi wetu hao wanashirikiana na mafisadi wa nje kuitafuna nchi yetu.
Kwa ujumla, nami nina hisia hizo. Kwanza kuna ukweli usiopingika kuwa maadili katika nchi yetu yanazidi kuporomoka. Vile vile nazingatia usemi wa wahenga kuwa lisemwalo lipo, na kama halipo laja. Pia tunaona taarifa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuhusu uozo wa rushwa katika masuala ya mikataba, zabuni, na kadhalika.
Lakini msimamo wangu hauishii hapa. Naamini kuwa hata kama tukiondoa kabisa rushwa na ufisadi, tukawa na watu wanaojali maslahi ya nchi na hao ndio wakawa wanaosaini mikataba yetu, bado tutaendelea kulizwa na mikataba bomu.
Kitakachosababisha janga hili ni kuanguka kwa elimu katika Tanzania. Kama ninavyosema daima katika blogu hii na sehemu zingine, wa-Tanzania tumejichimbia kaburi kwa kutothamini elimu ipasavyo. Ushahidi ni ufahamu wa lugha ulivyo duni, na utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ulivyofifia au kutoweka miongoni mwetu.
Nikifafanua suala la lugha na kulihusisha na suala la mikataba, napenda kusema kuwa tupende tusipende, mikataba ya kimataifa itaendelea kuandikwa kwa ki-Ingereza, nasi tutajikuta tunasaini bila kuelewa vizuri kilichomo. Kuna matapeli wengi duniani, ikiwamo katika uwanja wa biashara na uwekezaji.
Wajanja, kwa kutambua umbumbumbu wetu, watachukulia mwanya huu kama mbinu ya kutukomoa. Laiti tungekumbuka msisitizo wa Mwalimu Nyerere pale tulipopata Uhuru, kuhusu maadui watatu tuliopaswa kupambana nao: umaskini, maradhi na ujinga.
Mwaka jana, serikali ya CCM ilitamka mara kwa mara kwamba imefanya marekebisho katika mikataba ya madini, ili kuziba mianya iliyokuwepo, iliyokuwa inatukosesha mapato tunayostahili. Sasa hapo nina suali. Ni nini kilichotufanya tusione hizo dosari tangu mwanzo? Kama si ufisadi, labda ni huu ujinga ninaoongelea. Binafsi, nakerwa kwamba serikali haijatuelezea undani wa suala hilo.
Kashfa mpya ya Ufisadi TanescoTuesday, 26 April 2011 10:14
CAG ADAI IMEILIPA DOWANS BILIONI MOJA ISIVYO HALALIMwandishi WetuSHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limeingia katika kashfa nyingine ya ufisadi baada ya kubainika kuwa limeilipa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans dola za Marekani 1.2 milioni ikiwa ni gharama ya kusafirisha mitambo ya kampuni hiyo kuja nchini kwa ndege badala ya dola 120,000.
Matumizi hayo ya ziada yanayokadiriwa kufikia Sh1.4 bilioni za Tanzania yanaelezwa kwamba yaliingizwa katika akaunti ya Dowans kimakosa.
Hata hivyo, mpaka sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amesema Tanesco imeshindwa kumpelekea ripoti ya matumizi ya fedha hizo alizoziita kuwa ni ufisadi.
Mbali na hivyo CAG amelitaka shirika hilo limpelekee mchanganuo wa matumizi ya dola za Marekani 4,865,000 sawa na Sh6.8 bilioni.
Jana, alipotakiwa kufafanua kuhusu ripoti hiyo, CAG Ludovic Utoh alisema: “Nashukuru kwa kunipigia, lakini nyie si mnazo ripoti hizo, mnaweza mkasoma na kuendelea kuripoti.”
Kwa mujibu wa gazeti la The East African, toleo la Aprili 25, mwaka huu, ripoti ya CAG iliyoishia Juni 30, 2010 inaonyesha kuwa Tanesco ilifanya malipo hayo kupitia akaunti ya gharama za mikutano.
Taarifa hiyo imeonyesha kuwa Tanesco ilishindwa kutoa maelezo kuhusu malipo hayo kwa ajili ya kukodisha ndege maalumu ya kusafirishia mitambo hiyo. Pia inaonyesha kuwa kiasi cha Sh13,000,000 ziliripotiwa kimakosa kama Sh1,300,000,000 kwenye kifungu cha matumizi ya vikao na pia kiasi cha Sh11.0 bilioni kinachohusu malipo kupitia barua ya mkopo (letter of credit) na kuingizwa katika akaunti ya makusanyo ya shirika kupitia benki ya NBC.CAG pia alibaini kuingizwa mara mbili kwa Sh101 milioni katika akaunti ya mitambo ya Tanesco kinyume na taratibu.
CAG alisema kuwa ndani ya Tanesco hakufanyiki usuluhishi wa mapato yatokanayo na mauzo katika matawi yake kukiwemo pia jumla ya Sh103,000,000 za masurufu ambazo hazijarejeshwa. Pia umeme unaozalishwa na ule unaouzwa unaonyesha kwamba shirika hilo linapata hasara kutokana na sababu za kiufundi.
Ripoti hiyo inasema, Tanesco ilionyesha hasara za uniti 1,188 KwH’m kutoka katika uniti 4,831 KwH’m inazozalisha ikionyesha kwamba kuna hasara katika mapato. Hasara hizo zinachangiwa na kuwepo kwa wateja wasio waaminifu, bili za uongo na uunganishaji haramu wa umeme.
Imeeleza kwamba hata wateja waliokatiwa umeme, wanaendelea kutumia huduma hiyo kama kawaida licha ya kudaiwa wastani wa dola za Marekani 65,000.CAG, Utouh alikaririwa akisema manunuzi katika shirika la Tanesco yalirekodiwa kimakosa na kwa udanganyifu.
Utouh alisema wakati wa ukaguzi, iligundulika kwamba Tanesco, hawakuwa wakifanya ‘reconciliation’ (upatanisho) ya mwezi kati ya mauzo na mapato.Kwa mujibu wa CAG, kuna hasara katika idara za uzalishaji na usambazaji wa umeme kwenda wateja.
“ Kuna mapendekezo niliyoyatoa yanayotakiwa kuchukuliwa hatua na Serikali, Bunge, Kamati ya Hesabu za Serikali, Bodi ya Wakurugenzi na maofisa watendaji wakuu kupitia ripoti ya fedha iliyoishia Juni 30,2009,” ilisema ripoti hiyo.
Katika ripoti hiyo, CAG alisema katika ripoti ya mwaka uliopita ya ukaguzi katika mamlaka za umma na bodi nyingine kuna mapendekezo 15 yaliyotolewa kwa utekelezaji: “Lakini hadi sasa mapendekezo hayo hayajatekelezwa kikamilifu.”
Alisema mapendekezo hayo ambayo hayajatekezwa yanahitaji ufumbuzi wa Serikali ili kuyawezesha mashirika mengine ya umma kufanya vizuri.
Badra Masoud, Meneja mahusiano wa Tanesco hakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hiyo baada ya simu yake kuita muda wote bila kupokelewa huku simu ya Mkurugenzi wa Tanesco William Mhando ikiwa haipatikani.
CHANZO: New HabariFatuma Maumba, Mtwara
BAADA ya Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapila kuanza kutoa dawa ya kikombe katika Kijiji cha Samunge, kilichopo Loliondo Mkoa wa Arusha, mkoani Mtwara ameibuka mtu mmoja anayetibu kwa kutoa dawa ya kijiko.
Kutokana na kuwapo kwa mtu huyo, Ahmad Linangwa maarufu kama Mzee wa Kijiko, wananchi wengi wamekuwa wakifurika katika Kijiji cha Moma Wilaya ya Mtwara Vijijini, Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kupata dawa ya kijiko.
Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwake kijijini hapo juzi, Linangwa alisema kabla ya kuanza kutoa dawa hiyo inayotibu magonjwa sugu ukiwamo ukimwi, awali aliota na kupewa maelekezo na Mwenyezi Mungu namna ya kuchanganya miti ya aina tatu kwa ajili ya kupata dawa hiyo.
“Pamoja na kupewa maelekezo hayo Aprili 18 mwaka huu, pia niliambiwa baada ya kuchanganya miti hiyo, nivilige kitu kama goroli kisha nichanganye na maji pori ambayo nitayagema kwenye mti unaoitwa Mtamba.
“Nikishafanya hivyo, maji hayo niwape wagonjwa nao watapona magonjwa yanayowasumbua,” alisema Linangwa.
Kwa mujibu wa Lingangwa, kabla ya kuanza kuwapa wagonjwa dawa hiyo, alianza kuinywa yeye wakati alipokuwa porini akiiandaa.
“Nilianza kuinywa nikiwa kule porini, nilipomaliza kuinywa, nilikimbilia nyumbani haraka ili kama ni sumu iniue wakati nimeshafika nyumbani lakini sikufa.
“Kwa hiyo watu waje watumie dawa hii, haina masharti yoyote kwani kama mtu anatumia dawa za hospitali anaweza kuendelea na dawa hizo bila wasiwasi, kama unakunywa pombe, au unavuta sigara, dawa yangu haina matatizo,” alisema Mzee wa Kijiko.
Kutokana na kuwapo kwa matibabu hayo, nauli kwa pikipiki na bajaji zimepanda kutoka Mtwara Mjini hadi kijijini Moma.
Kichuguu;
Mimi kama mmoja wa wanachama waandamizi wa Jamii Forums ambapo nimekuwa mwanchama kwa karibu miaka mitano sasa tangu ikiwa Jambo Forums kabla ya kubadili jina na kuwa Jamiiforums nimekerwa sana na matamshi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM kuwa forums hii ni ya vijana wa CHADEMA. Naona kuwa amenivunjia sana heshima yangu mbele ya wenzangu kwa kunipa image ya kuwa mimi ni mpiga propaganda wa CHADEMA.
Baada ya kutafakari kwa kina matamshi ya Pius Msekwa na jinsi yalivyoathiri image yangu kama mwanachama wa JamiiForums, nimeamua kumfungulia mashtaka ya defamation kwenye mahakama ya Douglas County hapa Omaha Nebraska nchini Marekani. Nimejadiliana na mwanasheria wangu ambaye amenipatia kifungu cha sheria kinachoniruhusu kumshitaki raia wa nchi ya nje kwenye mahakama hii, iwapo marekani ina uhusiano wa kibalozi na nchi ya mshitakiwa. Sasa hivi tuko katika hatua za mwisho mwisho za kukusanya ushahidi imara.
Nimeshapata nakala za magazeti ya kiswahili na kiingereza ila nimekuwa natafuta video clip yenye kumwonyesha Msekwa akiwa anasema maneno hayo. Vile vile bado tunashauriana kiwango cha malipo ya Punitive Damages na Compensatory Damages; mwanasheria anashauri kuwa viwango hivyo vipimiwe zaidi kwa kuangalia jinsi gani Msekwa binafsi na chama chake walivyofaidika au watakavyofaidika kutokana na matamshi yake hayo, na kwa kiasi kidogo jinsi gani yalivyoathiri image yangu binafsi kama mwanachama mwanadamizi ambaye hujitambulisha kwa wenzagu wote kuwa mimi ni Premium Member wa JamiiForums.
Tukikamailisha taratibu zote, nitawaarifuni au mtasikia kwenye vyombo vya habari Msekwa akiwa subpoenaed kwenye kesi hii ambayo pamoja na mambo mengine ninataka kuwadhibiti wanasiasa wasiwe wanaropoka mambo bila kuwa na uhakika nayo.
Sasa unaweza kusoma tovuti hii katika mwonekano (sura) mbalimbali.Bonyeza maandishi 'yanayotembea' hapo juu yanayosomeka 'BONYEZA HAPA KUSOMA TOVUTI HII KATIKA MWONEKANO MBALIMBALI' kisha utahamishiwa katika ukurasa mwingine ambapo unaweza kuchagua kuisoma tovuti hii kama CLASSIC, FLIPCARD, MAGAZINE, MOSAIC, SIDEBAR, SNAPSHOT au TIMELINE.Bonyeza kimshale ← kwenye browser yako ili kurudi kwenye mwonekano wa kawaida wa tovuti hii.