23 Jan 2008

Rafiki yangu mmoja amenitumia barua-pepe muda mfupi uliopita baada ya kusoma makala yangu ndani ya toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema.Hakuwa na pongezi wala malalamiko bali alidai kwamba wakati anasoma makala hiyo alijiskia kama anaongea nami uso kwa uso japo tuko umbali wa maili elfu kadhaa.Ni kweli,napoandika makala huwa najitahidi kadri ya uwezo wangu kuiwasilishalisha kwa kutumia staili ya mazungumzo (conversational style).Lakini sio mazungumzo kama ndani ya semina-elekezi,warsha,kongamano au semina bali yale yanayoweza kuwa yanafanyika mahala ambapo "tunaongea kwa kijinafasi" (comfortably).

Tukiachana na hilo,makala yangu ndani ya toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema inagusia michuano ya soka ya Mataifa ya Afrika huko Ghana,na kuielezea kwamba ni moja ya habari njema chache kutoka bara hilo,hasa kwa vile kwa takriban mwezi sasa habari zinazotawala kutoka huko ni kuhusu vurugu zinazoendelea Kenya zilizotokana na matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo.Kwa kutumia mfano hai,makala hii pia inaelezea ugumu anaoweza kukabiliwa nao Mtanzania pindi akidadisiwa chanzo cha umasikini wa nchi yetu,kabla ya kuwachambua mafisadi wa fedha na wale wa mawazo.Pamoja na habari na makala nyingine zilizokwenda shule katika jarida hilo la Raia Mwema,bingirika na makala hiyo kwa KUBONYEZA HAPA.

Ukimaliza kusoma makala hiyo,unaweza kuangalia clips hizi za versions mbili za Jesus Walks ya Kanye West.Naamini nasi tunahitaji nguvu za kiroho kukomesha ufisadi huko nyumbani.



22 Jan 2008

Usiku huu (kwa saa za hapa Uingereza) msanii wa Bongofleva,T.I.D,alifanya mahojiano mafupi na kituo cha runinga cha BEN cha jijini London,kuhusu ziara ya msanii huyo nchini hapa.Inapendeza kuona msanii kutoka nyumbani akihojiwa,lakini nahisi kulikuwa na tatizo kidogo katika mfumo wa mahojiano hayo ambapo kwa mtizamo wangu,nadhani mtangazaji alitaka interview iwe ya Kiswahili lakini T.I.D alijibu maswali mengi kwa "Lugha ya Mama" (kimombo),japo sina budi kumsifu kwamba aliimudu kwa kiasi chake.Pia sidhani kama mtangazaji huyo atajiskia vibaya iwapo atatokea mtu wa kuhoji kama alijiandaa vya kutosha kufanya mahojiano hayo au ilikuwa ni ghafla.Anyway,kuna clips mbili hapa nilizozirekodi kwa kutumia simu ya zamani kidogo,Sony Ericsson W810i lakini nadhani itakuwa imejitahidi kwenye ubora wa video.Enjoy










Wafuatiliaji wa blog hii watakuwa wameshasoma mara kadhaa niki-confess kwamba mie nina "allergy" na masuala ya namba (hisabati).Sasa hii mada fupi nayoandika inahusu uchumi,na kwa "kilaza" wa namba kama mie,ipo kazi kuiwasilisha vema ieleweke.Ntajitahidi hivyohivyo.Jana,masoko mbalimbali ya fedha (au hisa?),kwa kimombo stock markets,yaliyumba sana kiasi cha kuleta hofu miongoni mwa wachumi.Index ya FTSE (Uingereza) ilianguka kwa asilimia 5.48,Paris CAC40 ya Ufaransa ilikuwa asilimia 6.83,Frankfurt DAX ya Wajerumani asilimia 7.16 na huko Japan,index ya Nikkei ilianguka kwa asilimia 4.Masoko ya Marekani yalikuwa yamefungwa kufuatia maadhimisho ya siku ya Dr Martin Luther King,Jr.

Sina idea yoyote kuhusu hizo asilimia,lakini angalau katika gazeti la The Sun la hapa Uingereza nimepata mwangaza kuhusu uzito wa ishu hiyo.Kwa mujibu wa gazeti hilo,jumla ya hisa zenye thamani ya pauni bilioni 77 "zimepotea" (ki-stock market),na limetafsiri "hasara" hiyo into pauni 1,266 kwa kila mkazi wa nchi hii (sawa na shilingi 2,816,261.95 za Kitanzania)

Je akina sie na kijisoko chetu pale Mtaa wa Samora tunapaswa kuhofu kufuatia kuyumba huku kwa masoko haya makubwa duniani?Au tunapaswa kuhofia zaidi kuhusu mabilioni (wengine wanadai ni zaidi ya trilioni) yaliyoibiwa huko BoT kuliko habari hizi zinazohusu FTSE,DAX,CAC,et cetera?Je wewe msomaji unaonaje?

Just a joke...Au baada ya kuondoka Alan Greenspan,Mervyn King na magavana wenzake wafikirie kuwataka ushauri hawa wanao-Make It Rain...a clip by Fat Joe ft Lil' Wayne (Caution:Explicit Lyrics)

20 Jan 2008

Siku chache zilizopita,ndege aina ya Boeing 777 ya British Airways ilinusukirka kusababisha maafa makubwa baada ya kupata matatizo wakati linajiaandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Heathrow.Marubani na wafanyakazi wengine wa ndege hiyo (iliyokuwa na abiria 152) waliibuka mashujaa kwa namna walivyoweza kuepusha balaa hilo.Kwa mujibu wa takwimu zilizopo,uwanja huo wa Heathrow ni wa tatu duniani kwa idadi ya abiria nyuma ya Hartsfield-Jackson Atlanta International Airport na O'Hare International Airport (vyote vya Marekani).Ukweli kwamba uwanja wa Heathrow uko pembezoni (magharibi) kidogo tu ya katikati ya jiji la London,inamaanisha kwamba laiti ndege hiyo ingeanguka kungetokea maafa makubwa.

Awali pongezi nyingi zilikuwa zikielekezwa kwa rubani mkuu wa ndege hiyo,Kapteni Peter Burkill,lakini alipohojiwa kwenye mkutano na vyombo vya habari alieleza kwamba shujaa halisi alikuwa rubani msaidizi ambaye ndiye aliyekuwa kwenye "usukani" wakati ndege hiyo inahangaika kutua,na alitumia jitihada zake zote kuepusha maafa makubwa.Kichekesho ni kwamba kwa Kiswahili jina la shujaa huyo ni MSALITI,anaitwa John COWARD.Baadhi ya magazeti yakapata element ya kuchekesha katika habari hizo kwa vichwa vya habari kama hiki (kwenye gazeti la The Daily Mail):A Hero Called Coward (yaani "shujaa aitwaye msaliti")

Lakini kama hiyo haitoshi,moja ya magazeti ya udaku ya hapa,News of The World,leo limetoa picha za zamani za Kapteni Burkill akiwa nusu mtupu wakati anakula maraha kwenye likizo nchini Marekani.Katika baadhi ya picha hizo,rubani huyo anaonekana akiwa amemwagiwa chokoleti huku akinadada wawili wakijibidiisha kumlamba.Katika moja ya vimbwanga hivyo,rubani huyo ambaye wakati ho alikuwa mwajiriwa wa shirika la ndege la Caledonian,alilazwa sakafuni na chokoleti kumwagwa kwenye makali yake katika mchezo uliolenga kufananisha suala la kuendesha ndege.

Clip hii ya Ludacris ft Nate Dogg katika wimbo Area Codes inaweza kuwa mwafaka kwa stori hii ya ndege na airports (Caution: explicit lyrics)



Makala hii ilitoka kwenye gazeti la Mtanzania siku ya Alhamisi 17Jan 2008.

Hatimaye ugavana wa Dkt Daudi Ballali katika Benki Kuu ya Tanzania umetenguliwa.Sijui kama utenguzi huo ni sawa na tunachosoma,kuona na kusikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwamba Balali amefukuzwa kazi.Pengine la muhimu kwa sasa ni kwamba mtu huyo ametolewa katika wadhifa huo japo la muhimu zaidi ni kuweka rekodi vizuri kwa minajili ya kuondoa utata uliojitokeza hasa katika neno “KUTENGUA”.

Kuna wanaosema kwamba Ballali ametolewa kafara hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba sio rahisi wizi mkubwa namna hiyo uwe umefanywa na mtu mmoja tu.Ni vigumu pia kuamini kwamba uamuzi wa gavana huyo wa zamani kuyazawadia makampuni yaliyotajwa kwenye ufujaji wa fedha hizo ulifanywa na mtu mmoja pekee (Balalli).

Sakata hili lilisabaisha,linasababisha na litaendela kusababisha maswali mengi zaidi kuliko majibu.Sijui kuna wazalendo wangapi hapo Benki Kuu, lakini nashawishika kuhoji uzalendo wao kwani japo si kila mtumishi angeweza kufahamu alichokuwa akifanya Balali na washirika wake,ni dhahiri wapo waliokuwa katika nafasi ya kutoa taarifa kwa vyombo husika lakini wakaamua kukaa kimya.

Nadhani kuna waliojua kinachoendela lakini wakaa kimya kwa vile nao walikuwa washiriki katika ufisadi huo.Hawa hawana cha kujitetea kwani hawana tofauti na Balalli na wanachostahili ni adhabu tu.Kikwazo kikubwa kinachojitokeza katika uwezekano wa kuwaadhibu waungwana hawa ni ukweli kuwa baadhi yao wamepewa nafasi ya kujichunguza wenyewe (kwa vile bado wako madarakani) na sote tunaelewa kwamba hawawezi kujihukumu.Sanasana wataishia kuharibu ushahidi muhimu katika uchunguzi mzima wa ufisadi huo.

Kundi la pili ni wale waliokuwa wakifahamu kinachoendelea lakini hawakuchukua hatua kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kauli za utetezi zilizokuwa zikitolewa na watu mbalimbali pindi tuhuma za ufisadi huo zilipoanza kuibuka.Tunakumbuka kwamba kuna wakati huko bungeni lilitolewa tishio la kumfikisha Dr Slaa mbele ya vyombo vya sheria akituhumiwa kwamba ameghushi nyaraka zinazohusiana na sakata hilo.Yayumkinika kusema kwamba kauli kama hizo zinaweza kuwa ziliwakwaza baadhi ya watumishi wa Benki Kuu (waliokuwa na ufahamu wa ufisadi huo) kuripoti kuhusu uhuni uliokuwa ukiendelea hapo.
Imeripotiwa pia kwamba moja ya makampuni ya ukaguzi wa mahesabu ya benki hiyo iliripoti kuhusu kasoro zilizokuwepo lakini ikaishia kuona mkataba wake na benki hiyo ukisitishwa.Ni rahisi kukubaliana na “busara” hii kwamba kama kampuni iliyolipwa kuchunguza mahesabu imepuuzwa je “nani atanisikiliza mie niliyeajiriwa kufanya majukumu mengine katika Benki Kuu”.

Miongoni mwa madhara ya kulea ubadhirifu ni kujengeka kwa imani (miongoni mwa wasiojihusisha na ubadhirifu huo) kwamba ubadhirifu sio dhambi kwani ingekuwa haukubaliki basi wahusika wasingeendelea nao pasipo kuchukuliwa hatua.Yeyote aliyehusika na skandali hiyo lakini bado yuko madarakani ni sawa na kansa ambayo isipodhibitiwa inasambaa katika mwili mzima.Ni kama katika familia yenye watoto kadhaa na baadhi yao wanajihusisha na tabia zisizofaa.Ni dhahiri wale wanaoepuka tabia hizo (ilhali wenzao wanaendelea nazo) wanaweza kushawishika kuiga tabia hizo hususan kama wanaona wenzao wananufaika kwa namna flani.

Nakumbuka hivi karibuni,mkongwe wa siasa Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alinukuliwa na gazeti moja akieleza masikitiko yake kuhusu namna uzalendo unavyopungua miongoni mwa Watanzania.Ni kweli uzalendo umepungua sana na tusipokuwa makini utapotea kabisa lakini kuwa na wasiwasi au kulalamika pekee hakuwezi kusaidia kurekebisha mambo.Ni dhahiri kwamba moja ya mambo yanayochangia kupungua uzalendo ni pamoja na ufisadi kama huo uliofanyika hapo Benki Kuu.

Hivi mtu atakuwaje mzalendo iwapo wakati yeye anahangaika kutafuta fedha za kumwezesha kupata angalau mlo mmoja wa siku kuna wajanja wanatumbukiziwa mamilioni ya shilingi kwenye makampuni yao pasipo kuvuja tone moja la jasho.Kibaya zaidi na pengine katika kuwaringia walipa kodi wanaoibiwa,mafisadi hawaogopi kuonyesha namna wizi wao “unavyolipa” kwa kuporomosha mahekalu ya gharama kubwa,magari ya thamani ya kutisha na vimbwanga vingine chungu mbovu.Ni kama mtu anakupora mke halafu kesho yake unamwona anatamba nae mtaani.Hii inaongeza chuki na hasira kwa aliyeibiwa.

Kila zinapojitokeza tuhuma za ufisadi huwa nashindwa kujizuia kuhoji uwezo wa TAKUKURU katika jukumu lake la kuzuia na kupambana na rushwa.Taasisi hii imekuwepo kwa muda mrefu sasa lakini bado ni legelege licha ya jitihada kadhaa zilizokwishafanywa iwe na ufanisi zaidi.Naafikiana na baadhi ya hoja kwamba matendo mengi ya ulaji fedha za umma hayafanyiki hadharani,hivyo kusababisha ugumu katika kuyabaini.Hata hivyo,katika sakata hili la ufisadi hapo BoT,tetesi zilikuwepo mtaani na magazetini kwa muda mrefu.Kama ilivyozeleka,kauli za TAKUKURU zilikuwa “taarifa hizo tunazo na tunazifanyia uchunguzi”.Ikumbukwe kwamba katika mazingira ambayo matatizo yanazaliana kila kukicha,kuchelewa kutatua tatizo moja ni sawa na kutengeneza mlima wa matatizo hayo ambapo mwisho wake itakuwa ni suala lisilowezekana kabisa kuyaondoa.

Pengine umefika wakati mwafaka kwa wawakilishi wetu huko bungeni kuhoji uhalali wa kuendelea kuwa na taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa.Kanuni ya haki katika sheria inatamka waziwazi kwamba haki sio tu itendeke bali pia ionekane imetendeka.Tunaweza kuitumia kanuni hiyo kwa TAKUKURU pia kwamba mapambano dhidi ya rushwa yasiishie tu kuwa ya dhamira bali yaonekane hadharani kuwa yapo na yana ufanisi unaotarajiwa.

Naweza kuonekana mtu wa ajabu iwapo nitashauri kuvunjwa kwa TAKUKURU lakini nina hoja ya msingi napofikiri hivyo.Mamilioni ya fedha yanayoelekezwa kwa taasisi hiyo kupambana na rushwa hayajasaidia lolote katika kupunguza tatizo hilo.Mabadiliko mbalimbali ya kisheria yaliyolenga kuipa meno taasisi hiyo nayo yameshindwa kuifanya iwajibike ipasavyo.Binafsi sioni cha ziada kinachoweza kubadili ulegelege wa taasisi hiyo zaidi ya kuivunjilia mbali na kasha majukumu yake kuhamishiwa kwenye taasisi nyingine kama vile kitengo cha upelelezi katika jeshi la polisi (CID).

Kwa kuzingatia rekodi ya TAKUKURU katika uendeshaji wa kesi inazopeleka mahakamani,sintoshangaa iwapo wanaotajwa kwenye sakata hilo wataishia kuibuka washindi kwenye kesi hizo.Tumeshuhudia namna taasisi hiyo ilivyokuwa “ikipelekeshwa” kwenye kesi dhidi ya Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia.Kama kesi ya mtu mmoja imekuwa ngoma nzito namna hiyo,tutarajie nini kwenye lundo la kesi linalowahusu watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha?

Wengi wanatafsiri vurugu zinazoendelea nchini Kenya kuwa ni matokeo ya ukabila.Lakini baadhi ya wachambuzi wa uchumi wananyumbulisha kwamba vurugu hizo ni sehemu tu ya mapambano ya kiuchumi kati ya wenye nacho na wasio nacho.Migongano ya kidini au kikabila hujichomoza zaidi kwenye jamii isiyo na uwiano wa kimapato kwani mara nyingi washiriki kwenye vurugu hizo huamini kwamba pindi zikifanikiwa zitarekebisha maisha yao ya kila siku.Tuna kila sababu ya kuzuia nchi yetu inayosifika kwa amani na utulivu isiingie kwenye machafuko yanayoweza kusababishwa na wengi wanaoona wachache wakinufaika kwa “ulafi wa kula keki ya taifa” huku wao (wengi hao) wakiendelea kutaabika.Kinachowezekana leo kisingoje kesho.

19 Jan 2008

Miongoni mwa matukio ya mwaka jana yaliyoathiri huduma hapa Uingereza ni pamoja na mgomo wa wafanyakazi wa Royal Mail (kufupisha maelezo,tuliite "shirika la posta la hapa").Pamoja na madai mengine yaliyopelekea mgomo huo,ni upinzani wa wafanyakazi hao dhidi ya mpango wa Royal Mail kuongeza teknolojia ambazo zingepelekea kupunguza wafanyakazi.Teknolojia ina faida na hasara zake,na moja ya "hasara" kubwa ni kupunguza utegemezi wa binadamu katika sehemu ya kazi.Ni dhahiri kwamba kiwanda "kikiajiri" robots basi kuna watu watakosa cha kufanya mahala hapo.

Bila shaka unakumbuka mada ya Mapinduzi ya Viwanda (Industrial Revolution) ambapo maendeleo katika sayansi na teknolojia yalipelekea baadhi ya vibarua kujikuta wanatimuliwa kazi.Katika kupambana na hali hiyo,ziliibuka harakati zilizojulikana kama Luddism.Kwa kifupi kabisa,harakati hizo zilihusisha hujuma dhidi ya mitambo iliyoonekana kama adui dhidi ya ajira.

Nimesoma habari flani ya kuchekesha katika tovuti ya Allhiphop.com kwamba rapa Mike Jones "ameboresha" video moja ya wimbo wake Drop&Gimme 50 kwa kutumia wanenguaji vikatuni (animated cartoon vixens).Nafahamu bayana kwamba vikatuni haviwezi kuchukua kabisa (completely) nafasi ya video vixens,lakini kwa kumbukumbu ya Luddism na mgomo wa Royal Mail,nikajikuta najiuliza:je hao warembo wanaonadhifisha video mbalimbali wangechukua hatua gani iwapo (kwa kufikirika) wanamuziki wengi wangeamua kutumia teknolojia ya vikatuni badala ya warembo hao?Au ndio akina Buffie the Body,Ki-Toy Johnson,KD Aubert,na wengineo wangeishia kuwa virtual tu (kama kwenye computer games) kama sio kusahaulika kabisa?Just thinking aloud.

Video nayozungumzia ni hii


Miongoni mwa video za nyimbo zilizotamba japo wahusika walikuwa vikatuni ni pamoja na Piggy Bank ya 5o Cent (Caution: explicit lyrics)


Na hii Be Faithfull ya Fatman Scoop

Siku chache zilizopita nilizungumzia kuhusu "afya" ya muziki wa Bongofleva.Dhamira ya makala hiyo ilikuwa ni kuwaamsha wahusika na kuwakumbusha kwamba japo ni vizuri kula matunda ya jasho lao,wanapaswa kuwa makini wasije kujikuta wanakata kabisa na mimea inayotoa matunda hayo.

Leo napenda kuzungumzia nafasi ya muziki huo katika kuleta mabadiliko kwenye jamii.Nilisoma mahala flani kuhusu lawama dhidi ya rapa maarufu huko Marekani,Jay-Z,baada ya kutoa albam yake mpya ya American Gangster.Katika makala hiyo,mwandishi alimlaumu Jay-Z kwamba sehemu kubwa ya albam hiyo ilikuwa imetawaliwa na "meseji za kawaida za marapa"...kujisifia kwingi,blings,warembo,nk.Mwandishi huyo alidai kwamba alitegemea,katika nafasi yake kama mmoja ya majina makubwa ya Weusi nchini Marekani, Jay-Z angeelekeza jitihada katika "kuzisaidia 'hoods katika mapambano ya ukombozi wa kweli wa mtu Mweusi".Anyway,sijapata fursa ya kusikia nyimbo zote zilizo katika albam hiyo,kwahiyo siwezi ku-comment lolote katika hoja ya mwandishi huyo.Hata hivyo,alichokisema kina mantiki kuhusiana na muziki wetu huko nyumbani.

Wasanii wa bongofleva na wale wa aina nyingie za muziki (kama taarabu na muziki wa dansi) ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa ufisadi.Wengi wao hugeuzwa,ashakum si matusi,mithili ya "kondom za kisiasa".Hapo namaanisha kwamba baadhi ya wanasiasa huwatumia wasanii hawa wakati wa kampeni zao za kusaka uheshimiwa lakini wakishapata madaraka huwapuuza kabisa wasanii hao waliowapigia debe.Ni mithili ya kondom,ambayo kwa kawaida huonekana yenye umuhimu mkubwa (kwa wale wanaojali) kabla ya tendo la ndoa,lakini hugeuka takataka baada ya kutumika.

Wapo watakaodai kwamba wanasiasa wana haki ya "kukatisha" mahusiano na wasanii hao kwa vile huwaalika kwenye kampeni baada ya kuwalipa.Hoja hiyo inaweza kupingwa na ukweli kwamba fedha au malipo sio kila kitu (money isn't everything).Chukulia mfano wa mwalimu.Anapokufundisha anafanya hivyo kwa vile ni mwajiriwa wa taasisi ya elimu,na analipwa kila mwezi kukupatia elimu,achilia mbali uwezekano kwamba unalipia (ada) elimu hiyo.Lakini (pamoja na kupuuzwa kwao) walimu wanaendelea kushikilia nafasi muhimu katika jamii kwani ndio wafunguzi muhimu wa jitihada za binadamu katika kukabiliana na mazingira yake.Mfano mwingine ni wazazi.Wametuzaa,kutulea na kutusapoti katika makuzi yetu.Wapo wanaoweza kudai kuwa huo ni wajibu wao.Lakini tunafahamu kwamba wangetaka,wangeweza kabisa kzuia ujio wetu duniani (kwa baba na mama kuamua kutokuwa na watoto zaidi,kabla sie hatujazaliwa,au hata kutoa mimba zilizosababisha tuzaliwe).Tunaendelea kuwajali wazazi licha ya ukweli kwamba uzazi ulikuwa ni jukumu lao.Mifano hiyo miwili inaweza kulinganishwa na hoja yangu kwamba malipo yoyote yanayofanywa baada ya kutendewa kitu kikubwa hayawezi kulinganishwa na thamani ya matendo hayo.For that matter,fedha yoyote inayotolewa kama malipo kwa wapiga debe kwenye kampeni ya mwanasiasa haiwezi kulingana na mchango wa wapiga debe hao.

Nirejee kwenye kichwa cha habari cha post hii.Wengi wetu tunamfahamu Masudi Kipanya,mchora katuni maarufu huko nyumbani.Katuni zake nyingi huzungumzia matatizo yanayoikabili jamii ya Watanzania,na kwa hakika amekuwa mwiba mkali kwa wanasiasa wababaishaji na mafisadi.Anafanya kazi halisi ya sanaa kwani sanaa ni kioo cha jamii.Kwa bahati mbaya,wasanii wa muziki (hususan bongofleva) wamekuwa "wapole" sana katika mapambano dhidi ya maovu katika jamii yetu.Unakumbuka tungo kama Wauguzi ya Wagosi wa Kaya,au Ndio Mzee ya Profesa Jay?Hizi zilikuwa zina ujumbe mzito ambao kwa hakika ulikuwa unawakilisha kilio cha jamii.Tatizo kubwa la muziki wetu ni kwamba umetawaliwa sana na mada ya mapenzi.Hakuna ubaya kuzungumzia mapenzi,lakini yayumkinika kusema kwamba ili mapenzi yaende vema,shurti kuwe na kitu tumboni,barabara ya kufika kwa mpenzio iwe inafikika kirahisi,ukifika kwao usiku kuwe na mwanga (kwa maana ya upatikanaji wa umeme)....yaani hoja hapa ni kwamba mapenzi yanastawi vema pale huduma muhimu kwa maisha ya binadamu zinapopatikana kwa ufanisi.Ufisadi ni moja ya sababu kuu zinazokwamisha upatikanaji wa huduma hizo,na kwa sababu hiyo,wasanii wenye mahaba na dhima ya mapenzi kwenye tungo zao wana kila sababu ya kupambana nao (ufisadi) kwani vinginevyo wanachokiongelea kitaendelea kuwa ndoto za kujiliwaza tu.

Wapo wasanii ambao wana sababu za ziada za kupambana na mafisadi.Hawa ni pamoja na wale walioporwa wapenzi wao ambao walirubuniwa na nguvu ya fedha za mafisadi.Na kila msanii ana sababu nyingine ya kukabiliana na mafisadi (wadosi) wanaowalipa ujira mdogo ilhali wao (wadosi) wanatengeneza mamilioni ya bure.Ununuzi wa kazi za wasanii zinategemea hali ya kipato cha wateja wao (ikizingatiwa kwamba wengi wenye uwezo wa kiuchumi wako bize sana na masuala yao mengine kuliko kusikiliza tungo za nyumbani,na mafisadi wako bize zaidi na kuimarisha mikakati yao ya kulikamua taifa,kuangalia maendeleo ya miradi yao na kuboresha nyumba zao ndogo),kwa hiyo wasanii wana wajibu wa kushiriki mapambano ya kuboresha maisha ya wateja wao wakuu (wengi wao wakiwa waathirika wakuu wa ufisadi).

Tunahitaji akina (Masudi) Kipanya wengine kwenye bongofleva na miziki mingine kushirikiana na wale wote walio katika mapambano dhidi ya ufisadi huko nyumbani.Kelele za aina yoyote dhidi ya wahalifu (mafisadi) hao zitasaidia angalau kuwakumbusha kwamba tamaa na furaha zao ni kilio kwetu.

Hebu msikie Skinnyman anavyolalamika katika clip hii ya Council Estate of Minds kuhusu hali halisi ya maisha kwenye maghorofa (yaliyosahaulika,na makazi maarufu ya watu wa kipato duni) ya manispaa (Council estates)


18 Jan 2008


Nimekuwa mwandishi wa makala magazetini tangu mwaka 1998,takriban miaka 10 sasa.Mtu aliyenipa changamoto la kufanya hivyo anaitwa Albert Memba,mwandishi wa zamani wa habari za michezo katika gazeti la Nipashe na Guardian.Huyu jamaa anaimudu lugha vilivyo.Nilianzaia kwenye magazeti "ya udaku" kama Sanifu (lilifariki zamani hizo) na baadaye Kasheshe na Komesha,ambako nilikuwa naandika unajimu "wa kuchekesha usio na chembe ya ukweli" (tuuite humorous horoscope) kwa kutumia jina la uandishi Ustaadh Bonge (hadi leo baadhi ya rafiki zangu wanaendelea kuniita hivyo).Baadaye nikamahimia kwenye uandishi wa makala za mambo muhimu zaidi ya vichekesho na udaku.Anyway,ni hadithi ndefu.

Nilipata wazo la ku-blog katikati ya mwaka juzi.Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sintampongeza Ndesanjo Macha,kwani mwongozo wake wa namna ya kuanzisha blogu ndio ulionifanya niwe hapa nilipo.Wazo la kuanzisha blog hii lilitokana na ukweli kwamba gazeti lililokuwa linatoa makala zangu halikuwa na tovuti,hivyo awali blog hii ilikuwa kwa ajili ya kuwawezesha watu wote wanaojua Kiswahili popote walipo duniani wapate fursa ya kusoma makala hizo ambazo hazikuwa mtandaoni.Baadaye nikatanua wigo wa uandishi wa makala kwa kuanza kuandika kwenye magazeti ya Mtanzania na Raia Mwema ambako makala zangu hutoka mara moja kwa wiki.

Mmmoja ya watu waliosaidia sana kuitangaza blog ni hii ni rafiki yangu Haki Ngowi.Huyu hana hiana linapokuja suala la kupromoti blog ya bloga mwenzie.Nakumbuka waungwana flani waliwahi "kunitosa" nilipowatumia ombi la kubadilishana vinganishi (exchange links) kwa vile sikuwa naendana na maudhui ya blog yao.Nawashukuru kwani walinipa changamoto kubwa sana.

Mie ni muumini wa msemo "beauty should never be imprisoned",kitu kizuri shurti kisifiwe.Lakini mpewa sifa asibweteke bali anapaswa kuendeleza jitihada (sio kwa ajili ya kupata sifa zaidi) bali kuhalalisha kwamba waliompa sifa hapo awali hawakuwa "wanampaka mafuta kwa mgongo wa chupa",au kwa lugha ya mtaani, hawakuwa "wanamzuga".Nawashukuru nyote mnaonitumia barua-pepe za pongezi kuhusu makala zinazotoka kwenye magazeti nayoandikia pamona na zile zinazotoka kwenye blog hii.Nyie ndio chachu ya ya mafanikio ya makala hizo.

Nina tabia moja ambayo imenitengenezra marafiki na maadui wengi,nayo ni kusema ukweli.Huwa sioni aibu kukiri kwamba nimejifunza kitu flani kutoka mahala flani,kama ambavyo huwa sioni dhambi kumkosoa mtu naedhani amekosea jambo flani.Huko nyuma nilishawahi kuingia kwenye mgogoro na kampuni flani ya magazeti kwa vile tu niliwakosoa pale nilipoona wamepotoka.Tofauti na matarajio yangu,waungwana hao wakaanza kuhoji kuhusu maendeleo yangu ya elimu.Binafsi,huwa sipendi kabisa majadiliano kuhusu masuala ya shule yangu kwani naamini ni suala binafsi (only exception,ni pale majadiliano hayo yanapokuwa ya kitaaluma).

Kuna bloga anaitwa Mpayukaji Msemaovyo.Laiti kungekuwa na mashindano ya kutafuta blogu zenye "kiwango cha juu cha uchungu kwa nchi" basi naamini Mpayukaji angekamata nafasi ya juu kabisa.Simsifii kwa vile tu napenda anachaondika,bali ni ukweli kwamba blog yake imekuwa ni darasa zuri kwangu kujifunza "uchungu kwa nchi yangu na mapambano dhidi ya ufisadi na mafisadi".Uzuri wa makala za Mpayukaji,ambazo hupatikana pia kwenye gazeti la Tanzania Daima,ni ile tabia yake ya kuliita jiwe ni jiwe na sio tofali (calling a spade a spade).Unajua,kuna kusifia kitu kwa matarajio ya kupewa asante flani (kitu ambacho nakipinga kwa nguvu zote) na kuna kusifia kitu kwa vile kina kila sababu ya kusifiwa,na hicho ndicho nachokifanya hapa.Kuna wakati huwa nasoma makala za Mpayukaji huko Tanzania Daima mpaka najikuta naijiwa na taswira ya nyuso za mafisadi zinavyokunjamana kwa hasira iliyochanganyika na aibu+maumivu (truth pains) kutokana na uzito wa hoja za Mpayukaji.

Nitaendelea kuwapongeza waandishi na bloggers wengine ambao wanawatumia Watanzania kwa upenyo huu "mpya" uliojitokeza (mtandao) kuwasilisha vilio,kero,manung'uniko,lawama na hata pongezi kuhusu taifa letu.Pia nitaendela kuwapongeza wenzetu wanaotuletea habari kwa njia ya picha kwani taswira (image) inaweza kuwakilisha maneno elfu kadhaa kwa wakati mmoja.

(Picha ya Mpayukaji nimeipata kutoka kwenye profile ya blogu yake pasipo idhini yake,nitaomba idhini baadaye).

Almanusura nisahau.Hivi huko nyumbani watoto wangapi wanaoamua kutoroka majumbani kwao kutokana na sababu moja au nyingine?Je kuna mahauzigeli wangapi wanaoamua kutoroka kwa waajiri wao kutokana na manyanyaso yaliyopita kiasi?Katika mfumo ambao mnyonge licha ya kutokuwa na haki ananyang'anywa hata ile haki ndogo aliyozaliwa nayo (utu),kundi hili linabaki kuwa halina mtetezi.Clip hii ya Ludacris ft Mary J. Blidge katika wimbo Runaway Love inaweza kutukumbusha wajibu wetu kama jamii


17 Jan 2008


Gavana mpya wa Benki Kuu,Profesa Benno Ndulu,amefanya mabadiliko kadhaa katika uongozi wa benki hiyo.Katika mabadiliko hayo,Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala (DAP) wa B.O.T,AMATUS LIYUMBA (pichani) ameondolewa katika wadhifa huo.Habari kamili soma hapa.
(Picha hii ya zamani ya Liyumba ni alipokuwa Mkuu wa Chuo cha BoT 1993-2000)

16 Jan 2008


Wiki iliyopita ilitawaliwa na surprises mbili:huko New Hampshire,Marekani,Hillary Clinton aliibuka mshindi kwenye primaries za chama cha Democrats,kinyume kabisa na utabiri wa awali wa waendesha kura za maoni na wachambuzi wa siasa za nchi hiyo.Na huko nyumbani,ugavana wa Daudi Balali ulitenguliwa.Wakati ili kuelewa nini kinaweza kuwa chanzo cha tofauti kati ya utabiri (kwamba Hillary angeshindwa) na matokeo (ambapo mwanamama huyo alishinda) kunahitaji upeo wa namna flani kuhusu siasa za Marekani na tabia ya chaguzi katika nchi hiyo (kwa mfano phenomenon kama Bradley effect),utenguzi wa ugavana wa Balali haukuhitaji hata short course ya uchambuzi wa siasa kubaini kwamba he had to go,pengine mapema zaidi ya wiki iliyopita.

Makala yangu ndani ya gazeti la Raia Mwema wiki hii inazungumzia surprises hizo mbili.Inakwenda mbali zaidi kwa kuhoji iwapo ufisadi uliopelekea Balali kupoteza unga wake ulihusisha mtu mmoja pekee.Kadhalika,inahitimisha kwamba kufanikiwa kwa ufisadi huo ni failure kwa TAKUKURU na jeshi la Polisi,taasisi ambazo kimsingi zilipaswa kuchukua hatua mapema kuzuia na/au kupunguza uhalifu huo.

Pamoja na makala nyingine zilizokwenda shule ndani ya Raia Mwema,bingirika na makala hiyo hapa.

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.